Uturuki na Siria:tetemeko limeharibu ofisi za Caritas,lakini wahudumu kibinadamu wanatoa msaada
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.8 lililotokea kaskazini-magharibi mwa Siria na Uturuki limesababisha maelfu ya watu kukosa makazi, chakula na mafuta. Caritas Uturuki na Caritas Siria walikuwa wakitoa msaada tangu mwanzo na Shirikisho la Caritas Internationalis linaunga mkono na kuratibu juhudi zao za kutathmini mahitaji na kutoa msaada kwa walioathiriwa na janga hili. Maeneo yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi tayari yalikuwa katika hali ngumu ya kibinadamu. Baridi kali katika msimu wa baridi na uharibifu au uharibifu mkubwa wa miundo ikiwa ni pamoja na hospitali kadhaa na wakati huo huo barabara kuzidisha ugumu wa shughuli za kibinadamu.
Riad Sargi, Mkurugenzi wa Caritas Siria, ameelezea kuwa nchini Siria, tetemeko la ardhi liliathiri sana kaskazini-magharibi mwa Siria, eneo ambalo watu milioni 4.1 wanategemea msaada wa kibinadamu. Takriban watu 5,000 waliokimbia makazi yao, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, ambao wamepata makazi katika shule na kumbi. Idadi ya vifo na majeruhi iliyorekodiwa inaendelea kuongezeka huku msako wa kuwatafuta watu waliopotea miongoni mwa vifusi vya majengo na nyumba zilizoharibiwa ukiendelea. Hospitali katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika zaidi zilizidiwa wakati zikifanya kazi ya kuwatibu waliojeruhiwa na tetemeko hilo la ardhi.
Caritas Siria kwa hiyo inafanya kazi ya kutoa vifaa vya usaidizi na kufungua makazi ili kuwahudumia wale wanaohitaji zaidi huko Aleppo, Hama na Lattakia. Ni baridi sana na inaendelea kuanguka na theluji. Wengi wamepoteza makazi yao na hata wale ambao bado wana nyumba hawarudi kwao kwa kuhofia kushtuka Zaidi,alisisitiza Sargi. Huko Aleppo, vitu vya msaada na makazi ya watu ambao nyumba zao zilibomoka zinahitajika. Ofisi ya Caritas Aleppo iliharibiwa, pamoja na nyumba nyingi za wafanyakazi. Nchini Uturuki, mikoa ya kusini-mashariki ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na Kahramanmaraş, Hatay, Osmaniye, Adıyaman, Gaziantep, Şanlıurfa, Diyarbakır, Malatya na Adana iliathiriwa na tetemeko la ardhi na mitetemeko midogo mfululizo 42, baada ya tetemeko, kubwa zaidi ikiwa na la ukubwa wa 6.6.
Jimbo la mkoa wa Anatolia limeathiriwa sana na tetemeko la ardhi na Kanisa kuu la Iskenderun lilianguka kabisa. Ofisi za Caritas Anatolia ziliharibiwa vibaya. Lakini “Nashukuru Mungu wafanyakazi wako salama, lakini tumepoteza watu wa kujitolea, wafadhili na hata ndugu” alisema, Giulia Longo, Meneja Programu wa Caritas Uturuki, ambaye alikuwa Italia wakati wa tetemeko la ardhi pamoja na rais wa shirika hilo, Monsinyo Paolo Bizzeti, na sasa amerejea Uturuki. Kwa upande wake alisema “Rais na mimi tuko hai kwa muujiza. Kama tungekuwa Iskenderun pengine tusingeokolewa,” Longo alisema.
Caritas Uturuki mara moja ilifungua simu ya dharura ya Kituo cha Kusikiliza ili kutoa msaada na usaidizi kwa wale walioathiriwa na maafa, na kwa sasa inafanya kazi pamoja na mamlaka mahalia katika kukusanya taarifa na kuandaa jibu la kibinadamu. Kwa kuongezea, timu za Caritas zimekuwa zikiwakusanya watu waliohamishwa katika maeneo salama na ya wazi na kujaribu kusambaza chakula cha moto na nguo. Shirikisho la Caritas linaunganisha juhudi zao na kufanya kazi kwa pamoja ili kutoa misaada ya kibinadamu kwa wale wanaohitaji zaidi na kuomba msaada na maombi endelevu ya jumuiya ya kimataifa katika kupunguza mateso ya watu nchini Siria na Uturuki kwa wakati huu.