Tafakari Dominika 25 ya Mwaka B: Uongozi Ndani ya Kanisa ni Huduma ya Upendo
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 25 ya Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni maonyo juu ya tamaa mbaya, chanzo cha vurugu, machafuko na malumbano kwanza kwa mtu binafsi ndani mwaka, halafu kati ya mtu na mtu mwingine, familia, jumuiya, Kanisa, taifa na ulimwengu kwa ujumla. Ili kuepuka haya yote sharti ni kuishi kwa kuongozwa na hekima itokayo juu kwa Mungu ambayo kwayo inatujalia amani, upendo, utulivu na moyo wa utumishi na kutufanya kuwa wana wa Mungu, warithi wa uzima wa milele. Maana tukiongozwa na hekima ya Mungu kila tumwitapo na kumlilia atatusikiliza kama wimbo wa mwanzo unavyosema; “Bwana asema: Mimi ni wokovu wa watu. Wakinililia katika taabu yo yote nitawasililiza, nami nitakuwa Bwana wao milele”. Na Mama Kanisa akilitambua hili katika sala ya mwanzo anasali hivi kwa haya matumaini; “Ee Mungu, umeziweka katiba zote za sheria takatifu katika amri ya kukupenda wewe na jirani. Utuwezeshe kuzishika amri zako tupate kustahili kuufikia uzima wa milele.” Somo la kwanza ni la Kitabu cha Hekima ya Sulemani (2:12, 17-20). Katika somo hili tunaona mtazamo wa Agano la Kale kuhusu mtu mcha Mungu. Mtu huyu aliitwa “mwana wa Mungu”. Lakini huyu mcha Mungu, mwana wa Mungu, alichukiwa na waovu maana matendo yake mema yaliwasuta na kuzishitaki dhamiri zao ovu na kuumiza mioyoni yao. Ndivyo wanavyoshuhudia wao wenyewe wakisema; “Zaidi ya hayo tumwotee mtu wa haki, maana hatuna haja naye, naye yu kinyume cha matendo yetu, atukaripia ya kama tumeiasi torati, na kutushitaki ya kama tumekosa adabu.”
Kwa kuwa ndani ya mioyo yao yamejaa mawazo maovu, basi wanapanga maovu kwa mtu mwema wakisema; “Haya na tuone kama Mungu atamtegemeza na kumwokoa mikononi mwa adui zake. Na tumhakikishe kwa jeuri na maumivu, ili tujifunze upole wake na kuithibitisha saburi yake akidhulumiwa. Hata tumhukumu auawe mauti ya aibu, maana ataangaliwa sawa sawa na maneno yake.” Mababa wa Imani wameona tangu mwanzo katika katika somo hili utabiri wa namna Yesu Kristo mtu mwema na mwenye haki alivyotendwa kwa jeuri na watu waovu na kuuawa kifo cha aibu msalabani ili atukomboe sisi watu waovu na wadhambi kutoka utumwa wa shetani. Ndio kusema kuwa Yesu ni hekima halisi iliyoshuka kutoka mbinguni kutufunulia mpango wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Lakini bado hata nyakati zetu, mtu mwema bado anaendelea kuteseka kwa mateso mengi kwa hila za waovu kwa sababu tu ya matendo yake mema. Tujiulize ni mara ngapi hata sisi tumepanga na kushiriki mipango miovo iliyo sababisha mateso na mahangaiko ya watu wengine tena bila hatia yoyote? Tuombe hekima ya Mungu ikae ndani mwetu ili ituepushe na mipango miovu ya kuwaumiza watu wengine hata kama ni waovu, Mungu aliye hakimu wa haki ndiye atakaye wahukumu na sio sisi. Lakini pia tukikumbana na magumu, mateso na changamoto katika maisha yetu tusikate tamaa bali tujikabidhi kwa Mungu Yeye atasikiliza sala na maombi yetu na kutuokoa kutoka mitego ya adui zetu.
Ndivyo hekima ya mzaburi inavyotuasa katika wimbo wa katikati ikisema; “Ee Mungu, kwa jina lako uniokoe, na kwa uwezo wako unifanyie hukumu. Ee Mungu uyasikie maombi yangu, uyasikilize maneno ya kinywa changu. Kwa maana wageni wamenishambulia, wote watishao wanaitafuta nafsi yangu; hawakumweka Mungu mbele yao. Tazama, Mungu anayenisaidia; Bwana ndiye anayeitegemeza nafsi yangu. Kwa ukunjufu wa moyo nitakutolea dhabihu, Ee Bwana, nitalishukuru jina lako, maana ni jema” (Zab. 54:1-4, 6). Somo la pili ni la Waraka wa Yakobo kwa Watu Wote (3:16-4:3). Somo hili linafundisha namna Mkristo anavyopaswa kuishi kwa hekima ya kikristo. Hekima hii ina sifa hizi; ni safi, ya amani, ya upole, iko tayari kusikiliza, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki wala hila yoyote. Ikikosekana hii hekima matokeo yake ni; vita, mapigano, wivu, ugomvi, machafuko, na kila tendo baya na tamaa zisizofaa miongoni mwa wakristo na watu wengine pia. Daima tuiombe basi hekima hii ya Mungu ituongoze katika maisha yetu ili tuweze kuishi kadiri ya mapango wa Mungu kwa amani, furaha na upendo. Injili ni ilivyoandikwa na Marko (9:30-37). Katika sehemu hii ya Injili Yesu anatabiri mara ya pili mateso, kifo na ufufuko wake akisema; “Mwana wa Adamu yu aenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka.” Katika maneno haya ya Yesu tunaonja mwangwi wa utabiri wa Nabii Isaya katika somo la kwanza juu ya kifo cha mtu mwema. Wanafunzi wake hawakuelewa fundisho hili. Lakini hata hivyo hakuna aliyedhubutu kumuuliza anachomaanisha maana walijaa woga, hofu na mashaka. Lakini Yesu alitambua mawazo yao, na walipofika Kapernaumu aliwauliza; “Mlishindania nini njiani?” Hakuna aliyedhubutu kujibu.
Marko anasema; “Wakanyamaza; kwa maana njiani walikuwa wakibishana wao kwa wao, ni nani aliye mkubwa kati yao.” Yesu akaweka wazi utume wake na kuwaambia kuwa; “Mtu anayetaka kuwa wa kwanza atakuwa wa mwisho kuliko wote, na mtumishi wa wote.” Kisha akatoa wosia wa kuwa na wasifu wa watoto wadogo maana wao matumaini yao yote kwa wazazi wao. Nasi tuweke tumaini letu lote kwa Mungu Baba yetu. Basi tujitahidi kuwa watu wema, wenye kuongozwa kwa hekima ya Mungu, ili tuwe watumishi wema na waaminifu wa wengine. Daima tuepuke tamaa mbaya ili tuweze kuishi kwa amani na furaha kwa pamoja kama watoto wa Mungu. Maana mwenye tamaa mbaya ya madaraka, mali na umaarufu atafanya kila jitihada kutimiza tamaa yake mbaya hata ikibidi kuwanyang’anya wengine haki ya kuishi. Tamaa mbaya inatufanya tuwe na wivu na hata uadui na watu wengine na kutenda dhambi mbaya zaidi. Tukumbuke kuwa tamaa mbaya inaaza taratibu katika mawazo ya mtu, ukiipalilia inatawala mawazo yako na kukufanya uifikirie kila wakati hata ukilala unaota unachokiwaza. Ukiamka unafanya mipango ili kutimiza ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wote wanaoweza kuleta kipingamizi mbele yako na hivyo sala yako. Tukumbuke kuwa ili tuweze kuondokana na tamaa mbaya sharti tukubali kuongozwa na Hekima ya Kikristo. Anayeongozwa na hekima hii: yuko tayari kusamehe. Yuko tayari kuachilia haki yake ikibidi kwa ajili ya amani. Yuko tayari kuwasikiliza wengine. Atazaa matunda mema; amani, uvumilivu na kusamehe.
Tumwombe Mungu atuepushe na tamaa mbaya na ubinafsi, atujalie unyenyekevu, tutambue kuwa maisha ni zaidi ya umaarufu, mali, mamlaka au madaraka. Maisha ni zaidi ya kujulika, maisha ni zaidi ya tamaa za mwili, maisha ni zaidi ya malumbano. Basi tuitafute kwa bidii Hekima itokayo juu ili ituwezeshe kuishi kwa amani na furaha na mwisho wa yote tukaurithi uzima wa milele. Lakini kwa nguvu zetu wenyewe hatuwezi kitu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatombea neema na baraka za kiekaristi akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uwe radhi kuzipokea dhabihu zetu sisi taifa lako; utujalie kupata katika sakramenti takatifu hayo tunayoungama kwa imani”. Na katika sala baada ya Komunyo anahitimisha maadhimisho haya akisali kwa matumaini haya; “Ee Bwana, sisi unaotuburudisha kwa sakramenti zako, utuinue kwa msaada wako wa siku zote, tupate matunda ya ukombozi kwa njia ya mafumbo yako na mwenendo wetu.” Tumsifu Yesu Kristo!