Tafuta

Papa Francisko: Anawataka viongozi wa Kanisa kuangalia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo katika ukweli na kujikita katika huduma kwa waathirika! Papa Francisko: Anawataka viongozi wa Kanisa kuangalia nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo katika ukweli na kujikita katika huduma kwa waathirika! 

Papa: Nyanyaso za Kijinsia Ndani ya Kanisa: Ukweli na Huduma Makini!

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu anakazia umuhimu wa kukabiliana na ukweli kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo; kutubu na kumwongokea Mungu, sanjari na kuomba kwa unyenyekevu msamaha kwa waathirika. Ni katika mazingira haya, Kanisa litaweza kurejesha hadhi yake ya kuwa ni mahali pa ukarimu, usalama na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM, kwa kushirikiana na Kituo cha Ulinzi wa Watoto Wadogo Poland “Centrum Ochrony Dziecka / Child Protection Centre, Kraków, Poland” imeandaa Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo huko Varsavia, Poland kuanzia tarehe 19 hadi 22 Septemba 2021 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utume Wetu wa Pamoja Ni Kuwalinda Watoto wa Mungu”. Mkutano huu unazishirikisha nchi 18 kutoka Ulaya ya Kati na Mashariki. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuwa na sera na mikakati ya pamoja kwa Makanisa yote mahalia Ukanda huu dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo. Huu ni muda wa kufanya tafiti makini, kujenga utamaduni wa kusikiliza, ili kubainisha hatua ambazo zimekwisha kuchukuliwa na Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya Kashfa ya Nyanyaso za Kijinsia ndani ya Kanisa. Ni fursa ya kuibua mambo msingi ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga ili kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa na Kanisa ni: Toba na wongofu wa ndani; Ukweli, Uwazi na Uwajibikaji, ili kutambua uzito na madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo katika maisha na utume wa Kanisa.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa mkutano huu anakazia umuhimu wa kukabiliana na ukweli kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo; kutubu na kumwongokea Mungu, sanjari na kuomba kwa unyenyekevu msamaha kwa waathirika. Ni katika mazingira haya, Kanisa litaweza kurejesha hadhi yake ya kuwa ni mahali pa ukarimu, usalama na upendo. Baba Mtakatifu anasema, Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo kwa mwaka 2019 ulijikita zaidi katika mchakato wa ukweli na uwazi; utambuzi wa makosa na uwajibikaji kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Tangu wakati huo, kumekuwa na hatua kubwa ambazo zimechukuliwa na Mama Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa maazimio yaliyotolewa na wajumbe wa mkutano huo. Sekretarieti kuu ya Vatican imejiwekea Sheria, Kanuni na Taratibu za Kufuatwa.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee kabisa kwa viongozi wa Kanisa kukabiliana na ukweli kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, kutubu na kuongoka na hatimaye, kuomba msamaha kutoka kwa waathirika na kwa njia hii, Kanisa linaweza kurejea kuwa ni mahali pa: Ukarimu na kimbilio la usalama kwa wahitaji. Toba na wongofu wa ndani ni mambo yanayopaswa kumwilishwa katika mageuzi makubwa, ili kuzuia kashfa kama hizi zisijitokeze tena ndani ya Kanisa, kwa kuwaaminisha viongozi wengine kwamba, Kanisa limedhamiria kufanya mabadiliko ya kweli! Baba Mtakatifu anawataka wajumbe kusikiliza kilio cha waathirika kwa umakini mkubwa, ili viongozi wa Kanisa wakiwa wameungana kwa pamoja na jamii katika ujumla wake waweze kufanya majadiliano kwa sababu yanagusa maisha na utume wa Kanisa: Ulaya ya Kati na Mashariki kwa siku za usoni.

Yote haya ni kwa ajili ya mustakabali wa Ukristo katika ujumla wake. Na huu ndio wajibu wao msingi. Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wao si wa kwanza wala wa mwisho kuwajibika katika kipindi hiki kigumu. Kutambua na kukiri udhaifu na makosa yaliyotendeka ni kielelezo cha udhaifu, lakini ni chemchemi ya neema, mahali pa kujimwaga ili kupata mwelekeo mpya wa upendo na huduma kwa watu wa Mungu. Ikiwa kama watoto wa Kanisa watatambua makosa na udhaifu wao, wala hawatakuwa na woga, kwani bila shaka huu ni mwongozo wa Mwenyezi Mungu ambaye amewaongoza hadi kufikia hapa! Asiwepo mtu anayenyooshewa kidole kwa maovu haya, bali upendo kwa wote, ili katika unyenyekevu wao, waweze kuwa ni vyombo vya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia, wawe ni wadau kwa mafao ya wengi kwa siku za usoni; viongozi wa Kanisa wajifunze kutoka kwa wengine, ili kuwa waaminifu zaidi na mashujaa, ili kwa pamoja kuweza kukabiliana na changamoto hizi kwa siku za usoni!

Papa Nyanyaso za Kijinsia

 

 

20 September 2021, 14:15