Tafuta

Harusi ya Kana ya Galilaya: Ishara ya Kwanza Ya Huruma na Upendo

Ishara hii ni mwanzo wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaodhihirisha ukaribu, upole na huruma yakee. Yesu anatenda ishara hii kwa wanandoa wapya, katikati kabisa ya furaha ya ndoa yao. Kutindikiwa divai, kungeharibu sherehe nzima na wageni wangetupa vijembe! Bikira Maria alikuwa wa kwanza kung’amua changamoto waliyokuwa nayo wanandoa hawa wapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tafakari ya Injili ya Yohane 2: 1-12 Dominika ya Pili ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa inajikita katika ufunuo wa huruma, upendo na furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu anayefungua ukurasa mpya wa uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake. Huu ni mwaliko wa kuendelea kudumu katika uaminifu, upendo, umoja na mshikamano na Kristo Yesu chimbuko la ukombozi wa mwanadamu. Ishara ya Harusi ya Kana ya Galilaya ni kielelezo cha upendo na uaminifu wa Mungu kwa watu wake. Mwinjili Yohane anamweka mbele ya macho ya waamini Bikira Maria anayeguswa na mahitaji ya wanandoa wapya waliotindikiwa na divai na hivyo kuomba huruma na upendo wa Yesu kwa niaba yao! Divai ni ishara ya furaha na upendo, lakini wakati mwingine, mwanadamu anatindikiwa na divai, kumbe, katika muktadha huu, waamini wajifunze kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, atakayewaonesha uwepo wa Mungu katika safari ya maisha yao ishara ya: Imani, furaha na upendo. Ujio wa Kristo Yesu ni chemchemi ya: upendo, furaha, huruma na utakaso katika maisha.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika, tarehe 16 Januari 2022 amesema, ni katika harusi ya Kana ya Galilaya, Kristo Yesu alifanya ishara yake ya kwanza kwa kugeuza maji kuwa ni divai, akaudhihirisha utukufu wake, wanafunzi wake wakamwamini. Mwinjili Yohane anakazia kuwa ni “Ishara” na wala si muujiza unaonesha nguvu na ukuu wake, ili kuwashikisha watu tama kwa mshangao. Ishara hii ni mwanzo wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaodhihirisha ukaribu, upole na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu anatenda ishara hii kwa wanandoa wapya, katikati kabisa ya furaha ya ndoa yao. Kutindikiwa divai, kungeharibu sherehe nzima na wageni waalikwa kuanza “kutupa vijembe.” Bikira Maria alikuwa wa kwanza kung’amua changamoto waliyokuwa wanakabiliana nayo wanandoa hawa wapya, akaamua kuingilia kati pasi na makuu wala kutaka “kujimwambafai” mbele ya wanandoa na wageni waalikwa, bali yote akayatenda katika hali ya kimya kikuu. Kristo Yesu akawaambia kuyajaliza mabalasi maji yaliyopata kuwa divai.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi ndivyo anavyotenda Mwenyezi Mungu, kwa kuonesha ukaribu kwa waja wake katika hali ya ukimya pasi na makuu. Wanafunzi wake walipoona ishara hii, wakafurahi kwa sababu sherehe hii ya ndoa ilipendeza zaidi, kiasi kwamba, yule mkuu wa meza akamwita bwana harusi na kumpongeza kwa kuandaa divai iliyo njema zaidi, bila kutambua kwamba, ishara hii ilitendwa na Kristo Yesu, aliyepaswa kusifiwa. Huo ukawa ni mwanzo wa mbegu ya imani yao kuanza kukua na kuchanua kwa kutambua uwepo wa Kristo Yesu, ufunuo wa upendo wa Mungu, ambao ni Mungu mwenyewe. Hii ni ishara inayotendeka miongoni mwa watu wa kawaida kabisa pasi na makuu. Waamini wajifunze kumkimbilia Bikira Maria katika furaha, shida na mahangaiko yao, kwani daima yuko tayari kuwasikiliza na kuwaombea. Waamini wakitambua ishara hii, wataweza pia kutekwa na huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, kiasi cha kugeuka na kuwa ni wafuasi wake. Kwa kawaida harusini, divai njema ilikuwa inatolewa mwanzoni mwa sherehe, waalikwa wakisha kulewa, wanapewa “divai iliyoongezwa maji” au “divai iliyochakachuliwa” Lakini, uwepo wa Kristo Yesu, unawawezesha wanandoa wapya kuhitimisha sherehe yao kwa divai njema zaidi, kwa sababu Mwenyezi Mungu anataka kuona watoto wake wakiwa na furaha ya kweli.

Ishara hii si kwa ajili ya Kristo Yesu “kujitafutia ujiko” kwa wanandoa wapya, anafanya yote kwa huruma na upendo wa kweli. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuchunguza kutoka katika undani wa maisha yao, ili kuweza kuona ishara ambayo Mwenyezi Mungu amewatendea kama kielelezo na ishara kwamba, anawapenda kwa dhati. Wachunguze na kuangalia ule wakati mgumu na tete, walipohisi huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Waendelee kujiuliza, Je, ni kwa jinsi gani wameweza kugundua ishara ya ukaribu na uwepo wa Mungu katika maisha yao? Je, walibahatika kuwa na furaha kubwa moyoni? Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutambua ishara ya ukaribu na uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa sala na maombezi ya Bikira Maria, kama ilivyokuwa kwenye harusi ya Kana ya Galilaya, daima yuko makini kuwasaidia ili waweze kufaidika na ishara ya uwepo wa Mungu katika maisha yao.

Divai Njema

 

16 January 2022, 14:28

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >