Tafuta

Ni ajira nyingi za watoto ambao wananyimwa haki na hadi zao Ni ajira nyingi za watoto ambao wananyimwa haki na hadi zao 

Papa,ajira za utoto:vyombo husika tafuta njia ya kulinda hadhi na haki za watoto

Papa Francisko katika ujumbe wake aliotuma kwa washiriki wa Mkutano wa V wa Kimataifa wa ILO uliofunguliwa Jumatatu 16 Mei huko Durban nchini Afrika Kusini na ambao unajikita na mada ya kuondoa unyonyaji wa ajira za watoto na vijana,amesema:"tupambane dhidi ya tukio hili kwa kutafuta suluhisho na maamuzi stahiki ya pamoja ili kurudisha maisha kwa walio wadogo na wenye haki.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani ILO, limeandaa Kongamano la V la kimataifa kuhusu kutokomeza ajira ya watoto duniani  lililifunguliwa mnamo mnamo tarehe 16 Mei 2022 huko mjini Durban nchini Afrika Kusini kwa kutoa  wito wa kutaka kuchukuliwa hatua za haraka ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya watoto wanaotumbukia katika ajira za utotoni. Katika fursa hiyo Papa Francisko ametuma  ujumbe wake Jumanne tarehe 17 Mei 2022  akiuelekeza kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi duniani (ILO), Bwana Guy Ryder, Baba Mtakatifu amesema katika tukio la Kongamano la Tano la Kimataifa la Kutokomeza Ajira za Watoto, anamtumia  salamu za joto na kwa wote waliokusanyika huko Durban kwa tukio hilo.

Licha ya mafanikio ya kuondoa janga hili,lakini bado utumikishwaji katika jamii umekithiri

Baba Mtakatifu Francisko amebainisha kwamba licha ya mafanikio makubwa yaliyo patikana katika kuondoa janga la utumikishwaji wa watoto katika jamii, lakini janga hili limezidishwa na athari za msukosuko wa kiafya duniani na kuenea kwa umaskini uliokithiri katika maeneo mengi ya dunia, ambapo ukosefu wa nafasi za kazi zenye staha watu wazima na vijana, uhamiaji na dharura za kibinadamu zinaona mamilioni ya wasichana wadogo na wavulana kuishi maisha ya umaskini wa kiuchumi na kiutamaduni. Cha kusikitisha ni kwamba mikono mingi  ya wadogo ina shughuli nyingi za kulima mashambani, kufanya kazi migodini, kusafiri umbali mrefu kuchota maji na kufanya kazi zinazowazuia kwenda shule, bila kusema lolote kuhusu uhalifu wa ukahaba wa watoto, ambao umewanyima mamilioni ya watoto furaha hiyo, ujana wao na hadhi waliyopewa na Mwenyezi Mungu.

Ushauri wao unaweza kuondoa kashfa ya umaskini katika familia

Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba,  "kwa kuwa umaskini ndio sababu kuu inayowaweka watoto kwenye unyonyaji wa kazi", ana uhakika kwamba "mashauri yao hayatashindwa kushughulikia sababu za kimuundo za umaskini wa kimataifa na ukosefu wa usawa kwa  kashfa inayoendelea  ya kuwepo miongoni mwa wanafamilia wa ubinadamu(rej. Fratelli Tutti,116). Vile vile, Papa anaamini kuwa Mkutano huo utaongeza uelewa na kujitolea kwa watendaji wa kijamii na vyombo husika vya kimataifa na kitaifa vinavyofanya kazi kutafuta njia zinazofaa na muhimu za kulinda hadhi na haki za watoto, hasa kupitia kuhamasisha jamii, mifumo ya ulinzi na upatikanaji wa elimu kwa wote.

Kanisa Katoliki na wasiwasi wa suala la ajira za utotoni

Suala la ajira kwa watoto linatia wasiwasi hasa kwa Kanisa Katoliki, ambalo mafundisho yake ya kijamii yanasisitiza kwamba: “kwa kuhakikisha maisha ya sasa na ya baadaye ya watoto, tunahakikisha pia maisha ya sasa na yajayo ya familia nzima ya kibinadamu. Kwa hakika, jinsi tunavyohusiana na watoto, kiwango ambacho tunaheshimu hadhi yao  ya kuzaliwa na haki zao msingi, huonesha kwa watu wazima ni wa aina gani na tunataka tuwe wa aina gani ya jamii tunayotaka kuijenga” (rej. Hotuba ya Papa kwa Washiriki katika Kongamano la Kimataifa la “Kutokomeza Ajira ya Watoto, Kujenga Wakati Ujao Bora”, 19 Novemba 2021).

Vatican iko bega kwa bega kuhakikisha jitihada dhidi ya ajira za utotoni

Vatican kwa upande wake Papa amebainisha kwamba itaendelea kufanya kazi ili kuhakikisha Jumuiya ya Kimataifa inadumisha juhudi zake za kupambana na unyonyaji wa utumikishwaji wa watoto kwa uthabiti, kwa pamoja na kwa dhati, ili watoto waweze kufurahia uzuri wa hatua hii ya maisha yao, huku pia wakikuza ndoto nzuru za siku zijazo. Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru Mkurugenzi wa ILO na Shirika la Kazi Duniani kwa kuandaa na kuendeleza Mkutano huo. Anaomba kwamba mashauri yao yawe ndiyo ahadi ya ukuaji wa kudumu na mustakabali mwema kwa watoto wa wakati wote, Papa amehitimisha ujumbe wake.

UJUMBE WA PAPA KWA ILO
17 May 2022, 13:53