Tafuta

Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Italia: Mambo msingi: Ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi, Sinodi na Huduma ya Upendo kwa watu wa Mungu Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa Nchini Italia: Mambo msingi: Ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi, Sinodi na Huduma ya Upendo kwa watu wa Mungu 

Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa Italia: Shule ya Upendo

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia imekuwa ni nafasi ya kutafakari: Umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Umuhimu wa kutambua kwamba, hii ni Sakramenti pacha na Sakramenti ya Upatanisho ili kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa kama ushuhuda wa Kanisa la Kisinodi: Ushiriki mkamilifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Septemba 2022, huko mjini Matera, yamenogeshwa na kauli mbiu: “Torniamo al gusto del pane. Per una Chiesa Eucaristica e Sinodale” "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate. Kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi." Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kimataifa katika maisha na utume wa Kanisa ni katekesi fungamani na endelevu inayogusa: Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Mwanga linalobubujika kutoka katika Neno la Mungu linalohitaji: kutangazwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Linahitaji usikivu wa kiibada na ukimya wa kitafakari uwezeshao Neno la Mungu kugusa akili na nyoyo za watu. Ekaristi Takatifu ni chakula cha maisha ya kiroho na kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake.  Ekaristi takatifu ni shule ya upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mungu. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na shule ya Upendo; ni zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayomwilishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani.

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unasimikwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia imekuwa ni fursa ya kulitafakari Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika maisha ya waamini, kwa kutambua kwamba, hii ni Sakramenti pacha na Sakramenti ya Upatanisho ili kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho haya. Wameshiriki “Njia ya Nuru ya Ekaristi Takatifu”: “Via Lucis Eucaristica.” Waamini wamepata nafasi ya: Kutafakari, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Kuabudu Ekaristi pamoja na kutolea ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Umoja na ushiriki katika maisha na utume wa Kanisa umejidhihirisha wazi. Kardinali Lazzaro You Heung-sik, “Yu Hung Shik” Mwenyekiti wa Baraza la Makleri, Ijumaa tarehe 23 Septemba 2022, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia na kukazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, mintarafu mang’amuzi na mwanga wa Neno la Mungu. Ni mwaliko wa kukimbilia na kuambata upendo na huruma ya Mungu kama ilivyo kuwa katika maisha ya watakatifu na wafiadini. Waamini wajenge utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, sanjari na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekarist Takatifu pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi takatifu; nafasi ya kukutana mubashara na Kristo Yesu.

Haki msingi za binadamu zipewe kipaumbele cha kwanza
Haki msingi za binadamu zipewe kipaumbele cha kwanza

Lengo ni kuwawezesha waamini kurutubisha maisha yao ya kiroho kwa kuupokea Mkate ulioshuka kuitoka mbinguni. Waamini watambue kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kumbe, wanayo dhamana na wajibu wa kujenga na kudumisha ushirika unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kiini cha upendo mkamilifu. Fumbo la Utatu Mtakatifu liwe ni changamoto kwa waamini kujenga na kudumisha ushirika wa watoto wa Mungu; waamini wawe ni mashuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ni katika muktadha huu, wanawajibika kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu unaobubujika kutoka katika: Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu. Na kwa njia hii, wataweza kuwa ni faraja na matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Upendo wa Kristo Yesu, uwabidiishe kuwa watu wema zaidi. Utenzi kwa upendo wa Mungu “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.” Rum 8: 35-39.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuonesha moyo wa upendo na mshikamano na Kristo Yesu, katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Kardinali Lazzaro You Heung-sik, “Yu Hung Shik” Mwenyekiti wa Baraza la Makleri, amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, Kristo Yesu, anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Utu wa binadamu.
Utu wa binadamu.

Kwa kushiriki Ekaristi Takatifu waamini wanahimizwa kujenga ushirika mkamilifu unaosimikwa katika udugu wa kibinadamu, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na hatimaye, kushiriki utume wa Kanisa. Waamini wanao wajibu wa kupyaisha na kuendelea kunogesha mahusiano na mafungamano ya kijamii. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, amekuwa ni Tabernakulo ya kwanza kumtunza Mwana wa Baba wa milele. Awe ni mfano bora wa kuigwa katika maisha ya sala na imani inayomwilishwa katika huduma ya huruma na upendo kwa watu wa Mungu. Waamini wameshiriki pia katika “Njia ya Nuru ya Ekaristi Takatifu”: “Via Lucis Eucaristica” muhimu sana katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, tayari kutoka kifua mbele kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kama sehemu muhimu sana wa utume wa Kanisa. Waamini wajitambue kuwa wao ni dhaifu na wadhambi, kumbe wanahitaji kufanya hija ya toba na wongofu wa ndani; kwa kusikiliza, kutafakari na hatimaye kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia na vipaumbele vya maisha yao. Roho Mtakatifu awasaidie waamini kujenga na kuimarisha umoja na udugu wa kibinadamu; kwa kuwajali na kuwasaidia “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi.” Hawa ndio maskini wapya wanaozalishwa kila kukicha kwenye ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.

Kongamano Ekaristi Italia

 

 

24 September 2022, 15:09