Tafuta

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni. Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni.  

Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa Italia: Kanisa, Ekaristi na Sinodi: Ushuhuda

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni. Papa Francisko anatarajiwa kuzindua rasmi Jengo Bwalo la Don G. Melle, kielelezo cha mshikamano wa udugu wa upendo na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume, “Kaa Nasi Bwana”: Mane, Nobiscum Domine”, anawaalika waamini kujenga utambuzi hai wa uwepo halisi wa Kristo Yesu, katika adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu na katika Ibada nje adhimisho la Misa Takatifu. Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22 hadi tarehe 25 Septemba 2022, huko Matera, yananogeshwa na kauli mbiu: “Torniamo al gusto del pane. Per una Chiesa Eucaristica e Sinodale” "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi." Ni katika muktadha wa maadhimisho haya, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuhudhuria na hatimaye kuadhimisha Ibada ya kufunga rasmi maadhimisho haya, Dominika tarehe 25 Septemba 2022, kwenye Uwanja wa Michezo wa “XXI Settembre.” Yaani “Septemba 21.” Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na kundi la wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 108 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2022 yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji” kwa “Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.” Ebr 13:14. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anakazia kuhusu: Hatima ya maisha ya mwanadamu, mbingu na nchi mpya, kujenga mustakabali wa wakimbizi na wahamiaji; mchango wao; Yerusalemu mpya ni kwa wote pasi na ubaguzi; mchango maalum wa vijana na mwishowe ni sala kwa ajili ya waamini. Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, kuongoza Sala ya Malaika wa Bwana.

Kongamano la 27 la Ekaristi Kitaifa Italia: Kanisa, Ekaristi na Sinodi
Kongamano la 27 la Ekaristi Kitaifa Italia: Kanisa, Ekaristi na Sinodi

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia yanakita mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni. Baba Mtakatifu anatarajiwa pia kubariki na kuzindua rasmi Jengo Bwalo la Don Giovanni Melle, ambalo limejengwa kama kielelezo cha mshikamano wa udugu wa upendo na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kardinali Matteo Maria Zuppi, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bologna ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Alhamisi tarehe 22 Septemba 2022 amezindua rasmi Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kwa Ibada ya Misa Takatifu, kwa mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Italia kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika maisha, kiini cha mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Hili ni Kanisa linalosimikwa katika umoja, ushiriki na utume wa Kanisa, tayari kutoka kifua mbele kwenda hadi miisho ya dunia, kumtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Huu ni mwaliko wa kuandamana na Kristo Yesu ili kusimama kidete dhidi ya upweke hasi, umaskini, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; rushwa na unyonyaji; mambo yanayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kanisa kama Mama na Mwalimu, anataka kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watoto wake, ili waonje: huruma na upendo wa Kristo Yesu; kwa wadhambi kusamehewa dhambi zao na wagonjwa, kutakaswa na kuponywa magonjwa na udhaifu wao wa kimwili. Jambo la msingi ni waamini kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Kardinali Matteo Maria Zuppi, anakaza kusema, ni katika ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu waamini wanaweza kuchota amana na utajiri wa upendo unaobubujika kutoka katika Ekaristi Takatifu, tayari kuwashirikisha jirani zao. Ibada ya Misa Takatifu inapaswa kuadhimishwa kwa uchaji na nidhamu ya hali juu kabisa, kwa kutambua kwamba, waamini wanashiriki Liturujia ya Neno la Mungu na Ekaristi Takatifu, chakula kinachorutubisha maisha ya kiroho na kimwili. Kanisa la Kisinodi liwe na uwezo wa kuwapatia watu wa Mungu mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Mama wa wote!

Kuna waamini wanashindwa kuadhimisha Ibada ya Misa kutokana na vita
Kuna waamini wanashindwa kuadhimisha Ibada ya Misa kutokana na vita

Huu ni wakati muafaka wa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, baada ya kunyong’onyeshwa na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Ni wakati wa ujenzi wa Kanisa kama familia ya Mungu inayowajibikiana. Kwa bahati mbaya, kuna waamini ambao hawana tena nafasi ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kutokana na vita inayoendelea kusigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watu wana njaa na kiu ya: maisha, matumaini na uhakika wa maisha bora. Kristo Yesu, Neno wa Mungu na Mkate wa Uzima “Corpus Domini, Verbum Domini”, awawezeshe waamini kushiriki maisha na uzima wa Kimungu, ili kukoleza na kunogesha upendo ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Chakula na kinywaji hiki cha mbinguni, kiwe ni chemchemi ya nguvu katika ujenzi wa Kanisa na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Huu ni upendo unaomwilishwa katika huduma, umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; haki na amani dhidi ya vitisho vya utengenezaji, ulimbikizaji na hatimaye matumizi ya silaha za maangamizi za nyuklia. Ekaristi Takatifu, iwawezeshe waamini na watu wenye mapenzi mema kutambua na kuthamini zawadi ya maisha, tayari kushiriki katika ujenzi wa udugu wa binadamu. Hiki ndicho kiini cha Mkate wa Malaika, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni, Mkate wa watoto wa Mungu.

Mji wa Matera: Mkate, Maji na Mshikamano wa Kibinadamu
Mji wa Matera: Mkate, Maji na Mshikamano wa Kibinadamu

Wakati huo huo, Askofu mkuu Antonio Giuseppe Caiazzo, wa Jimbo kuu la Matera-Irsina, amewakaribisha washiriki wa Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kwa kuelezea uzuri wa mji wa Matera, maarufu sana kwa kuoka mikate, tayari kutoa lishe kwa watu wa Mungu. Huu ni mji uliojengwa juu ya mawe, kielelezo cha ushirika na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kuondokana na uchoyo na ubinafsi. Huu ni mji wenye chemchemi ya maji, moja ya sababu zilizopelekea hata Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO, “United Nations Educational, Scientific and Cultural Organization” kuutambua mji wa Matera kuwa ni urithi wa binadamu kunako mwaka 1993, kuonesha kwamba, maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Huu ni mji ambao unasifika kutokana na ukusanyaji wa maji ya mvua, kwa ajili ya matumizi ya binadamu na kama sehemu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Vijana wa Italia wanalishukuru Kanisa kwa kuwashirikisha katika maisha na utume.
Vijana wa Italia wanalishukuru Kanisa kwa kuwashirikisha katika maisha na utume.

Wawakilishi wa vijana kutoka katika majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini Italia, wanalishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, kwa kuwashikirisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya ushiriki mkamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, vijana wataweza kujifunza kuondokana na upweke hasi, ubinafsi na uchoyo, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanapenda kuona ulimwengu unajengwa na kusimikwa katika msingi wa haki, amani na udugu wa kibinadamu, ili kuvunjilia mbali tabia ya ubaguzi na utengano. Vijana wanapenda kumwilisha upendo unaobubujika kutoka katika Ekaristi Takatifu katika medani mbalimbali za maisha, kama sehemu ya ujenzi wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kielelezo makini cha utimilifu wa maisha.

Kongamano Ekaristi Italia
23 September 2022, 17:12