Tafuta

Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa Italia: Kilio cha Papa Kwa Walimwengu

Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, Mama wa Ekaristi Takatifu, kulilinda na kulisindikiza Kanisa nchini Italia, ili liweze kutoa harufu nzuri ya Kristo Yesu, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni. Amewakumbuka na kuwaombea watu wenye mahitaji mbalimbali duniani: Myanmar ambao kwa takribani miaka miwili sasa wametumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, hatari sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia kuanzia tarehe 22-25 Septemba 2022 huko mjini Matera yamezamisha mizizi yake katika: Umoja, Ushiriki na Utume wa Kanisa mintarafu wongofu wa kiikolojia, kichungaji na kitamaduni, ili kunogesha mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi. Haya ni maadhimisho ambayo yamenogeshwa na kauli mbiu: “Torniamo al gusto del pane. Per una Chiesa Eucaristica e Sinodale” "Turudi Kwenye Ladha ya Mkate kwa Kanisa la Kiekaristi na Kisinodi." Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, kama sehemu ya kufunga Kongamano la 27 la Ekaristi Takatifu Kitaifa nchini Italia, amewashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu nchini Italia na kwa namna ya pekee Jimbo kuu la Matera-Irsina kwa kujisadaka kuandaa na hatimaye kuadhimisha Kongamano hili ambalo ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Baba Mtakatifu anawashukuru wote na kuwaombea watu wa Mungu nchini Italia wajibidiishe kuongeza idadi ya watoto wanaozaliwa kwenye familia zao. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria, Mama wa Ekaristi Takatifu, kulilinda na kulisindikiza Kanisa nchini Italia, ili liweze kutoa harufu nzuri ya Kristo Yesu, Mkate ulioshuka kutoka mbinguni.

Papa Francisko amesali kwa ajili ya mahitaji ya watu mbalimbali duniani.
Papa Francisko amesali kwa ajili ya mahitaji ya watu mbalimbali duniani.

Amewakumbuka na kuwaombea watu wenye mahitaji mbalimbali duniani.  Kwa namna ya pekee, watu wa Mungu nchini Myanmar ambao kwa takribani miaka miwili sasa wametumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha madhara makubwa kwa watu wa Mungu nchini humo. Baba amesikitishwa sana na kilio cha wanafunzi wa shule kutoka Myanmar ambao wamelipuliwa na shambulio la mabovu. Inasikitisha kuona kwamba, mashambulizi dhidi ya shule yanaendelea kuzoeleka taratibu, kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Walimwengu waoneshe uthubutu wa kusikiliza na kujibu kilio cha wanafunzi hawa, ili kukomesha vita isiyokuwa na mvuto wala mashiko. Baba Mtakatifu anamwomba, Bikira Maria, Malkia wa Amani, awafariji na kuwaombea watu wa Mungu nchini Ukraine, ili viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waongeze nguvu na utashi wa kisiasa, ili kuhitimisha vita nchini Ukraine inayoendelea kusababisha majanga kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu Francisko ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon ili watu zaidi ya nane waliotekwa nyara na watu wasiojulikana, kutoka Jimbo Katoliki la Mamfe, ili waweze kuwaachia huru mara moja. Kuna Mapadre saba na mtawa mmoja wametekwa nyara, huko Jimbo kuu la Bamenda, nchini Cameroon.

Kuna Mapadre na mtawa wametekwa nyara nchini Cameroon.
Kuna Mapadre na mtawa wametekwa nyara nchini Cameroon.

Kwa upande wake, Kardinali Matteo Maria Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, Mwaka wa Pili katika mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu; ambamo watu wa Mungu wanalishwa na Neno la Mungu pamoja na Ekaristi Takatifu: “Verbum Domini, Corpus Domini”, daima Kristo Yesu akipewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa nchini Italia. Amewashukuru watu wa Mungu kwa sadaka na majitoleo yao, kielelezo cha Kanisa lenye upeo mpana zaidi. Kutokana na maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, waamini wengi walishindwa kushiriki katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, lakini kirusi hatari zaidi ni tabia ya uchoyo na ubinafsi unaowanyima ile furaha, upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kiasi cha kutumbukia katika upweke, vita na mipasuko ya kijamii inayopandikiza utamaduni wa kifo na kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini, njaa na magonjwa, mambo yanayosigina utu na heshima ya binadamu. Huu ni wakati wa kujenga Kanisa la Kisinodi na Kiekarisiti linalosimikwa katika msingi wa ushirika na udugu wa kibinadamu, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote sanjari na kupambana na baa la njaa ndani na nje ya Italia.

Papa Matera

 

25 September 2022, 14:51

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >