Tafuta

Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.” Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.”  

Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Siku ya 9 ya Kimataifa ya Sala na Tafakari Dhidi ya Biashara ya Binadamu

Papa anakazia: Utu na haki msingi za binadamu; anawataka vijana kujenga mtandao wa mshikamano katika kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu anawataka vijana kupanua upeo ili kuona ni mambo yepi yanayowatumbukiza vijana katika biashara haramu ya binadamu; wawe na matumaini katika mapambano haya na hivyo washikamane na wahanga wa vitendo hivi viovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa likaanzisha Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari ili kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo inayoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni muda muafaka kwa ajili ya kusali, kutafakari na kuwaombea waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu. Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu tarehe 8 Februari 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Kutembea katika utu.” Huu ni mwaliko hasa kwa vijana kusaidia kuragibisha maadhimisho haya dhidi ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu na kama sehemu ya maandalizi ya Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku hii hapo tarehe 8 Febuari 2024 kwa utashi na busara za kichungaji za Baba Mtakatifu Francisko. Ni katika muktadha huu, kwa muda wa juma zima kumekuwepo na maadhimisho haya katika ngazi mbalimbali ndani na nje ya Italia na kilele chake ni Dominika tarehe 12 Februari 2023 kwa kushiriki kusali na Baba Mtakatifu Francisko Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kauli mbiu ya mwaka 2023 “Kutembea katika utu” mwaliko wa kutembea bega kwa bega na waathirika wa ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu sehemu mbalimbali za dunia na hasa wahamiaji na wakimbizi kama mahujaji wa utu na matumaini ya binadamu.

Tarehe 8 Februari Siku ya KImataifa ya Sala na Tafakari: Utumwa!
Tarehe 8 Februari Siku ya KImataifa ya Sala na Tafakari: Utumwa!

Ni kwa njia ya umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, biashara haramu ya binadamu inaweza kukomeshwa, ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni muda muafaka wa kuwaunga mkono wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwaokoa, kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa biashara hii, ili kuwapatia tena matumaini katika mahangaiko yao ya ndani, daima wakijiaminisha katika ulinzi na nguvu ya Mwenyezi Mungu inayoganga, kuiponya na kuokoa. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video katika Maadhimisho ya Siku ya Tisa ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu kwa mwaka 2023 anakazia: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; anawataka vijana kujenga mtandao wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili.Baba Mtakatifu anawataka vijana kupanua upeo ili kuona ni mambo yepi yanayowatumbukiza vijana katika biashara haramu ya binadamu; wawe na matumaini katika mapambano haya na hivyo kushikamana na wahanga wa vitendo hivi viovu ndani ya jamii. Baba Mtakatifu anasema maadhimisho ya Mwaka 2023 yanatoa kipaumbele kwa vijana kama wadau wakuu wa mapambano dhidi ya ubidhaishaji wa maumbile ya binadamu, huku wakiendelea kupyaisha matumaini yanayosimikwa katika furaha inayobubujika kutoka katika Neno la Mungu na kwamba, Kristo Yesu ndiye furaha ya kweli.

Wakimbizi na wahamiaji wako hatarini katika biashara ya binadamu
Wakimbizi na wahamiaji wako hatarini katika biashara ya binadamu

Biashara haramu ya binadamu inasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mfumo unaowatajirisha watu ambao dhamiri zao zimekufa, kwa kuwatumbukiza maskini katika biashara hii haramu inayowanyonya na kuwadhalilisha zaidi. Kwa hakika watu wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kutokana na myumbo wa uchumi Kitaifa na Kimataifa; kinzani, migogoro na vita; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mambo mengine kama hayo, ni rahisi sana kuweza kutumbukizwa katika biashara hii haramu. Biashara ya binadamu na viungo vyake, inazidi kuongezeka mara dufu sehemu mbalimbali za dunia na wahanga wakuu ni: wakimbizi na wahamiaji; wanawake na watoto bila kuwasahau vijana wenye ndoto na wanao tamani kuona utu na heshima yao vinadumishwa na wao kuishi kikamilifu utu wao. Baba Mtakatifu anakiri kwamba hizi ni nyakati ngumu, lakini ni ngumu zaidi kwa vijana wa kizazi kipya, ndiyo maana wanahitajika ili kujenga mtandao wa mshikamano katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili. Huu ndio mwanga wa Injili wanaokabidhiwa vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia ili kushiriki katika sala na tafakari jadidi kuhusu ubidhaishaji wa binadamu na viungo vyake. Kwa kitendo hiki, vijana watambue kwamba, wanatumwa kama wamisionari wa utu, heshima na haki msingi za binadamu, dhidi ya biashara haramu ya binadamu.

Siku hii ilianzishwa Mwaka 2015
Siku hii ilianzishwa Mwaka 2015

Hii ni sehemu pia ya mchakato wa maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 10 tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kimataifa ya Sala na Tafakari katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, itakayofikia kilele chake tarehe 8 Februari 2024. Vijana watunze mwanga wa tunu msingi za Kiinjili katika maisha na utume wao, ili hatimaye waweze kuwa ni baraka kwa vijana wenzao sehemu mbalimbali za dunia. Kamwe vijana wasisite kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mabadiliko ndani ya jamii, katika mapambano dhidi ya kashfa hii inayosigina utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni safari inayowataka kuwa na mwelekeo na maono mapana ili kutambua mchakato unaowatumbukiza mamilioni ya vijana na watoto katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Wawe na moyo thabiti wa kugundua maelfu ya watu wanaotafuta uhuru kamili na utu wao. Vijana wajenge mtandao wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu, tayari kujikita katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kujenga jamii shirikishi, yenye uwezo wa kuwatambua wale wanaonyanyasa na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, na hivyo kuonesha utashi wa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za kila binadamu.

Tarehe 8 Februari: Siku dhidi Biashara ya Binadamu
Tarehe 8 Februari: Siku dhidi Biashara ya Binadamu

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba watu wengi wenye mapenzi mema, watakubali wito huu na kuanza kutembea na wale wote ambao wametendwa vibaya kutokana na dhuluma na nyanyaso za kijinsia; watu wanaonyonywa kwa kufanyishwa kazi za suluba kwa “mshahara kiduchu.” Huu ni mwaliko wa kushikamana na wakimbizi pamoja na wahamiaji, ili watu wote katika umoja wao, waweze kwa ujasiri kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kusonga mbele kwa ujasiri, ari na moyo mkuu anasema Baba Mtakatifu Francisko, huku akiwazamisha vijana hawa katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Mtakatifu Josefina Bakhita aendelee kuwakumbuka na kuwaombea. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia baraka zake za kitume katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake.   Baba Mtakatifu Francisko daima anasema, uchumi unapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Sheria, kanuni na taratibu za uchumi fungamani zihakikishe kwamba, haki na usawa vinatendeka sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kanisa linapenda kuweka utu, heshima na haki msingi za wanawake kuwa ni kiini cha tafakari hii, kwani wanawake, wasichana na watoto ndio waathirika wakubwa wa ubidhaishaji maumbile ya binadamu “human trafficking.”

Talita Kum wakiwezeshwa utumwa mamboleo utakoma
Talita Kum wakiwezeshwa utumwa mamboleo utakoma

Itakumbukwa kwamba, “Talita Kum” ambao ni Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa unatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 77 sehemu mbalimbali za dunia, tarehe 8 Februari 2023 umeandaa Siku ya Sala na Tafakari kuhusu athari za biashara haramu ya binadamu na mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. Mtandao wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume Kimataifa, ukipewa ushirikiano wa dhati na vyombo vya ulinzi na usalama kitaifa na kimataifa, uhalifu dhidi ya ubinadamu unaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Kumbe kuna haja kuwatambua waathirika, kuwasaidia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatendewa haki, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama na sheria iweze kuchukua mkondo wake. Hapa kuna haja ya kujikita katika mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato kwa kutoa elimu makini; kwa kuendesha kampeni za uragibishaji sanjari na kuwalinda watu ambao wanaweza kutumbukizwa katika mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo. #PrayAgainstTrafficking."

Biashara ya binadamu
08 February 2023, 16:55