Tafuta

Kardinali Joseph Zen, Askofu Mkuu Mstaafu wa Hong Kong. Kardinali Joseph Zen, Askofu Mkuu Mstaafu wa Hong Kong. 

Vatican ina wasi wasi wa kukamatwa Kardinali Zen huko Hong Kong

Kadinali huyo mwenye umri wa miaka 90 ambaye alikamatwa Jumatano na kitengo cha polisi waliowekwa kuangalia usalama wa taifa ameachiliwa karibu saa kumi na moja jioni siku hiyo hiyo kwa saa za huko,akituhumiwa “kula njama na vikosi vya kigeni”kuhusiana na jukumu la msimamizi wa 612 wa Mfuko wa Misaada ya Kibinadamu.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kardinali Joseph Zen, mwenye umri wa miaka 90, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki la Jimbo Hong Kongo kuanzia mwaka 2002 hadi 2009, alikuwa  amekamatwa na Polisi, Jumatano 11 Mei 2022. Kardinali huyo ameachiliwa kwa dhamana tarehe hiyo hiyo  11 Mei 2022, majira ya saa 11 jioni kwa saa za Italia, kama ilivyotangazwa na waandishi wa habari wa Hong Kong ambao pia walichapisha picha za Kardinali  Zen akiwa nje ya kituo cha polisi cha Wan Chai kwenye mitandao ya kijamii. Alipotoka, Kadinali aliingia mara moja kwenye gari la kibinafsi lililokuwa limeegeshwa karibu, bila kutoa maoni yoyote. Alisindikizwa na watu watano. Kutokana na hilo Vatican imeelezea  wasiwasi  wake baada ya kupata habari za kukamatwa kwa Kardinali Zen na inafuatilia  hali halisi kwa umakini mkubwa. Alisema hayo alasiri Msemaji mkuu wa Vyombo vya Habari vya Vatican, Dk. Matteo Bruni, akijibu maswali ya waandishi wa habari.

Kukamatwa na kufunguliwa mashtaka

Kardinali Zen alikuwa amesimamishwa Jumatano na kitengo cha polisi kilichoundwa ili kuangalia usalama wa taifa la China na baadaye alihojiwa katika kituo cha polisi cha Wan Chai. Shutuma dhidi ya kadinali huyo wanabainisha kwamba ni ya kula njama na majeshi ya kigeni" kuhusiana na jukumu lake kama msimamizi wa Hazina ya Misaada ya Kibinadamu ya 612, mfuko ambao uliunga mkono waandamanaji wanaounga mkono demokrasia katika kulipa gharama za kisheria au afya walizopaswa kukabiliana nazo.

Wafungwa wengine watatu

Kadinali ni mtawa wa Kisalesian alikuwa mmoja wa wadhamini wa shirika hilo, lililoanzishwa mnamo 2019 na kufutwa mwezi Oktoba mwaka jana. Mbali na Kardinali Zen, mamlaka pia iliwakamata waendelezaji wengine wa Hazina, akiwemo mwanasheria maarufu Margaret Ng, mbunge wa zamani wa upinzani, mwanataaluma Hui Po-keung na mwimbaji na mtunzi wa nyimbo Denise Ho. Kukamatwa kwao kulithibitishwa na vyanzo vya kisheria vya Hong Kong. Kulingana na wanahabari wa Hong Kong, wao pia waliachiliwa kwa dhamana.

Uchunguzi

Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba uchunguzi wa polisi, ambao ulianza mwezi Septemba iliyopita, ulizingatia madai ya Kula njama ya Mfuko wa 612 na vikosi vya kigeni, kinyume na sheria ya usalama wa kitaifa iliyowekwa na Beijing mnamo Juni 2020. Ni moja ya makosa manne yaliyotazamiwa na Sheria ya Usalama wa Kitaifa na iliyolaaniwa kimataifa, kuzima maandamano ya demokrasia katika koloni hilo la kizamani. Makosa mengine ni uasi, kujitenga na ugaidi na inaweza kusababisha hukumu ya kifungo cha je ya maisha. Katika miezi ya hivi karibuni, baadhi ya magazeti ya Hong Kong yalimshutumu askofu huyo aliyeibuka kwa kuwachochea wanafunzi kuasi dhidi ya mfululizo wa hatua za serikali mwaka 2019. Katika siku za nyuma, Zen pia alikuwa mstari wa mbele kwa kukosoa Chama cha Kikomunisti cha China kwa kukemea shinikizo na mateso kwa jumuiya za kidini.

.

11 May 2022, 19:29