Tafuta

Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu. 

Vijiji Nchini Tanzania Kupatiwa Huduma ya Maji Safi na Salama!

Maji ni hitaji muhimu sana la binadamu linalopaswa kulindwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi kwa wananchi. Matumizi ya maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu yatasaidia kukuza na kudumisha haki jamii, maadili, mshikamano na katika kudumisha ikolojia endelevu.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Bukoba, Tanzania.

Maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu kwani ni muhimu sana katika maisha ya viumbe hai, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu katika Nyanja mbali mbali za maisha. Maji ni kito cha thamani ambacho Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii ya binadamu. Maji ni hitaji muhimu sana la binadamu linalopaswa kulindwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa. Kumbe, huduma bora za maji safi na salama ni kichocheo kikuu cha maisha na afya bora zaidi kwa wananchi. Matumizi ya maji safi na salama kama sehemu ya haki msingi za binadamu yatasaidia kukuza na kudumisha haki jamii na amani, kanuni maadili na mshikamano kati ya watu. Maji ni muhimu sana katika kudumisha ikolojia endelevu. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameweka mikakati madhubuti unayolenga kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyote nchini vikiwemo vya wilaya ya Bukoba mkoni Kagera.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza kampeni ya Rais Mheshimiwa Samia ya kumtua mama ndoo kichwani ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana karibu na kuwawezesha wanawake na vijana katika maeneo mbalimbali nchini hususani ya vijijini kupata muda wa kushiriki katika shughuli za kijamii. Mheshimiwa Majaliwa ametoa kauli hiyo Jumanne, Septemba 21, 2021 wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Kemondo baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji wa Kemondo-Maruku akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo. Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati madhubuti yenye lengo la kumaliza tatizo la maji nchini, hivyo wananchi waendelee kuwa na subra kwani mradi huo utakamilika kwa wakati na kwa viwango ili wapate huduma hiyo kama ilivyokusudiwa.

Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) wilaya ya Bukoba, Mhandisi Evaristo Mgaya alisema mradi huo unalenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika kata tano za wilaya ya Bukoba na moja ya wilaya ya Muleba. Mhandisi Mgaya alisema mradi huo unaotekelezwa kwa awamu na ya kwanza itahusisha kata mbili za Kemondo na Maruku kwa gharama ya shilingi bilioni 6.8, ambapo alitaja baadhi ya kazi zinazoendelea kuwa ni pamoja na ujenzi wa tanki la lita milioni tatu, uchimbaji wa mitalo ya kulazia mabomba ya kusambazia maji. “Mradi huu umelenga kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika vijiji vya kata za Kemondo, Maruku, Nyangereko, Bujugo na Katerero wilayani Bukoba na kata ya Muhutwe wilayani Muleba. Mradi huu unatekelezwa kwa awamu na umekadiriwa kunufaisha wananchi 117,461 kwa gharama ya shilingi bilioni 15.9.” Baada ya kukagua ujenzi wa mradi wa maji, Waziri Mkuu alikagua mradi mwingine wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Bukoba inayojengwa katika kata ya Bujunangoma, ambapo aliwaagiza viongozi wa mkoa wa Kagera na Wilaya ya Bukoba wahakikishe wanasimamia kwa karibu miradi hiyo.

“Mkuu wa Mkoa (Meja Jenerali Charles Mbuge) na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba (Moses Machali) simamieni na fuatilieni miradi yote, majengo yajengwe kwa kuzingatia viwango. Mkuu wa mkoa hakikisha unachukua hatua kali kwa maafisa manunuzi watakaobainika kununua vifaa vilivyo chini ya kiwango.” Kwa mujibu wa taarifa ya mkuu wa wilaya ya Bukoba, ujenzi wa hospitali hiyo unafanyika kwa awamu ambapo awamu ya kwanza ilihusisha majengo saba ambayo ni la: wagonjwa wa nje, maabara, mama na mtoto, mionzi, utawala, kufulia pamoja na la kuhifadhia dawa. Ujenzi huo umegharimu shilingi bilioni 1.8. Alisema awamu ya pili ya ujenzi huo ambayo inaendelea inahusisha ujenzi wa majengo ya wodi tatu ambayo ni jengo la wodi ya watoto, jengo la wodi ya wanaume na jengo la wodi ya wanawake. Ujenzi huo upo katika hatua ya upauaji. Ujenzi huo utakapokamilika utagharimu shilingi milioni 500.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekataa kuzindua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera kwa sababu gharama zilizotumika ni kubwa kuliko aina na idadi ya majengo yaliyopo. “Nikiweka jiwe la msingi nitakuwa nimehalalisha majengo mengine yajengwe kwa gharama hii. Siwezi kuweka jiwe la msingi, gharama zilizotumika ni kubwa kuliko majengo yaliyopo. Simamieni ujenzi wa majengo yenu na mjenge kwa kutumia mfumo wa force account.” Mheshimiwa Majaliwa amekataa kufungua ofisi hiyo Jumatatu, Septemba 20, 2021 wakati akiwa katika katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo. “Nini kilisababisha hadi kibanda kigodo cha mlinzi kikajengwa kwa shilingi milioni saba? Kina matofali mangapi kama sio ulaji nini? hii si sahihi sijaweka jiwe la msingi wala kufungua na kile kibao kilichoandikwa jina langu kiondolewe.

Serikali ipo makini katika usimamizi wa miradi na haya ni maelekezo ya Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.” Mradi wa ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 483.42, ambapo kibanda cha mlinzi kimegharimu shilingi milioni 7.03, uzio shilingi milioni 94.2, jengo la ofisi shilingi milioni 253.8 na stoo shilingi milioni 51.55. Waziri Mkuu amesema Serikali inajenga majengo makubwa ya vituo vya afya ambayo ni jengo la mapokezi ya wagonjwa, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto, nyumba ya daktari, chumba cha kuhifadhia maiti, kichomea taka na korido kwa gharama ya shilingi milioni 500. Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa TANESCO uhakikishe katika miradi yake mingine ya ujenzi gharama zilingane na aina na idadi ya majengo.

Naye, Meneja Mwandamizi Usambazi wa TANESCO Makao Makuu, Mhandisi Nathanasias Nangali ambaye alisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, amesema mradi huo ulianza Septemba 11, 2018 na kukamilika Februari 08, 2020 kwa gharama za shilingi 483,422,328.02. Amesema mkandarasi aliyejenga mradi huo ni kampuni ya M/S RK Ivestment chini ya usimamizi wa mkandarasi mshauri TANESCO kitengo cha miliki. “TANESCO imeendelea kutumia wataalamu wake katika kusimamia na kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa ofisi zake za mikoa, wilaya na vituo vya kupoza na kusambaza umeme.” Amesema TANESCO imeendelea kutenga fedha kwa awamu kila mwaka ili kutekeleza miradi kama hiyo ambapo katika mwaka huu inaendelea na ujenzi wa ofisi za wilaya za Buhigwe-Kigoma, Ruangwa-Lindi, Urambo-Tabora, Gairo na Malinyi-Morogoro, Nanyumbu na Tandahimba-Mtwara, Kilolo-Iringa, Rorya na Serengeti-Mara, Laela-Rukwa na Meatu-Simiyu. Akizungumzia huduma ya umeme inayotolewa katika wilaya hiyo amesema kati ya vijiji 99 vya wilaya hiyo vijiji 70 vina umeme na vijiji 29 vilivyosalia vitapata huduma hiyo kupitia mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unaoendelea kutekelezwa.

Awali, Mheshimiwa Majaliwa alitembelea na kukagua kiwanda cha kuchenjua madini ya bati (TIN) cha Kampuni ya African Top Minerals kilichopo wilayani Kyerwa ambapo alitumia fursa hiyo kumuhakikishia mwekezaji huyo kwamba Serikali itaendelea kumuunga mkono. Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hassan Ibar alisema mradi huo uliogharimu shilingi bilioni nne unalengo la kuboresha na kukuza sekta ya madini wilayani Kyerwa na Tanzania kwa kuongeza thamani ya madini hayo katika soko la dunia, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi. Aliishukuru Serikali kwa jitihada zake za kutambua mchango wa madini ya bati kwa kuzindua cheti cha uhalisia cha madini hayo ambacho kimewasaidia kutambulika kimataifa na kufanya biashara yao kwa uhakika. “Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia kwa jitihada zake za kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wawekezaji, tutaendelea kumuunga mkono.”

 

22 September 2021, 10:24