Tafuta

Ulimwengu Ulimwengu 

Ulimwengu na matukio yake tofauti:siasa,afya,uchumi na mazingira

Nchi za Afrika Magharibi za tangaza vikwazo kwa wanapinduzinchini Guinea.Sheria ya Chanjo kuwa ya lazima nchini Italia tangu 15 Oktoba.Dozi milioni 500 zinakosekana barani Afrika kufikia lengo la ulimwengu la asilimia 40%. Mkutano maalum G20 kuhusu Afghanistan utaandaliwa baada ya mkutano mkuu wa Baraza Kuu la UN kuhitimishwa Septemba 30.

Na Sr. Angela Rwezaula –Vatican.

Wakuu wa mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS) wametangaza vikwazo dhidi ya viongozi wa mapinduzi nchini Guinea, na kutaka uchaguzi uitishwe katika miezi sita ili kurejesha haraka utawala wa kiraia baada ya mapinduzi ya mwezi huu. Wakuu hao wa mataifa wameamua kuzuwia mali za kifedha na kuwawekea marufuku ya kusafiri wanachama wa utawala wa kijeshi na ndugu zao, huku wakisisitiza juu ya kuachiliwa kwa rais Alpha Conde. Rais wa jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS, Bwana Jean Claude Brou amesema viongozi wakuu wa mataifa ya Afrika Magharibi wamesisitiza pia kwamba hakupaswi kuwepo na haja ya kipindi kirefu cha mpito kwa taifa hilo kurejea kwenye mkondo wa kidemokrasia. “ipindi cha mpito lazima kiwe kifupi”, na wamesisitiza hata kwamba hakipaswi kudumu zaidi ya miezi sita, hivyo katika miezi sita, uchaguzi unapaswa kufanyika.

UVIKO-19: Sheria kupitishwa ya chanjo. Utaratibu wa Covax umeangaliwa kwa upya juu ya utabiri wake wa chanjo kwa nchi maskini kwenda chini. Dozi milioni 500 zinakosekana barani Afrika kufikia lengo la ulimwengu la asilimia 40% ya chanjo kufikia mwishoni mwa mwaka. Wakati huo huo nchini Italia kuanzia tarehe 15 Oktoba 2021, itatakiwa Kadi ya kijani ( Grren Pass) kwa wafanya kazi wote Milioni 23. Nchini Ufaransa, wafanyakazi wa afya 3,000 wamesimamishwa mara  baada ya kuanza kutumika sheria ya chanjo kwa watu hao.

Afghanistan: Shirika la Fedha Duniani lina wasiwasi juu ya uwezekano wa kuzuka kwa  mgogoro wa kibinadamu unaowezekana nchini Afghanistan

Urusi: Urusi imeanza zoezi la siku tatu la upigaji kura katika uchaguzi wa wawakilishi 450 wa bunge la Duma ambao hauoneshi uwezekano wowote wa kubadili sura ya kisiasa. Upigaji kura ulianza mapema Ijumaa tarehe 17 Septemba katika mikoa ya mbali mashariki ya Kamchatka na Chukotka, ambayo ina tofauti ya masaa tisa mbele ya Moscow. Wapigakura wataweza kuendelea kupiga kura zao hadi siku ya Jumapili. Ikulu ya Kremlin inataka kulidhibiti bunge jipya, ambalo litakuwepo bado mwaka 2024, wakati muhula wa sasa wa Putin utakapomalizika, na anapaswa kuamua juu ya kugombea tena au kuchagua mkakati mwingine wa kusalia madarakani

Silaha: mbio za silaha huko Asia zinaongezeka baada ya majaribio ya kombora la Korea mbili na makubaliano kati ya Marekani, Uingereza na Australia ya uuzaji wa manowari zinazotumiwa na nyuklia huko Canberra.

Mkutano maalum wa kundi la mataifa tajiri na yale yaliyo mbioni kiuchumi duniani, G20 kuzungumzia kuhusu Afghanistan utaandaliwa baada ya mkutano mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaokamilika mnamo Septemba 30. Haya yamesemwa na waziri wa mambo ya nje wa Italia Bwana Luigi Di Maio katika mahojiano yaliochapishwa na gazeti la ‘La Repubblica’. Di Maio amethibitisha kuwa baada ya mkutano huo wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kutakuwa na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo ya G20 kuandaa mkutano huo maalum. Di Maio amesema kuwa Italia ambayo mwaka huu inashikilia urais wa kupokezana wa kundi hilo la G20 imeyataka mashirika ya Umoja wa Mataifa na ya msaada yanayohusika kwa kiasi kikubwa nchini Afghanistan kuhusishwa katika mkutano huo.

Ugiriki inaandaa mkutano wa viongozi wa kusini mwa Umoja wa Ulaya utakaozingatia mabadiliko ya tabianchi na changamoto za usalama zinazojumuisha uhamiaji na mzozo nchini Afghanistan. Msemaji wa serikali ya Ugiriki Yiannis Economou, amesema kuwa mkutano huo wa siku moja utakaohudhuriwa na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen utazungumzia masuala yanayotatiza usalama na uthabiti katika eneo la Mediterenia. Economou ameongeza kuwa agenda ya mkutano huo inajumuisha uhamiaji na hali nchini Afghanistan kufuatia hatua ya Taliban kuchukuwa mamlaka nchini humo lakini Ugiriki inatilia mkazo haja ya kuchukuliwa kwa hatua za pamoja kushughulikia mabadiliko ya tabianchi. Ofisi ya waziri mkuu wa Ugiriki Kyriakos Mitsotakis imesema kuwa Von der Leyen ataungana na viongozi hao katika mkutano tofauti kuhusu mabadiliko ya tabianchi na athari zake katika eneo la Mediterenia. Mitsotakis amesema kuwa ulinzi wa bioanuwai na ushirikiano bora katika kukabiliana na majanga ya moto wa misitu ndiyo masuala yatakayopewa kipaumbele katika mkutano huo unaojulikana kama Med7.

17 September 2021, 16:48