Tafuta

Chanjo kwa wote sio hisani,ni kwa ajili ya faida ya kila nchi limesema shirika la Afya Duniani na kwamba nchi 103 bado hazijafikia lengo la kuchanja watu wake kwa asilimia 40%. Chanjo kwa wote sio hisani,ni kwa ajili ya faida ya kila nchi limesema shirika la Afya Duniani na kwamba nchi 103 bado hazijafikia lengo la kuchanja watu wake kwa asilimia 40%. 

Sisi si wafungwa wa hatima au asili.Dharura ya Omicron ni tosha kujua janga bado lipo

Katika Wiki iliyopita Shirika la Afya Ulimwenguni(WHO) ilitangaza uwepo wa aina mpya ya kirusi cha OMICRON ambacho shirika hilo limesema ni chakutiliwa mashaka wakati kikionekana kuwa na nguvu zaidi ya kushambulia kuliko kirusi aina ya Delta.Ulaya wanaendelea kujihami.Mkurugenzi wa Shirika hilo amesema Dharura ya Omicron ni kumbusho tosha kwamba ingawa wengi wanadhani tumemalizana na UVIKO-19,ukweli haijamalizana nasi.

Kutoka Tovuti ya Shirika la Umoja wa Mataifa.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya duniani WHO Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus,  Jumatatu tarehe 29 Novemba 2021, wakati wa kikao maalum cha dharura cha Baraza la Afya Duniani (WHO) huko Geneva, Uswisi, kinachowaleta pamoja nchi wanachama wa shirka hilo kujadili ajenda moja pekee, ya makubaliano ya mkataba wa Shirika la Afya Duniani juu ya kujiandaa na kukabiliana na janga la UVIKO-19 kwa kuzingatia ripoti ya kikosi kazi cha kuimarisha utayarishaji na mwitikio wa Shirika la Afya (WHO) kwa dharura za Kiafya amesema “Virusi vipya vya UVIKO-19, Omicron vimedhihirisha kwa nini ulimwengu unahitaji makubaliano mapya kuhusu magonjwa ya milipuko kwani mfumo wetu wa sasa unapuuza suala la nchi kutadhaharisha wengine kuhusu vitisho ambavyo vinaweza kuwakumba”. Wiki iliyopita WHO ilitangaza uwepo wa aina mpya ya kirusi cha OMICRON ambacho shirika hilo limesema ni chakutiliwa shaka huku kikionekana kuwa na nguvu zaidi ya kushambulia kuliko kirusi aina ya Delta. Kuhusu mlipuko wa magonjwa huo   Dkt. Tedross amesema kila mtu anajua kwamba magonjwa ya kuambukiza yana njia ya kutokea mara kwa mara duniani. Kumekuwa na tauni nyingi kama vile vita katika historia, lakini mara zote tauni na vita huwashangaza watu kwa njia sawa.  Milipuko, magonjwa ya kuambukiza na majanga ya milipuko ni ukweli wa asili, na hulka ya kuzuka mara kwa mara imerekodiwa katika historia kuanzia kwa tauni ya Athene mwaka 430 KK, hadi kifo cheusi, janga la mafua la 1918, na sasa UVIKO-19.

Lakini amesisitiza kuwa hiyo haimaanishi kuwa hatuna uwezo wa kuyazuia, kujitayarisha au kupunguza athari zake. Sisi si wafungwa wa hatima au asili. Zaidi ya wanadamu wowote katika historia, tuna uwezo wa kutazamia magonjwa ya milipuko, kujitayarisha, kubaini vimelea, kuvigundua katika hatua za mapema zaidi, kuvizuia kuenea na kuwa majanga ya kimataifa, na kukabiliana nayo yanapotokea.  Lakini cha kushangaza amesema sasa tunaingia mwaka wa tatu wa mgogoro mkubwa zaidi wa kiafya katika karne hii na dunia bado inadorora.  Virusi hivi ambayo inawezekana kuvizuia, kugundua na kuvitibu vinaendelea kuleta giza kubwa duniani. Badala ya kukutana baada ya janga hili, wanakutana wakati wimbi jipya la kesi na vifo vinavyoingia Ulka ya ikiongezeka na kukiwa na vifo visivyoelezeka na visivyohesabiwa duniani kote.  Mlipuko wa Omicron unaonesha ni jinsi gani hali ambavyo bado si shwari na kwamba ingawa kuna baadhi ya maeneo idadi ya wagonjwa na vifo inashuka kama kuna kitu kimoja cha kujifunza ni kwamba hakuna ukanda, hakuna nchi, hakuna jamii na hakuna mtu atakayekuwa salama hadi pale kila mtu atakapokuwa salama.

Ingawa uchunguzi na tathimini zaidi inaendelea kuhusu virusi vipya vya Omicron WHO imeonya kwamba kutokana na mabadiliko ambayo yanaweza kutoa uwezo wa kuepuka kinga na uwezekano wa uambukizaji, uwezekano wa kuenea zaidi kwa Omicron katika ngazi ya kimataifa ni mkubwa.  Kulingana na sifa hizi, WHO imesema “kunaweza kuwa na ongezeko la siku zijazo la UVIKO-19, ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa, kulingana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na mahali ambapo mlipuko utazuka. Hatari ya jumla ya kimataifa inayohusiana na VOC Omicron mpya inatathminiwa kuwa ya juu sana.”  Kwa upande mwingine WHO imesema Afrika Kusini na Botswana zinafaa kushukuriwa kwa kugundua, kupanga na kuripoti haraka aina hii mpya ya virusi na sio kuadhibiwa. Kwa maana hiyo amesisitiza kuwa “hatupaswi kuhitaji kengele nyingine ya kutuamsha, sote tunapaswa kuwa macho kwa tishio la virusi hivi. Dharura ya Omicron ni kumbusho tosha kwamba ingawa wengi wanadhani tumemalizana na UVIKO-19, ukweli ni kwamba haijamalizana nasi. Tunaishi katika mzunguko wa hofu na taharuki na tusipoangalia mafanikio tuliyopata yanaweza kutoweka haraka hivyo kibarua chetu kikubwa kwa sasa ni kutokomeza janga hili” Limesema shirika hilo la afya duniani.

Shirika la Afya ulimwenguni (WHO) limesisitiza kwamba hakuna nchi itakayoweza kumaliza janga la UVIKO-19 peke yake kwa maana hiyo ushirikiano na mashikamano wa kimataifa unahitajika na hasa usawa wa chanjo.   Limetoa mfano kwamba hadi sasa zaidi ya asilimia 80% ya chanjo zilizozalishwa duniani zimekwenda kwa mataifa Tajiri ya G20, nchi za kipato cha chini nyingi zikiwa za Afrika zimepokea asilimia 0.6% pekee ya chanjo zote.  “Chanjo kwa wote sio hisani, ni kwa ajili ya faida ya kila nchi “limesema shirika hilo likiongeza kwamba nchi 103 bado hazijafikia lengo la kuchanja watu wake kwa asilimia 40% sababu kubwa hazina fursa ya kupata chanjo hizo na nyingi ziko barani Afrika.  Hadi sasa COVID-19 imekatili maisha ya watu zaidi ya milioni 5, na hivyo ni vifo ambavyo vimeripotiwa tu inakadiriwa idadi inaweza kuwa kubwa zaidi.

Kikao kimeafikia kanuni katika maeneo muhimu manne kukabiliana na hali ya sasa: Kwanza ni utawala bora ili kuhakikisha hatua za pamoja zinafanyika na fursa ya usawa wa chanjo na nyenzo zingine. Pili ni ufadhili unaostahili ili kuimarisha kinga ya kimataifa ambayo ni endelevu, yenye ufanisi na inayoenda sanjari na vipaumbele vya kimataifa. Tatu ni kuwa na mifumo bora na nyezo kuweza kutabiri, kuzuia, kubaini na kukabiliana haraka na milipuko na uwezekano wa kuzuka majanga ya kiafya. Na nne: Dunia inahitaji Shirika la Afya (WHO) iliyoimarishwa, kuwezeshwa na yenye ufadhili endelevu kuwa kitovu cha mchakato wa kimataifa na masuala ya afya.  Kwa mantiki hiyo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limeweka bayana kwamba “Huu ndio wakati wetu wa kudhihirisha uwezo wetu mkubwa kuliko janga hili, kushinda masuala ya kutoamianiana, na kujenga mfumo ambao una faida kwa wote na kuwaachia urithi bora vizazi vijavyo.”

30 November 2021, 16:00