Tafuta

Raia 60 wameuawa wakati shambulizi la bomu la Urusi lilipoiharibu kabisa shule moja katika eneo la mashariki la Luhansk. Raia 60 wameuawa wakati shambulizi la bomu la Urusi lilipoiharibu kabisa shule moja katika eneo la mashariki la Luhansk. 

Ukraine:Shambulizi la bomu la Urussi limeharibu Shule na kuua raia

Rais wa Ukraine Zelenskyy anasema raia 60 wameuwawa wakati shambulizi la bomu la Urusi lilipoiharibu kabisa shule moja katika eneo la mashariki la Luhansk. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,UNICEF,limelaani vikali shambulio nchini Ukraine huku kukiwa na ripoti kwamba raia,wakiwemo watoto,waliathiriwa na shambulio hilo wakiwa wametafuta hifadhi katika chumba cha chini cha shule hiyo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kufuatia na mzozo unaondelea wa vita na mabomu yanayomwagika katika Nchi ya Mshariki mwa Ulaya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema raia 60 wameuawa wakati shambulizi la bomu la Urussi lilipoiharibu kabisa shule moja katika eneo la mashariki la Luhansk. Maafisa wamesema raia takriban 100 walikuwa katika vyumba vya chini vya jengo hilo katika kijiji cha Bilohorivka wakati liliposhambuliwa. Wakati haya yakiarifiwa viongozi wa nchi tajiri zilizostawi kiviwanda (G7) wanasema wataiwekea vikwazo zaidi Urussi kuhusiana na uvamizi wake nchini Ukraine. Taarifa ya kundi hilo imesema wanataka kufuta au kupiga marufuku uagizaji wa mafuta kutoka Urussi. Viongozi wa G7 wamesema wataimarisha vikwazo dhidi ya matajiri na jamaa wa familia wanaomuunga mkono rais wa Urussi Vladimir Putin katika vita vyake.  Kufuatia na shambulizi hili, naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake Stéphane Dujarric amerejea wito wake kwamba: "raia na miundombinu ya kiraia lazima iepushwe wakati wa vita. Vita hii lazima iishe, na amani ianzishwe kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa.  “Umoja wa Mataifa na wadau wake wa nchini Ukraine wataendelea kusaidia wale ambao maisha yao yameharibiwa na vita.”

UNICEF: shule hazipawi kuguswa

Kwa upande wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, limelaani vikali shambulio hilo huku kukiwa na ripoti kwamba raia, wakiwemo watoto, walikuwa wametafuta hifadhi katika chumba cha chini cha shule hiyo. Kupitia ukurasa rasmi wa Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Bi Catherine Russell ambaye ndiye mkuu wa shirika hilo, Dominika tarehe 8 Mei 2022 ameandika kwamba: “bado hatujui ni watoto wangapi wanaweza kuwa wameuawa au kujeruhiwa katika shambulio la bomu lililoripotiwa, lakini tunahofia shambulio hili limeongeza mamia ya watoto ambao tayari wamefariki dunia katika vita hii. Familia ambazo zilinaswa na shambulio hili zilipaswa kusherehekea Siku ya Mama leo huko Ukraine, sio kuomboleza kupoteza wapendwa wao.”   Bi. Russell ameongeza kusema kuwa: “shule hazipaswi kamwe kushambuliwa au kutumiwa kwa madhumuni ya kijeshi. Kuwalenga raia na vitu vya kiraia, ikiwa ni pamoja na shule, ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Shambulio hili la hivi punde ni moja tu ya matukio mengi katika vita hiii ambapo tumeona kupuuzwa kwa wazi maisha ya raia.” 

Juhudi za operesheni kufika watu zaidi ya 600

Bwana Guterres, Diminika tarehe 8 Mei  ametoa tamko la pili akikaribisha kuwasili kwa kundi jipya la zaidi ya raia 170 katika eneo la Zaporizhzhia wakitokea katika viwanda vya chuma vya Azovstal na maeneo mengine ya Mariupol. Operesheni iliyofanikiwa ya kuwahamisha watu iliratibiwa na Umoja wa Mataifa (UN) na Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Msalaba Mwekundu (ICRC). “Fikra zangu ziko pamoja na watu wote nchini Ukraine wanaoteseka katika vita hivi,” Alisema BwanaGuterres katika taarifa hiyo fupi iliyotolewa huko Marekani. Operesheni ya sasa inafanya kufikia watu zaidi ya 600 ambao wamehamishwa kwa usalama kutoka katika kiwanda cha chuma cha Azovstal na maeneo mengine ya Mariupol.  

09 May 2022, 09:57