Tafuta

Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda ameteuliwa na Kutangazwa na UNICEF kuwa Balozi Mwema wa Shirika hilo Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda ameteuliwa na Kutangazwa na UNICEF kuwa Balozi Mwema wa Shirika hilo  (AFP or licensors)

Vanessa Nakate ni Balozi mwema wa UNICEF

Vanessa Nakate,Mwanaharakati wa mazingira kutoka nchini Uganda ameteuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhuduima Watoto(UNICEF)kuwa balozi mwema mpya wa shirika hilo.Alitembelea Turkana kuona madhara ya ukame na hatua za UNICEF katika kusaidia wananchi na kuwaona watoto wa hospitali ya rufaa ya Lodwar nchini Kenya.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF tarehe 15 Septemba 2022  lilimteua na kumtangaza mwanaharakati wa mazingira kutoka nchini Uganda Vanessa Nakate kuwa balozi mwema mpya wa shirika hilo. Uteuzi wa Vanessa, mwenye umri wa miaka 25 unafuatia ziara yake kwenye Pembeme ya Afrika ambako alishuhudia jinsi gani mabadiliko ya tabianchi yalivyochangia athari mbaya kwa maisha ya watoto nchini Kenya kutokana na ukame unaoendelea. Pia uteuzi huo ni kuthibitisha ushirikiano wake na shirika la UNICEF na kutambua utetezi wake bora wa kimataifa wa haki za kimazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Vanessa alisafiri wiki iliyopita na UNICEF hadi Kaunti ya Turkana Kaskazini Magharibi mwa Kenya ili kujionea athari za uhaba wa maji na chakula unaosababishwa na ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika Pembe ya Afrika katika kipindi cha miaka 40.

Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda
Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda

Katika safari yake ya kwanza na UNICEF, alikutana na jamii zilizo katika kitovu cha  athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kinamama na watoto wanaopata matibabu ya kuokoa maisha kutokana na utapiamlo mkali na familia zinazonufaika na mifumo ya usambazaji wa maji inayotumia nishati ya jua kwa msaada wa UNICEF. Nitahakikisha sauti za watoto zinasikika. Baada ya kuteuliwa kwake Bi. Nakate amesema: "Kama balozi mwema wa UNICEF, itakuwa jukumu langu la kwanza kuwasilisha sauti za watoto na watu waliotengwa katika mazungumzo ambayo awali hawakujumuishwa. Jukumu hili na UNICEF litanipa fursa zaidi za kukutana na watoto na vijana katika maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi na jukwaa lililopanuliwa la kutetea kwa niaba yao. Nchini Kenya, watu niliokutana nao waliniambia kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na ukame katika maisha yao, huku misimu minne ya mvua iliyofeli mfululizo ikiwanyima watoto haki zao za msingi.”

Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda
Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda

Bi Nakate ameongeza kusema kuwa  moja ya jamii alizokutana nazo imemweleza kuwa haijashuhudia mvua kwa zaidi ya miaka miwili.  “Hii ni zaidi ya shida ya chakula na lishe, ni mwelekeo mwingine wa changamoto yetu ya mabadiliko ya tabianchi inayozidi kuwa mbaya.” Ombi la UNICEF la kuboresha na kusaidia maisha ya mamilioni ya watu walioathirika na ukame na kuwajengea huduma kwa muda mrefu kwenye Pembe ya Afrika na kuzuia athari za ukame kwa miaka ijayo zinagonga mwamba kwani hadi sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimia 3% pekee. Akiwa Sopel, kaunti ya Turkana nchini Kenya, Vanessa Nakate alitembelea shule ya msingi na kuzungumza na wanafunzi kuhusu changamoto wanazozipata kutokana na janga la ukame kwenye  eneo hilo la Afrika Mashariki.

Historia fupi ya mchakato wa uanaharakati ya Vanessa Nakate

Vanessa alianza harakati zake tangu Januari 2019 kwa maandamano na ndugu zake na binamu zake katika mitaa ya jiji la Kampala, nchini Uganda, maandamano yaliyochochewa na mwanaharakati mwingine nyota wa mabadiliko ya tabianchi na mazingira Greta Thunberg ambaye kwa sasa amejulikana ulimwengu mzima na vijana wengi wanamuunga mkono. Aliendelea kuandamana kila wiki, na kuwa sura inayojulikana katika harakati ya vijana kupiga mabadiliko ya tabianchi duniani kote. Mnamo mwaka 2020 alijulikana zaidi ulimwenguni wakati alipoondolewa kwenye picha ya habari aliyokuwemo pamoja na Thunberg na wanaharakati wengine wa mabadiliko ya tabianchi.

Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda
Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda

Kufuatia tukio hilo Vanessa alisema  kwamba chombo hicho cha habari "hakikufuta picha tu, bali kilifuta bara zima", kauli ambayo iligonga vichwa vya habari vya kimataifa. Vanessa amesema safari yake haikuwa rahisi: “Kama mwanamke mwanaharakati mchanga wa Kiafrika, imenibidi kupigana ili kusikilizwa na vyombo vya habari na watoa maamuzi. Wakati nina bahati ya kuwa na jukwaa sasa, ninakusudia kuendelea kupigania wengine. Watoto walio katika kitovu cha athari za mabadiliko ya tabianchi, kama wale niliokutana nao Turkana, Kenya, ni watu ambao nitapigania katika jukumu langu jipya na UNICEF,” alisema Nakate.

Rise Up Movement

Tangu wakati huo Vanessa ametumia jukwaa lake kutetea haki ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi kujumuisha kila jamii, haswa wale kutoka sehemu zilizoathiriwa zaidi.  Alianzisha Rise Up Movement, jukwaa la kupaza sauti za wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi wa Afrika, pamoja na mradi wa kufunga paneli za sola katika shule za vijijini za Uganda. Amehutubia viongozi wa dunia katika mikutano ya mabadiliko ya tabianchi ya COP25 na COP26 na alionekana na hisotria  yake kuchapishwa kwenye jarida la TIME. Vanessa Nakate, Balozi mwema wa UNICEF akiwa kwenye wadi ya watoto ya hospitali ya rufaa ya Lodwar, kaunti ya Turkana nchini Kenya. Vanessa alitembelea Turkana kuona madhara ya ukame na hatua za UNICEF kusaidia wananchi.

Ni furaha kwa UNICEF kumkaribisha Nakate

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell kwa upande wake amesema: "Nina furaha kumkaribisha Vanessa Nakate kwenye familia ya UNICEF kama Balozi wetu mwema mpya wa Kimataifa. Kazi ya Vanessa kusongesha hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi ambazo zinanufaisha jamii zilizoathirika zaidi na mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi zinalingana moja kwa moja na dhamira ya UNICEF ya kuleta mabadiliko kwa kila mtoto.

Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda akiwa na Greta
Vanessa Nakate Mwanaharakati wa Mazingira kutoka Uganda akiwa na Greta

Tunatumaini kuteuliwa kwake kama Balozi mwema wa UNICEF kutasaidia kuhakikisha kuwa sauti za watoto na vijana hazikatizwi kamwe katika mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kila mara zinajumuishwa katika maamuzi yanayoathiri maisha yao." Hata hivyo Vanessa Nakate anajiunga na mabalozi wengine mashuhuri walioteuliwa hivi karibuni kama vile mwigizaji Priyanka Chopra Jonas, wasanii wa muziki Katy Perry na Angelique Kidjo, mkimbizi wa Siria na mwanaharakati wa elimu Muzoon Almellehan na, hivi majuzi, Balozi mwema wa UNICEF mwigizaji Millie Bobby Brown.

16 September 2022, 14:02