Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika 5 ya Kipindi cha Mwaka A: Chumvi ya Dunia na Nuru ya Mataifa: Ushuhuda

Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Kristo Yesu ndiye “Mwanga wa Mataifa." Ni matumaini ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuona kwamba mng’ao wa nuru ya Kristo ung’aao juu ya uso wa Kanisa kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Injili inayowaangaza walimwengu wote, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti, Ishara na Chombo cha Umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa wa Radio Vatican katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya tano ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa, ilitoa fursa kwa waamini kutafakari Heri za Mlimani: Ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani, dira, mwongozo na muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu katika Agano Jipya. Kristo Yesu aliwafafanulia watu mapenzi ya Mungu kwa kuwaonesha njia inayowapeleka katika furaha ya kweli, ujumbe ambao tayari ulikuwa umekwisha fumbatwa hata katika vitabu vya Manabii katika Agano la Kale. Kimsingi, Mwenyezi Mungu yuko karibu na maskini na wale wote wanaoteswa, kudhulumiwa na kunyanyaswa, ili kuweza kuwapatia heri na furaha mintarafu utekelezaji wa masharti yake. Leo Kristo Yesu katika Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya V ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa Mt 5: 13-16 anawaambia wafuasi wake: Ninyi ni chumvi ya dunia… Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanakiri kwa kusema, Kristo Yesu ndiye “Mwanga wa Mataifa, Lumen Gentium.” Ni matumaini ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuona kwamba mng’ao wa nuru ya Kristo ung’aao juu ya uso wa Kanisa kwa njia ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inawaangaza walimwengu wote, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja, Ishara na Chombo cha kuwaunganisha wanadamu wote. Rej. Lumen gentium, 1.

Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa
Kristo Yesu ni mwanga wa Mataifa

Waamini wakumbuke kwamba, maji ya baraka katika mazingira, mila, desturi na tamaduni za watu zinazokubali huchanganywa na chumvi ambayo kadiri ya Mapokeo ya kale ya Mama Kanisa Mwenyezi Mungu alimwagiza Nabii Elisha, itiwe katika maji ili kuponya na kutakasa utasa wa maji. Maji ya baraka yanapotumika kadiri ya imani ya Kanisa kuwanyunyuzia watu yanafukuzia mbali kila uovu wa adui na kuwatunza waamini kwa uwepo wa Roho Mtakatifu. Chumvi ni kielelezo cha utukufu, utakatifu, huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Kumbe, waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo cha imani tendaji. Tunaalikwa kuwa ni chumvi ya ulimwengu kwa kutambua kwamba kwa kuzaliwa katika Maji na Roho Mtakatifu, Wabatizwa wote wamewekwa wakfu kuwa ni Makuhani, Manabii na Wafalme ili kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya sifa na shukrani; kutangaza fadhila za Mungu, ili kuwaita watu watoke gizani na kuingia katika nuru yake ya ajabu, kwa kujitoa wenyewe ili waweze kuwa ni sadaka safi na yenye kumpendeza Mwenyezi na kumshuhudia Kristo Yesu popote pale walipo kama majibu ya habari za tumaini na uzima wa milele lililoko ndani mwao. Rej. Lumen gentium 9-11. Tuwe mwanga, nuru ya Mataifa na chumvi ya dunia kwa kujichotea nuru na ladha kutoka kwa Kristo Yesu kwanza kabisa ndani ya familia zetu kwa kukomesha vitendo vya ukatili wa majumbani, yaani vipigo vya wanawake na kuondokana na dhuluma na nyanyaso mbalimbali, ili kuendelea kuishi vyema kama watoto wa mwanga wa Kristo Mfufuka. Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa nuru ya Mataifa kwa wale wote wanaotembelea kwenye giza na uvuli w mauti.

Watu wa Mungu wanaitwa na kutumwa kuwa chumvi na nuru ya mataifa.
Watu wa Mungu wanaitwa na kutumwa kuwa chumvi na nuru ya mataifa.

Wakristo wawe ni mwanga na chumvi inayochota nuru na ladha yake kutoka kwa Kristo Yesu, Njia, Ukweli na Uzima, chimbuko la imani ya Kikristo. Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matendo mema kama yanavyosimuliwa na Nabii Isaya katika Somo la Kwanza Isa 58: 7-10 akiwataka kuwagawia wenye njaa chakula chao, kuwaleta maskini waliotupwa nje, kuwavika walio uchi. Na kwa njia hii, nuru ya waamini itapambazuka kama nyota ya asubuhi na afya yao kuboreka, na haki kuwatangulia na utukufu wa Bwana utawafuata nyuma ili uwalinde. Huu ni mwaliko wa kuwa ni Wasamaria wema tayari kuganga kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini wale wote waliovunjika na kupondeka moyo. Kwa kusimamia haki msingi za binadamu kadiri ya Mafundisho Jamii ya Mama Kanisa na Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki Msingi za Binadamu pamoja na kuendelea kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Wimbo wa Katikati umekazia pamoja na mambo mengine haki na maisha adili, kwani hawa hawataogopa habari mbaya, kwani wanamtumainia Mwenyezi Mungu, kamwe hawataogopa, hadi pale watakapowaona watesi wao wakiwa wameshindwa, haki yake yadumu milele na pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.

Ushuhuda D5

 

04 February 2023, 18:18