Dominika ya XXVII Mwaka C:“Imani na Saburi Katika Safari ya Maisha ya Ushuhuda”
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya XXVII ya mwaka C, katika kipindi hiki cha Jubilei ya Matumaini 2025, Kanisa limetualika kuwa mahusika wa matumaini kati ya wale walio na wasiwasi au wakihangaika. Masomo ya leo yanatufundisha umuhimu wa saburi, ushawishi wa ahadi ya Mungu, na jukumu letu la huduma kwa imani inayoonyesha nguvu ya Roho Mtakatifu. Kuwa na ‘haya’ ni sawa na kuwa na aibu au soni, kusita katika kusema au kutenda, kushindwa kumtazama mtu machoni… ‘ushuhuda’ ni sawa na ushahidi au uthibitisho, maneno yenye kueleza jambo kama lilivyo au lilivyotokea. Ndio kusema ‘kuuonea haya ushuhuda wa Bwana wetu’ ni kuwa na aibu, kuona soni, kusitasita na hivi kushindwa “kumkiri Yesu kwa vinywa vyetu ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwetu ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu” (Rum 10:9).
Paulo anamtia moyo Timotheo Atie nguvu “zawadi ya Mungu... kwa moto”, Mungu huipa roho ya nguvu, upendo, na nidhamu, si hofu, inaonekana Jumuiya za Kanisa la mwanzo zilipata uchovu na kuwa na uvuguvugu katika maisha yao ya dini hivi Mtakatifu Paulo, kwa njia ya Askofu Timotheo, anatamani kuamsha tena ule moto wa zawadi ya Mungu ya Roho Mtakatifu ambaye sio roho ya woga bali ya nguvu, na ya upendo na ya kiasi akiwaasa kutovunjika moyo na kusimama imara katika imani. Hali hiyo tunaweza kuwa nayo sisi pia leo na hasa tunaponyeshewa mvua ya mambo mengi kila dakika kutoka kila kona kiasi cha kupungukiwa au hata kupoteza kabisa paji la imani… tunafanana na wayahudi katika somo I enzi za Nabii Habakuki (1:2-3, 2:2-4) tukimuona Mungu hajali tena, hasikilizi sala zetu na amegukia mbali na maombi yetu… katika mazingira kama hayo tuwe na moyo mkuu na utulivu, tujifunze maana ya mateso na umuhimu wa kuushiriki Msalaba wa Kristo katika maisha kwa “kutouonea haya ushuhuda wa Bwana wetu”… hata hivyo, bila bahati, ulimwengu na waliwengu vinatuelemea na ubinadamu wetu unatuangusha hivi tunapasika kusali pamoja na Mitume wa Kristo katika somo la Injili tukisema “Bwana, tuongezee imani” (Lk 17:5-10).
Imani ndilo hitaji la kwanza kabisa ili mtu awe Mkristo… baada ya kuipokea imani, tunatumwa leo na Mt. Paulo kuitolea ushuhuda kamili bila kuona ‘haya’ kwa kuilinda, kuitunza na kuikuza hivi tunawajibika kufanya bidii ya makusudi kujua, kuishi na kuwashirikisha wengine imani yetu… Imani huleta faida nne! Mosi, imani huunganisha roho na Mungu (Hos 2:20) na hili ni swali muhimu wakati wa ubatizo “Unamsadiki Mungu?” kwa vile “Aaminiye na kubatizwa ataokoka” (Mk 16:16), bila imani ubatizo hauna maana… Pili, imani inaanzisha uzima wa milele ndani yetu, nao huo uzima wa milele ‘ni kumjua Mungu wa pekee na wa kweli na Yesu Kristo aliyemtuma’ (Yn 17:3), hakuna atakayeweza kupata furaha ya mbinguni ambayo ni kumjua Mungu wa kweli bila kwanza kumjua kwa imani, ‘wa heri wale wasioona, wakasadiki’ (yn 20:29)…
Tatu, Imani ni kiongozi wetu katika maisha haya ya hapa duniani, tunajifunza kwa imani kwamba Mungu mmoja tu ndiye anayewatuza watenda mema na kuwaadhibu waovu, ‘mwenye haki ataishi kwa imani’ (Hab 2:4)… Nne, Imani inasaidia kushinda vishawishi (Ebr 11:33)… ‘Tuongezee imani Bwana’… ndilo tamanio letu, lakini kitu kinaongezwa ikiwa kimo kwa kiasi. Je, tunayo imani kidogo, Kristo amesema kiasi cha chembe ya haradali ili Yeye atuongezee? tazama, ‘yule Mwovu’ anatupeperushia mbali imani yetu, ulimwengu unatukimbizia imani yetu na pia sisi wenyewe, kwa tamaa ya miili yetu, tunaikausha imani yetu… Mifumo ya maisha na muundo wa jamii, makwazo kutoka kwa watu tunaowaamini, kuwaheshimu na kuwapenda.. ugumu wa maisha, mahusiano magumu, kupoa kwa roho ya sala na ibada,
Imani kama mbegu ndogo, lakini yenye nguvu, tuhudumu kwa unyenyekevu: “sisi ni watumwa wasiostahili,” tunafanya tu wajibu wetu bila kutarajia sifa. kuzoea mambo matakatifu na kuyachukulia “ya kawaida”, udadisi unaopitiliza na kuhojihoji mafumbo matakatifu kupita kiwango cha kawaida cha kutamani kuelewa, kutukuza malimwengu, kwamba maoni binafsi ndio msingi na kipimo cha maadili, kutofikia malengo ya maisha, kukosa ushirikiano na misaada tunayohitaji, kutojali na kutotazama, mtazamo mpya wa ulimwengu na wa wasomi kuhusu uwepo wa Mungu na maagizo yake, kwamba mwanadamu ni kila kitu na dini ni dawa ya kulevya wajinga, ubishi na ukaidi hasa kukiwamo masilahi ndani ya mada husika, umasikini, kukosa elimu, kukosa afya bora, ushirikina, Injili ya mafanikio, kuchanganya imani nyingi pamoja… na mengine yafananayo yanagandisha imani ndani mwetu, kama kuna kilichobaki huenda ni moshi tu ufukao, moto umezimika kitambo …
Kusadiki ni kuamini kuwa wema utashinda dhidi ya maovu hayo yote na jioni ya siku mwanadamu atakombolewa. Mifumo yote ya dhambi na mapato yake (magonjwa, mateso, machungu, hofu, kuchanganyikiwa, unyanyasaji na mambo yasiyo haki) yatashindwa… na nguvu pekee inayowezesha hili ni NGUVU YA IMANI inayoamini hilo kwa vile Imani ni nguvu ya wema, nguvu ya ukweli, NGUVU YA MUNGU. Kuishi imani inayostahimili magumu, kwa saburi na matumaini. Kufanyia kazi wito wa kuwa wajumbe wa huruma na matumaini, si tu kwa maneno bali kwa matendo Kuibariki jamii kwa huduma isiyotarajia sifa, iliyojaa unyenyekevu na kusubiri neema ya Mungu.
Tufanye nini basi… tusiseme tu ‘Nasadiki kwa Mungu mmoja…’ na kuishia hapo bali tupige hatua mbili tatu mbele… “zaidi ya yote mkiitwa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuzima mishale yote yenye moto wa yule mwovu” (Efe 6:16) kila mmoja wetu, bila kujali hali na mazingira yake ‘asiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu’… tusiketi sakafuni tukiusubiri ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo, bali moto wa imani yetu uangaze ulimwengu hivi kwamba kila anayetuona aseme “huyu ni mkristo na hii ndiyo imani yake!”
Tunahitaji malezi ya kina, mafundisho sahihi na endelevu, utayari wa kusikia na kufuata mafundisho yanayojenga, maisha ya imani, matumaini na mapendo, sala isiyokoma, ibada, matendo ya imani ya upendo, haki, amani na maelewano na matendo ya huruma ya kiroho na ya kimwili… na zaidi sana kukuza umoja wa kikristo kwa mapendo kamili. Dominika hii 27, tukumbuchwe kwamba imani ni njia ya maisha, si sababu ya sifa.Na katika safari yetu ya Hija wa Matumaini kwa Jubilei ya Mwaka 2025, Yesu anaita:“Tumshukuru Mungu kwa ujasiri uliotolewa kwetu” kwa saburi, nguvu, na huduma. Ee Roho Mtakatifu, ushike moto wa imani ndani yetu, utuonyeshe jinsi ya kusubiri kwa saburi, kushiriki mateso kwa upendo, na kufanyakazi bila kutarajia sifa.” Amina.
Asante sana kusoma makala hii, ikiwa unakata kubaki na masasisho zaidi, tunakualika kujiandikisha hapa: Just click here