Maadhimisho ya Hija Kuu Kwa Heshima ya Mitume wa Huruma ya Mungu Kiabakari
Na Daniel Benno Msangya, Musoma
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa maskini na wahitaji zaidi. Kilele cha Maadhimisho ya Hija Kuu kwa Heshima ya Mitume Wakuu wa Huruma ya Mungu - Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Huruma ya Mungu, Mwenye Heri Padre Mikaeli Sopoćko na Mtakatifu Yohane Paulo II, kimeadhimishwa Kiabakari katika Jimbo la Musoma kuanzia Oktoba 9 hadi Oktoba 12 katika Dominika ya 28 ya Mwaka C, wa Kanisa. Maadhimisho hayo yaliongozwa na Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma akisaidiwa na Padre Wojciech Adam Kościelniak, Mhifadhi wa Kituo cha Kitaifa cha Hija ya Huruma ya Mungu ambaye pia ni Paroko wa Kiabakari. Askofu Msonganzila Mlezi Mkuu wa Shirika la Mitume wa Huruma ya Mungu, Tanzania, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu sambamba na kuwapokea Wanashirika wapya wa Shirika la Mitume wa Huruma ya Mungu katika ibada fupi ya kuwasimika viongozi wapya wa Shirika hilo. Katika shamrashamra hizo Shirika la Mitume wa Huruma ya Mungu ambalo Makao yake Makuu yako Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma, limeadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake rasmi nchini Tanzania mnamo Oktoba 4, 2020.
Katika mahubiri yake Askofu Msonganzila alionyesha matumaini yake kwa Kituo hicho kuelekea hadhi ya kimataifa baada ya kuhudhuriwa hija kuu na waamini kutoka nchi mojawapo jirani. Hiyo ikiwa ni ishara kwa nchi nyingine kuanza kushiriki katika kipindi kifupi kijacho. Askofu Msonganzila ambaye ni Mlezi Mkuu wa Kituo hicho amesema kwa sasa bado kina hadhi ya Kitaifa huku kikimiliki haki na hati rasmi na kuzalisha vitabu chini ya mwanzilishi wake nay eye mwenyewe akiwa mtetezi mkuu wa ustawi wa Kituo hicho. “Masuala yote yanayohusu Huruma ya Mungu sisi tungeweza kujiita Mitume namba moja Tanzania kwa sababu tuna vitabu, tuna mwanzishili na bila kumung’unya maneno tuna mtetezi Baba Askofu ambaye ametetea mpaka kikafikia hadhi ya kitaifa.” Aliongeza Askofu Msonganzila. Aidha aliweka msisitizo katika mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu Huruma ya Mungu akiwataka waamini kubaki katika maneno yale ambayo kimsingi mwanzilishi wa Shirika la Huruma ya Mungu Mtakatifu Sista Faustina amepewa na Mwenyezi Mungu na Yesu Kristo mwenyewe. Aliwahimia kuzingatia matini ya asili aliyostadi Mtakatifu Faustina juu ya Mateso ya Yesu na kutaka Sala kwa mateso ibaki kama ilivyo: Kwa mateso yake utuhurumie sisi na dunia nzima.
Askofu Msonganzila alisema Mtakatifu Faustina hasemi kwa mateso yake Yesu Kristo bali kwa mateso yake, “Tuepuke kuongeza maneno mapya kwa sababu ni sawa na kuungana na waliomtesa Yesu. Tunapoongeza maneno maana yake tunakubaliana na wale waliomwambia Yesu anatoa mapepo kwa nguvu za Belzeburi yaani tunashabikia ushindani, utengano na udhalilishaji,” Aliongeza, “Badala yake sisi tumshukuru Mungu kwa historia ndefu sana, tuitunze historia hiyo na Mwenyezi Mungu atujalie nguvu ya pekee kwani ufalme unaopingana hauwezi ukadumu. Tusipingane katika ibada na visakramenti na hata ikibidi tuviangalie kwa makini. Hapa alitoa mfano wa rozari zinazotumiwa na baadhi ya watu zikiwa zimeficha maumbo na alama zinazopingana na tauhidi na imani ya Kikristo. Kwa upande mwingine aliwahimiza mahujaji kutumia fursa ya Kituo cha Huruma cha kitaifa Kiabakari kujifunza kutofautisha ibada za kweli na ibada zisizo kweli kwa kulishwa chakula kizuri kila wakati. “Hii ni nafasi ya kukaa kimya na kuongea na Yesu wa Ekaristi Takatifu katika ukimya kwa kuzingatia mafundisho yake aliyotoa kwa wanafunzi wake katika Bustani ya Getsemani. Tuige kwa kukesha kama Yeye Mwenyewe alivyokaa pekee yake akiongea na Baba yake, akitafakari mateso yake na utukufu wa Mungu Baba yake,” Alifafanua Askofu Msonganzila.
Mambo Yalianzia Hapa: Katika Mswada wa Kitabu cha Historia (Safari ya Imani Kanda ya Ziwa), simulizi ndefu ya Kituo hiki inampa kongole mwanzilishi mwendelezi Padre Wojciech Adam Koscielniak, mmissionari wa Huruma ya Mungu aliyeishi Tanzania kwa miongo zaidi ya mitatu. Huyo ndiye sonara wa uinjilishaji kupitia huruma ya Mungu. Katika mazungumzo yake na nyaraka mbalimbali anabainisha jinsi ambavyo cheche za huruma ya Mungu zilivyogusa maisha yake na waamini wengi katika utume wake akiwa shuhuda na mjumbe wa chombo cha huruma ya Mungu inayowaka huduma ya upendo; kiroho na kimwili, katika Kituo cha Hija Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma. Padre Wojciech anasimulia kuwa Kituo cha hija Kiabakari ni matunda ya huruma ya Mungu katika maisha yake ya upadre katika kipindi chake cha utumishi akiwa mmisisionari nchini Tanzania kwa takribani miaka 30. Katika ndoto zake alipenda kuona Kituo cha Hija Kiabakari kinakuwa ni mhimili wa huruma ya Mungu kwa njia ya Sakramenti za Kanisa hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Kitubio. Anakiri kuwa hiki ni kituo cha hija za kiroho, ambapo waamini wanaweza kujichotea tena nguvu na neema ya kusonga mbele katika maisha yao ya kiroho! Hiki ni kisima cha huruma ya Mungu!
Mbali na huduma za Kiroho kupitia Kituo cha Kitaifa cha Hija, Parokia ya Kiabakari kupitia Kituo cha Hija cha Kiabakari imefanikiwa kujenga shule ya awali, msingi na shule ya Sekondari na hatimaye, Chuo cha Ufundi – lengo ni kuwasaidia vijana kutambua, kukuza na kuendeleza vipaji vyao kwa ajili ya ujenzi wa Familia ya Mungu inayowazunguka. “Ni kituo ambacho kinataka pia kuwaonjesha wagonjwa na wale wanaoteseka kimwili, huruma ya Mungu kwa kujenga kituo cha afya! Hapa wahudumu wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!” anaandika Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. wa Radio Vatican. Katika mahjiano Maalum na Padre Radio Vatican anagusia kwa ufupi historia ya ujenzi wa Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma, mchakato ambao ulianza kunako mwaka 1991 chini ya Hayati Askofu Justin Samba aliyempatia kibali cha kuanza ujenzi wa Parokia ya Kiabakari. Kazi hiyo ilihitimishwa hapo Oktoba 3, 1991. Mwaka 1992, ujenzi motomoto ulifanyika kwa ajili ya nyumba ya Mapadre na kukamilika. Kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1997 Ujenzi wa Kanisa la Parokia ukakamilika na kutabarukiwa na Askofu mkuu Hayati Anthony Mayala wa Jimbo Kuu la Mwanza hapo Julai 3, 1997. Licha ya kutembelewa na viongozi wakuu wa Kanisa hapa Tanzania Agosti 17, 2001 Askofu mkuu Luigi Pezzuto, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania alitangaza Parokia ya Kiabakari Jimbo Katoliki la Musoma kuwa ni Kituo cha Hija ngazi ya Kijimbo. Muda mfupi baadaye kunako mwaka 2002 Padre Wojciech ambaye ni mhifadhi Mkuu wa Kituo hicho akahamishiwa Parokia ya Musoma mjini kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Miaka 50 ya Parokia ya Musoma mjini ambayo ni Kanisa Kuu la Jimbo la Musoma. Hata hapo Padre Wojciech hakupata usingizi. Alichapa kazi usiku na mchana. Leo atakumbukwa kwa kuacha alama katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Musoma ya mwelekeo mpya wa Ibada ya Huruma ya Mungu kutoka Ibada ya Kanisa Kuu lililokuwa chini ya usimamizi wa Bikira Maria wa Fatima. Historia imeandika kumbukumbu za kifo cha mwasisi wa Kituo cha Hija cha Kiabakari kwa maana ya kibali cha kwanza.
Huyo ni Hayati Askofu Justin Samba wa Jimbo Katoliki Musoma aliyefariki mwaka 2006. Miaka miwili ilipita kabla ya kupata Askofu mwingine. Hata hivyo Kanisa halikukaa kimya. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteua Askofu Mkuu Athony Mayala wa Jimbo Kuu la Mwanza kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki Musoma, akisaidiwa na Padre Julius Ogola (Msimamizi Mwenza). Askofu Mkuu Mayala alimwomba Padre Wojciech Adam Koscielniak, mmissionari wa huruma ya Mungu kurejea kwenye Kituo cha Hija cha Kiabakari, ili kukiendeleza huduma aliyoianzisha. “Huu ukawa ni mwanzo wa ukurasa mpya wa Kituo cha Hija Kiabakari. Baada ya Maaskofu wa Kanda ya Ziwa kuridhika na huduma ya kiroho inayotolewa na Kituo cha Hija hicho cha Kibakari, kufikia hadhi ya kituo cha Jimbo, jitihada hazikusimama. Ulianza mchakato ambao uliwasilishwa kwenye Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ili Kituo hiki kiweze kuwa ni Kituo cha Hija Kitaifa, mahali ambapo Wakleri kutoka Majimbo mbali mbali ya Tanzania wangeweza kufundwa kuhusu huruma ya Mungu. Jitihada hizo tayari zilikubalika na kuanza kuineza huduma za Huruma ya Mungu kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.
Sasa ni mahali pa waamini kujichotea ufahamu wa kina kuhusu huruma ya Mungu! Familia ya Mungu Parokia ya Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma na Taifa la Mungu Tanzania linasubiri kwa hamu kusikia maamuzi mengine iwe ni ya Jimbo la Musoma au Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania au vyombo vyote kwa pamoja kutimiza ndoto za kufikia hadhi ya kimataifa! Hapana shaka hii itakuwa ni Habari Njema ya Injili ya huruma ya Mungu nchini Tanzania, Afrika Mashariki na duniani kote, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu! Kwa ufupi hii ndiyo safari ya ufahamu wa Ibada ya huruma ya Mungu ambayo kwa sasa imeenea sehemu nyingi nchini Tanzania na cheche zake zimeanzia Kenya na muda usio na jina wimbo wa Huruma ya Mungu utaenea Rwanda, Bunjumbura na Uganda kabla ya kuangaza Afrika ukianzia Poland. Mwandishi wa Makala haya anamepokea vitabu kadhaa hasa Huruma ya Mungu na Mungu Aliye Mwingi wa Huruma ikiwa ni matunda ya awali ya huduma zilizoanza mwanzoni mwa Jubilei ya miaka 2000 tangu Kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Ni mkusanyo wa tafakuri na sala kwa Huruma ya Mungu ulioandaliwa kwa Lugha ya Kiswahili kutoka Kipolandi na Kiingereza. Inafurahisha kutambua kuwa tangu siku Hekalu la Huruma ya Mungu Parokia ya Kiabakari lilipowekwa wakfu na Hayati Baba Askofu Mkuu Anthony Mayala Julai 3, 1997 na tangu Mhashamu (Hayati) Baba Askofu Justin Samba wa Jimbo la Musoma alipotangaza Hekalu hilo kuwa Hija ya Kijimbo ya Huruma ya Mungu Agosti 17, 2001 na siku hiyohiyo Balozi wa Baba Mtakatifu nchini Tanzania Mhashamu Askofu Mkuu Luigi Pezzuto akazindua rasmi Hija ya Kijimbo ya Huruma ya Mungu, “Basi tangu wakati huo, tumeshuhudia jinsi Ibada kwa Hurua ya Mungu ilivyoenea kwa kasi katika Kanisa la Tanzania (Pd. Wojciech Adam Koscielniak, Musoma, Februari 2, 2006).