Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 19 Oktoba 2025. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 19 Oktoba 2025.  

Dominika ya 99 ya Kimisionari Nchini Tanzania: Mahujaji wa Matumaini

Papa Leo XIV anawaalika waamini kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 19 Oktoba 2025. Mchango wao wa hali na mali ni muhimu sana katika kusaidia kueneza Injili sehemu mbalimbali za dunia, kwa kusaidia kuendeleza katekesi, ujenzi wa Makanisa mapya pamoja na kusaidia kuendeleza huduma za afya, elimu, ustawi na maendeleo kwa watu wa Mungu katika nchi za kimisionari.

Na Askofu Jovitus Francis Mwijage, Dar Es Salaam, Tanzania

Wapendwa familia ya Mungu, kwa Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, ujumbe mkuu ni matumaini (taz. Bull Spes Non Confundit, 1), hayati Baba Mtakatifu Francisko alichagua kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini kwa Watu Wote". Lengo la Kauli Mbiu hii ni kutukumbusha sote juu ya wito wetu wa msingi wa kuwa, katika nyayo za Kristo, wajumbe na wajenzi wa matumaini. Tukiongozwa na Roho wa Mungu na kwa bidii takatifu, tunaalikwa kuwa washiriki katika msimu mpya wa uinjilishaji katika Kanisa ili kuvishinda vivuli vya giza ulimwenguni (taz. Fratelli Tutti, 9-55). Katika nyayo za Kristo tumaini letu: Kuadhimisha Jubilei ya kwanza ya Kawaida ya Milenia ya Tatu baada ya ile ya Mwaka Mtakatifu wa 2000, tunamkazia Kristo macho yetu, kitovu cha historia, "ambaye ni yeye yule jana na leo na hata milele" (Ebr 13:8) na ambaye Maandiko yalitimizwa katika “leo” ya uwepo wake katika historia (rej. Lk 4:16-21). Kristo ni Mmisionari wa kimungu wa matumaini na kielelezo kikuu kwa wamisionari wote vizazi hata vizazi. Katika maisha yake hapa duniani alitenda mema kwa wote na hivyo kuwarudishia wahitaji tumaini kwa Mungu. Kazi hiyo iliendelezwa na wanafunzi wake na Kanisa hata sasa. Kwa kuiga nyayo za Kristo, nasi tunaalikwa leo kuwa wajumbe wa matumaini kwa watu wote. Wakristo, wabebaji na wajenzi wa matumaini kati ya watu wote: Katika kumfuasa Kristo Bwana, Wakristo wanaalikwa kukabidhi Habari Njema kwa kushiriki hali halisi za maisha ya wale wanaokutana nao, na hivyo kuwa wabebaji na wajenzi wa matumaini. Hakika, "furaha na matumaini, huzuni na uchungu wa watu wa wakati wetu, hasa wale ambao ni maskini au wanaoteseka, ni furaha na matumaini, huzuni na uchungu wa wafuasi wa Kristo pia.

Papa Leo XIV baada ya kuchaguliwa na Baraza la Makardinali
Papa Leo XIV baada ya kuchaguliwa na Baraza la Makardinali   (@Vatican Media)

Hakuna kitu chochote ambacho ni cha kibinadamu kweli kinachoshindwa kupata mwangwi ndani ya mioyo yao" (Gaudium et spes 1). Injili, iliyogusa maisha ya jumuiya, inaweza kuturudisha katika ubinadamu mzima, wenye afya na uliokombolewa. Hivyo, Baba Mtakatifu Francisko anatualika sote kutekeleza kazi zilizotajwa katika “Bolla - Bull of Indiction of the Jubilee” (Na. 7-15), tukiwa makini hasa kwa walio maskini na wahitaji kwa kuwapa tumaini na faraja ambavyo nasi tumepokea pasipo mastahili yoyote (rej. 1 Pet 1:21 na 2Kor 1:3-4).   Kuhuisha utume wa matumaini: Wakikabiliwa na uharaka wa utume wa matumaini leo, wanafunzi wa Kristo wanaitwa kwanza kugundua jinsi ya kuwa "wataalamu" wa matumaini na warejeshaji wa ubinadamu ambao mara nyingi hukengeushwa na hauna furaha. Kwa ajili hiyo, tunahitaji kuhuishwa katika hali ya kiroho ya Pasaka inayopatikana katika kila adhimisho la Ekaristi na hasa katika Siku Tatu Kuu za Pasaka, kitovu na kilele cha mwaka wa liturujia. “Kristo, aliyefufuka na kutukuzwa, ndiye chemchemi ya tumaini letu, na hatatunyima msaada tunaohitaji ili kutekeleza utume ambao ametukabidhi” (Evangelii gaudium, 275). Wamisionari wa matumaini ni wanaume na wanawake wa sala, kwani “mtu anayetumaini ni mtu anayesali”. Sala ni shughuli ya msingi ya kimisionari na wakati huo huo "nguvu ya kwanza ya matumaini" (Katekesi, 20 Mei 2020). Aidha, uinjilishaji daima ni mchakato wa kijumuiya, kama vile tumaini lenyewe la Kikristo (taz. Benedict XVI, Spe Salvi, 14). Katika msingi huu, ni muhimu sana kudumisha muondoko wa kisinodi wa kimisionari wa Kanisa, pamoja na ushiriki hai katika huduma inayotolewa na Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari katika Kanisa. Bikira Maria, Mama wa Yesu Kristo tumaini letu na atuombee daima.

Papa Leo XIV akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama Papa Mpya
Papa Leo XIV akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama Papa Mpya   (ANSA)

SHUKRANI KWA MUNGU KWA ZAWADI YA PAPA MPYA LEO XIV

Baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Francisko tarehe 21 Aprili 2025, Kanisa zima ulimwenguni lilidumu katika sala kwa ajili ya kupata Papa Mpya. Kwa neema za Mungu tarehe 08 Mei 2025 alichaguliwa Kadinali Robert Francis Prevost, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini. Baada ya kuchaguliwa kwake alichagua jina la Papa LEO XIV. Hivyo, tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu ambaye amesikia sala za watu wake na hatimaye kutujalia zawadi ya Mchungaji Mkuu Mpya. Kwa nafasi yake kama Wakili wa Kristo na Halifa wa Mtume Petro, Baba Mtakatifu LEO XIV amekwishatoa Kauli Mbiu yake inayoonesha dira yake ya kichungaji. Kauli Mbiu hiyo ina maneno haya: “In ilo Uno Unum” (katika Kilatini), yaani “Katika Yeye Mmoja tu Wamoja.” Muasisi wa maneno hayo ni Mtakatifu Augustino wa Hippo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Mt. Augustino katika Mahubiri yake kuhusu Zaburi ya 127 anafundisha kuwa ingawa wakristo ni wengi, wote wanafanywa kuwa mwili mmoja katika Kristo. Kwa kuzingatia kuwa Papa Leo XIV kwa asili ni Padre toka Shirika la Waagustini, kwa vyovyote vile uchaguzi huu una msingi wake hapo. Kwa ufupi, ujumbe unaowasilishwa kwetu kupitia Kauli Mbiu hii ni kuwa, katika Kristo aliye mmoja, sisi sote tunafanywa kuwa wamoja kwa njia yake. Ni shauku ya Baba Mtakatifu Leo XIV kuwa familia ya Mungu aliyopewa dhamana ya kuichunga na kuiongoza idumu katika umoja na ushirika katika Kristo. Waamini walio wengi wanaungana pamoja kama mwili mmoja chini ya Kristo ambaye ndiye kichwa cha Kanisa (Kol. 1:15-20, Efe 5:22-25). Hivyo, tunaalikwa sote kuongozwa na dira hii inayotuwajibisha kudumisha umoja na mshikamano wa wanakanisa wote. Yaani, kudumu katika kuwa kundi moja chini ya mchungaji mmoja (Yoh 10:16). Kwa maneno mengine, tunaalikwa kudumu katika muondoko wa kisinodi kama Wanakanisa. Kwa namna ya pekee kabisa, tunapoihusianisha zawadi ya Papa Mpya Leo XIV na utume wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu. Kwetu kama wamisionari, kila mmoja kwa nafasi yake, tukitambua kuwa Mashirika haya yako moja kwa moja chini ya Baba Mtakatifu, tunao wajibu mzito mbele yetu wa kuunga mkono jitihada zake za kuhakikisha kuwa Injili inaenea kokote ulimwenguni. Katika ujumbe wake kwa Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari walipokutana naye kule Roma mnamo tarehe 22 Mei 2025 na kwa kurejea katika historia yake ya utume kule nchini Peru; anakiri na kuhimiza kuwa utume wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ni wa lazima sana hadi leo hii. Utambulisho msingi wa Mashirika haya unabaki kuwa ni Ushirika na Umoja wa Kiulimwengu (universality). Hivyo, kila mmoja kwa nafasi yake anaalikwa kustawisha roho ya umisionari chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Mwisho, tunahimizwa sote tumuombee Mchungaji wetu Mkuu katika utumishi wake. Hali tukitambua kuwa kwa nafasi yake katika Kanisa, Baba Mtakatifu ni kielelezo cha Umoja wa Wakatoliki wote, tunao wajibu wa kumuombea yeye binafsi na Kanisa kwa ujumla. Tumuombee ili adumu imara katika imani na aendelee kuwaimarisha ndugu zake. Aidha, kwa kutambua kuwa yeye ni wakili wa Kristo na Halifa wa Mtume Petro, tunawajibika kumuonesha heshima na utii wa kweli na hivyo kulinda na kudumisha umoja wa Kanisa.

Askofu mkuu Isaac Amani Massawe : Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre
Askofu mkuu Isaac Amani Massawe : Jubilei ya Miaka 50 ya Upadre   (© TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

PONGEZI KWA ASKOFU MKUU ISAAC AMANI WA JIMBO KUU LA ARUSHA: Mnamo tarehe 20 Julai 2025 shangwe na nderemo zilipamba katika Jimbo Kuu Katoliki la Arusha kufuatia maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya Upadre ya Mhashamu Sana Isaac Amani, Askofu Mkuu wa Jimbo hilo. Hakika lilikuwa ni tukio kubwa la kihistoria, furaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu na kwa watu wote ambao wameshiriki kwa namna mbalimbali katika kumsindikiza Baba Askofu Mkuu Amani katika safari yake ya wito na ya utumishi. Nasi tunaalikwa kuungana na familia ya Mungu ya Jimbo Kuu la Arusha kumshukuru Mungu kwa zawadi ya utumishi wa Mchungaji wao Mkuu. Itakumbukwa kuwa Baba Askofu Mkuu Isaac Amani alizaliwa tarehe 10 Julai 1951 katika kijiji cha Mloe – Kibosho Kati, Parokia ya Roho Mtakatifu Mango, Jimbo Katoliki la Moshi. Katika safari yake ya wito, amesoma katika Seminari Ndogo ya Mt. Yakobo Mtume, Kilema Chini. Baadaye alijiunga na Seminari Kuu ya Mt. Antoni wa Padua Ntungamo katika Jimbo Katoliki la Bukoba kwa masomo ya Falsafa tangu mwaka 1970 hadi 1971. Kwa masomo ya Teolojia alitumwa katika Seminari Kuu ya Mt. Paulo – Kipalapala, Tabora tangu mwaka 1972 hadi 1975. Hatimaye alipata Daraja Takatifu ya Upadre mnamo tarehe 29 Juni 1975 Jimboni Moshi mikononi mwa Baba Askofu Joseph Sipendi. Historia ya Utumishi wake kama Padre imesheheni utajiri mwingi kwa faida yetu sote, itoshe tu kuielezea kwa ufupi. Kwa kipindi chake cha Upadre kwa miaka 50 amehudumu kwa nafasi mbalimbali ndani ya Jimbo lake la kuzaliwa la Moshi na kwa sasa katika Jimbo Kuu la Arusha. Mnamo mwaka 1975 hadi 1979 alihudumu kama Paroko Msaidizi, Parokia ya Narumu Jimbo la Moshi; Mwaka 1976 hadi 1986 amehudumu kama Mwalimu na Mlezi kadhalika Makamu Gambera katika Seminari Ndogo ya Mt. Yakobo – Moshi; Mwaka 1986 hadi 1989 alitumwa Masomoni nchini Marekani; Mwaka 1990 hadi 2004 amehudumu kama Padre Mlezi wa Shirika la Mabruda wa Yesu Mkombozi Jimboni Moshi; Mwaka 1999 hadi 2004 amehudumu kama Makamu Askofu kwa ajili ya Watawa katika Jimbo la Moshi; tangu Julai 2004 hadi 2007 amehudumu kama Paroko wa Kanisa Kuu la Kristo Mfalme - Moshi. Mnamo tarehe 21 Novemba 2007 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Benedicto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi na kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi mnamo tarehe 22 Februari 2008 nafasi ambayo amehudumu kwa kipindi cha miaka 10 hadi tarehe 27 Desemba 20217 alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Arusha na kusimikwa rasmi tarehe 8 Aprili 2018. Baba Askofu Mkuu Amani, katika utumishi wake anakumbukwa sana kwa mambo mengi, hususan ari yake ya uchungaji kwanza kama Padre na baadaye kama Askofu. Hilo linajidhihirisha wazi katika Kauli Mbiu ya uchungaji wake isemayo: “MWONDOKO: Kujitambua, Kuwajibika, na Kushirikiana katika Kristo kwa Matendo.” Hivyo, ni vema na haki kabisa kumshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa ya utumishi uliotukuka wa miaka 50 ya Upadre wa Baba Askofu Mkuu Isaac Amani. Tuendelee kujifunza kutoka kwake na kumuombea afya njema ya roho na mwili ili aweze kuendelea vema na utumishi wake katika Kanisa. Mama Bikira Maria Malkia wa Mitume amsindikize daima katika kazi yake ya umisionari anayoendelea nayo hadi sasa.

Askofu Mkuu Mstaafu Paulo Ruzoka: Jubilei Miaka 50 ya Upadre
Askofu Mkuu Mstaafu Paulo Ruzoka: Jubilei Miaka 50 ya Upadre

PONGEZI KWA BABA ASKOFU MKUU MSTAAFU PAULO RUNANGAZA RUZOKA: Kwa kuhimizwa na mwaliko wa Kristo Mwenyewe, tunayo kila sababu ya kumshukuru ‘Bwana wa Mavuno’ ambaye anaendelea daima kulijalia Kanisa lake Watenda Kazi (Mt. 9:38). Tena, kama anavyohimiza Mtume Paulo, ambaye ni somo na msimamizi wa Mshashamu Baba Askofu Mkuu Mstaafu Ruzoka, Kristo haishii tu kuita na kuwaweka watendaji katika Kanisa lake, bali anaendelea daima kuwatia nguvu wale aliowachagua (Fil. 4:13). Ni katika msingi huu, siku ya tarehe 21 Septemba, 2025, kama familia ya Mungu, tuliungana kumshukuru Mungu pamoja na Askofu Mkuu Mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka kwa zawadi na utumishi wa upadre aliomkirimia kwa kipindi cha miaka hamsini. Historia ya maisha na utume wa Baba Askofu Mkuu Mstaafu Paulo Runangaza Ruzoka ni ushuhuda tosha kuwa hakika Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa zawadi ya pekee kupitia nafsi ya Askofu Mkuu Ruzoka. Alizaliwa mnamo tarehe 10 Novemba, 1948 huko Nyakayenzi Kigoma. Safari yake ya Wito wa Upadre ilianza rasmi mwaka 1966 alipojiunga na Seminari Ndogo ya Mt. Karoli Boromeo – Itaga, Jimbo Kuu la Tabora. Mwaka 1970 hadi 1971 alisoma Masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua iliyoko katika Jimbo la Bukoba. Baadaye alitumwa kwa ajili ya Masomo ya Taalimungu katika Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora tangu 1972 hadi 1975. Mnamo tarehe 20 Julai 1975 alipata Daraja Takatifu ya Upadre mikononi mwa Askofu Alphonce Daniel Nsabi aliyekuwa Askofu wa Jimbo lake la Kigoma wakati huo akiwa ni Padre wa Sita Mzalendo kwa Jimbo lake la Kigoma. Katika utumishi wake wa Upadre kwa miaka hii hamsini anayoadhimisha mwaka huu, Mwenyezi Mungu amemjalia fursa mbalimbali za kuhudumu katika Kanisa lake na hivyo kuacha alama inayodumu daima. Itoshe tu kwa uchache kuainisha maeneo ya msingi aliyotumwa kuhudumu kama ifuatavyo: Mnamo tarehe 13 Agosti alitumwa katika Parokia ya Kibondo ambako alihudumu kwa muda wa miezi michache tu hadi tarehe 15 Novemba mwaka huo huo alipopata uhamisho rasmi, japo aliendelea na utume hapo kwa muda kidogo hadi tarehe 07 Januari 1976 aliporipoti rasmi katika Kituo chake kipya cha utume, yaani Seminari Ndogo ya Mtakatifu Karoli Boromeo Itaga, Jimbo Kuu la Tabora. Kwa neema ya Mungu amehudumu katika Seminari hiyo kwa kipindi cha miaka kumi na nne, ambopo kwa miaka mitano ya mwanzo alikuwa Mwalimu na Mlezi na miaka tisa iliyofuata alihudumu kama Gambera wa Seminari hiyo Ndogo. Kadiri ya Mapenzi ya Mungu, mnamo tarehe 10 Novemba 1989 Baba Ruzoka aliteuliwa kuwa Askofu Mteule wa Jimbo Katoliki la Kigoma na hatimaye kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu mnamo tarehe 06 Januari 1990. Mnamo tarehe 25 Novemba 2006 Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alimteua kuwa Askofu Mkuu Mteule wa Jimbo Kuu la Tabora na hatimaye kusimikwa rasmi tarehe 28 Januari, 2007. Baada ya kutimiza umri wa miaka 75 alistaafu rasmi utumishi wa uaskofu mnamo tarehe 10 Novemba, 2023. Hakika, historia hii ni shule tosha kwetu sote na kielelezo cha maisha ya ushuhuda wa imani kupitia utumishi wa Upadre katika Kanisa. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria na Mtakatifu Paulo Mtume, tunazidi kumuombea utumishi mwema.

Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora
Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu ya Kipalapala, Tabora

SHUKRANI KWA MUNGU KWA JUBILEI YA MIAKA 100 YA SEMINARI KUU YA MTAKATIFU PAULO MTUME KIPALAPALA – TABORA: Kanisa linatambua kuwa miito mbalimbali ambayo Roho Mtakatifu analijalia ni udhihirisho wa utajiri wa Kristo (Efe 3:8), na hivyo inabidi iheshimiwe vilivyo na kulelewa vema ili iweze kukomaa na kuzaa matunda stahiki kwa wakati wake. Miongoni mwa miito hii ni UPADRE. Ni wajibu wa Kanisa kwanza kuitikia wito wa Bwana Mwenyewe wa kumuomba alijalie ‘Watenda Kazi” na kujibidisha kuilea miito hii mitakatifu. Ni katika msingi huu kanisa limeweka utaratibu wa kuwa na Seminari Kuu kwa ajili hasa ya MALEZI. Kadiri ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Seminari Kuu ni za lazima kwa malezi ya kipadre (Tamko Juu ya Malezi ya Waseminari, na.4). Kwa Kanisa Mahalia la Tanzania, hatuwezi kamwe kuielezea historia yake ya uinjilishaji bila kutambua uwepo na mchango wa Seminari zetu Kuu, kwa namna ya pekee Seminari Kuu ya Kipalapala ambayo mwaka huu imetimiza umri wa miaka mia moja tangu kuanzishwa kwake. Mwaka huu 2025 ni mwaka wa kihistoria sio tu kwa vile kiulimwengu tunaadhamisha Jubilei ya Miaka 2025, zaidi sana kwa vile tunaadhimisha Jubilei ya miaka mia moja ya uhai wa moja ya Seminari Kuu za Kanisa Mahalia la Tanzania. Historia ya Seminari Kuu ya Kipalapala inaonesha kuwa Seminari hii ilipitia katika maeneo matatu tofauti na kwa nyakati tofauti. Seminari hii ilianzia huko Ushirombo katika Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo mnamo tarehe 05 Septemba, 1918 katika Vikariati ya Unyanyembe (Kwa sasa - Jimbo la Kahama). Seminari hii iliwekwa chini ya usimamizi wa Mt. Karoli Borromeo na kwa wakati huo ilifundisha masomo ya Falsafa pekee. Baadaye, Maaskofu wa Vikariati za Unyanyembe, Tanganyika, Bangwelo (Zambia) na Nyasa (Malawi) waliazimia kuunda Seminari moja itakayohudumia maeneo yao ya utume. Hivyo, waliamua kwamba Seminari hiyo ianzishwe katika Vikariati ya Tanganyika katika eneo la Utinta mahali ilipokuwepo Seminari Ndogo ya Vikariati hiyo. Hivyo, tarehe 11 Julai 1921 Seminari ya Ushirombo ilifungwa na kuhamishiwa Utinta. Hatimaye, Seminari hiyo ya Utinta ilihamishiwa Kipalapala katika Vikariati ya Tabora (Kwa sasa – Jimbo Kuu la Tabora) mnamo mwaka 1925. Tangu mwaka 1964 Seminari hii iko rasmi chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC). Kwa hiyo, Seminari hii ni miongoni mwa Seminari Kuu Sita ambazo ziko chini ya uangalizi wa Bodi ya Kitaifa ya Seminari Kuu (NBMS).

Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu ya Kipalapala, 2025
Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu ya Kipalapala, 2025

Hivyo, kadiri ya historia iliyodokezwa hapo juu, kama tukichukulia mwanzo wa Seminari ya Kipalapala kuwa ni Ushirombo, ni ukweli usiopingika kuwa ilitimiza miaka mia moja mwaka 2018; endapo tutachukulia mwanzo wake kuwa Utinta – basi ilitimiza miaka mia moja mwaka 2021 na tukichukulia mwanzo wake kuwa Kipalapala, mahali ilipo sasa, ni dhahiri kuwa inatimiza miaka mia moja mwaka huu 2025. Ni katika kuutazama mwanzo wa Seminari hii kuwa katika eneo la Kipalapala, ndio maana, kwa moyo wa shukrani kuu kwa Mungu, mwaka huu, tunaadhimisha Jubilei hiyo ya miaka mia moja. Hakika jambo hili limefanywa na Bwana nalo ni la ajabu sana kwetu (Mk. 12:11). Kwa namna ya pekee kabisa tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya Wamisionari wa Afrika (White Fathers) ambao, pamoja na utume wao katika maeneo mengine ya kichungaji, waliwekeza pia katika kuandaa warithi katika kazi ya uinjilishaji wa maeneo ya Misioni ya Maziwa Makuu ya Ikweta ya Afrika na Afrika kwa ujumla chini ya uongozi madhubuti wa Kardinali Karoli Martial Allemand Lavigerie. Miongoni mwa vitalu vya kwanza vya malezi kuelekea upadre walivyoanzisha ni Seminari Kuu ya Kipalapala ambayo leo hii inatimiza miaka mia moja tangu ihamishiwe rasmi Kipalapala ambapo mafrateri na walezi wao waliwasili rasmi Kipalapala toka Utinta mnamo tarehe 04 Februari 1925 wakiongozwa na Padre Janmeeuwsen (Gambera wa Kwanza), na tarehe hii ikawa ndio mwanzo wake rasmi hapo Kipalapala. Hakika ni neno jema kumshukuru Mungu (Zab. 92:1-2). Tunapomshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa ya Seminari Kuu ya Kipalapala inayoadhimisha leo miaka mia moja tangu kuanzishwa kwake, tunawiwa kutoa shukrani zetu pia kwa makundi mbalimbali ya watu. Tunawashukuru Mababa Askofu ambao wameendeleza kazi hii nzuri sana iliyoanzishwa na Wamisionari wa Afrika kwa malezi na maongozi yao bora kwa kitalu hiki cha malezi ya upadre; tunawashukuru Walezi wote waliohudumu katika Seminari hii kwa kipindi hiki cha miaka mia moja, hasa Magambera Wamisionari (tangu 1925-1967) na Magambera Wazawa (1967 hadi sasa); Wanajimbo Kuu la Tabora (wenyeji wetu); wafadhili wote; wafanyakazi (watawa, walei na hata wasio wakristo); Mafrateri wote waliopata malezi katika Seminari Kuu hii wapatao 3,548 (miongoni mwao akiwemo Kardinali mmoja, Maaskofu 42, mapadre 1540 na walei wengi); wale wote walioratibu maadhimisho ya Jubilei hii ya miaka mia moja na watu wote wenye mapenzi mema walioitegemeza na watakaoendelea kuitegemeza Seminari hii. Mungu awabariki na kuwazidishia kwa ukarimu wao. Kwa Maombezi ya Mama Bikira Maria Malkia wa Mitume na Mt. Paulo Mtume Msimamizi wa Seminari Kuu ya Kipalapala, tunamwomba Mungu aendelee kuijalia seminari hii kudumu katika kuwa kitalu bora cha malezi kulingana na mahitaji ya nyakati za sasa na mapadre wengi na watakatifu wazidi kuzaliwa katika Kanisa kupitia MAMA huyu. HONGERA SANA MAMA KIPALAPALA.

Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari ya Mt. Yakobo Mtume, Kilema, Moshi
Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari ya Mt. Yakobo Mtume, Kilema, Moshi   (Missionaries of Africa - Padri Bianchi)

SHUKRANI KWA MUNGU KWA JUBILEI YA MIAKA 100 YA SEMINARI NDOGO YA MTAKATIFU YAKOBO MTUME KILEMA CHINI – MOSHI: Kadiri ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hasa kuhusu Tamko Juu ya Malezi ya Waseminari, malezi ya kiroho na kielimu katika Seminari Ndogo ni ya muhimu sana. Lengo la Seminari Ndogo ni kuotesha mbegu ya wito. Hivyo, wanafunzi wanatakiwa kutayarishwa kwa malezi pekee ya kidini na hasa kwa uongozi wa kiroho wa kufaa, kufuata Kristo Mkombozi kwa roho pendevu na mioyo mikunjufu (rejea Tamko Juu ya Malezi ya Waseminari, n.3). Ni katika msingi huu Seminari Ndogo zilianzishwa katika maeneo mbalimbali katika Kanisa. Kwa hapa kwetu Tanzania, itoshe kuienzi kwa namna ya pekee hapa, Seminari Ndogo ya Mt. Yakobo – Kilema Chini, Moshi ambayo mwaka huu imeadhimisha miaka mia moja tangu kuanzishwa kwake. Sifa na Utukufu kwa Mungu. Itakumbukwa kuwa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Yakobo Mtume – Kilema Chini ilianzishwa rasmi mnamo tarehe 25 Februari 1925 na Wamisionari wa Roho Mtakatifu (Holy Ghost Missionaries) waliokuwa wakiinjilisha maeneo hayo wakati huo chini ya uongozi wa Askofu Henry Aloysius Gogarty C.S.Sp., (1924-1931), kwa ajili ya kuandaa mapadre wazawa watakaohudumu katika Jimbo la Moshi na mahali pengine. Mithili ya chembe ndogo ya haradali, Malezi ya Wanafunzi waliokuwa wanaandaliwa kuwa mapadre yalianzia katika mazingira ya Parokia za Kibosho na Kilema. Walelewa waliokuwa katika Parokia ya Kibosho walihama na Padre Albrecht C.S.Sp., kuelekea Kilema ambako huko waliunganishwa na Walelewa waliokuwa tayari Parokiani Kilema. Hawa ndio wanafunzi wa mwanzo waliohamia katika eneo la Kilema Chini kuanzisha rasmi Seminari ya Mtakatifu Yakobo mnamo tarehe 25 Februari 1925 wakiungana na wanafunzi wengine wawili ambao walitokea katika Vikariati ya Zanzibar na wawili kutoka Kenya chini ya Padre Albrecht C.S.Sp., ambaye sasa alikuwa Gombera wa kwanza. Kwa kuzingatia misingi mizuri iliyowekwa na waaasisi wake tangu miaka hiyo mia moja iliyopita, Seminari ya Mtakatifu Yakobo daima imejitanabahisha kwa nguzo kuu tatu, yaani SALA, MASOMO NA KAZI. Nguzo hizi zinashabihiana fika na kanuni nyingine inayoongoza Malezi katika Semari Kuu na Ndogo, yaani MALEZI FUNGAMANO. Ni kiu ya Kanisa kuwa walelewa wa Upadre kwa ngazi zote walelewe kwa ukamilifu hali malezi yao yakiangazia nyanja zote hususan malezi ya kiutu, maisha ya kiroho, taaluma, na moyo wa uchungaji. Tunamshukuru Mungu kwamba Seminari hii Ndogo imebaki daima katika msingi huu imara. Ndio maana inasifika sana kwa matunda bora.

Papa Leo XIV akiwapongeza Majandokasisi na kuwatia shime katika wito
Papa Leo XIV akiwapongeza Majandokasisi na kuwatia shime katika wito   (@Vatican Media)

Tunapomshukuru Mungu kwa zawadi ya Seminari Ndogo ya Mt. Yakobo – Kilema Chini, ni fursa ya kuitambua kuwa Seminari hii imekuwa daima MAMA MWEMA anayetambulika kutokana na matunda yake. Ni kutoka katika Seminari hii Ndogo wamezaliwa Maaskofu kumi na mbili, mapadre wapatao 625, mabradha na waamini walei walio wema na wenye sifa njema katika nchi yetu na kwingineko wapatao 3,628. Itakumbukwa kuwa Padre wa kwanza ambaye ni tunda la Seminari hii Ndogo ni Padre Alfonsi Mtana kutokea Parokia ya Marangu – Makomu aliyepadrishwa Parokiani Kilema tarehe 8, Aprili 1939. Miongoni mwa Mapadre waliofuata baadaye ni pamoja na Askofu Joseph Kilasara C.S.Sp., ambaye alikuwa ni Askofu wa Kwanza Mzalendo wa Jimbo Katoliki la Moshi (1960 – 1966).Hakika, maadhimisho haya ya Jubilei ya miaka mia moja ya Seminari hii ya Mtakatifu Yakobo ni fursa pia ya kutoa shukrani kwa watu wengi ambao kwa nyakati mbalimbali wameshiriki katika ustawi wake. Tunawashukuru kwa namna ya pekee Mapadre wa Roho Mtakatifu (Holy Ghost Missionaries) ambao walianzisha Seminari hii; Maaskofu wa Jimbo Katoliki la Moshi walioisimamia na kuiendeleza kwa vipindi mbalimbali; Mapadre waliosoma na baadaye kushiriki katika kazi ya Malezi hapo; Wanafunzi Walei waliosoma hapo; Watawa ambao wamehudumu hapo kwa vipindi mbali mbali na ambao wanaendelea kuitegemeza seminari hii kwa sala na sadaka zao; wafanyakazi wote; wafadhili wote, ndugu, jamaa, marafiki na wote wenye mapenzi mema. Kwa nafasi ya upendeleo tunawashukuru wale wote wanaohudumu katika Seminari hii Ndogo kwa sasa: kwanza kabisa Baba Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS, Baba Gambera na mapadre wenzake saba, walimu – walei wanne, watawa wanne, wanafunzi wapendwa ambao ni sehemu ya familia kubwa ya Seminari hiyo kwa sasa na wale wote ambao wameshiriki kwa nafasi mbalimbali katika maadhimisho ya Jubilei hii. Mwenyezi Mungu awabariki na kuwafanikisha. Kwa maombezi ya Mt. Yakobo Mtume, Mwenyezi Mungu aendelee kuistawisha Seminari hii na kuifanya kuwa kitalu bora cha Malezi hata katika nyakati zetu. Kama Kauli Mbiu ya Seminari inavyosema: “Upendo Hushinda Yote” basi Upendo wa Kristo uzidi kutawala katika Kitalu hiki cha Malezi ya Upadre.

Tume ya Uinjilishaji ya TEC inawashukuru sana watu wa Mungu kwa ukarimu.
Tume ya Uinjilishaji ya TEC inawashukuru sana watu wa Mungu kwa ukarimu.

NENO LA SHUKRANI: Kwa niaba ya Tume ya Uinjilishaji ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC ambayo inawawakilisha Maaskofu wote katika masuala ya Umisionari katika nchi yetu ya Tanzania; ninapenda kutoa shukrani za dhati kabisa kwa makundi mbalimbali ya waamini kwa kuitikia wito wa Kanisa wa Ushirikiano wa Kimisionari Kiulimwengu. Ninawashukuru Mababa Askofu wote, Mapadre, Watawa (wa kike na kiume), waamini walei katika ujumla wao, Watendaji wote wa Utume wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari (kitaifa na katika majimbo yote), Marafiki wa Mashirika ya Kipapa na wote wenye mapenzi mema, kwa majitoleo yenu makubwa sana katika kuwezesha kazi ya Uinjilishaji kupitia Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari hapa Tanzania. Kwa neema za Mungu katika Mwaka huu wa Jubilei 2025 na kwa ushirikiano mkubwa wa waamini wote, UKARIMU wa Kanisa la Tanzania kwa Mfuko wa Uinjilishaji wa Baba Mtakatifu umepata matokeo mazuri sana. Kwa mwaka huu tulioumaliza 2024/2025 tumeweza kupata kiasi cha fedha tasilimu TZS 1,046,007,633.04 (Jumla Kuu), kiasi ambacho ni ongezeko la fedha tasilimu TZS 252,606,868.08 (sawa na asilimia 31.8%) tukilinganisha na makusanyo ya mwaka uliopita 2023/2024 ambapo tulipata kiasi cha fedha TZS 793,400,764.96 (Jumla Kuu). Hakika hii ni hatua kubwa sana na ishara wazi ya kukua kwa Kanisa la Tanzania. Tunamshukuru Mungu na kila mmoja aliyetolea UKARIMU wake kwa moyo mkunjufu. Mungu atubariki sote. Ninapenda kuhitimisha kwa kutoa mwaliko kwa kila mmoja wetu kujiandaa vema kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwezi Oktoba – Mwezi wa Kimisionari na baadaye Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, inayoongozwa na kauli mbiu: “Wamisionari wa Matumaini kwa Watu Wote.” Aidha, ni vema ikakumbukwa kuwa Dominika hii inatanguliwa na Novena ya Siku Tisa iliyoanza rasmi siku ya Ijumaa ya tarehe 10 Oktoba 2025 na kuhitimishwa siku ya Jumamosi ya tarehe 18 Oktoba 2025. Kwa kutambua kuwa sisi sote kwa ubatizo wetu ni Wamisionari, basi tujibidishe kuitumia vema fursa hii ya kiroho ambayo Mwenyezi Mungu kupitia Mama Kanisa anatujalia. Tujiandae vema kwa SALA kadhalika na UKARIMU kwa ajili ya kuwezesha kazi ya umisionari kiulimwengu kupitia Mfuko wa Uinjilishaji wa Baba Mtakatifu unaoratibiwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.

Tume ya Uinjilishaji TEC
17 Oktoba 2025, 15:48