Zakayo alitamani kumuona Yesu. Zakayo alitamani kumuona Yesu. 

Dominika 31 ya Mwaka C:“Mwana wa Adamu amekuja kumtafuta na kumwokoa aliyepotea”

Tumesikia Zakayo akitafuta kumwona Bwana wetu Yesu Kristo.Labda tunaweza kujiuliza ni kwa nini Zakayo alitaka kumwona Yesu?Hakika sababu ni nyingi za Zakayo kutaka kumwona huyo Yesu Kristo yupoje!Miongoni: kwanza alikuwa amesikia Yesu ni masiha aliyetamaniwa, pili ni mwokozi,tatu ni mponyaji,nne ni mtenda miujiza,tano umati wa watu uliokusanyika kumsikiliza ulimvuta na kumsukuma kumwona Yesu yupoje.Je wewe unavutiwa na nini kwa Yesu?

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Mwana wa Adamu amekuja kumtafuta na kumwokoa aliyepotea”( Luka 19:10). Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 31 Mwaka C. Leo tunaalikwa kutafakari juu ya huruma ya Mungu kwa wenye kutubu, na jinsi tumaini linavyozaliwa tena ndani ya mtu aliyeonekana kuwa amepotea, mfano wa Zakayo. Mungu anaonyesha uvumilivu mkuu kwa waovu, si kwa sababu hawezi kuwaadhibu, bali kwa sababu anawapa nafasi ya kutubu. Ana huruma kwa kila kiumbe, hata mdogo zaidi. Katika dunia ya leo yenye dhambi, vita, na ukosefu wa haki, Mungu bado anatupatia nafasi ya kubadilika. Hii ni roho ya Jubilei ya Matumaini: rehema kabla ya hukumu katika somo letu la kwanza tumesikia kwamba Mwenyezi Mungu huwahurumia watu wote wanaotubu na huwaachilia wanadamu dhambi zao ili wapate kutubu.

Huwahurumia wanadamu wanaotubu kwa sababu Yeye anavipenda vitu vyote alivyoviumba hapendi chochote kipotee na wala hakichukii chochote. Yeye pia ni mpenda roho za watu maana roho isiyoharibika imo katika mwanadamu kwa hiyo wanaokengeuka kutoka katika njia njema huwaonya na kuwakumbusha kwa mambo yale wanayokosa ili waokoke na kumwamini Bwana. Bwana ni mwingi wa rehema… huinua waliopondwa.” Dunia leo inahitaji huruma na rehema zaidi ya hukumu. Wanaokandamizwa, waliopotea matumaini  wanaalikwa kumgeukia Mungu mwenye hurumaYesu hajaja kwa walio wakamilifu, bali kwa waliopotea. Katika dunia ya leo, sisi sote tunaweza kuwa kama Zakayo, watu wa tamaa, waliopotoka, waliokata tamaa, lakini bado tunapewa nafasi ya kukutana na huruma ya Kristo.

Tumesikia mwanaharakati Zakayo akitafuta kumwona Bwana wetu Yesu Kristo. Labda tunaweza kujiuliza ni kwa nini Zakayo alitaka kumwona Yesu? Ni hakika Zakayo alikuwa na sababu nyingi zilizomfanya atake kumwona huyo Yesu Kristo yupoje! Miongoni mwa sababu hizo ni hizi; kwanza alikuwa amesikia kuwa Yesu ni masiha waliyekuwa wakimtamani na kumngoja kwa hamu, pili ni mwokozi, tatu ni mponyaji, nne ni mtenda miujiza, tano umati wa watu uliokusanyika kumsikiliza ulimvuta na kumsukuma kumwona Yesu yupoje  na zaidi sana neema ya Mungu iliyokuwa ikimsukuma toka ndani kumwona ili afanye toba. Simulizi la Zakayo, mtoza ushuru mfupi wa kimo aliyepanda mtini ili amwone Yesu. Yesu alikaa kwake, akampa wokovu. Yesu anasema:“Lazima nikae nyumbani mwako leo.” Na mwisho “Mwana wa Adamu amekuja kumtafuta na kumwokoa aliyepotea. Hili ni onyesho la upendo usio na mipaka. Yesu hahukumu kwanza, anakaribia moyo uliotayari kubadilika. Zakayo alikuwa tajiri aliyejua hali yake ya dhambi, na alipokutana na huruma ya Yesu, alibadilika, akawa mtu mpya.

Jubilei ya Matumaini ni wakati wa neema, toba, na kuanza upya. Masomo ya Dominika hii yanaelekeza katika, Huruma ya Mungu kwa wenye dhambi kama Zakayo. Uvumilivu wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa wote. Mwito wa kudumu katika imani, licha ya hali ngumu. Kuona kwamba hakuna aliye mbali sana asingeweza kurudi kwa Mungu. Huyu Zakayo ni myahudi tajiri, mfupi kwa kimo na mkuu wa watoza ushuru. Kwa kawaida watoza ushuru walikuwa wala rushwa wakubwa na wanaotoza ushuru zaidi ya kiasi kilichowekwa. Watoza ushuru wanapomuuliza Yohane Mbatizaji na sisi tufanyeje? Yohane anawajibu msitoze zaidi kiasi kilichowekwa. Kwa mtazamo huu Wafarisayo na Waandishi walimtazama Zakayo kama mdhambi mkuu. Ikumbukwe kwa Myahudi, mtu mfupi alionekana kuwa amelaaniwa na Mungu na hafai kwa kazi yoyote na mbaya zaidi kuwa jirani na Mungu, Myahudi awe mrefu mwenye sura nzuri ya kuvutia kwa sababu hizi ndio maana hawakushughulika kumsaidia Zakayo kumwona Bwana.

Bwana anatambua nia na kusudi la Zakayo anafika na kumwambia “Zakayo shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako” Yesu anamtaja kwa jina Zakayo hata kama hajawahi kumwona kabla, pana nini zaidi, hakika alitambua mahangaiko, nia na moyo wa Zakayo ulikua juu Yake. Zakayo alifurahi mno kwani hakutegemea kumkaribisha nyumbani kwake masiha, mtenda miujiza, mwokozi, mponyaji na mhubiri mzuri. Tendo hili lilimshangaza lakini alitiwa nguvu na heshima aliyopewa na Yesu Kristo. Vita na Mapigano, Zakayo ni mfano wa wale wanaoonekana kuwa "maadui wa watu", lakini bado Mungu anaweza kuwageuza. Hata katika migogoro ya kimataifa, Mungu bado anaita wakosaji warudi. Rehema mbele ya kulipiza. Utawala wa Sheria Zakayo alipotosha sheria kwa kujinufaisha,lakini alipoongoka, alirudisha mara nne.

Injili ya Dominika ya 31 Mwaka C inaelezea Mkutano wa Zakayo na Yesu
Injili ya Dominika ya 31 Mwaka C inaelezea Mkutano wa Zakayo na Yesu

Hili ni fundisho kwa viongozi na jamii, toba ya kweli huambatana na kurekebisha makosa, kwa bahati mbaya sana dunia na jmaii nyingi leo machafuko ana mapigano yanatokana na viongozi wasio waaminifu na wenye kuzinatia haki na sheria badala yake wanaendekeza uniafsi na kunyonya wanyonge, lakini basi leo Zakayo awe mfano wa kubadili maisha yao na wawe viumbe wapya ili kuepusha machafuko na maandamano ya kudai haki. Wengi wanaishi katika giza la kukataliwa, kutengwa, dhambi, na kutokujiamini. Zakayo anatufundisha kwamba Yesu anawakaribia walio mbali zaidi, na anaweza kubadili historia zao. simulizi la kuokoka kwa Zakayo linaletwa kwetu leo sio kama simulizi la kihistoria kwamba lilikuwa bali ni tukio hai kiroho linalotualika sote kumtafuta Bwana. Katika kumtafuta Bwana huku ufupi wa Zakayo ni kielelezo cha watu dhaifu, wadhambi,wazinzi na wanyonge wanaotafuta kumwona Bwana.

Na Waandishi na Wafarisayo ni kielelezo cha wale wanaojiona ni watu wa haki, waadilifu na  watakatifu na hivi wanawazuia watu hawa dhaifu kumwona Bwana kutokana na urefu walionao. Wanawazuia kwa maneno,matendo na kuwadharau, ooh huyu mzinzi, huyu mwizi, malaya, mlevi na mgomvi hivi hawasitahili kumwona Bwana. Lakini Yesu anamtaja Zakayo kwa jina sio kwa mapungufu au dhambi zake kwa hiyo tukio hili litufanye tujitambue kuwa sote sio wakamilifu. Kila mmoja anamapungufu yake na hayo ndiyo yanayofufanya tuitwe akina Zakayo; kinachotakiwa ni kugeuka na kupiga moyo konde na kumtafuta Bwana kwa udi na uvumba.

Tunapomzuia mtu kumwona Yesu sisi tunakuwa kikwazo kwa utume wa Bwana wa kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. Na pia aliye mzima hahitaji mganga wala dawa ila yule aliye hajiwezi, na Bwana alikuja kwa ajili ya hao ambao mimi na wewe tunawao ni wadhambi,wazinzi na watu wasiofaa. Mungu anatukaribisha tukubali kuponywa, kubadilishwa, na kufanywa wapya, kama Zakayo. Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini, sisi pia tuitike mwito wa kuishi upya kwa, Toba ya kweli, Rehema kwa wengine, Matendo ya haki na marekebisho ya maisha yetu. Mungu hutuonya akitumia mambo ya kawaida kabisa maishani mwetu kwa kuzigusa dhamiri hai zichukie ubaya na kutamani wema wa Mungu. Hivyo ndivyo mtoza ushuru Zakayo alivyoguswa na mafundisho yake Bwana wetu Yesu Kristo akitamaani kuacha ubaya kwa kumwamini Mungu akitenda mema yaendanayo na malipizi ya ubaya wa dhambi kwa Mungu na jirani.

Maswali Ya Kujiuliza Leo: Mimi ni kama nani? Zakayo aliyekuwa na tamaa, au Zakayo aliyebadilika?, Je, ninampokea Yesu nyumbani mwangu, moyoni mwangu?, Katika nafasi yangu ya kazi, familia, au jamii, je, naishi maisha ya matumaini, au ninakatisha wengine tamaa? Zakayo anatukumbusha na kutufundisha kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu katika dhamiri zetu, kutambua ni wadhambi tunaopaswa kutubu na toba yetu yatupaswa kudhihirika kwa vitendo kama alivyofanya yeye. Anatufundisha kutokuwa vipofu na mahakimu kwa wenzetu bali tuwasaidie ili  wale wanatafuta wokovu waupate kwa mapendo na matendo yetu hapa duniani hasa kwa kuwajali na kuwaongoza katika njia ilonyoka.

Ee Yesu, kama ulivyomwambia Zakayo: “Leo wokovu umefika nyumbani mwako,” sema vivyo hivyo kwetu leo. Tusaidie kuacha uovu, kupokea huruma yako, na kuwa mashahidi wa matumaini kwa dunia yenye giza. Tukiwa na imani kuwa Mungu ni mwingi wa rehema, tumwelekee katika sala, tukimwomba kwa unyenyekev Kwa Kanisa lote la Kristo duniani, Bwana, liwe chombo cha huruma yako, liwakaribishe wenye dhambi kwa upendo kama ulivyomkaribisha Zakayo. Wape moyo wa haki, uaminifu, na utawala wa sheria. Waepushe na tamaa ya mali na madaraka. Kwa wote wanaoteseka kwa vita, ukosefu wa haki, na kutengwa: Uwainue kama ulivyomwinua Zakayo. Uwape matumaini na amani. Ee Bwana, kama ulivyomwita Zakayo, tuitikie pia sisi. Acha neema ya Jubilei ya Matumaini itufikie na kutubadili. Tunakuomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu Amina.

Tafakari ya Dominika 31 Mwaka C
31 Oktoba 2025, 16:51