Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Toba, Wongofu na Moyo wa Shukrani. Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Toba, Wongofu na Moyo wa Shukrani.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Wongofu na Moyo wa Shukrani

Ujumbe wa tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa unahusu: Toba, wongofu na moyo wa shukrani kwa Mungu ili tuweze kukua katika mahusiano mema naye. Tukifanya hivyo tutakuwa na muunganiko naye, na ikitokea tumemkosea, tukitubu kwa moyo wote, kwa kukusudia kuachana na uovu na kutenda mema, tukimwomba msamaha, atatusamehe. Waamini wajenge moyo wa toba na shukrani, ili kupokea uponyaji: kiroho na kimwili.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 28 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe unahusu: Toba, wongofu na moyo wa shukrani kwa Mungu ili tuweze kukua katika mahusiano mema naye. Tukifanya hivyo tutakuwa na muunganiko naye, na ikitokea tumemkosea, tukitubu kwa moyo wote, kwa kukusudia kuachana na uovu na kutenda mema, tukimwomba msamaha, atatusamehe. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema; “Bwana, kama wewe ungehesabu maovu, ee Bwana, nani angesimama mbele yako? Lakini kwako kuna msamaha, ee Mungu wa Israeli” (Zab. 130:3-4). Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba neema yako ituongoze daima na kutusindikiza, itutie siku zote moyo wa bidii wa kutenda mema”. Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Pili cha Wafalme (2Waf 5:14-17). Nalo linahusu simulizi la kuponywa ukoma, na kuongoka kwa Naamani, Jemedari, mkuu wa Jeshi la Assiria. Katika simulizi hili tunajifunza kuwa uponyaji wa kimwili na wongofu wa ndani vinaenda hatua kwa hatua za kujishusha na kuuvaa unyenyekevu. Ndiyo maana Naamani, katika kutafuta uponywaji alipitia hatua kadhaa – kutoka hadhi ya juu, kamanda wa Jeshi, kuomba ushauri kwa mfalme, ushauri uliobaki tasa bila kupata tiba, hivyo akashuka kutafuta uponyaji kwa Nabii, akifuata ushauri wa msichana kijakazi, mateka toka Samaria, kutoka kuoga maji safi ya mito bora ya Damaski, mpaka kujichomvya katika maji ya mto Yordani, kutoka kutafuta ishara na maajabu makuu, mpaka kufanye tendo dogo la kujizamisha mara saba katika maji – ishara ya ubatizo.

Jemedari Naaman ni mfano wa toba, wongofu wa ndani na shukrani
Jemedari Naaman ni mfano wa toba, wongofu wa ndani na shukrani   (AFP or licensors)

Ni katika kujivika unyenyekevu na utii, kusikiliza na kufuata ushauri wa mtumwa wake, kufuata na kutekeleza maagizo ya Nabii Elisha, ndipo alipoponywa, akatakaswa ukoma wake, na kuongoka hata kukiri ukuu wa Mungu wa Isareli, na kutaka kumshukuru Nabii Elisha kwa kumpatia zawadi. Lakini Elisha alizikataa ili Mungu apewe sifa. Ndipo Naamani alipoomba udongo wa nchi ya Israeli, ili akamjengee Mungu madhabahu katika nchi yake na kumwabudu huko.Ndivyo Bwana alivyoufunua wokovu wake machoni pa mataifa kama zaburi ya wimbo wa katikati inavyosema; “Bwana ameufunua wokovu wake machoni pa mataifa. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu. Mkono wa kuume wake mwenyewe, mkono wake mtakatifu umetenda wokovu. Bwana ameufunua wokovu wake, machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake. Miisho yote ya dunia, imeuona Wokovu wa Mungu wetu. Mshangilieni Bwana, nchi yote, inueni sauti, imbeni kwa furaha (Zab. 98:1-4). Ujumbe kwetu; tujivike roho ya huduma na uwajibikaji kwa wote hata adui zetu, na tumpe Mungu vilivyo vyake, sifa, utukufu na heshima, kama Nabii Elisha. Tujivike moyo wa unyenyekevu, na upole ili tuweza kupokea mema kutoka kwa Mungu hata kupitia kwa adui zetu na kushukuru, kama Jemedari Naamani. Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo (2Tim 2: 8-13). Ni wosia na maagizo aliyoyatoa Mtume Paulo akiwa gerezani kuwa tukiyakubali mateso, tukayapokea, tukayavumia mpaka mwisho na kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya Injili, tutafufuka pamoja na Kristo na kushiriki naye furaha ya milele mbinguni. Kinyume chake, tukimkana, Naye atatukataa siku ya hukumu. Licha ya kuwa Yeye Paulo amefungwa kama mtenda mabaya kwa ajili ya Neno la Mungu, lakini anaamini kuwa Neno hili linaendelea kuishi kwa maana haliwezi kufungwa na cho chote. Kwa ajili ya hilo anastahimili yote, ili liwafikie na wengine waupate wokovu ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Basi tujivike ujasiri, tusirudi nyuma kamwe na kuiacha imani yetu kwa sababu yoyote ile, hata ikitupasa kujitoa sadaka, kwani hiyo ndiyo shukrani yetu kwa Kristo, aliyetoa maisha yake kwa ajili yetu, na ndiyo njia ya kutufikisha katika uzima wa milele mbinguni.

Msamaria ndiye peke yale aliyerufi kumpatia Mungu sifa na shukrani
Msamaria ndiye peke yale aliyerufi kumpatia Mungu sifa na shukrani

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 17:11-19). Ujumbe wake umejikita katika uponywaji wa kimwili kwa kwa wakoma 10, na kupokea wokovu kwa mmoja, Msamaria, aliyekuwa na moyo wa shukuruni kwa mema aliyopokea kutoka kwa Mungu. Katika simulizi wakoma 10 walisimama mbali, wakapaza sauti; “Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu”. Walisimama mbali kwa sababu sheria iliwakataza kuwakaribia watu ikisema; “Mwenye ukoma yeyote, atavaa nguo zilizochanika, nywele zake hatazichana, na mdomo wake wa juu ataufunika, na atapaaza sauti akisema; ‘mimi ni najisi, mimi ni najisi.” Ataendelea kuwa najisi kwa muda wote alio na ugonjwa huo. Yeye ni najisi na atakaa nje ya kambi” (Wal 13:45-46). Hawa wakoma walishika vizuizi vya Sheria hii na katika kusisima huko mbali walilia kwa sauti wakiomba; “Ee Yesu, Bwana mkubwa, Uturehemu!” Ni sala yenye imani kuu. Naye Yesu aliwaonea huruma, akawaamuru wakajionyeshe kwa makuhani, ili kutimiza sheria na wapewe kibali cha kuishi tena pamoja na watu wengine (rej. Wal 14:2-7). Nao kwa imani, walianza safari kwenda kwa makuhani, na njiani wakaponywa na kutakasika. Lakini alirudi mmoja tu, msamaria, kuja kushukuru. Kwa nini alirudi peke yake? Kwanza ifahamike kuwa Wasamaria, ni watu wa kabila la Efraimu na Manase, watoto wa Yosefu, wajukuu wa Yakobo, walioishi Samaria, mji mkuu wa ufalme wa kaskazini wa Israeli, nao walichukuliwa kuwa ni najisi, wenye dhambi, wapagani, sio tu kwa sababu walichangamana na kuzaliana na watu wa makabila mengine walioletwa na mfalme wa Ashuru, baada ya wengine kuchukuliwa mateka, bali pia ni uzao wa Yosefu na mke wake Aseneti, Mmisri  Dini yao ilikuwa ni mchanganyiko wa imani na desturi za kiyahudi na kipagani. Wayahudi asili waliporudi utumwani, walichukizwa nao, wakawaona ni waasi, wakawatenga, wakajenga ukuta ili wasiweze kuingia Yerusalemu (rej. 2Waf. 17:24-41; Ezra 4:2-11).

Waamini jifunzeni kuwa na moyo wa imani thabiti na shukrani
Waamini jifunzeni kuwa na moyo wa imani thabiti na shukrani   (ANSA)

Kumbe kilichowaunganisha msamaria mmoja na wayahudi kenda ni tatizo la ugonjwa wa ukoma. Mara nyingi matatizo yanawaunganisha maadui na kuwafanya wasahau tofauti zao. Hivyo wakoma katika ugonjwa wao walisahau tofauti zao za kiyahudi na kisamaria, wakaungana na kujiona wote ni sawa. Tatizo la kuungana katika shida tu, ni kwamba shida ikiisha, tofauti zinarudi. Ndiyo maana baada ya kutakaswa, walijitenga, na msamaria asingeweza kwenda hekaluni kujionesha kwa makuhani kwa sababu ya uadui uliokuwepo, na hawakuruhusiwa kuingia sio tu Hekaluni, bali pia katika mji wa Yerusalemu. Hivyo ilimbidi arudi kwa Kristo Yesu, Hekalu lililo hai. Kwetu sisi tunajifunza pia ubaya wa dhambi ya ubaguzi, chuki na uadui. Tuombe neema za Mungu kamwe tusiingie katika dhambi hizi. Na tukisongwa na matatizo katika maisha kwa pamoja bila kujali tofauti zetu tumkimbilie Yesu na kumwambia; “Yesu Bwana mkubwa uturehemu”. Na tukisha kupokea neema za Mungu, tukiponyaji na kutakaswa, turudi kumshukuru kwa Mungu kwa pamoja kwa zawadi ya mwanae Yesu Kristo anayetuunganisha sote, kwa Ekaristi Takatifu, kifungo cha umoja na mapendo. Tumshukuru Mungu kwa mahitaji ya kimwili kwani kila tulicho nacho ni zawadi kutoka kwake. Na daima tuyakumbuke matendo makuu ya Mungu katika maisha yetu, ili yatufanye tuwe na imani thabiti kwake. Basi tuweke ahadi imara na za kudumu katika imani kwake Mungu iliyosimikwa na Yesu Kristo katika Kanisa Moja Takatifu Katoliki na la Mitume, ili kwayo tuupate uzima wa milele. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, pokea sala za waamini pamoja na dhabihu tunayokutolea, ili kwa ibada hii takatifu tupate kuufikia utukufu wa mbinguni.” Nayo Antifona ya Komunyo inasisitiza tutakavyokuwa ikisema; “Bwana atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo (1Yn. 3:2). Na katika sala baada ya Komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali hivi; “Ee Bwana Mtukufu, sisi unaotulisha Sakramenti ya Mwili na Damu Takatifu, tunakusihi utushirikishe pia umungu wako.”.Na hili ndilo tumaini letu kushirikishwa umungu wa Mungu katika uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D 28
10 Oktoba 2025, 15:41