Tafakari Dominika 29 Mwaka C wa Kanisa: Fumbo la Maisha ya Sala!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 29 MWAKA C, Dominika ya leo inaenda sambamba na wito wa Yesu katika Injili: “kuomba kwa bidii, bila kuchoka” (Lk 18:1) ndiyo msingi wa maisha ya imani na neema. Ujumbe wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 19 Oktoba 2025 unanogeshwa na kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini Kati ya Watu Wote," himizo ni kwa Wakristo wote waliobatizwa kuwa wajumbe wa matumaini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Ujumbe huu unakazia pamoja na mambo mengine kwamba: tumaini si hisia tu bali ni zawadi ya kukumbatiwa na waamini wote, lakini hasa wale walio katika hali ngumu ya umaskini, nyanyaso na dhuluma. Unakazia mshikamano wa Kimataifa, matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lengo ni kupandikiza mbegu ya upendo kwa watu wote, lakini zaidi wale waliotengwa na wanaokabiliana na changamoto mamboleo: uchoyo na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; migogoro na kinzani. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kila mwaka Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya Kimisionari Ulimwenguni, hii ni siku ya sala kwa ajili ya kuwaombea wamisionari walionea sehemu mbalimbali za dunia, ili utume wao uweze kuzaa matunda mengi. Anasema, alipokuwa nchini Perù alihudumu kama: Padre na hatimaye kama Askofu na kwa macho yake alishuhudia jinsi waamini walivyo imarisha imani yao kwa njia ya sala na ukarimu, ulioweza kuleta mabadiliko makubwa kwa watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kutoka Parokia mbalimbali duniani kushiriki kikamilifu kwa hali na mali katika Maadhimisho ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayoadhimishwa Dominika tarehe 19 Oktoba 2025. Mchango wao wa hali na mali ni muhimu sana katika kusaidia mchakato wa kueneza Injili sehemu mbalimbali za dunia, kwa kusaidia kuendeleza katekesi, ujenzi wa Makanisa mapya pamoja na kusaidia kuendeleza huduma za afya, elimu, ustawi na maendeleo kwa watu wa Mungu katika nchi za kimisionari.
UFAFANUZI: Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa ni Mama, Mwalimu na Shule ya Sala. Imani inapyaishwa kwa njia ya sala. Kuna mitindo mbalimbali ya sala inayomwezesha mwamini kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Kuna Sala ya Sauti, Sala Fikara au Tafakari na Taamuli. Katika Katekesi kuhusu Fumbo la Sala, Baba Mtakatifu Francisko alikwisha kupembua kwa kina na mapana kuhusu: umuhimu wa utume wa sala na changamoto zake. Kanisa lina dhamana ya kusali na kufundisha namna ya kusali vizuri zaidi. Kanisa ni shule kuu ya sala. Katika Afrika na ulimwengu kote, wengi wanajaribu kulinda imani na kuendeleza majadiliano ya injili bila kuupa moyo; ni wakati wa kujenga imani hai na yenye nguvu. Musa alitetemeka kwa uchovu wakati wa kulisimamia vita – lakini kwa msaada wa Aharoni na Hur, mikono yake ilishikika hadi alisema “Hata jua litapozama.” aulo anamkumbusha Timotheo umuhimu wa, Kubaki imara katika mafundisho ya Kanisa. Ni swali lakini pia angalizo, ni matashi mema nayo ni matazamio, ni hamu ya Moyo wake Mtakatifu tena ndilo kusudio lake Kristo Bwana, kutoka kina cha upendo wake usioelezeka, kwamba ni muhimu kutunza, kuhifadhi, kulea na kutetea imani tuliyoirithi tangu alfajiri ya Ukristo wetu anapotuuliza sote “… walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, je, ataiona imani duniani? Ndio, kwa hakika ni wajibu wa kila mbatizwa kuthibitisha neno hili ya kwamba Bwana ajapo ataikuta IMANI hai iliyokomazwa na matendo ya utu, maadili, sala, matendo ya huruma na yote ambayo Mungu katika kutuumba anatutarajia tuyafanye ili kufaulu neno hili sharti tujipatie utulivu na usikivu tukijiweka mahali pa Mtakatifu Timotheo na kwa mkao mwema na utayari wa kufundishika tupokee “madini” kutoka kwa Mwalimu wetu Mt. Paulo ya kwamba tukae katika mambo yale tuliyofundishwa na kuhakikishwa tukidumu katika mafundisho ya kuaminika ya Maandiko Matakatifu kwani hayo yana pumzi ya Mungu na kwa hayo kufundisha, kuonya watu makosa yao, kuwaongoza na kuwaadabisha katika haki ili mtu wa Mungu awe kamili… tuyatunze tuliyofundishwa kwa kulihubiri neno wakati ufaao na wakati usiofaa, kukaripia, kukemea na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Tunahitaji neno hili sababu mwanadamu katika mahangaiko yake amevurugika na kutawanyika sana, pamoja na kufundishwa imani na maadili tangu utoto wake, na kushiriki yote yanayohusu malezi kutoka walimu na walezi wengi, si mtulivu kutosha, mbabaifu mwenye kupapasa vingi anavyoviona na kuvisikia na hivi kushindwa kuamua hasa lipi ni lipi... katikati ya magumu hayo Mtakatifu Paulo anatufundisha neno zuri kwamba vyovyote vile iwavyo “Wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa…"
Kuwa watu wa sala na maombi, watoa matumaini kwa wote, na wajumbe wa uaminifu” Neno La Mungu: Ni katika msingi huu tunaweza kusimama na kusimamia watu wengine katika huduma na shuhuda. Tulitendeje neno hili? … tunasafiri jangwani pamoja na Israel kuelekea nchi ya ahadi na mashambulio ya Waamaleki ni makubwa (somo I – Kut 17:8-13)… tumesimama na mwanamke mjane nje ya ofisi ya Kadhi asiyemcha Mungu wala kujali watu tukiililia haki yetu (Injili ya leo – Lk 18:1-8)… kwa ajili ya hayo, na kwa ajili ya amani na nafuu yetu, tunaweza “kukaa katika mambo yale tuliyofundishwa na kuhakikishwa” na hivi kutunza imani hadi mwisho wa nyakati ajapo Mwana wa Adamu kwa kunyoosha mikono yetu pamoja na Musa kwa msaada wa Haruni na Huri (wenzetu.) Tukimililia Mungu mchana na usiku kwa sala isiyoisha, sala isiyokoma itokayo katika chemchemi ya mioyo iliyojaa… sala ya moyo, ya kimya na ya sauti, ya kitabu na ya mshale, ya kuomba na ya kushukuru, ya kuabudu na ya kutukuza, sala ya kusifu na ya toba… tusali tukipiga magoti au tukisujudu, tukiinua juu mikono na vichwa vyetu, kuitandaza au kuifumbata vema vifuani petu, tusali kwa kusihi tukiomba mapenzi ya Mungu na si yetu yatimizwe… tusikate tamaa katika kumuomba, kumuamini na kumtumaini Mungu… tusaidiane kusali tukiomba pia kwa ajili ya wenzetu wanaohitaji sala zetu nyofu, changa na dhaifu ili kwa njia ya sala hizo Mwenyezi Mungu audhihirishe utukufu wake. Sala yetu inogeshwe na imani, katika kusali tuonje muungano na Mungu… katika sala tunaviringishwa na pendo lake kuu tukimpokea kama Yeye anavyotupokea sisi hivi tulivyo… vile tunasali kwa imani ndivyo sala yetu inavyojipatia uzito mbele ya Kiti cha enzi, tusali tukiamini, tuamini tukisali… sala imo katika imani vile rangi ilivyo kwa ua… tusaidiane kuomba na kuomba kwetu hakutaenda bure. Hata hivyo sala yetu iwe ya kweli, itiririke kutoka moyo mnyofu ikiinua roho ya mwana na binti huyu kwa Mungu na kutoka huko kupokea faraja na amani ipitayo faraja yote… si vema kusali wakati upo katika ugomvi na yeyote, au na kinyongo, au katika hali ya manung’uniko, au katika hali ya dhambi, au katika kutawanya mawazo… Padre , Jalimu na mlezi Antony Kolencherry akilitafakari Neno la Mungu Dominika hii anasimulia kisa cha mtu aliyeota ndoto amechukuliwa na malaika hadi Kanisani Jumapili fulani. Kanisani akamuona Mpiga Kinanda akipiga kwa mbwembwe nyingi lakini hakukuwa na sauti iliyotoka, akawaona na wanakwaya na waamini wote wakiimba na kucheza kwa nguvu kubwa lakini haukusikika muziki wowote, hata midomo ya Padre ilionekana ikiongea lakini hakikusikika chochote!
Tuombe kwa imani, ndugu zetu tuiminie, na tueneze injili bila kuchoka. Yesu anauliza: “Je, atakupata imani duniani?”, na sasa ndio fursa yetu kujibu. Neno la Mungu lina nguvu kubadilisha mioyo na kuhakikisha maono ya Jubilee. Umisionari wetu unahitaji ustahimilivu: kuhakikisha imani inaendelea, injili inaendelea kusikika – bila kujali hali. Katika muktadha wa Jubilee ya Matumaini, Kanisa lina wito kuwa “wajumbe wa Neno” wanaoendana na kazi ya Yesu: upendo unaoendelea, nguvu inayoongezeka, na afya ya roho. Kwa mshangao mkubwa alimgeukia Malaika wake na kumuuliza “unasikia chochote?” malaika akamjibu “wala!” Malaika akaendelea kusema “Upo sawa, hakuna kinachosikika ndani ya kanisa amabapo adhimisho la Ekaristi Takatifu linafanyika sababu wahusika wote, kuanzia Padre pale juu, kinanda na ngoma, wanakwaya na waamini wote hawapo katika kuabudu katika kweli bali wapo katika utaratibu tu wa kuabudu, mioyo yao haijaguswa, roho zao zi baridi na ukimya huu unaoushuhudia ni ukimya ambao bado kuondolewa na Mungu… ndio kusema Sala yetu ili iwe ya kweli na halisi sharti iuguse Moyo wa Mwenyezi, si huduma ya mdomo tu bali yawe ni mazungumzano ya moyo wako na Moyo wa Mungu… sasa basi, leo na siku zote, sala yako na imuelekee Mungu Baba, katika Roho Mtakatifu kwa njia ya Kristo Bwana wetu, amina… Basi ndugu zangu, kwa kuomba na kufunga, katika roho na katika kweli “tukae katika mambo yale tuliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana tunajua ni akina nani ambao tulijifunza kwao” (2Tim 3:14) kwa sifa na utukufu wa Mungu. “Ee Mungu Mpendo, utuonyeshe umuhimu wa maombi yasiyokata tamaa, utupe utulivu kati ya giza, ufanikishwe kupitia Neno lako, tufanye kazi bila kuchoka – kuwa vigumu vya matumaini katika watu waliovunjika. Amina.