Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa inatutafakarisha sisi sote kama Mahujaji wa Matumaini juu ya, “NGUVU YA SALA” Kwa nini tunasali na jinsi gani tunapaswa sisi kama wakristo kusali. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa inatutafakarisha sisi sote kama Mahujaji wa Matumaini juu ya, “NGUVU YA SALA” Kwa nini tunasali na jinsi gani tunapaswa sisi kama wakristo kusali.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika ya 29 Mwaka C wa Kanisa: Nguvu ya Sala katika Maisha

Ujumbe waPapa Francisko katika maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 19 Oktoba 2025 unanogeshwa na kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini Kati ya Watu Wote," himizo ni kwa Wakristo wote waliobatizwa kuwa wajumbe wa matumaini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 wanakumbushwa kwamba: tumaini ni zawadi; ujumbe unakazia mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa matendo; kiroho na kimwili.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 29 ya mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha sisi sote kama Mahujaji wa Matumaini juu ya, “NGUVU YA SALA” Kwa nini tunasali na jinsi gani tunapaswa sisi kama wakristo kusali. Katika Dominika hii, tumwombe Roho Mtakatifu atusaidie ili tuweze kufahamu namna itupasavyo kuomba, kama anavyotufundisha Mtume Paulo, kwamba, “Roho hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kama ipasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rum 8:26). Ujumbe wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni, tarehe 19 Oktoba 2025 unanogeshwa na kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini Kati ya Watu Wote," himizo ni kwa Wakristo wote waliobatizwa kuwa wajumbe wa matumaini katika Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Ujumbe huu unakazia pamoja na mambo mengine kwamba: tumaini si hisia tu bali ni zawadi ya kukumbatiwa na waamini wote, lakini hasa wale walio katika hali ngumu ya umaskini, nyanyaso na dhuluma. Unakazia mshikamano wa Kimataifa, matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Lengo ni kupandikiza mbegu ya upendo kwa watu wote, lakini zaidi wale waliotengwa na wanaokabiliana na changamoto mamboleo: uchoyo na ubinafsi, uchu wa mali na madaraka; migogoro na kinzani.

Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni, 19 Oktoba 2025
Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni, 19 Oktoba 2025   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake anasema, katika Dominika hii kila mwaka, Kanisa zima linaungana katika kusali kuombea Wamisionari na matunda ya kazi yao ya kitume wanayoifanya kwa nguvu na majitoleo makubwa ulimwenguni kote. Anaeleza uzoefu wake akiwa Padre na baadaye Askofu Mmisionari huko Peru katika Amerika ya Kusini, jinsi sala na matendo ya huruma yanayofanyika katika Dominika hii yanavyochangia kuleta mabadiliko makubwa katika kazi ya Uinjilishaji. Sala na michango mbalimbali imechangia kwa kiasi kikubwa katika programu mbalimbali za Katekesi, Ujenzi wa Makanisa na huduma za kijamii kama vile, Elimu, Afya, majanga ya asili na misaada kwa maskini. Hivyo anaomba Parokia Katoliki Ulimwenguni kote kushiriki kwa hali na mali katika kazi hii ya Umisionari, kumpeleka Kristo tumaini letu kati ya watu, tukitambua kuwa kila mbatizwa ni Mmisionari wa Matumaini.

Nguvu ya Sala katika maisha ya mwanadamu
Nguvu ya Sala katika maisha ya mwanadamu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la 1: Ni kitabu cha Kutoka 17:8-13. Somo la kwanza kutoka kitabu hiki cha kutoka latueleza juu ya Nguvu ya Sala.  Somo hili ni simulizi la vita ya kwanza kabisa katika historia ya wana wa Israeli baada ya kutoka utumwani Misri dhidi ya Waamaleki huko Refidimu, wakiwa safarini kuelekeea katika Nchi ya Ahadi. Kabila la Amaleki walikua hodari na walifahamika katika vita, waliogopwa kwa kuwa walivamia na kuteka makabila mengine, au wale waliopita katika nchi yao iliyokua karibu ya Bahari Nyekundu, huko jangwani, kusini mwa Nchi ya Kaanani. Musa akitambua kuwa Mungu alikua katikati yao, Mungu alikuwa Msaada na kimbilio lao, aliyewapigania tangu mwanzo wa safari yao kule Misri, aliyewavusha katika Bahari ya Shamu, aliyewalisha kwa Manna na kuwapa maji, hata sasa atawapigania. Hata sasa atawashindia. Hivyo anamwambia Joshua achague watu ili wakapigane na Waamaleki, wakati huo akiwa na hakika ya kuwa Mungu atawapigania. Hivyo akachukua ile fimbo ya Mungu, ishara ya uwepo wa nguvu ya Mungu kati yao, na anakwenda katika kilele, anakwenda kusali. Alipoinua mkono wake, Israeli alishinda na aliposhusha mkono wake kwa sababu ya uchovu, Amaleki alishinda. Akisaidiwa na Haruni na Huri ambao waliitegemeza mikono yake iliyoishiwa nguvu, Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa upanga. Baada ya kushinda vita hii, Musa alimjengea Bwana madhabahu akaiita, Yehova Nissi, yaani Bwana ni bendera yangu ya ushindi. Wimbo wa Katikati: Ni Zaburi ya 121: Zaburi ya 121 ni moja kati ya Zaburi zinazojulikana kama, “Songs of the Ascents” yaani, “Nyimbo za kupanda kuelekea Hekaluni Yerusalemu Wayahudi walikua na desturi kila mwaka kupanda kuelekea mjini Yerusalemu Hekaluni, kwa ajili ya maadhimisho ya sherehe kubwa za dini yao. Haikua safari rahisi hata kidogo, ilikua ni ndefu, kwenye njia mbaya na hatari za kila namna njiani.  Akitambua hilo, Mzaburi anasali sala hii muhimu, Nitayainua macho yangu niitazame milima, msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana aliyezifanya Mbingu na nchi. Kutazama milima ilimaanisha, kutazama Yerusalemu lilipokua Hekalu, alimokua Mungu, lakini pia ni kuinua macho na moyo kwa imani kutazama mbinguni alipo Mungu, ulipo msaada na tumaini letu la kweli na la daima.

Udumifu katika sala ni jambo muhimu sana
Udumifu katika sala ni jambo muhimu sana   (Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili ya Lk. 18:1-8: Katika somo la Injili Takatifu Kristo anatufundisha namna tunavyopaswa kusali, kusali na kuomba siku zote bila kuchoka. Anatoa mfano wa kadhi dhalimu na mwanamke mjane, aliyedai haki yake na adui yake. Mwanamke huyu mjane anawakilisha maskini, mdogo na mnyonge ambaye hana chochote isipokua Imani thabiti na uvumilivu katika kuomba haki yake. Mwanamke huyu alidumu daima katika kudai haki yake, kwa Imani na msisitizo (persistence), hakukata tamaa, hakuchoka, ijapokua kadhi alikataa. Kadhi huyu mwishoni anasema, ijapokua simchi Mungu, wala sijali watu, lakini kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha na kunijia daima. Kristo anatuhakikishia, kama kadhi huyu mwovu alitoa haki kwa mjane yule, ni wazi kwamba Baba yetu wa mbinguni, aliye mwema hawezi kutunyima lolote tumwombalo, iwapo tunamwomba kwa Imani thabiti na ustahimilivu. Ndugu zangu katika Masomo haya mawili tuna mafundisho matano ya kujifunza: Kwanza: Katika safari yetu ya maisha tunakutana na vita vingi. Katika somo la kwanza tumesikia, Taifa la Israeli wakiwa katika safari yao kuelekea nchi ya Ahadi wanakutana na vita dhidi yao na Waamaleki, na bado watakutana na vita vingine vingi huko mbeleni. Katika maandiko Matakatifu, Amalek inawakilisha mambo yote, au nguvu zinazowashambulia taifa la Mungu, hususani pale wanapokuwa dhaifu au wanapochoka. Kumbe vita hivi dhidi ya Amaleki na taifa la Mungu ni vita vyetu, sisi mahujaji, sisi taifa jipya la Mungu tulio safarini kuelekea katika Nchi yetu ya Ahadi, yaani mbinguni.

Kila mtu katika maisha ana vita na mpambano ya kiroho
Kila mtu katika maisha ana vita na mpambano ya kiroho   (AFP or licensors)

Ndugu mpendwa, katika maisha yetu ya kila siku kila mmoja ana vita vyake. Kuna mambo mengi tunakutana nayo yanayotutita hofu na mashaka, yanayotukatisha tamaa, yanayotuangusha chini, yanayotupotezea matumaini. Huenda ni familia imekua ngumu kuendesha, malezi yamekua na changamoto kwa Watoto wetu, huenda ni utume umekua mgumu kufanyika, huenda ni biashara haziheleweki, ni Masomo hayasomeki, mahusiano yanayumba yumba, familia haina amani, moyo umejaa, sioni njia mbele, sioni tumaini tena mbele, Imani yangu inajaribiwa, napita katika tanuru ya moto. Kila mmoja ana vita vyake, katika safari yake ya maisha. Tunakutana na Amalek katika nyakati mbalimbali za maisha. Huenda kuna watu pia wameshiriki kuwa Amalek, kutusababishia hofu na mashaka, kutukatisha tamaa, kusababisha huzuni na kuviongeza maradufu vita vyangu. Katika hayo yote usiogope. Mwenyezi Mungu atakupigania. Pili: Sio kila vita tunaweza kupigana na kushinda, tunahitaji msaada wa Mungu. Musa anapoiona hatari ya vita, anatambua mara namna Mungu alivyowapigania, tangu alipowatoa utumwani Misri, alivyowavusha katika Bahari ya Shamu, alivyowalisha kwa mana na hata sasa ana Imani kua atawapigania. Alijua ya kuwa sio kila vita waliweza kushinda kwa nguvu ya upanga, bali walipaswa kumtegemea Mungu aliyewatendea mambo makubwa mengi katika safari yao. Hivyo anakwenda mlimani kusali na hapo Mwenyezi Mungu akawasaidia wakashinda vita ile.

Bikira Maria Atufundishe namna bora zaidi ya kusali.
Bikira Maria Atufundishe namna bora zaidi ya kusali.   (@Vatican Media)

Ndugu mpendwa kama nilivyotangulia kusema, kila mmoja wetu ana vita vyake katika safari yake ya maisha ambavyo anapambana navyo kila siku ya maisha yake. Vita vyangu sio vyako, wala vyako sio vya yule. Katika hali hiyo tunapaswa kutambua kuwa sio kila vita tunaweza kupigana kwa nguvu na uwezo wetu wenyewe. Lazima tukubali kama Musa kupanda mlimani na kupiga magoti, kuinua moyo, mikono na macho yetu kutazama mbinguni na kuomba msaada wa Mungu. Kukumbuka na kushukuru pia namna Mungu alivyotupigania katika nyakati mbalimbali za maisha yetu hata sasa na kumwambia Mungu asante, ninakuomba Mungu usimame na unipiganie tena katika hili. Mungu naomba usimame na familia yangu, simama na ndoa yangu, simama na Watoto wangu, simama na biashara yangu. Inua macho yako, tazama milimani, weka nia na matamanio ya moyo wako mikononi mwa Mungu, weka hofu na mashaka yako mikoni mwa Mungu, weka kesho yako usiyoijua mikononi mwa Mungu na kwa Imani sema kama mzaburi kwamba, Mungu wewe ni Mungu ambaye husinzii wala hulali, Bwana hutaniacha kamwe niabike, Bwana nakuomba unikumbuke katika ombi langu hili, katika vita vyangu hivi Bwana simama nami. Msaada wangu u katika wewe ulizifanya mbingu na nchi. Sema na Mungu katika sala, ndani ya moyo, katika ukimya.

Kanisa ni Mwalimu wa sala
Kanisa ni Mwalimu wa sala   (AFP or licensors)

Tatu: Imani thabiti na tumaini lisilotetereka ni muhimu sana katika kusali kwetu. Usishushe mikono yako. Musa alikwenda mlimani kusali wakati Joshua alipokuwa akiongoza mapigano dhidi ya Waamaleki. Musa alipoinua mkono wake Israeli alishinda, na aliposhusha mkono wake kwa sababu ya uchovu na udhaifu Amaleki alishinda. Kumbe ushindi ulipatikana tu pale alipoinua mikono yake kusali. Mwanamke mjane hali kadhalika, aliendelea kudai haki yake ijapokuwa kadhi dhalimu alimkatalia. Hakukata tamaa, hakupoteza matumaini. Kristo anatuhakikishia ya kwamba, kama kadhi huyu mwovu alitoa haki, je Mungu aliye Mwema hatawapatia haki yake wateule wake wanaomlilia usiku na mchana naye ni mvumilivu kwao? Ndugu mpendwa, ili tushinde katika vita mbali mbali tunavyokutana navyo, ili Mwenyezi Mungu atujibu katika nia zetu mbalimbali kila tunapomwomba, tunahitaji Imani thabiti na tumaini lisilotetereka. Tunapaswa daima kuinua mikono yetu, kuinua mioyo na macho yetu kwa Mungu, bila kuchoka. Ni kweli kutokana na changamoto mbalimbali tunazokutana nazo kuna wakati tunachoka, pengine tumesali lakini hatuoni kama Mungu anafanya kitu katika yale tunayomwomba, kuna wakati tunaona kama Mungu ametuacha hivi. Kuna nyakati tunaweza kuona kama Mungu ana upendeleo, kwamba huenda Mungu pengine anawajibu wengine na mimi ananisahau, katika maradhi yangu, katika changamoto zangu, katika maombi yangu. Kumbe, kuna nyakati pengine tunaishiwa nguvu, kuna nyakati tunapoteza Imani na kuanza kusita juu ya utendaji kazi wa Mungu katika kujibu sala zetu. Tunaacha kutazama juu na kuanza kutazama kama Mungu amewajibu majirani zangu, au kama Mungu amewajibu hata watesi wangu, tunapoteza focus, tunashusha macho, tunashusha moyo, tunashusha mikono, matokeo yake ni kushindwa katika vita vyetu, tunashindwa kusali vyema. Katika yote, inua macho yako, usipoteze lengo la sala na maombi yako, kama yule mama Mjane katika somo la Injili ambaye alirudi kila mara kwa yule kadhi dhalimu kuomba ampe haki yake, na kisha akajibiwa sala yake. 

Tunahitajiana ili kukamilishana katika maisha ya sala
Tunahitajiana ili kukamilishana katika maisha ya sala   (AFP or licensors)

Nne: Tunahitaji msaada sala za wengine, tunawahitaji wengine watushikilie mikono tunapochoka. Musa baada ya kuinua mikono kwa muda mrefu alichoka, aliishiwa nguvu na hivyo akashusha mikono. Ni hapo Haroni na Huri walipomsaidia kwa kuitegemeza mikono yake, mmoja upande huu na mmoja upande huu, mikono yake ikathibitika hata jua lilipokuchwa, na Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa uali wa upanga. Msaada wa Haroni na Huri ulimpa Musa nguvu ya kuinua mikono tena juu. Sala zetu hazipaswi kuwa za kichoyo bali ziguse pia na mahitaji ya wengine, na hapo Mungu atatujibu nasi pia. Ndugu mpendwa, nilipokua natafakari somo hili nilimkumbuka marehemu mama yangu ambaye wakati nikiwa mseminari, kila mara nilipopata nafasi ya kumpigia simu na kuzungumza naye, hata siku aliyofariki, licha ya kuwa katika maumivu na ugonjwa, hakuacha kamwe kuniambia, “Ninakuombea Mungu mwanangu ufanikiwe katika yote huko”  Maneno haya yalikua yananipa nguvu, kwamba kumbe kuna nyakati nilikwisha kata tamaa, kuna nyakati nilishapoteza matumaini lakini huku nyuma alikuwepo mama aliyeniinua mikono, wakati nilipopigwa na changamoto mbalimbali katika safari yangu, hata nikawa dhaifu, nikaishiwa nguvu. Nina Imani kila mmoja wetu, ana watu wengi nyuma yake wanaomwinua, wapo watu wanaotuombea kila siku japo hawatuambii. Wapo watu ambao katika sala zao hawaachi kututaja, kwamba Mungu, naomba uwakumbuke na hawa. Huenda tupo hapa tulipo, huenda tulishinda nyakati mbalimbali kwa kuwa kuna watu walitushika mkono huku na huku ili tusipoteze Imani na matumaini. Tupo hivi leo kwa kuwa kuna watu walibaki katika magoti kutuombea pale tulipokua chini mavumbini. Katika sala zetu pia tusali kuwaombea wengine, huenda ninasema nawe ambaye hata sasa umechoka na huna nguvu tena ya kuendelea kuinua mikono, Mtume Paulo anatupa moyo kwamba, tunaye Roho Mtakatifu anatusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba kama ipasavyo. Lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa” (Rum 8:26).

Fumbo la Maisha ya Sala: Tuombeane
Fumbo la Maisha ya Sala: Tuombeane   (@Vatican Media)

Tano: Tunahitaji nasi ushiriki wetu ili Mungu atimize kusudio lake kwetu kupitia sala zetu. Musa hakuwashinda Waamaleki kwa nguvu ya sala pekee, bali alimwagiza Yoshua kuchagua watu na kutoka kwenda kupigana vita. Na hapo Mungu akawasaidia kushinda vita. Ushiriki wetu ni pamoja na Imani na ustahimilivu kama nilivyokwisha eleza. Na hapo Kristo anatuuliza swali mwishoni kabisa mwa Injili ya leo kwamba, walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, je ataiona Imani duniani? Ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu anahitaji Utayari na ushiriki wetu ili atimize hadi zake kwetu. Anatuhitaji nasi pia kufanya kitu ili sala yetu izae matunda. Kwa mfano, kama ninamwomba Mungu anisaidie kufaulu mtihani, ni kweli ana uwezo wa kunisaidia kwa kuwa yeye ni Mungu, lakini kama nisipojituma katika kusoma kwa bidii, kushirikiana na Mungu roho Mtakatifu aliyenipa mapaji yake mbalimbali, ni wazi nifeli katika mtihani vibaya sana. Hali kadhalika, ikiwa ninaumwa, nikaacha kwenda hospitali na kusema, Mwenyezi Mungu ataniponya, Mungu aliyeweka nguvu yake ya uponyaji kupitia kwa madaktari, wauguzi na dawa mbalimbali.

Tafakari D 29
18 Oktoba 2025, 12:55