Britain's King Charles and Queen Camilla on state visit to Vatican

Tafakari Dominika 30 Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu,Toba na Imani Thabiti

Ujumbe wa dominika ya thelathini ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa na masomo yake unatuleta kujikita kutafakati ujumbe mzito na wa kina kuhusu unyenyekevu, toba ya kweli na imani isiyotafuta sifa,hasa tunapoendelea na kusafiri kama mahujaji wa matumaini Jubilei ya Matumaini mwaka huu.Jubilei ya Matumaini ni mwaliko wa kurudi kwa Mungu kwa unyenyekevu,kutubu na kuishi kwa imani hai katika dunia iliyojaa giza,kiburi na kukata tamaa.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya 30 MWAKA C, Ujumbe wa dominika hii na masomo yake unatuleta kujikita kutafakati  ujumbe mzito na wa kina kuhusu unyenyekevu, toba ya kweli, na imani isiyotafuta sifa, hasa tunapoendelea na kusafiri kama mahujaji wa matumaini Jubilei ya Matumaini mwaka huu. Jubilei ya Matumaini ni mwaliko wa kurudi kwa Mungu kwa unyenyekevu, kutubu, na kuishi kwa imani hai katika dunia iliyojaa giza, kiburi na kukata tamaa. Mwezi Oktoba unakimbia sana, tunasali Rozari na kutafakari muhtasari wa injili ya wokovu pamoja na Mama Maria au tunafanya kama ratiba? Tusiache, japo fungu moja kwa siku! Neno la Kristo leo linakuja na uzani wa juu wa kimapinduzi kwamba tunapaswa kuwaje tuwapo mbele za Mungu kwa vile Yeye huitazama mioyo kwa macho tofauti na yetu hivi kwamba wale tunaowadharau na kuwaona si chochote kiroho, kijamii na hata kiuchumi, watu wasio haki, wanaweza kupata kibali mbele zake huku wale tunaowaheshimu na kuwanyenyekea mara si haba hukosa mastahili Masomo ya leo yanaleta ujumbe wa pamoja Mungu huwa upande wa mnyonge, wa yule  mwenye toba, na anayethamini neema za Mungu kuliko kuijona una haki na kujikweza. Tunaitwa kutubu na kuacha kiburi, kama yule Farisayo. 

Sala inasimikwa katika unyenyekevu, toba na imani thabiti
Sala inasimikwa katika unyenyekevu, toba na imani thabiti   (@Vatican Media)

Kuishi kwa imani ya kweli hadi mwisho, kama Paulo. Kuwa na mioyo safi na nyenyekevu, kama Daudi alivyotubu. Kuamini kuwa Mungu hasikii watu wa nguvu tu, bali maskini wa moyo na roho. ‘Ee Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi’ ni sala ya mtoza ushuru, mtu aliyeona hitaji la huruma na msamaha akimtazama Mungu kama Baba mwema yeye akiwa mtoto, ni sala inayomfanya mmoja ajiachie mikononi mwa Baba yake na hapo kujipatia amani na salama, ni sala inayomuonyesha mtu asiye na mengi, kwake pendo la Mungu wake linatosha na kuzidi… ni sala ya toba, kilele cha kujishusha na shule ya unyenyekevu… ni sala iliyofungasha dhabihu bora kwa Bwana “sadaka yangu kwako Ee Mungu ni moyo mnyofu na uliopondeka, wewe wapendezwa na kweli ya moyo...” (Zab 51:17), hakika kwa unyenyekevu wetu tutaziponya nafsi zetu… Ee Mungu utujalie moyo wa mtoza ushuru huyu tushuke nyumbani kwetu tumehesabiwa haki (aya 14a).

Mwenye unyenyekevu ataonewa huruma na kusamehewa
Mwenye unyenyekevu ataonewa huruma na kusamehewa   (ANSA)

UFAFANUZI: Mpendwa sikilizaji na msomaji, masomo ya leo yanatufundisha kuwa Mungu anasikia sala ya mnyonge, wala hahukumu kwa sura. Katika dunia yenye kiburi, ubinafsi, na kujisifu hata kwa dini, tunaitwa kuwa kama mtoza ushuru: watu wa unyenyekevu na toba ya kweli. Kama mzazi angeulizwa nyakati za Kristo ‘ungependa mwanao awe nani?’ jawabu daima lingekuwa ‘mfarisayo!’ sababu ya nafasi ya watu hawa kwa jamii… walisifika kwa muonekano wao na mavazi yao mazuri na marefu, misimamo, elimu, washika sheria, watu wa sala na mifungo, wakali kwa wakosaji wakiamini kwa moyo mmoja ufufuo wa wafu... Pamoja na sifa zote hizi sala ya farisayo wa leo haipati kibali cha Mungu kwa vile amesali kwa kiburi. Tazama kwa makini mkristo mwenzangu, hatwendi mbele za Mungu kuripoti mafanikio yetu, hatwendi kwenye Misa takatifu kumwambia Mungu jinsi tulivyo wakubwa, na zaidi sana hatwendi Kanisani ili kuwasema wadhambi, kuorodhesha makosa yao na kutoa hukumu… hivi pamoja na mema yote ya mfarisayo yule kiburi chake kilimwangusha na kumweka mbali na Mungu sababu kiburi ndiye mama ya mizizi yote ya dhambi, chanzo cha vingi vibaya… Kiburi ni adui mkuu ya utakatifu, kinashusha unyenyekevu na kupandisha dhahama… kwa kiburi mmoja atadharau wengine, atawahukumu, atawatazama kwa chini… lugha yake, sauti yake, majibu yake, mkao wake na kila kitu chake hukosa jotojoto na uvuguvugu wa kibinadamu.[ Photo Embed: Liturujia Neno la Mungu Dominika 3o: Unyenyekevu, toba na imani thabiti]

Mtume Paulo anatufundisha kuwa maisha ya imani ni mapambano, na tutazawadiwa taji la haki tukidumu hadi mwisho. Katika Jubilei ya Matumaini, tuache kujiona bora kuliko wengine, tuishi kwa toba, huruma, na upendo. Kwa hiyo, tujiulize. Dalili za kiburi ni pamoja na kujiona peke yako ndiye mwenye akili, peke yako upo sahihi, peke yako unajua yote, wengine wake pale wasubiri… Watakatifu wote wamafaulu kumfikia Mungu kwa kuuishi unyenyekevu, tuanze leo kuishi kawaida na kwa kuwajibika. Maisha ya mkristo ni mapambano ya kila siku, dhidi ya tamaa, dhambi, hali ngumu, dhuluma, vishawishi, hata upweke. Lakini Paulo anatufundisha imani ikidumishwa hadi mwisho, tunazawadiwa taji la haki. Hata kama dunia inatusahau au kutudharau, Mungu anatufahamu kuanzia mwazo wetu na mwisho wetu.

Mwenyezi Mungu anapendezwa na mioyo minyofu
Mwenyezi Mungu anapendezwa na mioyo minyofu   (@Vatican Media)

Katika Injili, Yesu anatupatia mfano wa watu wawili wanaosali, Farisayo: anajisifu mbele za Mungu, anajilinganisha na wengine, Mtoza ushuru: anapiga kifua kwa huzuni, anasema: “Ee Mungu nihurumie mimi mwenye dhambi.” Yesu anashangaza – anasema mtoza ushuru ndiye alirudi nyumbani akiwa amepewa haki mbele za Mungu. Inawezekana tunamuhukumu sana mfarisayo wa leo, na hivi kuingia katika mtego uleule… Yeye amesali sala ya kujisifu mbele za Mungu na kumuhukumu mwenzake, sisi pia huenda tunafanana naye kwa namna mbalimbali… kila mmoja anao ufarisayo fulani ndani mwake... Hatujawa wakweli, wanafiki kwa mengi, tunasifiana kwa uongo, mafuta kwa mgono wa chupa kwa maslahi tunayoyawania kimwili, kijamii, kiuchumi na kisiasa, tumekuwa na kiburi kwa mafanikio kidogo tu tuliyojaliwa, fedha kidogo hata majina yetu yanabadilika, huduma yetu imeambatana na gharama kubwa, hatupatikani, tumekuwa watu wa visingizio vingi… mmoja amesema 'siku hizi sifiki Kanisani kwa sababu kuna wanafiki wengi sana' hapa wenzake wanashawishika kumwambia 'uje tu sababu bado kuna nafasi ya mnafiki mmoja'...  Katika haya na mengine tuiname na kujipiga vifuani tukisema na mtoza ushuru “Ee Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi.” “Ee Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi’… hasa dhambi ya kupungukiwa mapendo na kushindwa kutimiza wajibu zangu vile inavyopasa, dhambi ya kuhukumu wenzangu na kuwaumiza, dhambi ya kujiona mimi ni bora kuliko yeyote, dhambi ya kushindwa kuona mema ya wenzangu, dhambi ya kuwaharibia na kuwachafulia majina yao… unipe moyo wa hekima nipambanue mema na mabaya.

Unyenyekevu, toba na ushuhuda wa imani thabiti ni muhimu
Unyenyekevu, toba na ushuhuda wa imani thabiti ni muhimu   (@Vatican Media)

Kwa vile hakuna mtu anayeweza kukufikia isipokuwa kwa unyenyekevu kamili, unyenyekevu ule wa Mwanao Kristo uliomfikisha kwenye utii wa kifo cha Msalaba (Filp 2:8), nisisahau hata mara moja kuwa njia ya kupanda juu ni kwa kushuka chini… nijalie niwe na jina jema mbele zako na mbele ya wenzangu tena niwasaidie wawe safi siku zote. Kwa sababu mmoja anapopoteza fedha au mali hapotezi chochote, akipoteza afya ya mwili kwa homa hupoteza kitu, lakini apotezapo jina jema hupoteza vyote… Hekima ya mzee Sira katika somo I (35:12-14, 16-19) inatuasa kusali sala ya unyenyekevu sababu sala hiyo hupenya mawingu tena haitulii hata itakapowasili, haiondoki hata Aliye juu atakapoiangalia. Katika dunia ya leo, Mungu anawaangalia watu wenye unyenyekevu wa moyo, walio tayari kukiri makosa yao, walio tayari kubadilika, na si wale wanaojiona bora au kujigamba kwa wema wao. Katika Jubilei ya Matumaini, Tunaitwa kutubu kwa dhati, si kwa maneno tu. Tunaitwa kuwa sauti ya wanyonge, si kuwaziba midomo. Tunaitwa kuishi kwa imani ya kweli, si ya kujionyesha. Tunaitwa kujenga jamii yenye haki, inayotazama moyo wa mtu, si sura yake. MASWALI YA KUJIULIZA: Je, mimi ni kama Farisayo, najiona bora kuliko wengine? Je, nawaombea na kuwatetea wanyonge – au nawapuuza? Je, ninafanya wajibu wangu kwa uaminifu, au natafuta sifa? Je, maisha yangu yanaonyesha matumaini, au ni ya kukata tamaa? Ee Mungu, tupe moyo safi, utuondolee kiburi, utufundishe kutubu kwa kweli. Katika dunia hii iliyojaa kelele za ubinafsi na vita, tufanye sisi kuwa mashahidi wa matumaini, watu wa haki na unyenyekevu. Tuombee Jumuiya zetu, ili tuwe wanyenyekevu kama yule mtoza ushuru, na tuishi kwa imani kama Paulo. Amina.

Tafakari ya Dominika Oktoba 26,2025.
23 Oktoba 2025, 15:35