Injili ya Dominika ya  XXXII mwaka 'C':Fumbo la kifo na ufufuko ni gumu na wengi tunajiuliza nini kitatokea baada ya kifo chetu? Injili ya Dominika ya XXXII mwaka 'C':Fumbo la kifo na ufufuko ni gumu na wengi tunajiuliza nini kitatokea baada ya kifo chetu?  

Dominika ya XXXII mwaka C:Mungu si Mungu wa wafu,bali wa walio hai

Ee Bwana,Mungu wa walio hai,tupe moyo wa uthabiti kama wa vijana wa Mmakabayo.Tuimarishe katika kazi njema,utuongoze kwenye uvumilivu wa Kristo,na utujalie kuishi maisha haya kwa macho ya matumaini ya milele. Ee Mungu wa walio hai, tukusikie katika sala hizi.Tufanye kuwa watu wa matumaini,tukimtazamia mwanao Yesu Kristo aliyefufuka na kutushindia kifo.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 32 MWAKA C Katika kuelekea kilele cha Jubilei ya Matumaini, na kuhitimisha mwaka mwaka wa litirujia mwaka C Kanisa linatualika kuishi kama watu wa tumaini. Katika Dominika hii ya 32 ya mwaka C, masomo yetu yanatufunulia uzito wa imani katika uzima wa milele, uthabiti katika majaribu, na matumaini yasiyotetereka hata katikati ya mateso. Haya yote yanaangazia kiini cha Jubilei ya Matumaini – kwamba Mungu bado anatembea nasi, na maisha yetu yana thamani ya milele.

Kristo Bwana anajibu swali la ufufuko wa wafu alililoulizwa na Masadukayo wakitumia mfano wa kubuni wa waume saba na mke mmoja. Masadukayo walikuwa ni watu gani na wenye msimamo au itikadi gani? hili lilikuwa ni kundi moja miongoni mwa vikundi vingi ndani ya jamii ya waisraeli, asili yao ni Kuhani Mkuu Sadoki (ndio maana wanaitwa masadukayo), walijumuisha koo za makuhani na za watu maarufu kisiasa na kiuchumi, Masadukayo walishika hatamu ya uongozi wa Israel tangu mwaka 142KK… walimiliki sehemu kubwa ya ardhi hivyo uchumi mkubwa na pia walimiliki Hekalu… kidini, Masadukayo walivitambua vitabu vya Musa tu kama mwongozo wao… walikataa kupokea maelezo ya Torati yaliyofanywa na wazee… aidha walikataa kupokea imani juu ya ufufuko wa wafu, maisha ya roho baada ya kifo, uwepo wa Malaika na Pepo wabaya… Masadukayo walikuwa wahusika wakuu katika kumtia Yesu nguvuni na hatima ya maisha yake. Waliendelea kuwa wapinzani wakubwa wa Mitume baada ya ufufuko wa Kristu (Mdo 4.1-7, 5:17-33).

Vijana saba wa Kiyahudi pamoja na mama yao, waliamua kupoteza maisha yao badala ya kuvunja sheria ya Mungu. Waliamini kuwa, “Mungu atatufufua tena na kutupa uzima wa milele.” Katika somo I (2Mak 7:1-2, 9-14) na Injili (Lk 20:27-38) tunaelezwa juu ya maisha baada ya kifo. Fumbo la kifo na ufufuko ni gumu na wengi tunajiuliza nini kitatokea baada ya kifo chetu? Masadukayo nao wakiwa katika hali ya kutoamini na kutokubali, wanamuhoji Kristo juu ya jambo hilo, ‘Je, katika ufufuo mke yule atakuwa wa nani kati ya wale saba?’ Yesu huenda alicheka kwanza na wote waliokuwepo juu ya swali hili, halafu akamsifu mama huyo kuwa na afya njema na nguvu ya kuolewa na watu 7 tena kuanzia mzee kutelemka kwa vijana na kuwa wa mwisho kufa… mimi pengine nisingejibu swali kama hilo… Yesu anajiweka vema na kulijibu ipasavyo kwa uhalisia wake wote.

UFAFANUZI

Katika dunia ya leo yenye giza la vita, mateso, dhuluma, ukandamizaji wa haki, watu wengi wanakufa wakiwa waaminifu kwa dhamiri zao.Hawa vijana ni mashujaa wa matumaini. Hawakuogopa kifo, kwa sababu waliamini kuwa mwisho wa mwili si mwisho wa maisha. Maisha baada ya kifo sio muendelezo wa maisha ya hapa duniani… kwamba tutaendelea huko kula na kunywa, bustani za matunda, ndoa na mabikira na wajane na nguvu za kuwaridhisha kindoa, divai, nyama, na kwa vile furaha ya akina mama wengi ni katika kuzaa, basi watazaa kila siku... La la, bali ni maisha ya ukamilifu ya utukufu yasiyo na hitaji la ndoa kwani katika Mungu hakuna kifo tena bali uzima wa umilele, utimilifu wa ukamilifu.

Bwana Yesu anadhihirisha kuwa ufufuko wa wafu upo, “lakini ya kuwa wafu hufufuliwa hata na Musa alionesha katika sura ya kijiti hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo” (aya 37-38). Musa alipoandika haya mababu hawa walikwisha kufa zamani. Kwa mantiki ya kiyahudi Mungu akiitwa Mungu wa Ibrahamu maana yake Ibrahimu yupo bado hai mbele ya Mungu. Kwa hiyo kama Masadukayo wangeelewa tafsiri halisi ya vitabu vya Musa wangeona mapema kuwa kwa tafsiri halali ya vitabu hivyo watu wangali hai mbele ya Mungu na siku moja watafufuliwa. Cf. Yesu alisema Lazaro hajafa amelala anakwenda kumuamsha (Yh 11:11-13)… Pia aliwakataza watu wasilie kwa vile binti Yairo hakufa alilala tu, wakamcheka (Mt 9:24)… Kumbe kwa Mungu hatufi, tunaishi... Kukoje huko? Hatujui, ni mafumbo ya Mungu, wanaojaribu kuieleza mbingu wanaishia kutuchekesha kama sio kutukwaza

Tunaalikwa kuwa mashahidi wa matumaini, si kwa maneno tu bali kwa maisha yetu, Kuisimamia imani bila woga, kama vijana wa Mmakabayo. Kudumu katika kazi njema licha ya mateso, kama anavyosema Mtume Paulo. Kuishi maisha ya sasa kwa mtazamo wa uzima wa milele, kama alivyofundisha Yesu. Paradiso sio nyumba kwamba tutaweza kuinunua na hivi ni lazima tujue kwanza ilivyo (idadi ya vyumba, umeme, maji, viyoyozi, bustani, parking nk) hayo ni ya duniani.. Paradiso ni matarajio ya zawadi ya Mungu Baba kwa wanawe. Imani hii inatupatia uhakika wa kufufuliwa, tutapata miili ya utukufu iliyokamilika, isiyohitaji kuoa/kuolewa, chakula/kinywaji, milango, matibabu, vyandarua… tutafanana na malaika, wana wa Mungu kwa vile ni wana wa ufufuo. Watu wengi wanakufa katika vita visivyoisha, Ukraine, Sudan, Gaza,  DRC... Je, tumaini lina nafasi gani? Masomo ya leo yanatuambia ndio, matumaini yapo, hata kifo hakiwezi kuliondoa. Wengine wanajiuza au kuua kwa kukata tamaa – kwa sababu maisha yamekuwa magumu mno. Yesu anasema: Mungu ni Mungu wa walio hai, upo uzima zaidi ya huu wa sasa. Viongozi wengi wanapuuza haki na maisha ya watu, kama mfalme katika somo la kwanza. Lakini vijana wale walichagua sheria ya Mungu kuliko amri ya wanadamu.

Wayahudi waliagizwa na Musa kurithi wajane (Kumb 25:5) na walishika agizo hilo. Mume alipofariki mke alitawa (eda) miezi 3 kuona kama mjamzito, ndipo alipoolewa na ndugu wa marehemu, kaka yoyote alipaswa kumrithi mjane. Akikataa mkubwa anaulizwa anayefuata hadi mdogo wa mwisho, hata wa umri wa siku 1 alipaswa kusubiriwa akue na mjane alitakiwa amsubiri mtoto huyo afike umri wa kuoa, ndio miaka ya barehe... kama marehemu alikuwa na mitala, basi wajane wake waligawanywa kwa wadogo zake wote japo kaka mkubwa aliruhusiwa kuwarithi wote. Ndoa hizi zilifungwa kwa kutoa kitu cha thamani na tendo la ndoa, na kukataa ilikuwa dhambi (Mwz 38:8-10). Anayegoma kurithi mjane alipaswa kutangaza mbele za watu kuwa hataki na walifanya sherehe ya kuvua kiatu (halizah) kisha mjane aliweza kuolewa na mtu mwingine yeyote... Wenzetu walirithi wajane, sisi inawezekana haturithi wajane leo lakini bado tuna mila na desturi zisizofaa, tuombe neema ya kuziacha

Kwa asili mwanadamu ni kiumbe wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yake yupo na Mungu, ndilo lengo la kuumbwa kwetu. Sote tuna hamu ya mbinguni, roho zetu zina kiu ya umilele. Je, imani yetu ni thabiti kutuimarisha sisi na hasa wakati wa mateso kama hawa tulio wasikia katika somo la kwanza? na Je, ni imara ya kutosha kutuvusha katika dunia hii? tuwe na matumaini. Mfalme mmoja anapokufa alisema ‘ninakufa na mwili wangu utarudishwa udongoni kuwa chakula cha minyoo! haya ndiyo maafa yaliyokuwa yakinisubiri..’ amekata tamaa, inaingia kweli akilini kuwa Mungu ametuumba kwa sura na mfano wake na kufanya nasi maagano, kutuahidi mengi, kutulinda, kutupatia baraka ya chakula na watoto, halafu tupotee na kuwa mavumbi, chakula cha minyoo na bacteria kwa milele yote? anakuwa na lengo gani?

‘Yeye si Mungu wa wafu bali wa walio hai’... ‘ninajua kuwa Mkombozi wangu anaishi na hivyo baada ya maisha haya Mtetezi wangu atasimama juu’ (Ayu 19:25-26)... ndio, ‘nangojea ufufuko wa wafu na uzima wa milele ijayo, amina’... tujikusanye vema. Mtume Paulo anasema: “Bwana awaonyeshe upendo wa Mungu na uvumilivu wa Kristo.” Anatuombea tutulizwe mioyo yetu, tusimame imara katika kazi njema, na tusifadhaishwe na hofu. Katika dunia ya leo iliyojaa habari za vita, ukosefu wa amani, mateso ya kijamii na kiuchumi, matumaini hayawezekani bila uvumilivu. Lakini Paulo anatuambia: Mungu yuko nasi – kutufariji na kututhibitisha.

Na kama mtu angejaribu kuijaribu imani yetu, je, tungalikuwa na ushujaa wa kuitetea? Imani yetu haijengwi juu ya hadithi au juu ya mazungumzo ya watu fulani, msingi wa imani yetu ndiyo hii, “Kutazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye”, tupokee baraka ya Mt. Paulo katika somo II (2Thes 2:16-3:1-5) ‘Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo’ amina.

Ee Bwana, Mungu wa walio hai, tupe moyo wa uthabiti kama wa vijana wa Mmakabayo.
Tuimarishe katika kazi njema, utuongoze kwenye uvumilivu wa Kristo, na utujalie kuishi maisha haya kwa macho ya matumaini ya milele. Ee Mungu wa walio hai, tukusikie katika sala hizi. Tufanye kuwa watu wa matumaini, tukimtazamia mwanao Yesu Kristo aliyefufuka na kutushindia kifo. Tunakuomba hayo kwa njia yake yeye anayeishi na kutawala milele.

Tufanye mashahidi wa uzima, hata katika dunia yenye kifo. Amina.

Liturujia ya Neno
07 Novemba 2025, 17:58