Jubilei ya Watawa Jimbo Tunduru-Masasi,Ask.Mhasi:kushukuru ni ustaarabu,utu na uungwana
Ndg.Lawrence Kessy SDS;- Masasi, Tanzania.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni fursa ya kukimbilia na kufumbata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelelea siku zijazo kwa matumaini. Ni katika kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho na kuwa jinsi tulivyo kwa njia ya imani huku tukiwa tunashuhudia ubora wa maisha ya kila siku.
Haya na mengine yamo katika Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanaoongozwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi,” Rum 5:5 na uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko na ambao umetuongoza kwa kipindi cha mwaka mzima ambao karibu tuko ukingoni mwa Jubilei hii.
Katika Tamko hilo Papa alisisitiza kuwa kiini cha maadhimisho ni matumaini yanayowawezesha watu waamini wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma, lakini pia hata katika maadhimisho ya Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa maisha na uzima wa milele.
Baba Mtakatifu Francisko katika tamko hilo alikumbusha pia Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo kujiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325, na ambapo Papa Mwenyewe Francisko alitamani kuudhuria, kunako Mwezi Mei, lakini kwa mapenzi ya Mungu akamwita katika nyumba yake ya milele kwa kumwachia kama jukumu la mfuasi wake.
Ni katika muktadha huo Ijumaa tarehe 21 Novemba 2025 Askofu Filbert Felician Mhasi, wa jimbo Katoliki la Tunduru Masasi, nchini Tanzania aliadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya Jubilei ya Watawa wa kike na kiume Kijimbo katika Mwaka Mtakatifu wa 2025. Misa iliyofanyika katika Kanisa la Masista Wasalvatoriani,(SDS) huko Migongo Masasi nchini Tanzania.
Misa ilianza kwa maandamano yaliyoanzia katika Parokia ya Masasi hadi Migongo na kupokelewa na Askofu Mhasi na kufuatiwa na Sakramenti ya Upatanisho na Tafakari.
Askofu Mhasi wakati wa mahuburi yake aliwaalika watawa hao “kuguswa na huruma na mapenzi ya Mwenyezi Mungu kwani Mungu hamwachi mtu aanguke. Kondoo alipotea kwa sababu alijeruhiwa au kuumizwa na matokeo yake ni kurudi nyuma kidogo na kutoweza kutembea na wenzake.” Askofu aidha alisisitiza kuwa kuwa “mchungaji mwema anawaacha kondoo walio na afya njema na kuwafuata wale waliopotea au kuanguka katika safari zao za maisha. Na aliyepotea akitafutwa akubali kumpokea yule anayemtafuta au anayetaka kumgusa ili amponye majeraha au maumivu yake.”
Askofu Mhasi akiendelea alieleza kwamba “kwa kutokujikubali ni rahisi mno kuendelea kuwapotosha na kuwaangusha wengine kitu ambacho siyo kizuri bali kinachotakiwa ni kupokea huruma na upendo wa Mungu.
Kwa upande wa Padre Mukasa Mwajombe,(SDS) katika tafakari yake aliyoitoa kwa watawa hao alisema kwamba Jublei ni siku ya kumbukumbu au ukumbusho wa miaka kadhaa kama vile miaka 25, 40, 50, 75 na kuendelea. Alisisitiza kuwa “Jublei hizo zinaitwa kwa majina ya madini kuendana na thamani yake na jambo la maana katika Jublei ni kushukuru Mwenyezi Mungu na makuu yake.”
Padre Mwajombe alisema “shukrani ni tendo au hali ya kusema asante kwa mema uliyotendewa. Na vile vile “ kushukuru ni ustaarabu, utu na uungwana.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here