Moja ya Misa iliyoongozwa na Papa Francisko kwa ajili ya marehemu wote(Novemba 2023). Moja ya Misa iliyoongozwa na Papa Francisko kwa ajili ya marehemu wote(Novemba 2023).  (Vatican Media)

Fumbo la Kifo:Kifo si mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa maisha ya milele

Kanisa linawaombea wafu kwa sababu linaamini kuwa upendo wa Mungu unafanya kazi hata baada ya mtu kufa,na sala inaweza kuwasaidia wazidi kukaribia ukamilifu wa kiroho wale waliokufa wakiwa katika hali ya neema ya utakaso ila wana madoa ambayo hayakulipwa wakiwa hapa duniani.Kwa hivyo wako mahali pa utakaso(Toharani).Wanahitaji sala zetu.

Sr Grace Hashim,CMC, na  Joackim Abel Makaya.

Mama Kanisa kila ifikapo mwezi wa Novemba, uwakumbuka kuwaombea marehemu wote. Tnapohitimisha mwezi huu wa Novemba tukiwa ukingoni mwa hitimisho la Mwaka Mtakatifu wa Jubilie ya 2025 ya Ukristo ikiongozwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa Matumaini: tujikite kutafakari tena juu ya mada hiicna fumbo la ‘kifo’. Awali ya yote swali linakuja kwetu ndugu msomaji wa makala hii:  Je, kwanini Kanisa linawaombea wafu? Katika kujibu swali hili ni vema kwanza kupitia baadhi ya mafundisho msingi wa Imani ya Kanisa juu ya maisha baada ya kifo. Kanisa linafundisha uwepo wa mambo makuu manne mwishoni mwa mwa maisha ya mwanadamu hapa duniani. Mambo hayo ni: Kifo, Hukumu, Jehanamu, na Mbingu au(Paradiso.) Kila kiumbe hai huitimisha safari ya maisha yake hapa duniani kwa kifo. Kwa mwanadamu, baada ya kifo hufuata hukumu ambayo itaamua hatima ya mtu huyo kuwa au ni kuishi milele na Mungu mbinguni(Paradiso) ama ni kutegwa na upendo wa Mungu kwa milele yote (Jehanamu).

Kanisa humlea na kumfundisha kila mwanaye aliyeshilikishwa kifo cha Kristo, Bwana wake, kwa Ubatizo, anapokielekea kifo au anapotafakari juu ya kifo chake, aunganishe kifo chake na kifo cha Yesu, na hivyo akiangalie kifo kama safari ya kumwendea Yesu na kuingia maisha ya milele, kwani kifo huhitimisha maisha ya mtu kama muda wa wazi wa kupokea au kukataa neema ya Mungu iliyotolewa na Kristo, na si mwisho wa maisha, bali ni mwanzo wa maisha ya milele. Sasa, kama tulivyosema hapo juu baada ya kifo hufuata hukumu. Mafundisho ya Kanisa yanasema: “Kila mtu toka saa ya kufa kwake hupokea katika roho yake isiyokufa tuzo la milele katika hukumu ya pekee kuhusiana na maisha yake na Kristo, au kwa kupitia utakaso, au kwa kuingia moja kwa moja katika heri ya mbingu, au kulaaniwa moja kwa moja kwa milele.”

Katika Kanuni yake ya Imani, Kanisa huungama na kukiri kusadiki juu ya ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo. Imani hiyo, juu ya uwepo wa ufufuko wa miili na uzima wa milele baada ya kufa, inapelekea Kanisa kuwaombea wafu. Ebu tujiulize: Uzima wa milele ndio nini? “Uzima wa milele ni ule unaoanza mara baada ya kifo. Hautakuwa na mwisho. Kwa kila mmoja wetu utatanguliwa na hukumu ya binafsi ambayo itatolewa na Kristo, hakimu wa wazima na wafu, na itathibitishwa katika hukumu ya mwisho.” Sasa tumefahamu kuwa kutakuwa na hukumu moja itakayotolewa katika nyakati mbili tofauti.

KAZI YA UUMBAJI
KAZI YA UUMBAJI

Ebu tujue juu ya hukumu hizi na kile kitolewacho kwazo: Tunaona sasa, mara baada ya kifo huja hukumu ya pekee, ambayo kama ilivyoelezwa hapo juu, hupelekea roho za marehemu kuhukumiwa kupata au mbingu, au toharani au Jehanum. Tufahamu sasa, nini mafundisho ya Kanisa juu ya hali au sehemu hizi. Kanisa linafundisha kuwa: “Mbingu” maana yake ni hali ya heri kuu na ya kudumu. Hali waiishio wale ambao wanakufa katika neema na urafiki na Mungu, na waliotakaswa kikamilifu, hao wanaishi kwa daima pamoja na Kristo. Wanafanana na Mungu daima, kwa sababu wanamwona “kama alivyo”, uso kwa uso. “Toharani ni hali ya wale waliokufa katika urafiki na Mungu na wana hakika ya kuokolewa milele, lakini wanahitaji bado kutakaswa waingie katika heri ya mbinguni.”  

Na linatofautisha mbingu na toharani mbali kabisa na Jehanum kwa kusema kuwa: Jahanum ni neno linalotumika kuelezea hali au hatima ya wale waliochagua kwa hiari na utashi kamili kujitenga na upendo wa Mungu kwa kwa milele yote. Ndiko kulaaniwa milele kwa wale waliochagua kwa hiari kufa wakiwa na dhambi ya mauti. Neno lingine litumikalo kuelezea hali ya hao ni moto wa milele10. Yesu Kristo alitangaza ukweli huo akisema: “Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele”. (Mt 25:41).Kwa jinsi tulivyoona hadi sasa, ni kwamba kati ya hukumu ya pekee na Hukumu ya mwisho, ambayo “itakuwa tamko la heri au la laana ya milele ambalo Bwana wetu Yesu, atakaporudi kama hakimu wa wazima na wafu, ataitoa kuhusu “wenye haki na wasio haki” (Mdo 24:15), waliokusanyika wote pamoja mbele yake”. Na ambayo baada yake (hukumu ya mwisho), mwili uliofufuka utashiriki malipo ambayo roho yake ilipewa katika hukumu ya pekee. Basi sasa katika muda kati ya hukumu ya pekee na hukumu ya mwisho kutakuwa na nafasi ya Toharani kuwepo, kama tulivyoona maana yake hapo juu. Na sasa, msingi wa sala ya Kanisa kwaajili ya waamini wake marehemu huletwa na uwepo wa hali hizi tangu kabla ya hukumu ya mwisho.

Basi, kutokana na maelezo tuliyoyatoa hadi sasa, ebu tuingie moja kwa moja kwenye kujibu swali letu: Je, kwa nini Kanisa linawaombea wafu? Kwa ufupi kabisa, tunaweza kusema kuwa: Kanisa linawaombea wafu kwa sababu linaamini kuwa upendo wa Mungu unafanya kazi hata baada ya mtu kufa, na sala inaweza kuwasaidia wazidi kukaribia ukamilifu wa kiroho wale waliokufa wakiwa katika hali ya neema ya utakaso ila wana madoa ambayo hayakulipwa wakiwa hapa duniani; hivyo wako mahali pa utakaso (Toharani). Kumbe msingi wa Kanisa kuwaombea wafu umejikita katika Imani yake juu ya Uwepo wa Mungu. Mungu aliye Upendo (Taz. 1 Yoh 4:8). Ambaye fadhili zake ni za milele (Taz. Zab. 107:1) Mungu anayewapa wanae walioishi wakimwamini na kulishika Neno lake, kipindi cha utakaso kamili pale wanaomfikia wakiwa bado na vivumbi vichache vya safari.

Katika hili, Mtakatifu Gregorio Mkuu, Papa na Mwalimu wa Kanisa, alifundisha akisema: Kwa ajili ya makosa fulani madogo, lazima kusadiki kwamba kuna moto utakasao kabla ya hukumu ya mwisho. Kwa kweli Yule ambaye ni ukweli athibitisha kwamba, kama mmoja anamkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa wala katika ulimwengu wa sasa wala katika ulimwengu ujao. Kutokana na tamko hili tunaweza kufahamu kwamba makosa fulani yanaweza kusamehewa katika ulimwengu huu, lakini makosa mengine katika ulimwengu ujao. Hivyo basi, kwa maneno mengine tunaweza kusema: katika Kanisa Katoliki, kuna imani ya toba ya baada ya kifo (utakaso wa Toharani). Hii ina maana, kwamba mtu anayekufa, ikiwa ana mapungufu au madhara ya dhambi ambayo hayajakamilika kuponywa wakati wa uhai hapa duniani, anapokufa hahukumiwi kwenda Jenaham kwani hana uadui na Mungu, bali hupitia hali ya utakaso (Toharani). Katika hali hiyo, sala za walio hai zinachukuliwa kama msaada wa upendo kwa roho hizo iliyo Toharani - kama vile kumwombea mtu aliye mgonjwa ajaliwe uponyaji. Mafundisho ya Kanisa yanaiita hali hiyo Utakaso wa Mwisho, au Mahali pa Utakaso (Purgatorio)13 .

Msingi wa Kanisa kuwaombea watu ni sehemu ya Mapokeo ya tangu zamani sana: Kuombea wafu ni desturi iliyokuwepo katika Kanisa la karne za awali kabisa (kabla hata Biblia haijakamilishwa kwenye kanoni tuliyonayo leo). Hivyo, Kanisa Katoliki tunaona desturi hii ni sehemu ya urithi wa imani. (Jaribu kupitia historia ya Kanisa tangu baada ya Pentekoste, utaliona hili fundisho au hii imani).

MAMA MARIA NA MWANAE ALIYEKUFA
MAMA MARIA NA MWANAE ALIYEKUFA

Msingi wa kuombea wafu katika Maandiko Matakatifu:

Ndugu zangu, ni wazi kwamba katika Biblia hakuna sura hata moja inayoelezea juu ya Toharani moja kwa moja, lakini Biblia inatoa kanuni na mifano inayoelekea huko. Nukuu zifuatazo zinaonesha hilo: 2 Wamakabayo 12:38 - 46: Hiki ndicho kifungu kilicho wazi zaidi, kinachoonyesha maombi kwa ajili ya wafu. Inasimulia askari wa Yuda Makabayo waliokufa, na jumuiya ilitoa sadaka ya kujitoa kwa ajili yao ili wapate msamaha na kutakswa dhambi zao. Vitabu vya Makabayo viko kwenye orodha ya vitabu vya Orodha ya pili, ambavyo Kanisa Katoliki linavitumia, lakini madhehebu hayavichukulii kuwa sehemu ya Biblia. Hilo hufanya kukosa fundisho hili. Ila mtu akifa wanamfanyia maombi na ibada, sijui kwa msingi upi?

Mathayo 12:32: Yesu anasema: “Naye mtu yeyote atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali yeye atakayenena neno juu ya Roho Mtakatifu hatasamehewa katika ulimwengu wa sasa, wala katika ule ujao”. Hapa tunapata dokezo kuwa kuna dhambi “ zinazosamehewa, na zisizosamehewa katika ulimwengu huu wala ule ujao”. Kauli hii inaonesha kuwa huruma ya Mungu inaweza kuendelea hata baada ya kifo.

1 Wakorintho 3:13-15: Paulo anasema kazi ya mtu “itasafishwa kama kwa moto”, na mtu “ataokoka, lakini kama kupitia moto”. Kanisa Katoliki linakitafsiri kifungu hiki kama dokezo ya utakaso wa baada ya kifo, ambao linaufundisha.

1 Petro 3:18-20. 4:6: Petro anataja Kristo “kuwahubiria roho walioko kifungoni.” Hivyo inaonyesha kuwa roho bado inaweza kupokea neema katika hali tofauti na maisha ya sasa. Ni wazi kuwa kifungu hiki kwa namna fulani akifafnui moja kwa moja juu ya Toharani; ila vidokezo vyake hatuwezi kuvipuuzia tukiunganisha na mafundisho mengine ya Maandiko Matakatifu juu ya maisha baada ya kifo. Je, kuwaombea marehemu kutanisaidie mimi? Ndugu zangu, Kanisa Katoliki linaamini maombi kwa wafu ni kama kumwambia Mungu: “Hawa watu wetu tunaowapenda, tukutane nao tukiwa tumesafishwa kabisa. Wasimame mbele Yako wakiwa wameng’aa”.

Kumbe, kuombea wafu kunanisaidia mimi kwanza kabisa kuzidi kuamini juu ya uzima wa milele, na hivyo kujibidisha kuutafuta uzima huo. Pili, kwa kuwa ninawaombea wafu wapate msamaha wa Mungu na uzima wa milele, sala yangu bila shaka inajengwa katika msingi wa kile ninachokiona kuwa ni chema na heri, sio tu kwao hao marehemu bali na kwangu pia; hivyo, kwa kuwa ninautazamia uzima ule, kuwaombea wao kwanivuta kuishi vema ili nami nije niungane nao mbinguni. Tatu, japo si la kiimani sana ila ni wazi kuwa: akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki. Kwa mantiki hiyo sasa, endapo sasa huyu marehemu yupo katika utakaso wa toharani na anahitaji msaada wangu; na toharani haidumu milele; pale anapotoka toharani na hata akiwapo bado, ataniombea na mimi pia. Basi, kuombea wafu kuna lipa tena bila usumbufu.

MSHUMAA
MSHUMAA

Njia au namna zinazopendekezwa na Kanisa katika kuwaombea wafu

Misa za wafu (na za mazishi): lengo la misa hizi si “kumtoa mtu motoni,” kama watu wengine wanavyowaza, bali ni: Kumkabidhi marehemu kwa Mungu, Kumuombea neema ya kuingia katika mwanga wa milele, na kuifariji familia. Katika taalimungu ya Kanisa Katoliki, Sadaka ya Ekaristi Takatifu pia ni “sadaka ya upatanisho.” Kwa hiyo inapotolewa kwa ajili ya marehemu, ina thamani ya kipekee na nguvu ya kuwaokoa hao ambao kwaajili yao Kristo aliutoa uhai wake. Sala na ibada mbalimbali (Rozari takatifu, na Rozari za aina mbalimbali: ya Huruma ya Mungu, ya Mateso saba, nk.

Ibada ya Njia ya Msalaba, Kuabudu Ekaristi Takatifu binafsi au na Jumuiya: Kanisa linaamini mambo mawili ambayo yanaunganika kama tungeita kwa lugha ya kidijitali(Wi-Fi) ya kiroho:  1. Waamini wote ni mwili mmoja katika Kristo: ikiwa tuko “umoja” ndani ya Mungu, kifo hakikatishi huo umoja. Ni kama kusema: Kama mimi na wewe tuko kwenye network moja, hata ukihama chumba, bado tuko connected. 2. Sala ni tendo la upendo linalomgusa Mungu: Upendo unaoombwa kwa mtu mwingine unaonyesha huruma, na Kanisa linaona Mungu hupokea upendo huo na kuugeuza kuwa neema kwa huyo mtu. Ni kama kumwambia Mungu, “Ee Bwana, tafadhali akumbuke huyu ndugu yetu, mfanye awe karibu Zaidi na Uzuri Wako.” Kwa hiyo, sala si “kuwatoa motoni,” ni kuomba neema iendelee kufanya kazi kwa roho ambayo iko safarini kuelekea ukamilifu.

Kutoa sadaka (matendo ya huruma): Kanisa huona kuwa sadaka inayotolewa kwa upendo kwa ajili ya marehemu inachukuliwa kuwa tendo la upendo linaloweza kupata neema kwa ajili yao. Mfano: kusaidia maskini, kutembelea wagonjwa, au kufanya tendo la huruma na kulitoa kiroho kwa ajili ya marehemu. Rehema (Indulgences): Hii si “tiketi” inayonunuliwa ili mtu atoke toharani, kama ambavyo wakati fulani iliwahi kuelekea kupotoshwa. “Rehema ni msamaha mbele ya Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha huo ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata, kwa masharti fulani yaliyopangwa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo na ya watakatifu”. “Rehema ni ya muda au kamili kutokana na kwamba yaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi”. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu” (rej.KKK 1471).

TUTAFUFUKA KAMA BWANA YESU
TUTAFUFUKA KAMA BWANA YESU

Kuwa na moyo wa msamaha: Mtu akifa na kulikuwa na maumivu au chuki, msamaha wa walio hai unaonekana kuwa tendo la huruma ambalo lina “fungamana” na sala kwa marehemu. Kanisa halisemi moja kwa moja kwamba msamaha unabadilisha hatima ya marehemu, lakini linaona kuwa unafungua neema ya upendo kwa pande zote mbili.

Hitimisho: Kwanza kabisa tukitafakari katika upana wake mada hii ya kuombea wafu ni pana na ya muhimu sana katika tafakari ya maisha ya kila mwamini Mkristo. Mbali na faida au lengo kusudiwa katika dhamira hiyo ya kuombea wafu, lakini kwa undani wa pekee tendo la kusali ni tendo jema na la muhimu sana kwa maisha ya kiumbe chochote kile kiaminicho uwepo wa Mungu na maongozi yake (Mungu). Kumbe, jibu kwa swali hili, ningependa tulitangulize kwa ufufanuzi walau kwa ufupi juu ya sala / kusali/ kuomba / kuombea.

Katika Maandiko matakatifu, tunaona watu mbalimbali wanaomjua Mungu na kumwamini mara nyingi wamekuwa wakimwomba mema na neema mbalimbali kwa njia ya sala. Bwana wetu, Yesu Kristo, mwenyewe Maandiko Matakatifu yanamdhihirisha jinsi alivyokuwa mpenda kusali na alivyowahimiza wanafunzi wake kusali, na pia kuwafundisha kusali. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea, naye atufutaye huona, naye abishaye atafunguliwa.” (Mt. 7:7-8). “Kwa sababu hiyo nawaambia: Yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu”(Mk. 10:24).

TUWAOMBEE MAREHEMU WETU
TUWAOMBEE MAREHEMU WETU

“Nanyi mkiniomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya.” (Yh. 14:13-14) Vifungu hivi ni sehemu tu ya yale aliyoyafundisha Yesu na kuhimiza kuhusiana na kusali / sala. Ili tusirefushe sana mada hii, tuingie katika kujibu swali letu kwa ufupi tukisimamia vifungu tajwa hapo juu. Kwa ushahidi wa sehemu hizo za Maandiko, tunaweza kujibu kwa kifupi tu kuwa Kanisa linawaombea wafu kwa kuwa Yesu aliwahimiza kusali na kuomba na kuwathibitishia kuwatimizia yale wayaombayo kwa imani.

Basi mbele ya vifo vya wapendwa wetu, Kanisa halisiti kufuata agizo na mfano wa Bwana wake, kwa kuomba na kuililia huruma ya Mungu kwa ajili ya watumishi wake waliofariki dunia. Kwenye vifungu tajwa hapo juu, tunaona wazi Yesu hatuambii tuombe nini na tusiombe nini. Kwa mfano, anaposema: “Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya” (Yh 14:14). Yesu ameacha uhuru kwetu wa kuomba lolote, kumbe kuwaombea wafu, kwa mantiki ya kawaida kabisa tunaelewa kuwa inaingia kati ya “lolote” tuhimizwalo kuomba. Hadi hapo tumejaribu kujibu lakini yanayoibua mengine mengi ndani ya “moyo wetu ambao hauwezi kutulia hadi ufike kwake mbingu”kama alivyosema Mtakatifu Agostino, Baba wa Kanisa.

Kufufuka kwa Yesu
Kufufuka kwa Yesu
MAREHEMU
29 Novemba 2025, 12:32