Moja ya mazishi ya aliyeuawa wakati wa uchaguzi Mkuu nchini Tanzania. Moja ya mazishi ya aliyeuawa wakati wa uchaguzi Mkuu nchini Tanzania.  (AFP or licensors)

Tanzania,Jimbo Kuu Arusha kuwaombea waliopoteza maisha,majeruhi na ndugu zao

"Tulisali kuombea uchaguzi mkuu tukitamani kwamba zaoezi hilo lingefanyika kwa utulivu na kwa amani kama chaguzi nyingine zilizopita.Yaliyotokea Tanzania siku ya Uchaguzi Mkuu 29 Oktoba yametushangaza na kushangaza Ulimwengu kwa sabau siku hiyo ilituzalia kiumbe cha ajabu mno katika historia yetu."Ndivyo Askofu Mkuu Amani wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha,anaanza katika mwaliko wa kuombea waliopoteza maisha na majeruhi.

Jimbo Kuu Katoliki Arusha - Tanzania.

Tunachapisha Tafakari ya Askofu Mkuu Isaac Aman, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha nchini Tanzania, iliyotiwa saini tarehe 7 Novemba 2025 yenye kichwa:

 KUWAOMBEA WALIOPOTEZA MAISHA, WALIOJERUHIWA NA WALIOPOTEZA NDUGU NA JAMAA KATIKA VURUGU ZA UCHAGUZI MKUU.

Wapendwa katika Kristo,

Tulisali na kuombea uchaguzi mkuu tukitamani kwamba zoezi hilo lingefanyika kwa utulivu na kwa amani kama chaguzi nyingine zilizopita. Yaliyotokea Tanzania siku ya Uchaguzi Mkuu 29.10.2025 yametushangaza na kushangaza ulimwengu kwa kuwa siku hiyo ilituzalia kiumbe cha ajabu mno katika historia yetu. Nawiwa na dhamiri yangu kuandika waraka huu mfupi kwa lengo moja tu. Tumwendee Mungu Baba yetu kwa kufunga na kusali kwa Imani. Nawaalika waamini wote tusali tukiwaombea watanzania na hata wageni wema waliopoteza maisha katika vurugu hizo. Mwenyezi Mungu awapokee kwake mbinguni na kuwapa pumziko la Amani. Tuliyoyaona hapa Arusha yalitendeka pia katika miji na maeneo mengine. Yalisikitisha na kubadili jina na hadhi ya Tanzania.

Tuwaombee pia waliojeruhiwa katika vurugu hizo na sasa hivi wengine wako hospitalini na wengine wanaugulia nyumbani. Wako waliopata ulemavu wa maisha wasiweze tena kujitegemea kama hapo awali. Mwenyezi Mungu awape uponyi wa mwili na roho na awajalie ndugu na jamaa zao moyo na nguvu ya kuwasaidia jinsi itakavyowezekana na kwa muda wote watakaohitaji msaada wao. Aidha wako waliopoteza ndugu na jamaa zao katika vurugu hizo na hakuna mawasiliano ya uhakika kwamba wataonana tena au la! Kweli ni huzuni. Wako watoto walioshuhudia umwagikaji wa damu nyumbani kwao! Waliona kwa mshtuko na hofu kubwa mashambulizi na maangamizi ya baba, mama, babu, bibi, shangazi wakiwa ndani ya nyumba sio barabarani! Watoto hao watasaidiwaje kisaikologia? Watakuwa raia wa namna gani? Tuwaombee wote walioshuhudia kwa macho jinsi risasi zilivyoteketeza uhai. Tuombe uponyi wa Mwenyezi Mungu.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu awe faraja na matumaini yao. Tunawaombea Imani kwa Mungu Mwumba wetu na Mweza wa yote; awe kwao msaada wa kipekee. Wakati fulani Nabii Yeremia alieleza huzuni ya mama aliyelilia watoto wake akisema: "Bwana asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi: Raheli akiwalilia watoto wake, asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako." Yer 31:15. Tanzania inaomboleza kutokana na vurugu za siku ya uchaguzi mkuu. Hakuna mwingine wa kutupatia faraja na matumaini zaidi ya Mungu. Ndiyo maana mimi kwa mujibu wa nafasi yangu. ya kichungaji nawapeni pole kwa hayo yaliyotokea kwa nchi yetu nikiwasihi sana tuendelee kusali ile sala ya kuombea Tanzania Haki na Amani. Tusali Misa nyingi za kumlilia Mungu. Tusichoke kuomba mpaka Mungu ajibu kwa wakati wake na kwa namna yake. "Utakalo lifanyike duniani kama Mbinguni". Hiyo ni sehemu ya sala tuliyopewa na Yesu mwenyewe; kwa hayo yaliyotokea twapaswa kujitafakari kama taifa.

Kama nilivyosema hapo awali, waraka huu ni mwaliko wa kumkabidhi Mungu katika sala, hayo yaliyotokea siku ya uchaguzi mkuu na kesho yake. Tumwombe Mwenyezi Mungu atufungulie njia ya kwenda mbele kama taifa huru lenye umoja na upendo wa kweli na lenye kuthamini uhai, ubinadamu na kutendeana kwa haki jinsi atakavyo Mungu. Tukumbuke kwamba Mungu alimwonya Kaini akimwambia: "Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde." Mwa 4:6-7. Watanzania tumetendeana kwa ghadhabu na kusababisha vurugu iliyoangamiza uhai na kuteketeza mali na heshima yetu kitaifa na kimataifa. Kaini hakumsikiliza Mungu bali "alimwinukia Habili nduguye, akamwua" Mwa 4:8. Mungu akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi! Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako' Mwa 4:10-11. Tumeacha undugu, tukaangamizana!

Kristo alimwaga damu yake yenye kutualika tuache uhasama ili tutoke kwenye laana na kuishi maisha mapya ya furaha na Amani ya Waliokombolewa Ebr 12:24. Kwa upande wake, Mwenyezi Mungu ametujalia nchi nzuri yenye utajiri mwingi. Ni wajibu wetu tuheshimu na kulinda majaliwa ya Mungu tukijifunza kwa hayo magumu yaliyotokea. Kila raia anayo thamani itokayo kwa Mungu. Hakuna mwenye haki au uhalali wa kumwumiza au kumwua mwingine. Uhai wa mwanadamu ni mtakatifu wapaswa ulindwe na kustawishwa kwa gharama yoyote. Katika sala ya kuombea taifa letu haki na Amani tuliomba mioyo yetu ijazwe na mapendo ya kimungu ili wote tuwajibike kiaminifu na kuunganishwa kama ndugu wa familia moja. Vurugu zilizotokea hazikubariki sala yetu. Kaini alimwinukia ndugu yake akamwua! Tutafakari hilo na kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo. Tuendelee kuomba viongozi wema na waadilifu watakaoliongoza Taifa letu kuishi tunu za Upendo, Ukweli, Haki na Amani. Tumwombe Bikira Maria Mtakatifu Mkingiwa dhambi ya asili na Mlinzi wa Taifa letu, atuombee tuweze kutafuta kwa pamoja usitawi na usalama wa Taifa letu Tanzania katika roho ya Uzalendo.

Nahitimisha kwa kuwapa tena pole walioathirika na vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi mkuu; wagonjwa wapone na waliopoteza maisha wajaliwe pumziko la milele. Tuombe neema ya kutatua changamoto zetu kwa upendo na kwa busara.

Nawatakieni neema na Amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo pamoja na faraja za Roho Mtakatifu.


10 Novemba 2025, 09:21