Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa: Tema kuu: Toba ya kweli na wongofu wa ndani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa: Tema kuu: Toba ya kweli na wongofu wa ndani.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Pili Kipindi Cha Majilio: Toba Na Wongofu wa Ndani

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio Mwaka A wa Kanisa: Ujumbe mkuu umejikita katika toba ya kweli na wongofu wa ndani, kuondoa uovu unaoleta utengano ili kuisikimika amani ambayo ni tunda la haki. Hii inawezekana tu kwa kumpokea Masiha Bwana wetu Yesu Kristo na kumruhusu atawale mioyo yetu. Katika Kipindi hiki cha Majilio, Mama Kanisa pamoja na mambo mengine anakazia: Toba ya kweli na Wongofu wa ndani!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya Majilio mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Ujumbe mkuu umejikita katika toba ya kweli na wongofu wa ndani, kuondoa uovu unaoleta utengano ili kuisikimika amani ambayo ni tunda la haki. Hii inawezekana tu kwa kumpokea Masiha Bwana wetu Yesu Kristo na kumruhusu atawale mioyo yetu. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Enyi watu wa Sayuni, tazameni Bwana atakuja kuwaokoa mataifa; naye atawasikizisha sauti yake ya utukufu katika furaha ya mioyo yenu” (Isa.  30:19, 30). Na ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi Rahimu, tunakuomba mambo ya dunia yasitupinge sisi tunaomkimbilia Mwanao tupate kumlaki, bali hekima yako itufanye tumshiriki yeye.” Somo la kwanza ni kutoka katika Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 11: 1-10). Ni utabiri wa kuja kwa Masiha kutoka ukoo wa Yese. Kazi yake ni kuwakomboa watu wote kutoka katika taabu zao na kuwapa amani na usitawi. Ili aweze kutimiza hilo roho ya Bwana itakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kufuata ayaonayo kwa macho yake; bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.” Utabiri huu unamhusu Bwana wetu Yesu Kristo, Mwokozi wetu, nao wanaompokea wanaishi kwa kutenda haki, hivyo amani inatawala maisha yao. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zake, na mwana wa mfalme haki yako; Naye atawaamua watu wako kwa haki. Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma. Na awe na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya dunia. Kwa maana atamwokoa mhitaji aliapo, na mtu aliyeonewa, iwapo hana msaidizi. Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, na nafsi za wahitaji ataziokoa. Jina lake na lidumu milele. Pindi ling’aapo jua, jina lake liwe na wazao; Mataifa yote na wajibariki katika yeye, na kumwita heri (Zab. 72: 1-2, 7-8, 12-13, 17).

Mwenye Haki Atastawi kama mtende
Mwenye Haki Atastawi kama mtende   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum 15: 4-9). Ni maonyo na mausia ya Mtume Paulo kwa Wakristo Warumi ili waishi katika amani ya Kristo Yesu, na kumtukuza Mungu. Hii ni kwa sababu nyakati zile kulizuka ugomvi kati ya wakristo Warumi, Wayahudi na walioongokea kutoka upagani. Kisha kuwausia na kuwaonya waache tofauti zao, anawaombea kwa Mungu mwenye saburi na faraja, awajalie kunia mamoja wao kwa wao, kwa mfano wa Kristo Yesu; ili kwa moyo mmoja na kwa kinywa kimoja wapate kumtukuza Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ujumbe kwetu ni huu; tusiishi kwa kutengana, bali tunie mamoja na tuishi pamoja kwa amani na upendo. Kristo awe dira na mfano wetu. Tuwe na Roho moja na Moyo mmoja tushikamane na kuwa wamoja. Tutakiane baraka na kuonyana kindugu. Katika yote tutendayo Mungu apewe sifa. Tulete amani palipo na vita na utengano. Furaha palipo na huzuni, mwanga palipo na giza, mapendo palipo na chuki, msamaha kwa waliokoseana, matumaini kwa waliokata tamaa, tuiseme kweli ili uongo ujitenge. Tujenge utamaduni wa uhai na sio wa kifo, haki palipo na uonevu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 3: 1-12). Ni tangazo la kukaribia kwa ufalme wa mbinguni kwa kuja kwake Kristo hakimu mwenye haki na mwaliko wa kuongoka, kutubu na kuacha dhambi, ili kuiepuka hukumu ya milele. Huu ni mwaliko wa kuitengeneza njia ya Bwana, na kuyanyoosha mapito yake, kung’oa visiki vilivyo ndani ya mioyo yetu – kiburi, wivu, mawazo machafu, tamaa mbaya, ubinafsi, kupigania madaraka, kujilimbikizia mali kwa rushwa, dhuluma na ufisadi. Hivyo haya mambo yasipopigwa vita na kuangamizwa, yanaleta mgawanyo, utengano, chuki na ugomvi katika kila nyanja ya maisha ya mwanadamu. Lakini hizi ni dalili za nje ya uovo uliopo ndani ya mtu unaosababishwa na dhambi. Kwa maana dhambi inaleta utengano kati ya mtu na Mungu na kati ya mtu na jamii inayomzunguka. Dhambi inaondoa neema ya utakaso, uzima wa Kimungu, Roho wa Mungu anayepaswa kutuongoza katika haki, amani na uelewano. Ni katika misingi hii Mzaburi anasema; “Dhambi huongea na mtu mwovu ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya” (Zab.36:1-4).

Masiha wa Bwana, atavikwa Karama za Roho Mtakatifu
Masiha wa Bwana, atavikwa Karama za Roho Mtakatifu   (@Vatican Media)

Hivyo basi ili tuweze kujiepusha au kujitoa katika hali na mazingira kama hayo, tunaalikwa kukiri makosa yetu, kutubu dhambi zetu na kumrudia Mungu, ili tupate uwezo, nguvu na ari ya kujijengea utamaduni wa kutenda haki na kuishi kwa amani. Ni mwaliko wa kufanya “metanoia”, kuuvua utu wa kale na kuuvaa utu upya wa kikristo. Ili kufanikiwa katika hili lazima Kristo Yesu awe mizani yetu ili tuweze kutambua dhambi zetu na kuona uhitaji wa kufanya toba ya kweli. Tukumbuke wosia wa Mtume Yohane kuwa; “Tukisema kwamba hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani mwetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu hata atusamehe uovu wetu” (1Yn 1:8). Basi, tumwombe Mungu atujalie Roho Mtakatifu atuangaze, ili tuzitambue na kuziungama dhambi zetu, tuweze kurudishiwa neema ya utakaso ndani mwetu, na katika jamii zetu. Ni katika muktadha huu kutubu na kuungama linakuwa ni tendo la upendo, kwa mtu binafsi, kwa Mungu na kwa wengine. Hivyo, hata kama hutaki kutubu na kuungama kwa ajili yako binafsi, walau utubu na kuungama kwa ajili ya wengine, maana dhambi yako inaathiri pia wengine. Hivyo, tuhimizane kuungama ili kwa pamoja tushirikiane kurudisha neema ya utakaso katika familia, jumuiya, taifa na dunia kwa ujumla. Hii itatusaidia kumaliza migogoro, malumbano na ugomvi na kuleta furaha na amani na kusherehekea Noeli kwa furaha. Kwa nguvu zetu hatuwezi kufanikiwa maana adui yetu shetani anatuandama kila siku. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba sala na sadaka zetu sisi wanyonge zikutulize; na kwa kuwa sala zetu hazitoshi kutupatia mastahili utujalie shime kwa rehema yako”. Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Bwana, baada ya kutushibisha chakula cha roho, tunakuomba kwa unyenyekevu sisi tulioshiriki fumbo hili, utufundishe kuyapima kwa hekima mambo ya dunia na kuyazingatia ya mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D Majilio
04 Desemba 2025, 14:15