Kutoa sadaka kwa ajili ya Nchi Takatifu 2026:Toa matumaini,panda amani

Kanisa la Ulimwengu wote linarejea ishara ya kale na ya kina ya kikanisa.Katika ujumbe wa video,Msimamizi wa Nchi Takatifu anawaalika wamini kusali na kuunga mkono jumuiya mahalia kwa ukarimu na ukaribu,ishara ya thamani ya udugu na matumaini hasa katika Mkusanyo wa sadaka kwa ajili ya Nchi Takatifu ambao unakuwa jibu la amani kwa wakati huu mgumu.

Na Francesco Ricupero na Angella Rwezaula – Vatican.

Mwaka huu pia, katikati ya Kipindi cha  Kwaresima na Ijumaa Kuu inapokaribia, Kanisa la ulimwengu wote linarejesha ishara ya kale na ya kina ya kikanisa ile ya mkusanyo wa Sadaka kwa ajili ya (Pro Terra Sancta)Nchi Takatifu. Sio tu mkusanyio wa majitoleo, bali ni tendo halisi la ushirika na Wakristo wanaoishi katika maeneo ambayo Injili ilifanyika mwili.

Toa Matumaini, Panda Amani

Kwa kauli mbiu ya: "Toa Matumaini, Panda Amani," mpango huo unawakilisha ishara halisi ya ushirika na matumaini. Juma Takatifu linapokaribia," Msimamizi wa Nchi Takatifu, Ndugu  Francesco Ielpo(OFM), alisema katika ujumbe wake kwa njia ya video, kuwa "mioyo yetu na macho yetu yanarudi hapa kwenye nchi ambayo Mwana wa Mungu alitoa maisha yake 'hadi mwisho' na ambayo Kanisa lilizaliwa. Leo pia, kutoka sehemu hizi Takatifu, tunaendelea kupata kutoka chanzo cha Pasaka maana na tumaini la huduma yetu. Lakini hatuwezi kuficha ukweli kwamba hizi ni nyakati ngumu.

Vita vimeathiri sana Gaza, Palestina, Israel na Lebanon

Ndugu Ielpo alikumbuka kwamba "vita, vurugu, na ukosefu wa usalama vimeathiri vibaya Gaza, Palestina, Israeli, Lebanon, na Siria. Kinachoongezwa kwa haya yote ni kutokuwepo kwa mahujaji kwa muda mrefu, jambo ambalo limezidisha hali ya kiuchumi ambayo tayari imejaa mgogoro mkubwa." Hakika, "familia nyingi za Kikristo, ambazo hapo awali ziliishi kutokana na hija, sasa zinajitahidi kujikimu.  Vijana wanazidi kupata ugumu wa kufikiria mustakabali hapa, katika nchi yao. Matumaini yenyewe yanaonekana kujeruhiwa, huko Bethlehemu, Yerusalemu, kaskazini mwa Israeli, na pia Lebanon na Siria. Katika muktadha huu," alisisitiza, "maneno ya Baba Mtakatifu yanasikika sana, alipotukumbusha umuhimu wa sala na kufunga kwa ajili ya amani, akitoa wito kwa nguvu wa kukomesha mgogoro katika Nchi Takatifu."

Ishara halisi ya ushirika

Msimamizi huyo aidha alieleza kwamba "Mkusanyio wa Kipapa kwa anjili ya Nchi takatifu (Pro Terra Sancta), si ishara tu ya mshikamano: ni ishara halisi ya ushirika na Kanisa la Yerusalemu. Shukrani kwa mkusanyo huu, tunaweza kusaidia shule, parokia, mashirika ya upendo, mipango ya kijamii, na hatua za dharura, tukiweka uwepo wa Kikristo hai katika maeneo ya Ukombozi. Leo, zaidi ya hapo awali aliongeza kuwa, tunaitwa kujenga upya: si majengo tu, bali mahusiano, uaminifu, na matumaini. Na hii inatokana zaidi na elimu, vijana, familia, na mahali ambapo utamaduni wa kukutana na amani unaweza kuzaliwa.” Kwa hivyo, mwaliko wa kutosahau Nchi Takatifu. "Tukumbuke katika sala na mtuunge mkono kwa ukarimu wenu. Ukaribu wwenuni ishara ya thamani ya udugu na matumaini kwetu."

Kuhakikisha mustakabali wa jumuiya za Kikristo

Kuunga mkono Nchi Takatifu kunamaanisha kuhifadhi kumbukumbu hai ya Umwilisho na Ufufuko, lakini pia kuhakikisha mustakabali wa jamii za Kikristo ambazo zinaendelea, katikati ya matatizo elfu, kuwa ishara ya amani na mazungumzo katikati ya Mashariki ya Kati. Kwa hivyo, ishara ya sadaka, mara nyingi inayofanywa katika ukimya wa sherehe ya kiliturujia, inaweza kuwa kitendo cha uwajibikaji wa pamoja wa kimisionari. Kutoa kunamaanisha kushiriki katika usimamizi wa mahali patakatifu na katika ushuhuda wa Kikristo ambapo yote yalianzia.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku. Just click here

19 Februari 2026, 09:18