Maaskofu Ghana:Uchunguzi wa kina ufanyike dhidi ya ufisadi wa maafisa wa uchimbaji haramu wa dhahabu
Na Sr Ernestina Patrick Lasway – Vatican.
“Wakati mamlaka ya umma inabadilishwa kuwa faida ya kifedha na uhaharibifu wa mazingira kuwa chanzo cha mapato, utawala wa sheria unapungua na manufaa ya jamii yanadhurika,” hayo yalisemwa na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ghana katika taarifa kuhusu kashfa inayohusiana na ufisadi wa baadhi ya maafisa katika uhusiano wao na shughuli za wamiliki wa migodi haramu ya dhahabu(maarufu kama Galamsey) katika Wilaya ya Amansie ya kati katika Mkoa wa Ashanti.
Kutafuta ukweli
Utafiti uliofanywa na kituo cha Television cha habari “Joy News” uliokuwa na kichwa cha habari “Kodi ya Galamsey: Mtandao wa ulaghai unaochochea uchimbaji haramu,” ulifichua ufisadi wa baadhi ya maafisa wa ngazi serikali za mitaa na kitaifa waliovumilia shughuli za uchimbaji zisizoidhinishwa za kubadilishana na malipo haramu. Baraza la Maaskofu linaeleza shukrani zake kwa dhati kwa uongozi na timu ya uchunguzi, “kwa kazi yao ya kitaaluma na kujitolea kiukweli.” “Katika kipindi hiki ambacho kutafuta ukweli kunaweza kugharimu sana, kazi yao inajali maslahi umma na kuonyesha umuhimu wa vyombo vya habari vilivyo huru na vyenye kuwajibika katika kulinda uwajibikaji wa kidemokrasia,” inasomeka taarifa ya Maaskofu iliyotumwa kwa Shirika la Kipapa la Habri za Kimisionari Fides.
Kwa miongo mitatu maaskofu Ghana wamezungumziwa athari kuhusu uchimbaji haramu
Kuhusu uchunguzi huo, Maaskofu wanasisitiza kwamba “unawasilisha ushahidi wa kile kinachoonekana kuwa mfumo sambamba na utozaji wa kodi unaofanywa ndani ya Wilaya ya Amansie ya Kati. Taasisi za serikali zilizopewa jukumu la kulinda mazingira na kusimamia utekelezaji wa sheria zinadaiwa kushiriki katika shughuli zilezile ambazo zinapaswa kuzuiwa. Hati hiyo inakumbusha kwamba, “Katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Ghana, tumekuwa tukizungumza mara kwa mara kuhusu athari za mazingira na kijamii za uchimbaji haramu.”
Maaskofu walilaani vikali uharibifu wa mazingira
Maaskofu wamelaani vikali uharibifu wa mazingira na kijamii unaofanywa na uchimbaji haramu wa madini, ambao humwaga taka chafu zenye sumu kali katika mito: “Vyanzo vya maji vimechafuliwa, ardhi ya kilimo imeharibiwa na jamii zimehamishwa. Familia zimepata majereha na kupoteza maisha kutokana na njia zisizo salama za uchimbaji. Madhara ya muda mrefu kwa afya ya umma na uharibu wa mazingira ni bado ni endelevu. Changamoto ya uharibifu unaoletwa na uchimbaji haramu ni swala la kitaifa. Hii inahusu ulinzi wa mazingira, utawala wa kisheria na wajibu kwa vizazi vijavyo. Wakati huu unahitaji uwazi, uadilifu na uongozi thabiti.”
Kwa hiyo, Baraza la Maaskofu nchini Ghana linasisitiza hatua zilizopendekezwa na waandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha “Joy News:” kufanyika kwa uchunguzi huru unaoongozwa na Rais; kusimamishwa kazi kwa maafisa waliotajwa katika waraka huo hadi uchunguzi utakapokamilika; ukaguzi wa kifedha wa Halmashauri ya Wilaya ya Amansie ya Kati; na kuanzishwa kwa wakala wa kitaifa wa kufuatilia shughuli za uchimbaji haramu wa madini,” walisisitiza Maaskofu.