Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha. 

Tafakari Dominika ya Kwanza Kwaresima Mwaka A: Jangwa la Maisha Ya Binadamu

jangwa ni mahali ambapo Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi. Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Vatican News, ikiwa tunaanza dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A wa Kanisa. Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka huu 2026 kinanogeshwa na ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV kwa kauli mbiu: “Kusikiliza na kufunga: Kwaresima kama Kipindi cha Wongofu wa ndani.” Kwaresima ni kipindi ambacho Kanisa kama Mama na Mwalimu, anawaalika watoto wake kutoa kipaumbele cha pekee kwa Fumbo la Mungu katikati ya maisha yao, ili imani ipate tena nguvu na mioyo ya waamini isipotee katikati ya mahangaiko na bughudha za maisha ya kila siku. Kila safari ya wongofu wa ndani huanza pale waamini wanaporuhusu Neno la Mungu liwafikie na kulikaribisha kwa moyo wa unyenyekevu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna uhusiano kati ya karama ya Neno la Mungu, Nafasi ya Ukarimu na mabadiliko ambayo Neno hili linaleta. Kwa sababu hiyo, safari ya Kwaresima inakuwa ni fursa muafaka ya kusikiliza sauti ya Mungu na hivyo kupyaisha tena maamuzi ya kumfuasa Kristo Yesu, kwa kutembea katika njia ile iendayo Yerusalemu ambako Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko vinapata utimilifu wake. Hii ni safari ya siku arobaini, safari ya ndani ya moyo, safari ya toba, wongofu na matumaini. Kanisa linatualika tuache kelele za dunia, tuingie jangwani pamoja na Kristo, ili huko tupate nguvu mpya za maisha ya Kikristo.

Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga
Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga

Somo la Kwanza linatukumbusha mwanzo wa safari ya binadamu. Mungum anamwumba Adamu kwa upendo, anamwekea mazingira mazuri, anamwonyesha njia ya uzima. Lakini binadamu anaanguka pale anapomsikiliza mjaribu badala ya kumsikiliza Mungu. Jaribu halikuwa njaa, bali lilikuwa tamaa ya kujitegemea, ya kuwa kama Mungu bila Mungu. Matokeo yake yanakuwa ni hofu, aibu, lawama na kuvunjika kwa uhusiano. Hili, ni simulizi la maisha ya binadamu wa leo. Tunaishi katika dunia iliyojaa maendeleo, lakini mioyo imejaa wasiwasi. Tuna teknolojia, lakini hakuna amani ya ndani. Binadamu anahangaika, anatafuta furaha katika mali, madaraka, umaarufu, lakini bado anaishi jangwani la ndani. Katika somo la kwanza, tunaletewa masimulizi juu ya dhambi ya wazazi wetu wa kwanza dhambi ya kukosa utii kwa Mungu. Masimulizi haya ni mepesi na yenye kueleweka kwa watu wa rika zote, hata hivyo yanabeba mafundisho mazito juu ya maisha yetu ya kila siku. Mwanzoni, Adam na Eva walikuwa wanaishi kwenye bustani iliyojaa matunda. Mungu aliwaruhusu kula matunda ya bustanini isipokuwa yale ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Zaidi ya hilo Mungu aliwaumba wazazi wetu wa kwanza wakiwa huru. Kwa kuwa, uhuru bila mipaka ni utumwa ndiyo maana Mungu aliwawekea mipaka juu ya uhuru wao. Mungu hakuwaruhusu waamue juu ya  lipi ni jema na lipi ni baya – kazi ambayo ni ya Mungu peke yake. Je, kwa nini Mungu aliwakataza binadamu juu ya hilo? Ni kwa sababu: Mosi, binadamu hawezi kuchagua kwa usahihi. Pili, uchaguzi wa binadamu huongozwa na vionjo, hisia na mapendeleo binafsi – matokeo yake ni kuchanganya kati ya mema na mabaya. Mara zote binadamu anapotamani na kufanya majaribio ya kufanana na Mungu anajikuta akijiangamiza yeye mwenyewe.Ndipo Injili ya leo inatuonesha tumaini letu. Yesu naye anaingia jangwani. Anakutana na majaribu yale yale, geuza mawe yawe mkate, jioneshe kwa miujiza, abudu mali na madaraka ulio ugonjwa sugu katika maisha ya mwanadamu lakini Kristo anatupa tiba kuwa imenenwa umwabudu Mungu wako tu. Yesu anatuonesha kwamba nguvu ya kweli haiko katika kumiliki, bali katika kumtii Mungu. Anashinda si kwa nguvu za miujiza, bali kwa Neno la Mungu. Yesu anabaki mwaminifu pale ambapo Adamu alishindwa.

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani   (@Vatican Media)

UFAFANUZI: Mtume Paulo katika Somo la Pili analiweka wazi fumbo hili: kupitia Adamu dhambi iliingia, lakini kupitia Kristo neema imefurika. Kristo ndiye Adamu mpya, ndiye mwanzo wa maisha mapya. Ndiyo maana kauli mbiu yetu leo inasema kwa ujasiri: “Katika Jangwa la Maisha, Kristo Ndiye Nguvu Yetu.”Ndugu wapendwa, jangwa la maisha lina sura nyingi: kwa vijana, ni kuchanganyikiwa na kukosa mwelekeo; kwa familia, ni changamoto za uchumi na mahusiano; kwa wagonjwa na wazee, ni upweke na maumivu; kwa dunia nzima, ni vita, njaa, ukosefu wa haki na uharibifu wa mazingira. Lakini ujumbe wa leo ni mmoja: hatuko peke yetu jangwani. Kristo yupo, anatembea nasi, na anatupatia nguvu ya kushinda. Katika mwaka huu ambapo Kanisa linaadhimisha miaka 800 tangu kifo cha Mtakatifu Fransisko wa Assisi, tunakumbushwa ushuhuda wa mtu aliyelielewa vyema hili. Mt. Fransisko aliuacha ulimwengu wa mali na fahari, akaingia katika “jangwa” la unyenyekevu, umaskini na sala. Na huko jangwani alipata furaha ya kweli, amani ya moyo na uhuru wa ndani. Kristo alikuwa nguvu yake pekee. Tofauti iliyopo kati ya Adamu na Bwana wetuYesu Kristo. Adamu wa kwanza alitamani kuwa sawa na Mungu, matokeo yake ni kwamba kwa dhambi yake kifo kiliingia duniani – adhabu isiyochagua mtu. Adamu wa pili (Yesu Kristo) alitambua kuwa anamtegemea Mungu, hivyo akabaki mwaminifu na mtiifu kwa Baba yake. Mwisho mwishoni aliwekwa kuwa ndiye Bwana wa uzima. Wale watakaonyenyekea kama Yesu hawatakosa thawabu yao. Hivyo ni jukumu letu kama waamini kuchagua upande upi tuufuate?

Nyoka ni kielelezo cha Ibilisi, Shetani
Nyoka ni kielelezo cha Ibilisi, Shetani   (AFP or licensors)

Nyoka amewekwa kama mfano wa kishawishi. Ukweli ni kwamba kishawishi hutujia mara tu tunapoanza kuwa na mwono potofu juu ya Mungu. Daima binadamu hufikiri kwamba Mungu hatupendi, kwani mara zote hutunyima uhuru na furaha yetu. Kwa bahati mbaya kishawishi huwa hakipigi baragumu kuwa sasa kinakuja kutushawishi, ndiyo maana akili huja baadaye baada ya kutenda dhambi, mfano kuangukia katika ulevi, uuaji, uasherati, udanganyifu, a kulipiza kisasi nk. Kwa kutenda dhambi tunajitenga na Mungu. Kwa kujitenga na Mungu tunakuwa watumwa, tunajikuta watupu- kwani kwa dhambi tunalaaniwa. Hata hivyo ikumbukwe kuwa, Mungu hamwadhibu mtu, bali kwa kutenda dhambi binadamu anajiadhibu mwenyewe, mfano kuharibu ndoa, kazi, urafiki, mahusiano ya kifamilia,kuharibu uumbaji, na kukosa amani ya kweli katika moyo  wake. Hii ndiyo hali halisi inayojitokeza katika maisha yetu ya kila siku. Katika Injili tunaletewa masimulizi juu ya vishawishi ambavyo Bwana wetu Yesu Kristo alivipata mwanzoni  mwa kazi yake ya utume. KISHAWISHI kwa chenyewe si dhambi, bali ni changamoto inayotupa wasaa wa kujipima juu ya uchaguzi wetu katika maisha. Vishawishi vilivyoorodheshwa hapa ni muhtasari tu wa vishawishi vingi ambavyo Yesu alikumbana navyo katika maisha yake hapa duniani. Katika yote haya Yesu hakufadhaishwa, daima alimshinda shetani.

Kwaresima ni kipindi cha sala, toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni kipindi cha sala, toba na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

Katika kishawishi cha kwanza, Yesu anashawishiwa atumie vibaya uwezo wake wa kimungu. Hata hivyo anamjibu shetani kuwa maisha ya binadamu hayategemei tu chakula cha kimwili, bali pamoja na mambo mengine binadamu anahitaji pia chakula cha kiroho ambacho ndiyo Neno la Mungu. Kama wakristo hatuwezi kukwepa kukumbwa na vishawishi kwani Yesu mwenyewe  alishawishiwa. Je, tunafanya nini baada ya kushawishiwa? Daima tusiruhusu hata mara moja vishawishi vitutawale,badala yake tuvitawale kama Yesu  alivyofanya. Katika vita hivyo hatuna budi kwanza kutambua uwepo wa vishawishi katika mazingira tulipo na kisha kupigana navyo. Tusivitoroke vishawishi, bali tukabiliane navyo. Vile vile tusiwe na mwono hasi tu juu ya vishawishi kwani vinatusaidia kwa namna moja ama nyingine  kujipima ni kwa kiasi gani tu thabiti katika ukristo wetu. Wakristo tujijengee fadhila ya unyenyekevu kwani itatusaidia kuipokea hali yetu tuliyonayo ya kuwa viumbe. Kwa kufanya hivyo hatutatamani mambo makubwa yapitayo uwezo wetu na daima tutamtegemea Mungu aliye muumba wetu katika yote tufanyayo. Tumwombe Mungu atujalie neema yake ili tuzing’amue hila za shetani na kuzishinda, mwisho mwishoni tuurithi uzima wa milele mbinguni. Hivyo basi, Kwaresima si kipindi cha kujiumiza, bali ni kipindi cha kuimarishwa. Kwa sala, tunapata nguvu ya kusikiliza Mungu. Kwa kufunga, tunapata uhuru dhidi ya tamaa. Kwa matendo ya huruma, tunavunja jangwa la ubinafsi. Leo Bwana anatualika tujiulize, Ni jangwa gani ninalopitia katika maisha yangu? Ni jaribu lipi linanirudia kila mara? Je, Kristo ndiye nguvu yangu, au bado ninategemea vitu vya dunia? Tukiikubali safari hii ya Kwaresma kwa moyo wazi, basi jangwa halitakuwa mahali pa kuangamia, bali mahali pa kukutana na Mungu. Na Pasaka itatukuta tukiwa watu wapya, mioyo iliyobadilika, na tumaini jipya. Katika jangwa la maisha, Kristo kweli ndiye nguvu yetu.Tukishikamana naye, hatutashindwa katika safari hii ya jangwani ya siku arobaini za mapambano ya maisha ya kiroho.Amina.

Liturujia D Kwanza Kwaresima

 

21 Februari 2026, 15:33