Alhamisi Takatifu:Siku ya kukumbuka zawadi ya Ukuhani Alhamisi Takatifu:Siku ya kukumbuka zawadi ya Ukuhani  (Vatican Media)

Alhamisi Kuu-Karamu ya Bwana:Upendo,Ekaristi Takatifu na Upadre

Siku ya Alhamisi Kuu,Kanisa linaadhimisha kuwekwa kwa;Sakramenti ya Ekaristi Takatifu,Sakramenti ya Daraja Takatifu–Upadre na Amri Kuu ya mapendo.Ni katika mukatdha huu Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali:“Ee Mungu, tunaadhimisha Karamu Takatifu ya Mwanao wa pekee.Yeye alilikabidhi Kanisa kwa siku zote sadaka mpya na karamu ya upendo wake.Tunakuomba utujalie,tujipatie wingi wa mapendo na uzima katika fumbo hili kubwa.”

Na Padre Paschal Ighondo -Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, siku ya Alhamisi Kuu, siku ya kwanza kati ya siku kuu tatu za kuadhimisha Fumbo la Wokovu wetu, Pasaka - Mateso, Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hili ni adhimisho moja tu, linalodumu kwa muda wa siku tatu - Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Takatifu. Siku ya Alhamisi Kuu, Kanisa linaadhimisha kuwekwa kwa; Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu – Upadre, na Amri Kuu ya mapendo. Ni katika mukatdha huu Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali: “Ee Mungu, tunaadhimisha Karamu takatifu ya Mwanao wa pekee. Yeye alilikabidhi Kanisa kwa siku zote sadaka mpya na karamu ya upendo wake. Tunakuomba utujalie, tujipatie wingi wa mapendo na uzima katika fumbo hili kubwa.”

Kateksimu ya Kanisa Katoliki kwa kunukuu maandiko matakatifu inafundisha kuwa; Mwokozi wetu, katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake. Alifanya hivyo ili kuendeleza sadaka ya msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo chake na ufufuko wake: sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo tunapewa amana ya uzima wa milele (KKK 1323). Kumbe Alhamisi Kuu, ndiyo siku inapoanza Pasaka ya Kikristo. Tukumbuke kuwa hii ni siku ya mapadre, tuwaombee na kuwaenzi kwa kuwapongeza, inapobidi na kuwezekana.

KUMBUKIZI YA PAPA FRANCISKO WAKATI AKIOSHA MIGUU WAFUNGWA WA KIKE 2024
KUMBUKIZI YA PAPA FRANCISKO WAKATI AKIOSHA MIGUU WAFUNGWA WA KIKE 2024   (Vatican Media)

Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka (Kut 12:1-8, 11-14). Ni simulizi la mwanzo, wa Pasaka ya Wayahudi, namna walivyopaswa kuiadhimisha na masharti yake walipokombolewa kutoka utumwani Misri. Sikukuu hii ya Pasaka kwa Mayahudi ilikuwa ukumbusho wa kukombolewa kutoka utumwani mwa Wamisri. Nayo ilikuwa ni dokezo la Pasaka yetu - wokovu ulioletwa na Kristo: Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Ndiyo maana Katekisimu ya Katisa katoliki inatufundisha hivi; “Taifa la Mungu, tokea sheria ya Musa, lilijua sikukuu zisizobadilika kuanzia Pasaka, kwa ajili ya kukumbuka matendo mastaajabifu ya Mungu Mwokozi, kumshukuru na kudumisha kumbukumbu na kufundisha vizazi vipya ili mwenendo wao ulingane nazo. Nyakati za Kanisa, katika Pasaka ya Kristo iliyotekelezwa mara moja kwa nyakati zote na utimilifu wake katika ufalme wa Mungu, liturujia inayoadhimishwa imejazwa kabisa upya wa fumbo la Kristo” (KKK 1164).

Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je! si ushirika wa damu ya Kristo? (1Kor. 10:16). Nimrudishie Bwana nini, kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; na kulitangaza jina la Bwana. Ina thamani machoni pa Bwana, Mauti ya wacha Mungu wake. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, mwana na mjakazi wako, umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; na kulitangaza jina la Bwana; Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana, naam, mbele ya watu wake wote” (Zab. 116:12-13, 15-18).

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 11:23-26). Nalo linatueleza kuwa Ekaristi Takatifu hutuunganisha wakristo wote kuwa ndugu. Pia kila tunapokula vema karamu hii tunashiriki na kutangaza kifo na ufufuko wake Kristo. Tunasoma hivi; “Bwana wetu Yesu Kristo, usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema; Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema; “Kikombe hiki ni Agano Jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo kwa ukumbusho wangu…Maana kila mlapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo”. Katekisimu ya Kanisa Katoliki ikifuata haya maandiko matakatifu inafundisha hivi; “Komunyo takatifu ya Mwili na Damu ya Kristo hukuza umoja wa yule anayeshiriki pamoja na Bwana na humuondolea dhambi ndogo na kumkinga na dhambi kubwa. Zaidi ya hayo huimarisha vifungo vya mapendo kati ya mshiriki na Kristo. Kupokea sakramenti hii huimarisha umoja wa Kanisa, Mwili wa fumbo wa Kristo” (KKK 1416).

YESU AKIOSHA MIGUU MITUME WAKE
YESU AKIOSHA MIGUU MITUME WAKE

Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 13:1-15). Ni maelezo na ufafanuzi wa tendo la Yesu kuwaosha miguu mitume wake baada ya mlo wa kipasaka, Alhamisi Kuu. Tendo hili ni alama ya utumishi na upendo wake kwa wanadamu wote. Kwa tendo hili, Yesu alituachia wosia wa kupendana sisi kwa sisi. Yeye aliye Bwana na Mwalimu, Mfalme, Masiha, Mwokozi, Mungu kweli katika nafsi ya pili, alijishusha, akajinyenyekeza, na kwa upendo mkubwa aliwaosha wanafunzi wake miguu. Kisha aliwaambia; “Kama mimi niliye Bwana na mwalimu nimefanya hivi, ninyi nanyi fanyeni vivyo hivyo”. Ujumbe kwetu ni kuwa tupendane kama Kristo anavyotupenda. Upendo ni utambulisho wetu – “mkipendana ninyi kwa ninyi watu watawatambua kuwa mu-wafuasi wangu”. Kupendana ni kukaa ndani ya Kristo na kulishika neno lake; “Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu” (Yn.15:4), “mtu akinipenda atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda nasi tutakuja kwake na kukaa naye” (Yn. 14:23).

Kwa tendo la kuwaosha mitume miguu, Yesu aliwasimika kuwa makuhani kwa ajili ya kutolea dhabihu na sadaka kwa Mungu katika maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu kama ilivyokuwa desturi katika Agano la Kale kwa makuhani kuosha miguu kabla ya kumtolea Mungu dhabihu. Mwenyezi Mungu alimwambia Musa; “Utatengeneza birika la shaba la kutawadha…uliweke katikati ya hema la kukutania na madhabahu, na kutia maji ndani yake. Aroni na wanawe watatumia maji hayo kunawia mikono na miguu kabla ya kuingia kwenye hema la kukutania au kukaribia madhabahu ili kunitolea dhabihu mimi Mwenyezi Mungu…hii itakuwa kanuni kwao daima, tangu Aroni na uzao wake, vizazi hata vizazi” (Kut.30:17, 21).

Kusimikwa kwa mitume kuwa makuhani, ilikuwa ni maandalizi ya kuendeleza sadaka ya Kristo ambayo alikuwa anaenda kuitoa kwa kuyatoa maisha yake kwa kufa msalabani. Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya utangulizi wa siku hii anasali hivi; “Ndiye kuhani wa kweli na wa milele, aliyeanzisha sadaka hii ya daima. Ndiye wa kwanza aliyejitoa mwenyewe kwako Mungu kuwa sadaka ya wokovu, akatuamuru tuitoe kwa kumkumbuka yeye. Tunapata nguvu tuulapo mwili wake uliotolewa sadaka kwa ajili yetu; tunatakaswa tuinywapo damu yake aliyomwaga kwa ajili yetu sisi”. Na katika sala ya kuombea dhabihu anasali; “Ee Bwana, tunakuomba utujalie kuadhimisha vema mafumbo haya, kwa maana kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inafanyika” (rej. SC 2).

FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA
FANYENI HIVI KWA KUNIKUMBUKA

Huu ndio utajiri tulionao katika Ekaristi Takatifu kwamba tunasamehewa dhambi zetu na kurudishiwa uhusiano na urafiki wetu na Mungu katika Sadaka ya Misa Takatifu. Hivyo Ekaristi Takatifu, hutuunganisha na Kristo, hudhoofisha nguvu ya dhambi na ni amana ya uzima wa milele, aliyotuachia Yesu Kristo siku ya Alhamisi Kuu. Mama Kanisa akilitambua hili, ameweka utaratibu wa kukesha na kuabudu Ekaristi Takatifu Siku ya Alhamisi Kuu baada ya Misa ili kukaa pamoja na Yesu, tukitafakari upendo wake kwetu sisi, upendo alioudhihirisha katika kujitoa kwake Sadaka msalabani na sasa yupo katika Ekaristi Takatifu. Kateksimu ya Kanisa Katoliki inafundisha hivi; “Kwa kuwa Kristo mwenyewe yumo katika sakramenti ya altare ni lazima kumheshimu kwa ibada ya kuabudu. Maonano ya Sakramenti Takatifu Sana ni kipimo cha shukrani, ishara ya mapendo na mujibu wa kumwabudu Kristo - Bwana wetu” (KKK 1418).

Basi, tutumie vema muda huo kumwabudu na kumshukuru Kristo kwa zawadi ya ukombozi na tumwombe neema ya kuweza kuwa waaminifu katika maisha yetu ya kiimani na kimaadili ili mwisho wa maisha ya hapa dunia tukafurahi naye milele yote mbinguni. Ndiyo maana Kateksimu ya Kanisa Katoliki inafundisha hivi; “Kwa kuwa Kristo ametoka katika ulimwengu huu kwenda kwa Baba, katika Ekaristi tunapata amana ya utukufu ujao pamoja naye” (KKK 1419). Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho ya siku hii anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, kwa vile tunavyotiwa nguvu na karamu ya Mwanzo hapa duniani, utujalie tuje tushibe karamu ya milele mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu.

PAD IGHONDO:TAFAKARI YA ALHAMISI KUU

Tumsifu Yesu Kristo.

31 Machi 2026, 16:47