Kard.Pizzaballa huko Getsemani:"Wakati mgumu sana,tunataka amani"
Roberto Paglialonga na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Pierbattista Pizzaballa, Patriaki wa Kilatini wa Yerusalemu, aliongoza sala maalum ya amani kutoka Gethsemane, chini ya Mlima wa Mizeituni, katika sherehe ya Dominika ya Matawi. Sala hiyo ilifanyika saa chache tu baada ya mamlaka ya Israeli kuwazuia Kardinali Pizzaballa na Padre Francesco Ielpo, Msimamizi Nchi Takatifu, kuingia kwenye Kaburi Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Misa. "Tunapitia hali ngumu sana, tumekusanyika kwa sababu tunataka kujenga amani, undugu," Patriaki huyo alisisitiza mwanzoni mwa sherehe hiyo, ambayo ilifanyika bila mahujaji.
Bila maandamano,bila matawi
Kardinali Pizzaballa aliendelea kusema kuwa "Leo alasiri hii ya Dominika ya Matawi, tuko hapa bila maandamano, bila matawi ya kupunga mikono juu mitaani. Na si kutokuwepo rasmi, lakini ni kutokana na vita, ambavyo vimesimamisha safari yetu ya sherehe, na kufanya hata furaha rahisi ya kumfuata Mfalme wetu kuwa ngumu. Kaka na dada zetu katika Nchi Takatifu leo hawawezi kujaza mitaa au kujiunga na sauti zao katika maandamano ya sherehe," alisema. Hata hivyo, "kutokuwepo kwao si tupu mbele ya Bwana," kwa sababu "Hatafuti njia za ushindi; Anaingia mahali ambapo mlango upo wazi, ambapo uaminifu ndio mkate wetu wa kila siku."
Aliyefufuka miongoni mwetu,hata Barabara inapokuwa imezuiwa
"Aliyefufuka Aliyesulubiwa Haachi kamwe kupita miongoni mwetu. Hata barabara inapokuwa imezuiwa," alisisitiza, akizungumza kutoka madhabahuni katika Kanisa Kuu la Gethsemane linaloangalia kuta za Jiji Takatifu, na kuzungukwa na wakonselebranti wengi, "Anakaa mioyoni mwa wale ambao hawajaacha kumfuata. Lakini haswa katika ukimya huu wa kulazimishwa, liturujia hii inakuwa halisi zaidi. Kwa sababu kilio cha 'Hosana' hakihitaji matawi kupanda mbinguni, na imani haipindi wakati ibada za nje zinakosekana."
Yesu analia juu ya Yerusalemu na Nchi Takatifu bila amani
Lakini leo Yesu anarudi kulia juu ya Yerusalemu. "Analia juu ya mji huu, ambao unabaki kuwa ishara ya matumaini na maumivu, ya neema na mateso. Analia juu ya Nchi hii Takatifu ambayo bado haiwezi kutambua zawadi ya amani. Na tena: "Analia juu ya waathiriwa wote wa vita ambavyo havionyeshi dalili yoyote ya mwisho, juu ya familia zilizogawanyika, juu ya matumaini yaliyovunjika. Lakini machozi ya Yesu hayajawahi kuwa tasa: yanatufumbua macho, yanatupinga, yanatufunulia ukweli."
Mashahidi wa upendo usiokata tamaa,nguvu ya kweli haiko katika vurugu
Kwa hivyo, Pizzaballa aliendelea, "katika nchi hii inayoendelea kusubiri amani, tumeitwa kuwa mashahidi wa upendo usiokata tamaa. Safari yetu ya imani, hata leo, iwe safari ya matumaini. Na maisha yetu, licha ya ukali wa sasa, yaweze kuleta upendo wa Kristo na nuru yake ambapo yote yanaonekana kuwa giza."
Akitoa maoni kuhusu Mateso, Patriaki, huyo kisha alizingatia usaliti wa Yuda, kukataa kwa Petro, ukimya wa Pilato, vilio vya umati unaoita msalaba na kifo cha Yesu, lakini pia juu ya umbo la akida: "anagundua kwamba nguvu ya kweli haiko katika vurugu au katika upanga unaoua, bali katika maisha yaliyotolewa bure." Na hivyo, katika wakati huo wa kusisimua, "anakiri kwa nguvu zote: mtu huyu ni Mwana wa Mungu. Wakati hasa ambapo kifo kinaonekana kushinda, ukweli unafunuliwa, upendo unadhihirishwa na wokovu unatimizwa."
Amani ni tunda la Msalaba: Mungu anajitoa kikamilifu
Hata leo, huku vita vikionekana kukandamiza kila neno la amani, hapa, ambapo Yesu alilia, tunaweza kusikia ungamo lile lile likivuma. Neno la mwisho la Mungu ni kaburi tupu. Ni Bwana anayewatangulia wanafunzi huko Galilaya na ambaye pia anatutangulia, akituongoza kuelekea amani ambayo si udanganyifu, bali tunda la Msalaba," kardinali alisema. Kwa hivyo, "amani ambayo Yesu anatoa si makubaliano dhaifu kati ya maadui, bali amani iliyozaliwa kutokana na Msalaba, amani inayotoka kwa Mungu anayejitoa kikamilifu na hana haja ya nguvu au silaha. Hiki ndicho kitendawili tunachoitwa kukikumbatia leo. Kwa sababu Yerusalemu, Nchi Takatifu, si eneo la kijiografia tu; ni moyo unaopiga wa imani yetu. Kila jiwe hapa linazungumzia wokovu; kila kilima kina kumbukumbu ya Mungu aliyechagua kukaribia," aliongeza. Kwa sababu hiyo "kuishi imani katika nchi hii kunamaanisha kukubali utata unaojitokeza: mahali pa ufufuo pia ni mahali pa Kalvari; mahali pa kukumbatiwa na Mungu bado pana alama ya chuki nyingi."
Kubeba msalaba na kuwa wajenzi wa upatanisho
Hata hivyo, hasa kutoka mahali hapa patakatifu, "tunajifunza kutazama mji kwa macho ya Kristo. Tunajifunza kulia pamoja naye, lakini pia kutumaini pamoja naye. Kwa sababu Yerusalemu ile ile iliyomkataa Mkuu wa Amani pia iliona kaburi tupu. Vita haitafuta ufufuo. Maumivu hayatazima tumaini. Leo, bila mitende, badala yake tunabeba msalaba, si mzigo usiofaa, bali chanzo cha amani ya kweli. Tusipunge matawi ya mizeituni; badala yake tuchague kuwa wajenzi wa upatanisho, kupitia kila ishara, kila neno, kila uhusiano,” alihitimisha Patriaki.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.