Maaskofu wa Cameroon katika maandalizi ya kufika kwa Papa Leo XIV. Maaskofu wa Cameroon katika maandalizi ya kufika kwa Papa Leo XIV.  

Cameroon yatoa wito wa kupyaishwa na haki kabla ya Ziara ya Papa

Ziara inayotarajiwa ya Papa Leo XIV nchini Cameroon,imefufua upya matumaini ya amani na haki na ufufuko wa mataifa huku kukiwa na migogoro inayoendelea. Askofu Mkuu Samuel Kleda wa Douala ametoa wito wa kuachiliwa kwa wafungwa waliofungwa bila kushtakiwa na kuhimiza mabadiliko ya pamoja ya mawazo.Ziara hiyo inaonekana kama wakati mwafaka kwa watu wa Cameroon kukumbatia maridhiano,kupambana na ufisadi na kujenga upya Taifa lao.

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Cameroon inapojiandaa kumkaribisha Papa Leo XIV, Askofu Mkuu Samuel Kleda wa Douala alitoa wito wa dhati kwamba ziara hii ya kihistoria inayoweza kuhamasisha kuachiliwa kwa watu waliofungwa bila kushtakiwa na kuchochea mabadiliko mapana ndani ya jamii. Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari mnamo tarehe 9 Aprili 2026,  Askofu Mkuu aliita ziara ya Kitume ya Papa kama wakati wa neema, unaozingatia kutangazwa kwa Habari Njema ya amani, upyaishaji na haki.

Shirika la habari la Kipapa la Kimisionari Fides, linabainisha kwamba kwa Askofu Mkuu Kleda, alisisitiza kwamba amani si wazo dhahania bali ni hitaji la dharura. "Kwa wakati huu, sote tunahitaji amani nchini Cameroon," alisema huku akisisitiza umuhimu wa uwepo wa Papa kama wito kwa kila raia kuwa mleta amani.

Migogoro na mateso ya wanadamu

Cameroon inaendelea kukabiliana na migogoro mingi, hasa mgogoro unaoendelea katika maeneo yake yanayozungumza Kiingereza. Machafuko haya ya muda mrefu yamesababisha watu wengi kuhama makazi yao, mateso, na kutokuwa na utulivu. Askofu Mkuu alitaja ukweli huu kama muhimu kwa hitaji la nchi la uponyaji na maridhiano. Mbali na changamoto za usalama, taifa linakabiliwa na mdororo mkubwa wa kiuchumi. Kuongezeka kwa ukosefu wa ajira na umaskini kumewaacha raia wengi wakipambana kukidhi mahitaji ya msingi. Askofu Mkuu Kleda alisisitiza uharaka wa kushughulikia maswala haya magumu, akielezea matumaini kwamba ziara ya Papa inaweza kuhamasisha mabadiliko yanayoonekana na kujitolea upya kwa manufaa ya wote.

Mvutano baada ya Uchaguzi na wito wa haki

Hali ya kisiasa nchini Cameroon bado ni tete kufuatia uchaguzi wa rais wenye utata uliofanyika Oktoba iliyopita. Kuchaguliwa tena kwa Rais Paul Biya, huku kukiwa na madai ya ukiukwaji wa sheria, kulisababisha maandamano yaliyoenea, haswa huko Douala. Baadaye, watu wengi walikamatwa. Ingawa baadhi ya wafungwa wameachiliwa huru tangu wakati huo, wengi bado wamefungwa na wengine bado hawajafikishwa mahakamani. Askofu Mkuu Kleda alielekeza umakini kwenye hali yao, akielezea hali hiyo kama dhuluma kubwa. Alitoa wito kwa mamlaka kutumia fursa iliyotolewa na ziara ya Papa kurekebisha makosa haya na kuhakikisha kuachiliwa kwa wale waliofungwa bila haki.

Ni wakati wa upyaishaji wa maadili na kiroho

Hii ni ziara ya nne ya Papa ya kihistoria nchini Cameroon, jambo ambalo Askofu Mkuu Kleda alilielezea kama "baraka maalum." Lakini pia alikiri kwamba ziara za awali hazikuleta mabadiliko ya kudumu ya kijamii. "Sisi si watakatifu," alikiri, akibainisha mapambano ya nchi kuishi kwa maadili ya Injili. Askofu Mkuu alisisitiza kuwa ziara hii kama mwaliko mpya wa uongofu wa kibinafsi na wa pamoja. Kadhalika alifafanua umuhimu wa kushiriki rasilimali za kitaifa kwa usawa, akipata msukumo kutoka kwa jamii ya Wakristo wa kale kama ilivyoelezwa katika Matendo ya Mitume.

Kukabiliana na rushwa na kujenga manufaa ya wote

Kitu muhimu katika ujumbe wa Askofu Mkuu Kleda ni hitaji la haraka la kupambana na ufisadi, ambalo alilielezea kama nguvu iliyoenea inayodhoofisha maendeleo na haki. Alionya kwamba ufisadi huharibu kila kitu na kuzuia taifa kutambua uwezo wake kamili. Alihitimisha kwa wito wenye nguvu wa kuchukua hatua kwamba kila mzaliwa wa Cameroon awe tayari kwa uongofu na kujitolea kwa haki. Ziara ya Papa Leo XIV si tu tukio la kusherehe bali ni wakati muhimu unaotupa fursa kama wenyeji wa Cameroon kufungua ukurasa mpya na kuelekea mustakabali wa amani, utu, na ustawi wa pamoja.

CAMEROON ASKOFU MKUU KLEDA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

14 Aprili 2026, 10:05