Watawa wa Pallotini nchini Tanzania wanaweka Kipaumbele cha Elimu. Watawa wa Pallotini nchini Tanzania wanaweka Kipaumbele cha Elimu.  #SistersProject

Miujiza ya Kimungu:Jinsi watoto Walemavu Tanzania wanavyopata Faraja kituoni Singida

“Watoto walemavu wanahitaji matunzo,heshima na fursa sawa kama watoto wengine kwenye jamii.Katika kuwahudumia nimeng’amua maana ya wito wangu na furaha ya kuwatumikia wengine,”alisema Sr. Rosemary Ombay,Mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha Watoto wenye ulemavu Siuyu.

Na Sr. Ernestina Patrick Lasway SAC

Sr.Rosemary alijiunga na Shirika la Masista Wapallottini, akiitika wito wa kumtumikia Mungu kwa maisha ya wakfu. Ingawa mwanzoni alikuwa na matamanio ya kumtumikia Mungu kwa njia ya uuguzi, alielekezwa baadaye kuwa mtaalamu wa Tiba Kazi (Occupational Therapy),kazi aliyoipenda na kuifanya kwa imani na uaminifu kwa Mungu. Kama Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Watoto Walemavu Siuyu, anatoa huduma kwa watoto hawa.

Kwa zaidi ya miaka 15 sasa, Sr. Rosemary amekuwa akisimamia shughuli na mwenendo wa kituo, huku akihakikisha kuwa kila kitu kinafanyika kwa umakini na ufanisi mkubwa. Anasimamia matunzo na huduma zitolewazo kwa watoto,akitetea utoaji wa elimu sawa kwa watoto hasa katika madarasa ambayo hushiriki pamoja na watoto wasio na ulemavu.

Kusaidia watoto walemavu kwa upendo na unyenyekevu

Nipo kwa Sababu Tupo

Katika mkoa wa Singida, watoto wenye ulemavu, huonekana kama balaa kwenye jamii. Familia nyingi huwaficha ndani ili kutoeneza balaa hili. Kuanzisha kwa kituo cha watoto wenye ulemavu, kimesaidia kubadilisha mtazamo huu na kuwasaidia watoto hao kupata elimu ya msingi na sekondari, kwenye shule iliyopo karibu na kituo. Hii imesaidia na kuwajengea uwezo watoto wengi. Baadhi yao wamefikia taaluma zao na kuchagua kusoma ualimu, uhasibu na sheria. Kwa kuchangamana na watoto wasio na ulemavu shuleni, imewasadia kujisikia kuwa wao ni sehemu ya jamii.

Watoto kutoka kituoni wakielekea shuleni

Kuwajengea watoto uwezo

“Lengo langu ni kuwasaidia watoto wenye ulemavu na kuwaelekeza wazazi kuendeleza mazoezi na matunzo wawapo nyumbani,” alisema Sr.Rosemary. Watoto wengi hukaa kituoni. Wengine, hasa wenye umri chini ya miaka 6 wanaishi kwenye familia na hufika katika mazoezi kituoni walau mara mbili kwa Juma. Hii ni kwa sababu ya miundo mbinu kutokukidhi mahitaji.

Sr. Rosemary anaeleza furaha aliyo nayo anapoona watoto wanasaidiwa na baadhi yao kuweza kujitegemea.  Wengine hufika kituoni wakiwa hawawezi kutembea. Baada ya mazoezi stahiki na huduma bora za afya, taratibu wanasaidika na kurudi nyumbani kwa miguu yao. Watoto wanashukuru sana, na huwa tayari kushiriki kufanya kazi ndogondogo kituoni, huku wakiamini kuwa “Ulemavu siyo kutokuwa na uwezo.”

Kufanya kazi katika Jamii

Kwa takribani miaka 15 ya huduma katika kituo cha Walemavu cha Siuyu huko Singida, Sr. Rosemary anabainisha kuwa kazi hii siyo rahisi. Lakini pia anabainisha jinsi ambavyo ni kazi yenye manufaa kwa jamii. Jumuiya iliyokuwa ikitazama ulemavu kama balaa, awali hawakuona sababu ya kutafuta usaidizi kwa watoto wao. Baada ya kushuhudia jinsi watoto wanavyosaidiwa kupitia kituo hiki, wameanza kuwaleta kituoni katika mazoezi. Kituo kimeendelea kukua kutoka idadi ya watoto 6 kilipoanzishwa mwaka 2017, hadi zaidi ya watoto 60, 2026, na kuhudumia watoto kutoka Singida na mikoa jirani.

Kwa kugundua kuwa watoto wengine wenye ulemavu bado wanabakizwa majumbani, Sr. Rosemary alianzisha mafunzo kwa vitendo kwa kikundi cha akina mama wanaosaidiana naye kuwafanyia watoto mazoezi kituoni. Kwa uzoefu huu wa mafunzo kwa vitendo, akina mama hawa wamekuwa msaada mkubwa kwa wazazi na jamii, kwa kuelimisha namna ya kuwatunza na kuwasaidia watoto.

Mafunzo haya yamezaa matunda makubwa hasa kwa Singida vijijini, ambapo wakina mama wenye uzoefu wamejitolea muda na nguvu zao kuleta mabadiliko kwenye jamii. “Ninaguswa na kujifunza mengi kutoka kwa watoto hawa. Nafurahia upendo kati yao, hasa wanapoonesha jitihada za kusaidiana wenyewe kwa wenyewe, kwa kadiri inavyowezekana,” alitamatisha Sr. Rosemary.

KITUO CHA WATOTO SIUYU SINGIDA

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.

08 Aprili 2026, 09:04