Sudan Kusini:Mgogoro wa kibinadamu bila mazungumza nchi inabaki mateka wa migogoro
Na Patriza Caiffa – SIR.
Askofu Christian Carlassare, wa Jimbo Katoliki la Bentiu nchini Sudan Kusini, alilaani kuibuka tena kwa migogoro na kuongeza kwa vurugu za kibinadamu, huku makumi ya waathiriwa, maelfu ya watu waliokimbia makazi yao, na upatikanaji mdogo wa misaada. Alisema hayo katika Mahojiano yaliyofanywa na Shirika la Habari Katoliki Italia (SIR). Operesheni za kijeshi pia zinaathiri raia, huku mchakato wa amani ukibaki haujakamilika na umegawanyika. Mazungumzo ya kisiasa yamekwama, na uchaguzi wa Desemba 2026 uko hatarini kuzuka tena kwa vurugu. Kwa maelezo ya Askofu, mzizi, ni mivutano ya kikabila na mapambano ya rasilimali, katika nchi isiyo na utambulisho wa kweli wa kitaifa na serikali zikiwa zimefungiwa mazungumzo. Kanisa linatoa wito wa maridhiano na kuweka matumaini hai katika vizazi vijavyo.
"Sudan Kusini itaendelea kuwa mateka wa migawanyiko na migogoro hadi lini, na kuwazuia watu wake kunufaika na rasilimali zake? Sio nchi maskini, bali ni nchi: tajiri ya rasilimali, lakini yenye watu wanaoishi katika umaskini na ukosefu wa usalama." Swali muhimu linalopendwa na moyo wa Askofu Christian Carlassare, Askofu wa Bentiu na mmisionari wa Comboni. Ameijua Sudan Kusini kwa zaidi ya miaka ishirini na anaipenda sana. Asili yake ni kutoka Vicenza nchini Italia, Askofu Carlassare mwenye umri wa miaka 49 amehudumu katika majimbo kadhaa kama vile (Malakal, Rumbek), ambapo nchi hiyo ilipata uhuru mwaka 2011, akiwa na shauku ya amani mpya, lakini pia alipitia vurugu moja kwa moja: Mwaka 2021, alipata jeraha la mguu kwa risasi, lakini kwa bahati nzuri, amepona kikamilifu. Leo hii anatazama kwa wasiwasi jinsi mivutano na mauaji yanavyoibuka, na kuwaacha makumi ya maelfu ya watu wakimbizi, wakiteseka na utapiamlo na njaa.
Matatizo ni mengi na ni kufanya kila kitu
Ripoti za hivi karibu zinazungumzia janga la kibinadamu linaloendelea Nyatim, Kaunti ya Nyirol, Jimbo la Jonglei, huku zaidi ya watu 30,000 wakikimbia vurugu huko Lankien na Pieri. Kulingana na Madaktari Wasio na Mipaka, (MSF),karibu watu 58 wamekufa katika majuma manne yaliyopita (makadirio ya chini), huku mamlaka zikizuia ufikiaji wa mashirika ya kibinadamu. Jimbo la Bentiu lilianzishwa na Papa Francisko mwaka mmoja na nusu uliopita. Askofu Carlassare anafanya huduma yake ya kiaskofu kwa njia isiyo ya kawaida kutokana na hali za ndani. "Hatuna matatizo yanayofanana sawa na Maaskofu katika sehemu zingine za dunia," alisema kwa simu akitokea Bentiu. "Hapa, kila siku tunapaswa kufanya kila kitu: kuanzia mfagiaji wa barabarani hadi mpishi, kuanzia kufua nguo hadi kuondoa matope. Lazima ufanye." Jimbo pia linawakaribisha watawa kumi wa majimbo kutoka Jumuiya ya Wamisionari wa Comboni, na jumuiya ya Wafransiskani Wakapuchini.
Hatua ya kijeshi ya serikali, majeruhi wengi mno wa raia
Tangu mwezi Aprili 2026, baada ya mabomu huko Nasir na Dacobo, serikali ya Sudan Kusini, inayoongozwa na Rais Salva Kiir, ambayo mwaka 2025 ilimkamata Makamu Rais, Riek Machar, imepeleka hatua za kijeshi katika maeneo kadhaa ili kuzima makundi ya upinzani: "Lakini inaishia kuwalenga raia pia. Silaha ziko kila mahali, mikononi mwa wengi: kila mtu anaweza kuwa mpiganaji. Kwa mantiki hii, wanaishia kuwalenga kila mtu." Askofu huyo anasimulia tukio la kutisha. Alipoulizwa kwa nini raia pia walikuwa wakilengwa, alijibu: "Israeli inafanya nini huko Palestina? Tatizo, kulingana naye, ni kwamba raia wako pamoja na 'magaidi,' pamoja na wale wanaopinga serikali; kwa hivyo, ni kosa lao ikiwa wakilengwa."
Mkataba wa amani ulilenga jeshi lililoungana, likiwaunganisha tena wanamgambo wote, "lakini hilo halikutokea," Askofu Carlassare alithibitisha. Kulikuwa na ujumuishaji upya kuanzia 2019 hadi 2021; hata hivyo, kwa kukamatwa kwa Riek Machar na baadhi ya watu wa upinzani, jeshi liligawanyika tena: makundi hayo yaliachwa kujikusanya tena ndani ya vikosi vya upinzani, na kuna mkanganyiko mwingi miongoni mwa wanamgambo."
Kufungwa kwa mazungumzo. Uchaguzi uko hatarini kwa vurugu?
Askofu Carlassare alibainisha mtazamo wa kufungwa kwa mazungumzo, pia kufuatia kushindwa kwa Mazungumzo ya Tumaini, mazungumzo kati ya serikali na makundi ambayo hayakusaini makubaliano ya amani ya 2018 yaliyosimamiwa na Kenya. "Watu wameacha kuwachukulia wengine kama waingiliaji kati, hata wanapokuwa serikalini wakiwa na mawazo tofauti. Wanapendelea kuwatenga, ili kufikia kura bila njia mbadala yoyote halisi," akusema. Uchaguzi huo, ambao uliahirishwa kila mara, umepangwa kufanyika Desemba 2026. Askofu ana shaka: "Masharti ya kuyapanga hayapo: hakuna vyama vilivyopangwa, majimbo ya uchaguzi, au sensa. Bila masharti ya chini kabisa, hatari ni kwamba uchaguzi utaongeza vurugu."
"Jambo la kusikitisha ni kwamba watu ndio wanaoshindwa"
Maneno ya Askofu Carlassare yanaelezea janga la nchi ambapo "kila mtu anajaribu kudumisha msimamo wake," huku usalama, huduma, na matarajio ya maendeleo yakibaki kuwa kama ndoto. "Watu wanaomba tu kiwango cha chini cha usalama," lakini msaada unapungua, na mashirika ya kibinadamu yanaonekana kwa mashaka, "kwa sababu yanachukuliwa kuwa hayana msimamo." Kwa mfano, wakati wa operesheni huko Jonglei, "mashirika yote yaliombwa kuhama eneo hilo wakati wa mashambulizi, rasmi kwa sababu za kiusalama, lakini pia kuepuka mashuhuda." Matokeo yake ni dharura inayozidi kuwa mbaya: "idadi halisi ya watu waliokimbia makazi yao ni kubwa zaidi." Wale wanaokimbia "hawawezi kupata huduma na lazima wasaidiwe bila kujali," huku wakimbizi wa Sudan pia wakiwasili kando ya Mto Nile. "Ni aina ya athari ya kutawala: migogoro inaingiliana na kuathiri nchi nzima."
Katika muktadha huu, vurugu zinaenea ndani ya nchi
"Lazima tujiulize ni nani anayewapa vijana hawa silaha na kwa nini," alisema Askofu huyo, akikumbuka mauaji ya Biennom mnamo Mei 2023: Nuer dhidi ya Dinka, 170 walikufa katika siku moja. Mzizi wa mgogoro huo pia ni rasilimali: "Mafuta, dhahabu, ardhi kavu ya malisho," ambayo huchochea mvutano na mgawanyiko. Shida pia ni utambulisho: "Nchi ni moja, lakini inaonekana imegawanywa katika makundi kadhaa ya kikabila. Utambulisho wa kitaifa haujajengwa; kinyume chake, mgawanyiko umeonekana zaidi."
Ishara ya Papa ya kubusu miguu
Kitendo cha Papa Francisko cha kumbusu miguu ya Kiir na Machar mnamo Aprili 11, 2019, kilileta matoke makubwa sana miaka iliyofuata, hadi ziara yake mnamo 2023. "Lakini hakujawa na msamaha wa kweli kati ya viongozi. Bila msamaha, hakuna uaminifu, na tuhuma hutawala," alisema Askofu Carlassare. "Ni vigumu kuwazia wakishirikiana tena."
Kanisa, ni "sauti inayolia nyikani"
Wakati huo huo, uaskofu huo ambao unajumuisha Maaskofu wa Sudan na Sudan Kusini, unaendelea kutoa wito wa "mazungumzo ya kitaifa yanayojumuisha wote," lakini mara nyingi ni "sauti inayolia nyikani": "Tunasikilizwa, lakini bila matokeo ya vitendo. Hatua thabiti kuelekea kuleta amani zinahitajika." Hata hivyo, matumaini yanabaki: katika jumuiya na shule, ambapo vijana kutoka makabila tofauti bado wanaweza kujifunza "kuishi pamoja" na kufikiria nchi tofauti.
Ziara ya Kitume ya Papa Leo Barani Afrika
Kuanzia tarehe 13 hadi 23 Aprili, Papa Leo XIV atakuwa barani Afrika kwa safari yake ya kitume kwenda Algeria, Camerun, Angola, na Guinea ya Ikweta. Ingawa maeneo haya yako mbali, Askofu wa Bentiu alisisitiza umuhimu wa "kuendelea kuvutia umakini kwa Sudan na Sudan Kusini, kama Papa Francisko alifanya tayari. Itakuwa muhimu kuunganisha migogoro hii na kuiweka katikati ya umakini wa kimataifa."
Imetasfiriwa na Angella Rwezaula.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata taarifa mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku:Just click here.