Tafakari Dominika ya Huruma ya Mungu: Chanzo cha Maisha na Matumaini Mapya
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa familia ya Mungu, ni Jumapili ya 2 ya Pasaka mwaka A wa Kanisa. Ni siku ya nane tangu kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Dominika hii huitwa Dominika ya Huruma ya Mungu au “Dominika Nyeupe.“ Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatutafakarisha kuwa, “Ufufuko wa Kristo Yesu ni zawadi huruma na chanzo cha tumaini jipya “Sala ya mwanzo katika Dominika hii inaanza kwa maneno, “Ee Mungu wa rehema ya milele... “Huruma ni sifa ya milele ya Mungu. Ameidhihirisha huruma yake kuu tangu alipomwumba Mwanadamu, hadi kilele cha Ukombozi wa Mwanadamu katika Fumbo Takatifu la Pasaka. Kwa njia ya Mama Kanisa Mtakatifu, ameendelea kuidhihirisha Huruma yake kuu katika Sakramenti mbalimbali za Kanisa, kwa njia ya Roho Mtakatifu, zawadi ya Kristo Mfufuka kwa Mitume wake baada ya ufufuko wake. Katika dominika hii tunaalikwa sote, tuitumainie huruma ya Mungu isiyo na mipaka, nasi kama walivyokuwa mitume wa Yesu baada ya Pentekoste, tuwe mashuhuda imara wa Huruma ya Mungu kwa njia ya maisha na utume wetu.
Chanzo cha Sherehe hii ya Huruma ya Mungu. Sherehe hii ilitokana na maagizo ya Yesu kwa mtawa huko Poland, Mtakatifu Maria Faustina Kowalska. Yesu alimtokea mara nyingi kuanzia mwaka 1930 na kumwambia kuwa anatamani Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka iwe Sikukuu ya Huruma ya Mungu ili kuwa kimbilio la wakosefu. Kwa nini katika Dominika ya pili ya Pasaka? Yesu alifundisha kuwa Mateso, Kifo, na Ufufuko wake ndio kilele cha Huruma yake. Hivyo, sherehe hii inakuja kukamilisha siku nane (Oktava) za Pasaka, ikionyesha kuwa matunda ya kufufuka kwa Kristo ni msamaha na huruma kwa wanadamu wote. Miali myekundu na myeupe iliyotoka katika Moyo wake Mtakatifu ni Ishara ya Damu na Maji vilivyomwagika alivyochomwa ubavu wake kwa mkuki. Damu, alama ya Ekaristi Takatifu, inayotupa uzima rohoni mwetu na maji Ishara ya Sakramenti ya Ubatizo, inayotusafisha na kutufanya kuzaliwa upya ndani ya Kristo. Sherehe hii ilianzishwa rasmi katika Kalenda ya Liturujia ya Kanisa Katoliki na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 30 Aprili 2000, siku ileile aliyomtangaza Faustina kuwa Mtakatifu wakati wa maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Mwaka 2000, ili kutimiza agizo hili la Kristo Yesu kwa Sr. Maria Faustina. Na kuanzia hapo, Baba Mtakatifu alitangaza rasmi kwamba Dominika hii ya pili ya Pasaka itajulikana na itaadhimishwa duniani kote kama Dominika ya Huruma ya Mungu. Bwana wetu Yesu Kristo alitoa Ahadi ya rehema kamili, yaani msamaha kamili wa dhambi na adhabu zake kwa yeyote atakayekwenda kwenye Sakramenti ya Kitubio na kupokea Ekaristi Takatifu siku hiyo. Kiini cha siku hii tunaweza kusema, kimefupishwa katika maneno “Yesu, Nakutumaini Wewe.” Ni wito kwetu sote wa kuachana na mashaka (kama Tomaso) na kuamini kuwa Huruma ya Mungu ni kubwa kuliko udhaifu wetu. Ni siku ya kuponya majeraha ya nafsi kupitia Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi Takatifu. Masomo yetu yote katika Dominika hii yanatusaidia kutafakari juu ya Huruma kubwa ya Mungu katika maisha yetu sisi wafuasi wake. Hebu tutazame kwa kina Masomo yetu katika Dominika ya leo, tukianza na kiini cha Masomo haya, yaani somo la Injili Takatifu.
Somo la Injili: Ni Injili ya Yohane 20:19-31. Somo la Injili Takatifu katika Dominika hii ya Pili ya Pasaka, limegawanyika katika sehemu kuu tatu. Katika sehemu ya kwanza, (19-23) Yesu anawatokea mitume waliokuwa na hofu na mashaka, anawapa Amani, na kuwapa mamlaka ya kusamehe dhambi kwa kuweka rasmi Sakramenti ya Kitubio. Sehemu ya pili, (24-30) Mtume Tomaso anayeashiria mashaka ya binadamu anakutana na Yesu baada ya siku nane, anagusa madonda yake, na kukiri, “Bwana wangu na Mungu wangu!” sehemu ya mwisho ya Injili hii, (30-31) Mwinjili Yohane anaeleza kuwa ishara hizi zimeandikwa ili tuamini kuwa Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu, na kwa kuamini tupate uzima, na hili ndilo kimsingi lengo la Injili hii. Katika somo hili ningependa tujadili mambo makubwa manne kama ifuatavyo: Jambo la Kwanza: Huruma ya Mungu inatusaidia kushinda Hofu na Mashaka, Kristo Mfufuka anatupa Amani. Katika sehemu ya kwanza ya Injili, 20:19-23, Mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo mara baada ya mateso na kifo cha Bwana, walijawa na hofu na mashaka makubwa. Walijifungia ndani wakiogopa Wayahudi. Katikati ya hofu, mashaka, sintofahamu na kukata kwao tamaa, Kristo Mfufuka anatokea katikati yao akiwaambia, “Amani iwe kwenu”. Yesu hawahukumu, wala hawalaumu kwa nini walimkimbia katika mateso yake, bali anawatangazia Amani. Nao walifuraha walipomwona Bwana.
Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka anakuja kwetu katika kila nyakati ya maisha yetu. Sisi sote kwa namna mbalimbali tuna milango iliyofungwa katika maisha yetu, mioyo iliyofungwa na huzuni, hofu, chuki, visasi, mashaka ya wakati ujao, aibu, fedheha na kushindwa, hofu na aibu ya dhambi na udhaifu wetu wa zamani, maumivu na vidonda katika historia za maisha yetu. Dominika hii inatukumbusha kuwa Huruma ya Mungu ina nguvu ya kupenya pale ambapo binadamu hawezi kufika. Hata kama tumejifungia kiasi gani, Yesu hangojei tuwe sawa ili atutembelee bali anakuja hapo hapo tulipo, katika udhaifu wako na wangu, ili akupate, ili anipate. Ndio maana katika picha ya Huruma ya Mungu tunamwona Kristo aliyeinua mkono wake kubariki, anayetuangalia kwa huruma na kupiga hatua kutufuata. Hatuelekezei tu macho bali anakuja kutufuata pale tulipo, hata kama tunaona kila kitu kuwa kimefungwa, na hakuna mwanga tena. Huruma yake inapenya vifungo na vikwazo vyote. Tunakutana naye katika Neno lake na na katika sakramenti zake. Tunaalikwa kufurahi kila tukutanapo na Bwana. Kutaniko letu na Kristo halituachi vile tulivyokuwa, bali tunakuwa wapya tena, tunapata amani na furaha tena moyoni, hata katika maumivu yetu. Jambo la Pili: Huruma ya Mungu inageuza maumivu na madonda kuwa alama ya upendo na ushindi. Kristo akiisha kuwatangazia amani Mitume wake waliokuwa wamejawa hofu na Mashaka, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Hakufuta makovu ya mateso yake baada ya kufufuka. Yesu alionyesha madonda ili kuthibitisha kuwa yeye aliyefufuka ni yuleyule aliyeteswa na kusulubiwa na kufa msalabani. Madonda yake ni kitambulisho chake. Madonda haya yanatukumbusha kwamba, ingawa Yesu amefufuka, alama za majeraha yake zimebaki kama ushahidi wa Huruma na upendo wake mkuu na ushindi wake dhidi ya dhambi na kifo.
Ndugu mpendwa, mara nyingi nasi pia tunadhani kuwa madonda yetu (makosa ya zamani, kuumizwa na watu, au kufeli) ni alama za kushindwa. Dominika hii ya Huruma ya Mungu inatufundisha kuwa madonda yetu yanaweza kuwa chanzo cha nuru mpya ndani mwetu. Tunapopata huruma ya Mungu, yale makovu yetu ya zamani yanakuwa ushuhuda wa jinsi Mungu alivyotuokoa. Huruma ya Mungu haifuti historia yetu, bali inaipa historia yetu maana mpya. Hii inatupa uhakika kuwa Mungu wetu anaelewa maumivu ya kibinadamu kwa sababu anayabeba yeye mwenyewe mwilini mwake. Hakimbii historia ya mateso yetu, bali anaingia ndani yake. Madonda haya ya Kristo yanatukumbusha kuwa upendo wa kweli una gharama. Tunapomtazama Yesu mwenye madonda, tunaona thamani ya nafsi zetu mbele za Mungu, nasi twapaswa kuona thamani ya wengine hata kama ikitubidi kujitoa nasi sadaka kwa ajili yao. Jambo la Tatu: Huruma ya Mungu inatupatia msamaha wa Dhambi, na kututuma kuwa Wamisionari wa Huruma hiyo. Kristo Yesu akiisha kuwaonesha madonda yake wanafunzi wake, Ishara ya upendo na huruma yake isiyo na mipaka, anawavuvia mitume wake, akiwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” Kitendo cha kuvuvia ni ishara ya uumbaji, tukirejea katika Kitabu cha Mwanzo 2:7, Mwenyezi Mungu alipomwumba mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai, na mtu akawa nafsi hai. Kumbe Yesu anawavuvia Mitume wake, anawapa nguvu ya kusamehe watu dhambi kwa njia ya Kanisa, ambapo tunakuwa wapya kila tunaposamehewa dhambi zetu. Ile furaha ninayopata moyoni katika sakramenti ya kitubio kwa kuambiwa, “Mwenyezi Mungu amekusamehe dhambi zako, nenda na amani” Ni furaha ya namna gani! Nakua mpya kabisa rohoni. Kisha kuwavuvia, anawatuma kuwa Wamisionari wa huruma yake.
Ndugu wapendwa, ni Bwana wetu Yesu Kristo kwa huruma yake kubwa aliweka Sakramenti hii ya muhimu kabisa katika Kanisa, Sakramenti ya upatanisho ili kutuondolea dhambi, kutusafisha na kutufanya wapya tena machoni pa Mungu. Sakramenti ya Kitubio inatuondolea dhambi zetu zote, inatupatanisha sisi na Mungu inatupatanisha sisi na nafsi zetu, na sis na wenzetu, kisha tunapata amani na furaha ya kweli ndani ya mioyo yetu. Ni Yesu mwenyewe aliwapa Mitume wake uwezo huu wa kuwaondolea watu dhambi zao. Nasi mapadre, kwa njia ya sakramenti ya Daraja Takatifu, tunapokea uwezo huu, kwa mamlaka ya Kanisa na kwa niaba ya Kristo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Tunaalikwa kuikimbilia huruma ya Mungu ambaye hafurahii tufe katika dhambi bali anatupa nafasi ya kujipatanisha naye na kujipatanisha sisi na wenzetu. Tusione aibu, kwenda kuungama mara nyingi iwezekanavyo, hakuna kikomo cha huruma ya Mungu. Kila mara tunapoanguka dhambini tukumbuke kuwa Yesu anatuita kwake katika sakramenti hii ya huruma yake. Tunakumbushwa kuwa sisi sote tunaopokea kila siku huruma hii kubwa ya Mungu nasi pia kwa njia ya ubatizo wetu kila mmoja ametumwa kuwa shuhuda na mmisionari wa Huruma ya Mungu. Mungu anayetusamehe anatutuma nasi kusamehe, Mungu aliyeguswa na maumivu ya wanadamu anatualika nasi kuguswa na shida za ndugu zetu wanaoteseka. Hatuwezi kuwa wajumbe wa huruma ya Mungu kama tunakaa na vinyongo na chuki, hatuwezi kusamehewa dhambi kama sisi hatuwasamehi wengine.
Jambo la Nne: Huruma ya Mungu inatuvumilia hata katika kutokuamini kwetu, Ni mlango wa Imani. Wakati Bwana wetu Yesu Kristo alipowatokea Mitume wake, Thomaso hakuwapo kati ya wale kumi na mmoja, pengine alikwisha kata tamaa, alipoteza matumaini. Wanafunzi wengine walipomwambia tumemwona Bwana, yeye hakusaidiki, na anasema wazi, “Nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.” Kisha baada ya siku nane, Kristo aliwatokea tena na kujidhihirisha mbele yao. Anamwimarisha Thomaso Imani yake, na Thomaso anaamini na kukiri Imani, “Bwana wangu na Mungu wangu.” Ndugu mpendwa, Mtume Thomaso anawakilisha wale wote ambao katika nyakati mbalimbali za maisha yao wamekua katika hofu na mashaka. Badala ya Yesu kumfukuza au kumhukumu Thomaso kwa kutokuamini kwake, Yesu anarudi tena baada ya siku nane kwa ajili ya Thomaso mmoja tu. Kumbe Mungu ana subira na sisi. Hata tunapotia shaka, yeye hatuachi, anakuja kukutana nawe katika kiwango chako cha imani ili akusaidie kukua. Yesu anamwambia Thomaso, lete hapa kidole chako, utazame mikono yangu, ulete mkono wako utie katika ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye. Ndugu mpendwa Imani ya Kikristo haijengwi juu ya nadharia, bali juu ya uhalisia wa kuteswa na kufufuka kwa Kristo. Madonda ya Yesu ni ushahidi wa upendo wake. Tomaso alipogusa madonda yale, hakugusa nyama tu, bali aligusa bahari ya huruma ya Mungu. Thomaso anamtambua na kumkiri Kristo si kama Mwalimu tu bali kama Mungu kweli. Hili ndilo lengo la huruma ya Mungu, kutufikisha hatua ya kumkiri Kristo kuwa mtawala wa maisha yetu. Thomaso hakuwepo mara ya kwanza Yesu alipowatokea Mitume. Alipokuwa peke yake, alikata tamaa na kutokuamini. Alipokuwa ndani ya jumuiya (pamoja na Mitume wengine) baada ya siku nane, ndipo alipokutana na Kristo Mfufuka. Kumbe nasi tunakutana na Huruma ya Mungu kwa namna ya pekee tukiwa ndani ya Kanisa (Jumuiya). Hauwezi kuishi imani yako peke yako; unahitaji wenzako ili kuimarika. Yesu alimalizia kwa kusema kuwa heri wale ambao hawajamwona kwa macho ya nyama lakini wanaamini. Hili ni tangazo la heri kwa sisi waamini wa leo. Inatufundisha kuwa hatuhitaji miujiza ya kuonekana au kumgusa Yesu kimwili ili tupokee huruma yake; Neno lake na Sakramenti zinatosha kabisa. Tumwombe Kristo daima atuongezee Imani, tutambue uwepo wake wa daima Katikati yetu katika Sakramenti za Kanisa na katika Neno lake Takatifu.
Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume Mdo 5:12-16. Maisha ya wakristo wa kwanza ni kilelezo bora cha agizo la Kristo aliyewatuma kuwa mashuhuda na watangazaji wa huruma yake, alipowatokea na kuwavuvia Roho Mtakatifu. Wakiwa chini ya uongozi wa Mitume, Wakristo hao waliishi maisha ya ushirikiano, walikua wakipendana, wakisaidiana wakisali na kushiriki Ekaristi Takatifu pamoja na matokeo yake yalionekana wazi. Tuanaambiwa, Wakristo hawa walikua na moyo na roho moja. Walishirikiana kila kitu kwa umoja, wengine waliuza mali zao na vitu vyao walivyokuwa navyo na na kugawia watu wote kama kila mtu alivyokuwa na haja. Hapa tunaona Huruma ya Mungu ikionekana kwa vitendo. Somo hili linatufundisha kuwa Mungu anatumia mikono yetu kutoa huruma yake kwa maskini na wahitaji. Kanisa la kwanza, lilikuwa uso wa huruma ya Mungu kwa vitendo. Kumbe huruma ya Mungu inavunja kuta zote za uchoyo na ubinafsi, kuta zote za chuki, uvivu, dhuluma, unyanyasaji nk. Somo la 2: Ni Waraka 1 Pet 1:3-9. Somo hili linafundisha kuwa hatukupata wokovu kwa sababu ya juhudi zetu, bali ni kwa sababu ya Huruma ya Mungu. Huruma hii ndiyo inayotufanya kuwa viumbe wapya. Mtume Petro anatukumbusha kuwa kila siku ni nafasi mpya ya kuanza upya, bila kujali makosa ya nyuma. Huruma ya Mungu kumbe ni kama bahari kubwa, lakini imani twaweza kusema ndiyo ndoo tunayotumia kuchotea maji hayo. Bila kumwamini Yesu (kama alivyofanya Tomaso katika Injili), hatuwezi kuonja nguvu ya huruma yake. Ni mwendelezo wa maisha ya mfano ya jumuiya ya wakristo wa kwanza, ambao ingawa walipitia magumu na mateso kwa sababu ya Imani yao, mtume Petro anawapa moyo waendelee kuvumilia. Kumbe nasi sote, Huruma ya Mungu inatupa nguvu ya kuvumilia maumivu ya sasa kwa sababu tunajua kuna urithi usioharibika mbinguni. Tunapata ujasiri kwa Imani na matumaini kwamba mateso tunayopitia sasa si mwisho wa habari, bali Huruma ya Mungu inatulinda hadi mwisho wa safari ya maisha yetu. Mwisho tunaona kuwa Huruma ya Mungu inatupa uwezo wa kupenda. Hatuwezi kudai kuwa tunaipokea Huruma ya Mungu wakati hatuwaonei huruma wengine. Huruma inatufanya tuwe watii kwa amri ya upendo kwa Mungu na kwa Jirani zetu. Hitimisho. Katika dominika hii tunaalikwa sote, tuitumainie huruma ya Mungu isiyo na mipaka, nasi kama walivyokuwa Mitume wa Yesu baada ya Pentekoste, tuwe mashuhuda imara wa Huruma ya Mungu kwa njia ya maisha na utume wetu.