Tanzania,Ask.Nzigilwa:Uinjilishaji ni kiini cha matumizi ya Vyombo vya habari Katoliki
Na Sr.Ernestina Patrick Lasway,SAC,-Dar-Es-Salaam,Tanzania.
Lengo la kuwa na vyombo vya habari vya Kanisa ni kwa ajili ya kuipeleka Injili ya Kristo kwa watu wote, na kujikita katika uinjilishaji. Alisema hayo Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC), Mhasham Askofu Eusebius Nzigilwa, na Askofu wa jimbo Katoliki la Mpanda katika Mkutano Mkuu wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza hilo, uliofanyika katika makao makuu ya Baraza la Maaskofu, mnamo tarehe 12 na 13 Mei 2026. Mkutano huu ulihudhuriwa na Wakurugenzi 30 wa mawasiliano kati ya Wakurugenzi wa Majimbo 37 Katoliki ya Tanzania pamoja na wasimamizi wa vyombo vya habari vya Kanisa Katoliki nchini Tanzania.
Uinjilishaji ni kiini cha matumizi ya Vyombo vya habari
Akihutubia wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya TEC, Askofu Nzigilwa, alibanisha kuwa, “lengo la kuwa na vyombo vya habari vya Kanisa ni kwa ajili ya kuipeleka Injili ya Kristo kwa watu wote, na kujikita katika uinjilishaji.” Mara baada ya kusikiliza mawasilisho ya mwenendo wa utendaji kutoka vyombo mbalimbali na majimbo tofauti nchini, Askofu Nzigilwa alikazia “umuhimu wa kujikita katika mahusiano ya karibu na Kristo Yesu, ili kuzaa matunda katika utume wa uinjilishaji.” “Uhusiano wa mtu binafsi na Yesu ni wa muhimu sana katika utume, kwani ni kwa njia hii tunaweza kumfunua Kristo kwa watu,” alikazia Askofu.
"Ukweli utawaweka Huru"
Katika nafasi nyingine, Askofu aliwaalika wakurugenzi na waandishi wa habari kusimamia na kutangaza ukweli katika hali zote. Alibainisha kuwa, “ukweli ni jina jingine la Kristo, na hivyo anayekataa ukweli anamkataa Kristo,” akinukuu Injili ya Yohane, “Mimi ndimi njia, na uzima na ukweli.” Katika kujikita kusimamia ukweli, kamwe mwandishi asitafute umaarufu katika utendaji, alikazia. “Tangazeni ukweli hata kama watu wote wataukataa, simama katika ukweli.”
Jenga Urafiki na Kristo
Ufanisi katika utume wa uinjilishaji, unaenda sambamba na ukaribu wetu na Kristo” alibainisha Askofu Nzigilwa. Ni katika muktadha huo ambapo Askofu alibainisha kuwa waandishi wataweza kuwa na ufanisi mkubwa katika utendaji iwapo watajenga urafiki wa karibu na Yesu Kristo. “Nguvu ya Uinjilishaji wetu ipo katika ukaribu wetu na Kristo kuliko vitendea kazi,” kwa njia hiyo watu watavutwa na ukaribu wetu na Kristo katika maisha yetu kabla ya utekelezaji wa majukumu yetu.
Ushirikiano kama chachu ya mafanikio
Askofu kadhalika alitoa mwaliko kwa vyombo vya habari kuwa na ushirikiano katika utendaji kwani “vyombo hivi vya uinjilishaji vya Kanisa ni washiriki pamoja nasi na wala si washindani.” Kwa kutambua hilo “tunaweza kuunganisha nguvu na kurusha pamoja matukio makubwa ya kitaifa.” Wanavyombo vya Habari vya Kanisa “shirikianeni na shirikishaneni changamoto na fursa katika uendeshaji wa taasisi zetu za mawasiliano, kama njia ya kufanikiwa katika utume,” alisisitiza.
Akili Unde(AI)na Uinjilishaji
Wakati huo huo, mwanasheria wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padre Damian Dulle katika ufunguzi wa mkutano huo mkuu wa mwaka, aliwaalika waandishi kujikita katika matumizi sahihi ya Akili Unde (AI) katika uinjilishaji. Alibainisha kuwa, “siyo kila jibu la imani linaweza kupatiwa majibu na Akili Unde, hivyo watumiaji wawe na busara na umakini katika kuitumia.” Ni muhimu kwa wanahabari “kuwa waangalifu katika matumizi ya AI katika kuhabarisha na kuelimisha jamii na ulimwengu kwa jumla.”
AI itumike katika kuimarisha na kuboresha mawasiliano ya Kanisa
Kwa upande wake Padre Dulle, alianisha kuwa, “Akili Unde yafaa itumike katika kuimarisha uinjilishaji, kuboresha mawasiliano ya Kanisa, kuelimisha viongozi wa Kanisa, kulinda maadili na ukweli, kuongeza ufanisi wa utendaji katika taasisi, kuandaa sera na miongozo na kuwasaidia vijana kuitumia kwa manufaa chanya katika jamii na si vinginevyo.” Katika wakati wa sasa, “Kanisa lina wajibu wa kushirikiana na dunia ya kisasa ili kwenda sambamba na maendeleo ya sayansi na teknologia, na kuendelea kuwa sauti yenye mwanga na matumaini katika ulimwengu wa kidigitali,” alibanisha Padre Dulle. Akili Unde(AI), katika muktadha wa Kanisa la Tanzania, “ni muhimu kuhakikisha inatumika kwa manufaa ya binadamu, uinjilishaji, kuelimisha na kuhamasisha maendeleo ya jamii kwa kuzingatia maadili ya Kikristo,” alikazia.
Sheria za Matumizi ya Akili Unde nchini Tanzania
Mpaka Mei, 2026, alibanisha Padre Dulle kuwa “nchi ya Tanzania bado haina sheria ya matumizi ya Akili Unde. Kwa sasa, matumizi ya akili unde nchini Tanzania yanaathiriwa na sheria mbalimbali zilizopo kuhusu matumizi ya teknologia, mawasiliano, faragha, haki miliki na usalama wa taarifa binafsi.” Hii ni pamoja na sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi 2022 (Personal Data Protection Act), pamoja na Kanuni za ukusanyaji na uchakataji wa taarifa binafsi za mwaka 2023. Hata hivyo, serikali imeanzisha Personal Data Protection Commission kusimamia utekelezaji wa sheria ya ya ulinzi binafsi ya mwaka 2022. Sheria za matumizi ya Akili unde “ni muhimu katika kuviongoza vyombo vya habari vya Kanisa katika matumizi sahihi ya video za waamini, utunzaji wa taarifa binafsi,matumizi ya AI katika habari na mawasiliano, kuepuka taarifa za uongo na picha bandia pamoja na kulinda maadili na utu wa binadamu” alisisitiza padre Dulle.
Uzuri wa Teknolojia
Akitoa mada katika semina hiyo Kaimu Mkurugenzi -Kurugenzi ya Mawasiliano ya (TEC), Padre Faustine Furaha, alijikita katika mangamuzi ya matumizi ya Teknolojia katika mrengo wa Kanisa Katoliki, na kuhimiza kuwa, “tenkologia ni nzuri katika maisha yetu ya sasa. Kwa kuwa hatuwezi kukwepa matumizi ya teknolojia, ni muhimu waandishi na watangazaji kung’amua matumizi sahihi kwa ufanisi katika shughuli za mawasiliano.” Ili kufanya matumizi sahihi “ni lazima kila wakati kuhakiki kile unachohitaji katika matumizi haya na kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi kwa ujenzi wa taifa na jamii,” alitamatisha Padre Furaha.
Ujumbe wa Papa Leo XIV kwa Siku ya 60 ya Hupashanaji Habari 2026
Ikumbukwe, Baba Mtakatifu Leo XIV katika ujumbe wake wa Siku ya 60 ya Uhapashanaji Habari iliyofikia kilele chake tarehe 17 Mei 2026, kwa kuongoza na kauli mbiu: "Kulinda sauti na nyuso za wanadamu" lakini pia hata Ujumbe aliouandika kwa ajili ya tukio hilo, ambao alilaani hatari za ulaghai, uonevu wa mtandaoni, na uzushi wa kina na ilionya dhidi ya matumizi mabaya ya udanganyifu, udukuzi wa data, upotoshaji, na "uhalisia sambamba" unaoundwa na akili unde.
Katika ujumbe wake Papa alibainisha kuwa “Changamoto iliyo mbele yetu si kuzuia uvumbuzi wa kidijitali, bali kuuongoza, kutambua asili yake ya kutofautiana. Ni jukumu la kila mmoja wetu kupaza sauti zetu katika kuwatetea wanadamu, ili zana hizi ziweze kuunganishwa kweli nasi kama washirika.”
"Uso na Sauti ni vitakatifu"
"Uso na sauti ni vitakatifu. Tulipewa na Mungu, aliyetuumba kwa mfano na sura yake," Papa anathibitisha. “Sisi si spishi iliyotengenezwa kwa algoriti za kibiokemikali, zilizoainishwa mapema. Kila mmoja wetu ana wito usioweza kubadilishwa na usioweza kuigwa unaoibuka kutoka katika maisha na kujidhihirisha hasa katika mawasiliano na wengine."Kwa hivyo, changamoto si ya kiteknolojia, bali ya kibinadamu. Kuhifadhi nyuso na sauti hatimaye kunamaanisha kujilinda." Kwa hivyo, sehemu kubwa ya tasnia ya ubunifu ya binadamu ina hatari ya kubomolewa na kubadilishwa na lebo "Inayoendeshwa na AI," ikiwabadilisha watu kuwa watumiaji tu wa mawazo yasiyofikiriwa, bidhaa zisizojulikana, zisizoidhinishwa, na zisizopendwa. Wakati huo huo, kazi bora za kipaji cha binadamu katika muziki, sanaa, na fasihi zimepunguzwa kuwa uwanja wa mafunzo tu kwa mashine.”
Kuzika vipaji tulivyopokea
Kwa hiyo ombi ni muhimu: "Kuacha mchakato wa ubunifu na kusalimisha kazi za akili na mawazo ya mtu kwa mashine" ni sawa na "kuzika vipaji tulivyopokea ili kukua kama watu kuhusiana na Mungu na wengine." "Inamaanisha kuficha nyuso zetu na kunyamazisha sauti zetu." Teknolojia inayotumia hitaji letu la muunganisho haiwezi kuwa na matokeo machungu tu kwa hatima ya watu binafsi, bali pia inaweza kuharibu muundo wa kijamii, kiutamaduni na kisiasa wa jamii. Tukibadilisha mahusiano na wengine na wale walio na AI "waliofunzwa kuorodhesha mawazo yetu" na hivyo "kujenga ulimwengu wa vioo vinavyotuzunguka," Papa alionya, "tunajiruhusu kunyang'anywa uwezekano wa kukutana na wengine." Bila kukumbatia utofauti, hakuwezi kuwa na uhusiano wala urafiki.
Sifa nzuri kwa waandishi wa habari na waundaji wa maudhui
Kwa upande wa waandishi, Papa Leo XIV katika ujumbe wake anakazia kusema kuwa, makampuni ya vyombo vya habari na mawasiliano hayawezi kuruhusu "algorithms zinazolenga kushinda vita kwa sekunde chache za ziada, ya umakini kwa gharama yoyote ile kushinda uaminifu wao kwa maadili yao ya kitaaluma, yanayolenga kutafuta ukweli." Uaminifu wa umma hupatikana kupitia usahihi na uwazi, si kwa kufuata aina yoyote ya ushiriki. Maudhui yanayozalishwa au kudanganywa na AI lazima yajulikane waziwazi na kutofautishwa na maudhui yaliyoundwa na watu. Kwa kifupi, "uandishi na umiliki huru wa kazi ya waandishi wa habari na waundaji wengine wa maudhui lazima ulindwe," kwa sababu "taarifa ni jambo la umma" na haliwezi kutegemea uongo, bali uwazi na kiwango cha juu cha ubora wake .
Umuhimu wa kuelimisha na kuelimishwa kutumia AI
“Ni muhimu kuelimisha na kuelimishwa kutumia akili unde (AI) kimakusudi, na katika muktadha huu kulinda picha ya mtu (picha na sauti), uso wake na sauti yake, ili kuzizuia kutumika katika kuunda maudhui na tabia zenye madhara kama vile ulaghai wa kidijitali, unyanyasaji wa mtandaoni, uzushi wa kina unaokiuka faragha na ukaribu wa watu bila idhini yao.” Baba Mtakatifu Leo XIV anakazia kuwa"Kama vile mapinduzi ya viwanda yalivyohitaji uelewa wa msingi ili kuwawezesha watu kujibu uvumbuzi, vivyo hivyo mapinduzi ya kidijitali yanahitaji uelewa wa kidijitali.” Papa anabainisha kuwa, “Tunahitaji kuthamini zawadi ya mawasiliano kama ukweli wa ndani kabisa wa ubinadamu, ambao kila uvumbuzi wa kiteknolojia lazima uongozwe.”
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.