Sherehe ya Pentekoste: Kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa Sherehe ya Pentekoste: Kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa 

Sherehe ya Pentekoste 2026: Roho Mtakatifu Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Siku ya Pentekoste, mwisho wa juma saba za Pasaka, Pasaka ya Kristo inatimilika kwa kumimina Roho Mtakatifu, ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama nafsi ya Mungu: kutoka utimilifu wake Kristo, Bwana anamimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Utatu Mtakatifu ulifunuliwa katika ukamilifu wake. Kwa ujio wake ambao hauna mwisho, Roho Mtakatifu anauingiza ulimwengu katika nyakati za mwisho, nyakati za Kanisa, ufalme uliorithiwa tayari...

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, sherehe ya Pentekoste, siku ya hamsini baada ya ufufuko wa Bwana. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 731 hadi 732, inafundisha hivi; Siku ya Pentekoste, mwisho wa juma saba za Pasaka, Pasaka ya Kristo inatimilika kwa kumimina Roho Mtakatifu, ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama nafsi ya Mungu: kutoka utimilifu wake Kristo, Bwana anamimina Roho kwa wingi. Hii ni siku ambayo Utatu Mtakatifu ulifunuliwa katika ukamilifu wake. Kwa ujio wake ambao hauna mwisho, Roho Mtakatifu anauingiza ulimwengu katika nyakati za mwisho, nyakati za Kanisa, ufalme uliorithiwa tayari, lakini bado haujakamilika. Kwa njia yake tunaiona Nuru ya kweli, tunampokea Roho wa mbingu, tunapata imani ya kweli na tunauabudu Utatu usiogawanyika, kwa sababu umetukomboa. Pentekoste ni siku ya kuzaliwa kwa Kanisa la kimisionari kwa njia ya Roho Mtakatifu. Mama Kanisa kupitia Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Katiba juu ya Fumbo la Kanisa, Mwanga wa Mataifa – Lumen gentium namba 4, anatufundisha hivi; “Pale ilipotimilika kazi Baba aliyomkabidhi Mwana afanye duniani, basi Roho Mtakatifu akatumwa siku ya Pentekoste ili kulitakatifuza Kanisa siku hadi siku, na waamini wapate njia ya kumkaribia Baba kwa Kristo katika Roho mmoja. Huyo ndiye Roho wa uzima au chemchemi ya maji yabubujikiayo uzima wa milele.” Na katika Tamko juu ya kazi za kimisioni za Kanisa – Ad gentes – namba 4, anatufundisha hivi; “Roho Mtakatifu alitenda kazi ulimwenguni hata kabla ya Kristo kutukuzwa. Lakini katika siku ya Pentekoste aliwashukia wanafunzi ili kukaa nao milele, na kulifanya Kanisa liokaonekane wazi mbele ya umati wa watu, na uenezaji wa Injili kati ya mataifa yote ukaanza rasmi kwa njia ya mahubiri.”

Roho Mtakatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa
Roho Mtakatifu ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa   (@Vatican Media)

Hivyo Pentekoste ni kilele cha sikukuu ya Pasaka, utimilifu wa fumbo la ukombozi kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, ishara ya umoja wetu na Mungu. Ni katika muktadha huu mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wewe unalitakasa Kanisa lako lote lililo kati ya makabila na mataifa yote kwa fumbo la sikukuu ya leo. Eneza mapaji ya Roho Mtakatifu popote duniani; na zile karama ulizozitoa tangu mwanzo wa kuhubiri Injili, hata sasa uzieneze kwa juhudi ya waamini wako”. Nao wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Roho ya Bwana imeujaza ulimwengu, nayo inaviunganisha viumbe vyote, hujua maana ya kila sauti” (Hek.1:7). “Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi, Aleluya” (Rm 5:5). Somo la kwanza ni la kitabu cha matendo ya Mitume (Mdo. 2:1-11). Ni simulizi ya nini kilitokea siku ya Pentekoste: “upepo wa nguvu” na “ndimi za moto,” alama za Roho Mtakatifu aliyewajaza mitume nguvu na ujasiri wa kuhubiri habari za Kristo Mfufuka na wongofu wa watu vilivyotokea. Umoja na uelewano uliopotea sababu ya dhambi uliletwa tena kwa watu wa mataifa mbalimbali kuwasikia mitume wakihubiria kwa lugha yao wenyewe. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 1076, ikinukuu maandiko matakatifu inafundisha hivi; “Siku ya Pentekoste, kwa mmimino wa Roho Mtakatifu, Kanisa limedhihirishwa kwa ulimwengu kuwa la nyakati zote. Na katika kipindi hiki cha Kanisa, Kristo anaishi na kutenda sasa katika Kanisa lake, na pamoja nalo, kwa namna iliyo mpya inayofaa nyakati hizi mpya. Naye anatenda kwa njia ya Sakramenti.”

Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na huduma ndani ya Kanisa
Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na huduma ndani ya Kanisa

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto (1Kor. 12:3b-7, 12-13). Linatueleza kuwa Roho Mtakatifu ni msingi wa karama na hudumu mbalimbali katika Kanisa. Yeye ndiye anayefanya karama hizo zilete umoja katika kuihudumia jumuiya nzima ya waamini kama viungo mbalimbali vya mwili vinavyosaidiana kwa faida ya mwili mzima. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko juu ya kazi za kimisioni za Kanisa – Ad gentes – namba 4, ukinukuu maandiko haya matakatifu unasisitiza hivi; “Roho Mtakatifu katika nyakati zote hulifanya Kanisa kuwa moja katika ushirika na huduma, na kulifadhili vipawa mbalimbali vya kihierarkia na vya kikarama. Tena, huzitilia uhai taasisi za kikanisa, akiwa ni mtima wake, na akimimina katika nyoyo za waamini roho ya kimisioni, ambayo Yesu mwenyewe alisukumwa nayo”. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:19-23). Mazingira yake ni siku ya kwanza ya Juma, Dominika, siku ya ufufuko wa Bwana. Kristo Yesu mfufuka anajidhihirisha kuwa yu-mzima, amefufuka kwa kuwatokea mitume na salamu yake ya kwanza ni “Amani iwe kwenu.” Kisha aliwavuvia Roho Mtakatifu na kuwapa uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Hivyo pato la kazi ya Roho Mtakatifu ni upatanisho kati ya Mungu na sisi kwa kutuondolea dhambi na kufanywa wana wa Mungu. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika utangulizi sherehe hii anasali; “Wewe umetimiza fumbo la Paska na kuwajalia Roho Mtakatifu wale uliowafanya kuwa wanao, kwa sababu ni ndugu zake Mwanao wa pekee.”

Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana ameshuka kutoka mbinguni
Roho Mtakatifu atokaye kwa Baba na Mwana ameshuka kutoka mbinguni

Hivyo Roho Mtakatifu aliyemiminwa siku ya Pentekoste ndiye chanzo na nguvu ya uzima mpya ndani mwetu” (1The 4:8), anatuwezesha kumjua Mungu sawa sawa (1Kor 2:10-16), na kumtambua kama Baba (Gal 4:6), “hushuhudia pamoja na roho zetu ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu” (Rum. 8:9,16), naye anatufanya kuwa watoto wa Mungu kwa njia ya ubatizo (Rum 8:14-16), ni chanzo cha ufufuko wa Mkristo (1Kor 6:19), ni chanzo cha imani, uhai na utakatifu (1Kor 12:30), ni chanzo cha utakaso wetu (Rum 15:16; 2The 2:13), ni nguvu ya maisha adili na matunda yake ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, na kiasi (rej. Gal 5:16-25). Ndiye anayeleta nguvu na imara ya kitume (Fil. 1:19; 2Tim 1:7-8), mapendo kwa sala (Rum 8:26) na anatuunganisha na Kristo kuwa mwili mmoja (1Kor 12:13; Efe 2:16-18).  Ndiyo maana Mtume Paulo anatuonya tusimzimishe (1The 5:19) wala kumhuzunisha Roho Mtakatifu (Efe 4:30). Sherehe hii ya Pentekoste inatukumbusha kuwa Kanisa ni kusanyiko la watu wote kwa ajili ya wokovu, na kwa tabia yake ni la kimisionari, limetumwa na Kristo kwa mataifa yote ili kuwafanya wafuasi (KKK 767). Na kusudi liweze kutekeleza utume wake, Roho Mtakatifu analipa vipawa vya mwanzilishi wake na kuliongoza kwa njia ya vipawa vya namna mbalimbali vya kihierakia na karama (KKK 768). Hivyo Roho Mtakatifu anaendelea kumiminwa juu yetu tunapokusanyika mahali pamoja, kwa moyo mmoja katika kusali ili kutukumbusha yote aliyosema Yesu na kutulea katika maisha ya sala (rej. KKK 2623).

Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu
Waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya wokovu   (@Vatican Media)

Tumruhusu basi atuwezeshe kuzitambua siri za Mungu na kuishi vyema maisha ya hapa duniani kadiri ya karama anazotujalia kama anavyosali mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisema; “Ee Bwana, tunakuomba Roho Mtakatifu atufumbulie zaidi siri ya sadaka hii, kama alivyotuahidia Mwanao. Atujulishe pia ukweli wote kwa rehema yake”. Na katika sala baada ya komunyo inasali; “Ee Mungu, umelijalia Kanisa lako mapaji yako ya mbinguni. Uilinde neema hiyo uliyotujalia, ili mapaji ya Roho Mtakatifu tuliyoyapokea yasitawi daima, nacho chakula cha roho kituongezee ukombozi wa milele”.Tukikumbuka kuwa, Pentekoste ni siku ya kuhitimisha kipindi cha Pasaka na kuendelea na kipindi cha kawaida cha mwaka, Mshumaa wa Pasaka uliowashwa na kusimikwa mahali pa patakatifu karibu na Altare usiku wa vijilia vya Pasaka, unazimwa rasmi na kuwekwa karibu na kisima cha ubatizo kama kipo au sehemu nyingine, na utakuwa unawashwa wakati wa ubatizo ili mishumaa ya wabatizwa iwashwe kutoka katika mshumaa huu ishara ya kufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo, na wakati wa mazishi unawekwa kando ya jeneza ishara ya ufufuko wa uzima wa milele kwa mkristo aliyekufa akiwa na muunganiko na Kristo. Nawatakieni sherehe njema ya Pentekoste, tufungue mioyo yetu, tumapokee Roho Mtakatifu ili atuongoze katika kweli yote.Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Pentekoste 2026
22 Mei 2026, 16:33