Sherehe ya Pentekoste: Mama Kanisa anaadhimisha Ujio wa Roho Mtakatifu; Nguvu ya Roho Mtakatifu kwa Mitume, kiasi cha kupata ujasiri wa kumshuhudia Kristo Yesu na Mwanzo wa Kanisa Sherehe ya Pentekoste: Mama Kanisa anaadhimisha Ujio wa Roho Mtakatifu; Nguvu ya Roho Mtakatifu kwa Mitume, kiasi cha kupata ujasiri wa kumshuhudia Kristo Yesu na Mwanzo wa Kanisa  (@VATICAN MEDIA)

Sherehe ya Pentekoste: Ujio wa Roho Mtakatifu; Ushuhuda na Kuzaliwa Kwa Kanisa

Sherehe hii katika Kanisa: “Ujio wa Roho Mtakatifu, ushuhuda wa Mitume na kuzaliwa rasmi kwa Kanisa." Yesu Kristo alikwishawaahidia Mitume wake kwamba, hatowaacha yatima, alipokuwa nao katika karamu ya mwisho kabla ya kuingia katika Fumbo Takatifu la Pasaka. Baada ya kupaa kwake Mbinguni, Kristo anatimiza Ahadi hii ya Baba, anawepelekea Msaidizi mwingine, ndiye Roho Mtakatifu, nafsi ya Tatu ya utatu Mtakatifu. Kisha Mitume wanapata nguvu na ujasiri!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Familia ya Mungu, siku ya Hamsini baada ya Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Pentekoste. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Juma la “Laudato si”, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 23 Mei 2026 anafanya hija ya kichungaji eneo la Acerra, maarufu kama "Terra dei Fuochi" yaani “Ardhi ya moto” eneo ambalo limeathiriwa sana na taka maalum na hatari zilizotupwa eneo hili kinyume cha sheria, taratibu na kanuni za nchi na mashirika pamoja na makampuni ya uhalifu. Sumu zitokanazo na taka ni tishio kwa usalama, ustawi na mendeleo ya wengi. Mambo makubwa matatu yanaipambanua Sherehe hii kubwa katika Kanisa: “Ujio wa Roho Mtakatifu, ushuhuda wa Mitume na kuzaliwa rasmi kwa Kanisa” Bwana wetu Yesu Kristo alikwishawaahidia Mitume wake kwamba, hatowaacha yatima, alipokuwa nao katika karamu ya mwisho kabla ya kuingia katika Fumbo Takatifu la Pasaka. Baada ya kupaa kwake Mbinguni, Kristo anatimiza Ahadi hii ya Baba, anawepelekea Msaidizi mwingine, ndiye Roho Mtakatifu, nafsi ya Tatu ya utatu Mtakatifu. Kisha Mitume wanapata nguvu na ujasiri wa kutoka na kuhubiri, Matendo makuu ya Mungu. Watu wengi waliipokea Habari Njema ya Injili siku hiyo, na hapa ikazaliwa rasmi jumuiya ya Wakristo wa kwanza, ndilo Kanisa. Nasi sote tuliompokea Roho Mtakatifu katika ubatizo na kuimarishwa kwa mapaji yake katika Sakramenti ya Kipaimara, tunaitwa kuishuhudia Injili, kwa maneno na kwa matendo yetu.

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu, Ushuhuda na Kanisa
Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu, Ushuhuda na Kanisa   (@Vatican Media)

Maana na chimbuko la Sherehe ya Pentekoste: Sherehe ya Pentekoste ni moja kati ya sherehe kubwa tatu kwa Wayahudi, nyingine mbili zikiwa ni sherehe za Pasaka na sherehe za Vibanda. Katika sherehe hizi Wayahudi wote, waliokuwa ndani na nje ya Uyahudi, walipaswa kupanda kwenda Yerusalemu kila mwaka kwa ajili ya maadhimisho hayo makubwa. Ni nini hasa msingi na maana ya Sherehe hii ya Pentekoste? Neno Pentekoste limetokana na Neno la Kigiriki “pentēkostē” lenye maana ya “hamsini.” Sherehe hii ilipewa jina hili kwa kuwa iliadhimishwa siku ya 50 baada ya Sherehe ya Pasaka, siku ambapo Wayahudi walikumbuka na kusherehekea kutoka kwao utumwani Misri na kuanza safari mpya ya ukombozi kuelekea nchi ya Ahadi (Kumb 16:10.) Hivyo ilikua ni siku ya shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya Ukombozi na kwa zawadi ya mavuno mapya, mavuno ya kwanza ya ngano mara baada ya kuingia katika nchi ya Ahadi (Kut 34:22; Hes 28:29). Pamoja na hayo, Wayahudi walikumbuka pia Agano la Mungu alilofanya na Nuhu, siku ya 50 baada ya Gharika ile kuu. Hali kadhalika, walikumbuka pia Agano lao walilofanya na Mungu katika Mlima Sinai, siku ya 50 baada ya kutoka kwao utumwani Misri na kupokea sheria ya Mungu. Lakini kwetu sisi Wakristo, Sherehe hii ina maana gani hasa? Kwa wakristo, sherehe ya Pentekoste tunaweza kusema inapata msingi wake kutoka kwenye uelewa huu huu wa Pentekoste katika Tamaduni za Kiyahudi.

Roho Mtakatifu ni chanzo na asili ya karama ndani ya Kanisa
Roho Mtakatifu ni chanzo na asili ya karama ndani ya Kanisa   (@Vatican Media)

Kimsingi Sherehe ya Pentekoste inaadhimishwa siku ya Hamsini baada ya Sherehe ya Pasaka, baada ya Kristo kufufuka katika wafu, aliposhinda kifo na mauti na kutukomboa sisi Taifa jipya la Mungu kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Ni siku ambapo Roho Mtakatifu aliwashukia Mitume kwa uvumi wa upepo wa nguvu na katika ndimi zilizogawanyika, walipokuwa pamoja na Mama Bikira Maria katika chumba cha juu (cenacolo) kule Yerusalemu baada ya Kristo kupaa kwenda kwa Baba. Hivyo, ni kilele cha Fumbo Takatifu la Pasaka, Kristo anapowatumia Mitume tunda la kwanza la ufufuko yaani Roho Mtakatifu, yule msaidizi mwingine ambaye yeye mwenyewe alinena habari zake. Kama wayahudi walivyosherehekea kupewa kwao sheri ya Mungu mlimani Sinai, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho wake Mtakatifu anaandika sheria yake ndani ya mioyo yetu. Kwa njia ya Hotuba ya Mtume Petro, watu wengi (takribani 3,000) waliongoka na kuwa wakristo siku hiyo, na hapo jumuiya mpya ya Wakristo ikazaliwa rasmi, ndilo Kanisa. Ni mwanzo wa taifa jipya la Mungu, kwa njia ya Agano jipya na la Milele alilolifanya Kristo katika Fumbo la Pasaka. Roho Mtakatifu ameendelea kuliongoza Kanisa, na kama Kristo alivyowaahidi mitume kwamba, “Tazama mimi nipo pamoja nanyi siku zote hata utimilifu wa dahari” ndivyo Roho huyo anavyoendelea kufanya kazi ndani ya Kanisa na ndani ya kila mmoja aliyempokea. Kwa kuadhimisha Sherehe hii, tunahitimisha rasmi kipindi cha Pasaka na kuendelea na kipindi cha kawaida cha mwaka wa Kanisa. Masomo yetu yote katika Sherehe hii yanatutafakarisha juu ya kazi ya Roho Mtakatifu katika Kanisa na katika maisha yetu sisi tulio viungo vya mwili wa Kristo.

Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa
Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa   (Vatican Media)

Somo la Injili: Ni Injili ya Yohane 20:19-23. Somo la Injili Takatifu (Yn 20:19-23) latueleza tokeo la Bwana wetu Yesu Kristo kwa wanafunzi baada ya ufufuko wake. Mitume, baada ya mateso na kifo cha Yesu, walijifungia ndani, walijawa na hofu, huzuni na mashaka, walipoteza kabisa matumaini. Milango ikiwa imefungwa, Kristo anaingia katikati yao, na Neno lake la kwanza kwao ni “Shalom”, Amani iwe kwenu. Katika somo hili, ningependa tutafakari pamoja kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha ya Mitume na utume wa Kanisa, na nafsi ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu sisi wafuasi wa Kristo. Fundisho la kwanza: Roho Mtakatifu anatusaidia kushinda hofu, anatupa utulivu wa ndani. Mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo, mara baada ya Bwana wao kukamatwa, kuteswa na kufa, wengi walikimbia. Walijawa na hofu, huzuni na mashaka makubwa sana. Hawakuona tumaini tena, ni kama ndoto na matarajio yao kwa Kristo yalikufa. Tunaona namna wanafunzi wengine walivyoanza kukimbia kutoka Yerusalemu katika simulizi ya wanafunzi wawili wa Emaus ambao kimsingi wanawakilisha mitume ambao walikuwa wamekata tamaa kabisa. Ni katika hali hiyo Kristo anawatokea, milango ikiwa imefungwa na kuwatangazia “Amani” nao wanafurahi sana walipomwona Bwana. Mitume hawa baada ya Pentekoste walipata nguvu mpya kabisa, walipata moyo na ari, walijawa furaha na matumaini mapya, wakaanza upya kuhubiri na kuishuhudia Injili. Hofu ya kifo, hofu ya maumivu, hofu ya kukata tamaa, hofu ya matarajio, haikuwa tena tatizo kwao. Ni Roho Mtakatifu aliwaimarisha, zawadi ya Mungu mwenyewe. Ndugu mpendwa, katika safari yetu ya maisha kuna nyakati nasi tunajawa na hofu, huzuni, mashaka, na kupoteza kabisa matumaini. Yawezekana tumepitia katika vipindi vya majaribu makubwa ndani ya familia zetu, katika miito yetu, katika kazi zetu, katika ndoa, majaribu yaliyotutikisa na kutuangusha kabisa chini, majaribu yaliyotupasua vipande vipande, kiimani, kiuchumi, kiafya, kisaikolojia, kimahusiano nk. Tumepoteza matumaini na kujihisi kama tumefungiwa ndani ya chumba chenye giza, upweke, huzuni na ukiwa. Matarajio yote yamekufa kama walivyokuwa wale mitume wa Yesu. Kristo hatuachi kamwe, anafahamu uchungu, hofu, huzuni na mashaka yetu. Kristo anasema nasi kila siku anapokutana nasi, Shalom. Kristo hakuwaondolea mitume wake changamoto, wala hakuwaahidi maisha rahisi, bali aliwapa nguvu, ambayo ilikamilishwa kwa ujio wa Roho Mtakatifu katikati yao siku ya pentekoste. Licha ya magumu waliyopitia, Roho Mtakatifu aliwapa utulivu wa ndani. Sisi tumempokea katika ubatizo wetu, na tumeimarishwa kwa mapaji yake saba katika Sakramenti ya Kipaimara. Tunayo nguvu ya kuzibeba changamoto zetu zote kwa ujasiri, tukijua kuwa hatupo peke yetu. Licha ya mateso bado tunapata furaha ya ndani ya moyo katika kuunganika na Kristo.

Roho Mtakatifu ni Zawadi ya Baba wa Milele
Roho Mtakatifu ni Zawadi ya Baba wa Milele   (Vatican Media)

Fundisho la Pili: Roho Mtakatifu anatukumbusha nguvu ya Huruma na Upendo wa Mungu. Kristo akiisha kuwatangazia amani Mitume wake waliokuwa wamejawa hofu na Mashaka, aliwaonesha mikono yake na ubavu wake. Hakufuta makovu ya mateso yake baada ya kufufuka. Yesu alionyesha madonda ili kuthibitisha kuwa yeye aliyefufuka ni yuleyule aliyeteswa na kusulubiwa na kufa msalabani. Madonda yake ni kitambulisho chake. Madonda haya yanatukumbusha kwamba, ingawa Yesu amefufuka, alama za majeraha yake zimebaki kama ushahidi wa Huruma na upendo wake mkuu na ushindi wake dhidi ya dhambi na kifo. Ndugu mpendwa, mara nyingi huwa nasi pia tunadhani kuwa maumivu, madonda na makovu yetu mbambali, yaweza kuwa makosa ya zamani, historia zetu za kukatisha tamaa, za kushindwa, yaweza kuwa maumivu tuliyosababishiwa na watu, yaweza kuwa maumivu ya kupoteza watu au vitu katika maisha, pengine ni alama ya kushindwa au hata tunafikiri tumeachwa na Mungu. Roho Mtakatifu tuliyempokea anatusaidia kutambua kuwa madonda na majeraha yetu ni chanzo cha nuru mpya ndani mwetu kila wakati tunapomtazama Kristo, yeye aliyeteseka, kufa na kufufuka kwa ajili yetu na bado akaendelea kutupenda. Roho Mtakatifu anatupa nguvu ya kusimama tena na kuwa imara zaidi ya tulivyokuwa mwanzo. Lakini pia, Kristo hakuwalaumu Mitume wake, wala hakuwaalaani wale waliomtesa, waliomuuwa bila kosa, bali anaonesha nguvu ya upendo ulioshinda hata mauti na kifo. Kama Kristo aliteseka namna hii na bado akasamehe, Roho Mtakatifu anatupa nasi sote nguvu ya kusema daima, “Nimesamehe” Sio jambo rahisi, wapo wengi walioumizwa kwa kiasi kikubwa, wapo waliojeruhiwa kwa sababu mbalimbali hata kufikia hatua ya kusema, “Mimi siwezi kukusamehe kamwe” kutokana na uzito wa maumivu waliyopitia. Lakini hakuna maumivu, yanayoweza kushinda maumivu aliyopitia Kristo kwa ajili ya uzima wetu. Roho Mtakatifu anatukumbusha wajibu wetu kila mara tunapopata changamoto kuendelea kupenda, tumtazame Yesu, Tazama madonda yake, tazama alivyotupenda. Omba neema ya kuendelea kupenda bila kipimo!

Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu Katika Fumbo la Utatu Mtakatifu
Roho Mtakatifu ni Nafsi ya Tatu Katika Fumbo la Utatu Mtakatifu   (@Vatican Media)

Fundisho la Tatu: Kwa njia ya Roho Mtakatifu tunapata msamaha wa dhambi, na kutumwa kuwa Wamisionari. Kristo akiisha kuwaonesha madonda yake wanafunzi wake, Ishara ya upendo na huruma yake isiyo na mipaka, anawavuvia Mitume wake, akiwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” Kitendo cha kuvuvia ni ishara ya uumbaji mpya, tukirejea katika kitabu cha Mwanzo 2:7, Mwenyezi Mungu alipomwumba mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai, na mtu akawa nafsi hai. Kumbe Yesu anawavuvia Mitume wake, anawapa nguvu ya kusamehe watu dhambi kwa njia ya Kanisa, ambapo tunakuwa wapya kila tunaposamehewa dhambi zetu. Ile furaha ninayopata moyoni katika Sakramenti ya Kitubio kwa kuambiwa, “Mwenyezi Mungu amekusamehe dhambi zako, nenda na amani” Ni furaha ya namna gani! Nakua mpya kabisa rohoni. Kisha kuwavuvia, anawatuma kuwa Wamisionari wa huruma yake. Ndugu wapendwa, ni Bwana wetu Yesu Kristo kwa huruma yake kubwa aliweka sakramenti hii ya muhimu kabisa katika Kanisa, sakramenti ya Upatanisho ili kutuondolea dhambi, kututakasa, kutusafisha na kutufanya wapya tena machoni pa Mungu. Sakramenti ya Kitubio inatuondolea dhambi zetu zote, inatupatanisha sisi na Mungu, sisi na nafsi zetu, na sisi na wenzetu, kisha tunapata amani na furaha ya kweli ndani ya mioyo yetu. Ni Yesu mwenyewe aliwapa Mitume wake uwezo huu wa kuwaondolea watu dhambi zao. Nasi mapadre, kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu, tunapokea uwezo huu, kwa mamlaka ya Kanisa na kwa niaba ya Kristo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Tusione aibu, kwenda kuungama mara nyingi iwezekanavyo, hakuna kikomo cha huruma ya Mungu. Kila mara tunapoanguka dhambini tukumbuke kuwa Yesu anatuita kwake katika Sakramenti hii ya Huruma yake, na Roho Mtakatifu anatusaidia katika udhaifu wetu. Tunakumbushwa katika sherehe hii kwamba kuwa sisi sote tunaopokea kila siku huruma hii kubwa ya Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu tuna wajibu wa kuwa Wamisionari wa Huruma ya Mungu.

Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume wakapata ujasiri wa kumtangaza Kristo
Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume wakapata ujasiri wa kumtangaza Kristo   (@Vatican Media)

Somo la 1: Ni Kitabu cha Matendo ya Mitume 2:1-11. Somo la Kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume laeleza tukio la kushuka kwa Roho Mtakatifu juu ya Mitume wa Yesu siku ya Pentekoste. Kristo anatimiza Ahadi yake kwa Mitume wake, Ahadi ya kuwapelekea Msaidizi, Roho Mtakatifu, atakayewafundisha na kuwakumbusha yote walioyofundishwa na kuyaona kutoka kwake. Ishara ya uwepo wa Roho Mtakatifu ni Upepo wa nguvu, ndimi za moto na kunena kwa lugha. Ni baada ya kumpokea Roho Mtakatifu Mitume hawa wakiwa katika chumba pamoja na Mama yetu Bikira Maria, wanapata nguvu ya kutoka nje na kuanza kutangaza matendo makuu ya Mungu bila hofu na woga tena. Katika somo hili tunashuhudia kwa namna ya pekee kabisa kazi za Roho Mtakatifu katika maisha mapya ya mitume na utume wa jumuiya ndogo ya wakristo wa kwanza, na kuanza rasmi kwa utume wa Kanisa. Fundisho la kwanza: Roho Mtakatifu anafanya uumbaji mpya ndani mwetu. Upepo mkali uliokuja ghalfa kutoka mbinguni ilikuwa ni ishara ya wazi ya Roho Mtakatifu. Ni ishara ya pumzi ya Mungu (Ruach) inayotia uzima, inayoleta mabadiliko ya ndani, yenye mamlaka ya kuumba na kufanya upya. Kama vile Mungu alivyompulizia Adamu pumzi ya uhai naye akawa nafsi hai (Mwanzo 2:7) ndivyo Mungu anavyopuliza pumzi yake ya uhai ndani ya Kanisa ili liwe hai na imara katika kuishuhudia Injili.

Roho Mtakatifu awape waamini nguvu na ujasiri wa kumtangaza
Roho Mtakatifu awape waamini nguvu na ujasiri wa kumtangaza

Ndugu wapendwa, kwa njia ya ubatizo, sisi tunazaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Tunakuwa hivyo watoto wa Mungu, tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo, tunavua utu wa kale na kuvaa utu mpya. Tunapokea utimilifu wa mapaji yake saba katika Sakramenti ya kipaimara. Hatupaswi kurudi tena katika utu wetu wa kale, hatupaswi kurudi tena katika maisha ya dhambi. Ni roho huyo ndiye anayetia uzima wa kimungu ndani mwetu. Kwa njia ya sakramenti nyingine mbalimbali katika kanisa, Kristo anaendelea kwa njia ya Roho Mtakatifu kulipa kanisa uhai. Katika sakramenti Takatifu ya Ekaristi, ni kwa njia ya Roho Mtakatifu (epiclesis), Kristo anakuwa hai na mzima katika maumbo ya mkate na divai. Anatupa uzima ndani ya Roho zetu.  Fundisho la pili: Roho Mtakatifu anatutakasa na kuondoa ubaridi ndani ya mioyo yetu. Ishara ya pili ya uwepo wa roho Mtakatifu ilikua ni ndimi za moto zilizowashukia mitume. Ndimi za moto, ni ishara ya utakatifu na uwepo wa Mungu (Kut. 3, Musa na kichaka kinachowaka moto). Ndimi za moto ni ishara ya mtendaji mpya wa ndani, Roho Mtakatifu akiwasha mioyo ya waamini kwa mapaji yake saba ili yawaimarishe katika kuishuhudia Imani yao kwa Kristo. Ndimi nyingi za moto ni ishara ya karama mbalimbali ambazo zote zatoka kwa Roho yule yule mmoja. Ndugu mpendwa, kwa muda wa siku tisa tumesali Novena ya Pentekoste kwa tukimwomba Mungu Roho Mtakatifu awashe moto wa mapaji yake ndani mwetu mara zote ambapo tunakuwa baridi na kulala kiroho. Tumwombe Roho Mtakatifu aendelee kututakasa, atakase fikra na mawazo yetu, atakase akili na mioyo yetu, atakase mitazamo yetu ili daima tuendane na mapenzi yake na kutenda tu yale yampendezayo Mungu.

Pentekoste ni Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa: Ushuhuda wa Tunu Msingi
Pentekoste ni Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa: Ushuhuda wa Tunu Msingi   (Vatican Media)

Fundisho la tatu: Roho Mtakatifu analeta umoja na Mshikamano kati yetu. Ishara nyingine ya ujio wa Roho Mtakatifu ilikua ni kunena kwa lugha. Na watu wa kila taifa waliokuwepo Yerusalemu walisikia kila mmoja kwa lugha yake, matendo makuu ya Mungu. Kunena kwa lugha, ni ishara ya wazi kuwa, ujumbe wa Injili sio kwa Wayahudi pekee bali na kwa watu wa mataifa yote. Roho Mtakatifu analeta tena umoja kati ya watu wa mataifa yote, anaondoa mkanganyiko uliotokea katika mnara wa Babeli (Mwanzo 11) ambapo lugha ziliwagawanya watu. Katika Pentekoste, lugha zinawakusanya tena watu, zinaleta umoja katika Kristo na kuvuja kuta zote za utengano na chuki kati ya watu. Walipokea karama mbalimbali na zote chanzo chake ni kimoja, ni Roho Mtakatifu. Waliweza kunena kwa lugha mbalimbali, licha ya utofauti huo, waliweza kuhubiri na kusema matendo makuu ya Mungu na kila mmoja akaelewa kwa lugha yake. Ndugu wapendwa, katika sherehe hii ya Pentekoste, tusali na kuomba umoja kama Kristo mwenyewe alivyotuombea katika sala yake ya kikuhani kwamba, ili wote wawe na umoja (Et unum sint). Tunaishi katika ulimwengu, katika jamii zilizopasuka nyufa nyingi, chuki, visasi, mauaji ya wenyewe kwa wenyewe, migogoro mbalimbali baina ya dini nk. Tumwombe Roho Mtakatifu atuunganishe sote, tuwe wamoja katika Kristo aliyetuleta pamoja watu wa kila kabila, lugha jamaa na taifa kwa Damu yake Msalabani. Tuombee umoja katika familia zetu, tuombee haki na amani katika taifa letu na dunia yote. Lakini umoja na amani ya kweli vinaanza ndani ya mioyo yetu, tujiombee kila mmoja ili awe chombo cha umoja, haki, amani, na mshikamano uletwao na Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba wa Milele
Roho Mtakatifu ni zawadi ya Baba wa Milele   (Vatican Media)

Somo la Pili: Ni Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 12:3b-7, 12-13. Katika somo hili la pili, Mtume Paulo anafundisha kuwa, Roho Mtakatifu ni msingi wa karama zote na huduma mbalimbali katika kanisa. Aliwaandikia waraka huu Kanisa la Korintho ambalo lilikuwa limegawanyika kwa sababu ya mashindano, majivuno, kiburi na maoni mbalimbali juu ya karama za roho Mtakatifu. Wengine walijiona bora kwa sababu walikuwa na karama fulani (kama kunena kwa lugha) na kuwadharau wengine waliokuwa na karama zisizoonekana kama huduma na msaada. Mtume Paulo anawaandikia kusisitiza mambo kadhaa kuhusu karama za Roho Mtakatifu. Jambo la Kwanza: Roho Mtakatifu ni chanzo cha karama zote za kiroho. Mtume Paulo anawafundisha Wakorintho na anatufundisha sisi sote kwamba karama zote chanzo chake ni roho Mtakatifu. Hakuna mtu anapaswa kujivuna kwa kuwa hatuna karama yoyote inayotoka kwetu bali ni Roho Mtakatifu ndiye mgawaji wa karama zote. Ndugu mpendwa, Pentekoste inatukumbusha juu ya ukarimu wa kimungu, anayegawa karama na vipaji mbalimbali kadiri apendavyo. Wengine wamepewa vingi kuliko wenzao, wengine wamepewa vichache. Hatupaswi kujivuna na kujiona kwamba sisi ni wa pekee sana kuliko wengine, pale Mungu alipotupa zaidi, tukawadharau na kuwanyanyasa wengine ambao pengine hawana karama na vipaji kama vile Mungu alivyonijalia mimi na wewe. Tunapaswa kumshukuru Mungu na kuvipokea vyote kwa unyenyekevu mkubwa tukijua kuwa ni Mungu ametupatia bure.

Roho Mtakatifu: Ubatizo na Sakramenti ya Kipaimara
Roho Mtakatifu: Ubatizo na Sakramenti ya Kipaimara

Jambo la pili: Karama zote za Roho Mtakatifu zapaswa kutuunganisha na kujenga jumuiya moja. Mtume Paulo anaelezea karama za roho Mtakatifu kwa mfano wa mwili wenye viungo vingi, yaani kanisa moja ambalo kichwa chake ni Kristo nasi sote tu hivyo viungo vya mwili wa Kristo. Karama zote ambazo tunazo ndugu wapendwa ni kwa ajili ya kuleta umoja na mshikamano kwetu sisi sote tulio ndani ya kanisa. Roho Mtakatifu ni chanzo cha umoja, na hivyo karama yoyote yenye lengo la kuleta utengano hiyo sio karama ya Roho Mtakatifu. Je, ninatumia karama za Roho Mtakatifu katika kuleta umoja na mshikamano katika ufuasi wangu kwa Kristo? Jambo la Tatu: Karama zote za Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya huduma kwa wengine. Mtume Paulo anawafundisha wakorintho nasi sote pia kwamba karama zote za Roho Mtakatifu lengo lake ni huduma kwa wengine. Katika kanisa la Korintho, karama za kiroho zilianza kutumika vibaya, waliokua nazo wakazitumia kwa ajili ya kujipatia sifa na utukufu badala ya kulenga katika kuhudumia wengine katika jumuiya. Tumwombe Roho Mtakatifu atusaidie tukumbuke kuwa tumepewa karama hizi bure, nasi tunapaswa kuzitoa bure kwa wengine bila majivuno, tukilenga katika kuhudumia na kuwastawisha wengine ili wakue na kuimarika kiroho. Hitimisho: Katika Sherehe hii ya Pentekoste, tumshukuru Kristo Yesu ambaye kwa njia ya Roho Mtakatifu sisi sote tumezaliwa upya, tumeimarishwa na kutiwa nguvu ili tuwe mashuhuda Hodari wa Injili ya Kristo kwa watu wote. Tunaposherehekea siku lilipozaliwa rasmi kanisa, tuliombee Kanisa, ili liendelee kuwa chombo cha huruma ya Mungu isiyo na mipaka, na kwa njia hiyo sisi sote tuupate uzima wa milele.

Pentekoste 2026 Roho Mt.
22 Mei 2026, 17:17