Sudan Kusini,Askofu wa Tombura Yambio:tufufue utamaduni wa mazungumzo
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ikweta ya Magharibi haikujulikana tu kama kikapu cha mkate cha Sudan Kusini, lakini pia kama kimbilio la kuishi kwa amani, moyo wa kijani wa Sudan Kusini, bustani ya ukarimu, nchi ya mazungumzo, nchi ya kufanya kazi kwa bidii, mahali patakatifu pa utu wa binadamu. Hivi ndivyo aliandika waraka wake Askofu Eduardo Hiiboro Kussala wa Jimbo katoliki la Tombura Yambio, akiwaelekea mamlaka, viongozi wa kidini, na idadi ya watu wote. Aliandika hayo katika fursa ya Mwezi wa Mei ambao unagusa hisia hasa Sudan Kusini yote kutokana na sherehe ya kitaifa, ambapo matukio ya ukumbusho na mikusanyiko ya kijamii hufanyika ili kuheshimu historia ya uhuru. "Pamoja na hayo kwa miaka mingi, changamoto chungu zimeingia katika jamii yetu," Askofu Hiiboro anaendelea, Vurugu, ukosefu wa utulivu wa kisiasa, ugumu wa kiuchumi, ukosefu wa usalama, uhamisho, kutoaminiana, na mgawanyiko vimeharibu mfumo wetu wa kijamii."
Baada ya miaka mingi ya uchungu
Askofu anabainisha kuw, "sehemu tofauti za jimbo letu tunalopenda, kuanzia mashambulizi ya Jeshi la Upinzani la Lord's Resistance Army (LRA) hadi migogoro huko Mundri, Maridi, Yambio, Ezo, na Tombura, zimepitia maumivu, hofu, uhamisho, na mateso.” Hata hivyo “baada ya miaka hii yote yenye uchungu, ukweli mmoja umekuwa wazi sana: vurugu hazijaponya jamii zetu. Chuki haijarudisha uaminifu. Kisasi hakijaleta amani.” “Amani ya kweli huzaliwa kutokana na mazungumzo. Hii ndiyo sababu leo hii ninawasihi watu wetu wote: tufufue utamaduni wa mazungumzo ya heshima, upatanisho, na umoja.”
Waache viongozi,makanisa,vijana,wanawake,wasomi,asasi za kiraia,na familia wawe madaraja
Askofu Kusala kadhalika anatoa mwaliko kuwa, “Viongozi waache wazungumze kwa uaminifu na jamii. Waache viongozi, makanisa, vijana, wanawake, wasomi, asasi za kiraia, na familia wawe madaraja ya uponyaji na amani. Zaidi ya yote, tulinde utakatifu wa maisha ya mwanadamu. Maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu.” Akitafakari pia matumizi yasiyofaa ya vyombo vya habari, Askofu Hiiboro anakisi jinsi matumizi ya haraka yanavyoweza kuwa na madhara. “Leo, ujumbe usio na mawazo unaweza kuharibu mahusiano yaliyojengwa kwa vizazi vingi,” anasema Askofu mkuu. “Tusi lililoandikwa nyuma ya skrini ya simu linaweza kupanda chuki katika mioyo mingi.”
Maneno yanaweza kuponya au kuharibu,kuunganisha au kugawanya
Maneno yana nguvu. Yanaweza kuponya au kuharibu, kuunganisha au kugawanya. Jamii inakuwa kile ambacho wanachama wake hupanda kila mara kupitia maneno, mitazamo, na vitendo. Kwa hivyo, tujenge lugha inayounganisha ya heshima, hekima, uponyaji, kutia moyo, na uwajibikaji. Maneno yetu yalinde mahusiano badala ya kuyaharibu. Ninawaalika watu wetu wote warudi kwenye maombi na kushikamana kwa nguvu na Kristo, Mfalme wa Amani. Maombi hubadilisha mitazamo, huponya kumbukumbu, hupunguza uchungu, na huifanya upya jamii.
Kwa vijana:tumie nguvu na akili zenu kujenga mustakabali kupitia elimu,kilimo,uvumbuzi
Askofu wa Tombura Yambio, ambaye kwa muda mrefu amejitolea kukuza mazungumzo na kutetea haki za binadamu, anahitimisha wito wake kwa kuwaita kila mtu kwenye umoja, sio mgawanyiko. "Kwa viongozi wa kisiasa: uongozi ni huduma, sio mgawanyiko.” Kwa vijana: tumieni nguvu na akili zenu kujenga mustakabali kupitia elimu, kilimo, uvumbuzi, ujasiriamali, na ujenzi wa amani. Kwa wanawake: endeleeni kuwa walinzi wa maisha, uponyaji, na upatanisho. Kwa viongozi wa kiutamaduni: tambueni upya hekima ya mazungumzo, uvumilivu, na uongozi wa maadili. Kwa viongozi wa kidini: endeleeni kutetea ukweli, haki, amani, na umoja bila woga au ukabila. Na kwa watu wetu wote: tufanye kazi pamoja kurejesha Ikweta Magharibi katika amani na maendeleo, ili jimbo letu liweze kutoa mchango mkubwa kwa umoja na mustakabali wa Sudan Kusini.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.