“Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, aleluya” (Mdo. 1:11). “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, aleluya” (Mdo. 1:11). 

Tafakari Neno la Mungu Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni: Tumaini Letu!

Kristo ni kiini na mtendaji mkuu wa Liturujia inayomheshimu Baba. Yesu ameketi kuume kwa Baba, maana yake: ameketi katika utukufu na heshima ya Kimungu, ambaye Yeye aliyekuwako kama Mwana wa Mungu kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili, baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa. Kuanzia hapo Mitume wamekuwa ni mashuhuda wa Ufalme wa Mungu. Ni Siku ya 60 ya Upashanaji Habari.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Kupaa Bwana. Sherehe hii inaadhimishwa siku ya 40 baada ya ufufuko. Lakini kwa sababu za kichungaji inahamishiwa dominika ya karibu. Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kwamba, Kristo Yesu baada ya kusema nao, akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu. Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka kama zinavyoshuhudia hali mpya na za kimungu ambazo tokea hapo umebaki nazo daima. Lakini kile kipindi cha siku arobaini ambako alizoea kula na kunywa pamoja na wafuasi wake, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa mbinguni, utukufu wake bado ulifunikwa na alama za ubinadamu wa kawaida. Tokeo la mwisho la Yesu linakamilika na kuingia bila kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu uliojionesha katika sura ya wingu na mbingu (Lk 24:51) ambako tangu hapo ameketi kuume kwa Mungu. Kwa namna moja tofauti kabisa na ya pekee atajionesha kwa Paulo “kama mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake” katika tokeo la mwisho lililomfanya kuwa Mtume. Hali iliyofunikwa ya utukufu wa Kristo Mfufuka kipindi hiki inaonekana katika maneno yake ya fumbo kwa Mariamu Magdalena: “Sijapata kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ninapaa kwenda kwa Baba yangu, naye ni Baba yenu.” Yn 20:17. Hii inaonesha tofauti ya kujidhihirisha kati ya utukufu wa Kristo Mfufuka na ule wa Kristo aliyetukuzwa kuume kwa Baba. Tukio ambalo kwa upande mmoja ni la kihistoria na bora sana linaloonesha kupita toka upande mmoja kwenda upande mwingine. Lakini yote yanabaki yakiwa yameungana kabisa na lile la kwanza yaani kushuka kutoka mbinguni kulikotekelezwa katika Fumbo la Umwilisho. Ubinadamu ukiachiwa katika nguvu zake za maumbile hauwezi kufika kwenye nyumba ya Baba wa milele. Kristo Yesu peke yake ameweza kumfungulia mwanadamu njia hii “ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu na kwamba, akiisha inuliwa juu ya nchi atawavuta wote kwake.” Huku ni kuinuliwa juu ya Msalaba ambako huonesha na kutangaza kuinuliwa kwa kupaa mbinguni. Huo ndio mwanzo wake.

Mtakuwa Mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia
Mtakuwa Mashuhuda wangu hadi miisho ya dunia   (@Vatican Media)

Mbinguni Kristo Yesu anatekeleza Ukuhani wake daima, Yeye ni kiini na mtendaji mkuu wa Liturujia inayomheshimu Baba wa mbinguni. Kristo Yesu ameketi kuume kwa Baba, maana yake: ameketi katika utukufu na heshima ya Kimungu, ambaye Yeye aliyekuwako kama Mwana wa Mungu kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili, baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa. Kuanzia hapo Mitume wamekuwa ni mashuhuda wa Ufalme usiokuwa na mwisho. Rej. KKK 659-664. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 17 Mei 2026, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 60 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kuhifadhi Sauti na Nyuso za Binadamu.” Baba Mtakatifu Leo XIV anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuhakikisha kwamba, uvumbuzi wa teknolojia, hasa matumizi ya teknolojia ya akili unde, inamhudumia binadamu badala ya kuchukua nafasi au kupunguza utu, heshima na haki msingi za binadamu. Wimbo wa mwanzo unaashiria tukio hili ukisema; “Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Atakuja vivyo hivyo mlivyomwona akienda zake mbinguni, aleluya” (Mdo. 1:11). Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 666 inatupa faraja na matumaini ikituambia kuwa; “Yesu Kristo, kichwa cha Kanisa, ametutangulia katika ufalme mtukufu wa Baba, ili nasi viungo vya huo mwili, tuishi katika tumaini la kuwa pamoja naye milele, siku moja huko mbinguni.” Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utufanye tuwe na furaha takatifu na shukrani; kwa maana kupaa kwake Kristo Mwanao ni mfano wetu; na huko alikotangulia Yeye kichwa chetu, ndiko tunakotumaini kufika sisi tulio mwili wake.”

Nendeni Duniani Kote mkatangaze habari Njema ya Wokovu
Nendeni Duniani Kote mkatangaze habari Njema ya Wokovu

Somo la kwanza ni la kitabu cha matendo ya Mitume (Mdo. 1:1-11). Mwandishi wa kitabu hiki, Mwinjili Luka, anatueleza kilichotokea kabla ya kupaa kwake Yesu mbinguni. Kuwa baada ya mateso, kifo na ufufuko wake, aliwatokea mitume wake kwa muda wa siku arobaini kuwadhihirishia ya kwamba yu hai, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu. Alipokutana nao mara ya mwisho aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali wakae humo waingoje ahadi ya Baba, yaani Roho Mtakatifu akiwaambia; “Mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Akiisha kusema hayo, akainuliwa, wingu likampokea, nao hawakumuona tena kwa machoni yao. Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 665 na 668, inafundisha hivi; “Kupaa kwa Kristo ni alama dhahiri ya kuingia ubinadamu wake ndani ya makao ya mbingu ya Mungu, ambako toka huko atarudi, lakini ubinadamu huu kwa sasa unamficha mbele ya macho ya watu. Hivyo kupaa kwake mbinguni kunaonyesha kushiriki kwake, katika ubinadamu wake, nguvu na mamlaka ya Mungu mwenyewe. Yeye sasa anashika mamlaka yote mbinguni na duniani…yu juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani kwa sababu Baba amevitia vitu vyote chini ya miguu yake. Kristo ni Bwana wa ulimwengu na wa historia. Ndani yake historia ya mwanadamu na pia uumbaji wote hujumlishwa na kutimilizwa kwa namna iliyo bora kabisa”. Huu ndio ukuu wa Mungu wetu aliaoudhihirisha katika Mwanae Yesu Kristo ambao zaburi ya wimbo wa katikati inauimba ikisema hivi; “Enyi watu wote pigine makofi, mpigieni Mungu kelele kwa sauti ya shangwe; Kwa kuwa Bwana aliye juu mwenye kuogofya, ndiye mfalme mkuu juu ya dunia yote. Mungu amepaa kwa kelele za shangwe, Bwana kwa sauti ya baragumu. Mwimbieni Mungu, naam, imbeni; Mwimbieni mfalme wetu, naam, imbeni. Maana Mungu ndiye mfalme wa dunia yote, imbeni kwa adili. Mungu awamiliki mataifa, Mungu ameketi katika kiti chake kitakatifu (Zab 47:1-2, 5-6, 7-8).

Mtakuwa Mashuhuda wangu hadi miisho yote ya dunia
Mtakuwa Mashuhuda wangu hadi miisho yote ya dunia   (@Vatican Media)

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Ef. 1:17-23). Ni sala inayokiri uweza na utajiri wa Mungu uliofunuliwa katika Yesu Kristo. Inasema hivi; “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua Yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.”Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 669-670, ikinukuu maandiko haya inafundisha hivi; “Bwana Yesu Kristo ni kichwa cha Kanisa ambalo ni mwili wake. Akiwa ameinuliwa mbinguni na kutukuzwa, baada ya kumaliza kikamilifu utume wake, anabaki duniani katika Kanisa lake. Ukombozi ni chemchemi ya mamlaka ya Kristo, ambayo anayatekeleza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu juu ya Kanisa. Utawala wa Kristo uko tayari kwa namna ya fumbo katika Kanisa, mbegu na mwanzo wa ufalme huu duniani. Baada ya kupaa, mpango huo wa Mungu umeingia katika utimilifu wake. Sisi tumo tayari katika saa ya mwisho. Kipindi cha mwisho cha nyakati kimeshafika, na kufanywa upya kwa ulimwengu kumepangwa bila kutenguliwa, na kwa hakika kabisa kumetangulizwa: toka sasa; kwa kweli tayari hapa duniani Kanisa limepambwa na utakatifu wa kweli, ingawa si mkamilifu.”

Nendeni duniani kote mkatangaze na kushuhudia Injili
Nendeni duniani kote mkatangaze na kushuhudia Injili

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 28:16-20). Ni maagizo ya mwisho ya Yesu kwa wanafunzi wake kabla ya kupaa kwake akiwaambia; “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi…Na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 667 anatufundisha hivi; “Yesu Kristo, akiwa ameingia mara moja kwa daima ndani ya hekalu la mbingu, anaomba daima kwa ajili yetu kama mshenga anayetuhakikishia kumiminwa kwa daima Roho Mtakatifu”. Hii inatueleza maana ya kupaa kwake, kuwa sio kwenda juu kijografia, bali ni kuingia katika hali ya utukufu wa Mungu, kutokufungwa na nguvu za kimaumbile, kitendo kilichotokea mara baada ya ufufuko wake. Na katika namba 659-664 inatufundisha hivi; Mwili wa Kristo ulitukuzwa wakati ule ule alipofufuka na umebaki na hali hiyo daima hata kipindi kile cha siku arobaini alizakuwa anawatokea mitume wake. Na tokeo la mwisho la kuingia bila kurudi kwa ubinadamu wake katika utukufu wa Mungu ulijionyesha katika sura ya wingu ambako tangu hapo ameketi kuume kwa Mungu. Hii inaonyesha tofauti ya kujidhihirisha kati ya utukufu wa Kristo Mfufuka na ule wa Kristo aliyetukuzwa kuume kwa Baba. Hivyo tunaposema ameketi kuume kwa Baba, tunamaanisha utukufu na heshima ya kimungu, ambamo Yeye aliyekuwako kama Mwana wa Mungu kabla ya nyakati zote, kama Mungu, na mwenye uwamo mmoja na Baba, anaketi kimwili baada ya kumwilishwa na baada ya mwili wake kutukuzwa. Ndio kuonyesha kuanzishwa kwa utawala wa Masiha, kwa Mwana wa mtu kupewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na mataifa yote na lugha zote, wamtumikie. Na mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo haitapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. Kuanzia hapo mitume wamekuwa mashahidi wa ufalme usiokuwa na mwisho.

Mtakuwa ni Mashuhuda wa Injili Hadi Miisho ya Dunia
Mtakuwa ni Mashuhuda wa Injili Hadi Miisho ya Dunia   (@Vatican Media)

Hivyo tunapoadhimisha sherehe hii ya kupaa Bwana, tunakumbushwa wajibu wetu wa kikristo tulioupokea kutoka kwa Mitume kwa njia ya ubatizo, wajibu wa kuyafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wake. Hivyo kila mmoja akitimiza wajibu huu wa uinjilishaji, tunakuwa tunashughulika na mambo ya mbinguni kama sala baada ya komunyo inavyosisitiza; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe watujalia sisi tulio hapa duniani kushughulika na mambo ya mbinguni. Tunakuomba uelekeze moyo wetu wa ibada huko aliko Bwana wetu, Mungu-mtu”. Na hivyo kila tunaposhughulika na mambo ya mbinguni tungali bado tuko duniani tunayakaribia ya mbinguni kama sala ya kuombea dhabihu inavyotilia mkazo ikisema; “Ee Bwana, tunaleta sasa kwa unyenyekevu sadaka yetu kwa heshima ya kupaa kwake Mwanao. Tunakuomba utujalie kila tunapoyapokea mafumbo haya matakatifu, tuzidi kuyajongea ya mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Sherehe ya Kupaa Bwana
15 Mei 2026, 15:04