Ekaristi Takatifu: Chanzo na Kilele Cha Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Ekaristi Takatifu, mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Sherehe hii inapaswa kuadhimishwa Alhamisi baada ya Utatu Mtakatifu kwa kuwa ilikuwa ni Alhamisi Kuu, Yesu alipoisimika Ekaristi Takatifu. Lakini inahamishiwa dominika baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu waamini wote wapate nafasi ya kushiriki. Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku tarehe 6 Juni 2026 anafanya mkesha na vijana wa kizazi kipya kutoka Hispania, kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo, yaani Ekaristi Takatifu: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini inayoadhimishwa Dominika tarehe 7 Juni 2026. Hii ni fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha imani yao katika Fumbo hili kuu la Ekaristi Takatifu, kwa kuunganisha sauti za nyimbo kama kielelezo cha moyo wa shukrani, kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake. Ni wito kwa waamini kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, kwani Mwenyezi Mungu kwa wingi wa baraka na neema zake ni Mhusika mkuu, lakini anategemea pia ushiriki wa waamini katika kuganga na kuponya magonjwa ya waamini kiroho na kimwili. Kristo Yesu ni daktari wa roho na mwili! Baba Mtakatifu Leo XIV amesema, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu ni fursa ya kuzama zaidi katika imani katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na hivyo kuendelea kupyaisha upendo kwa Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.
Lakini kwanini tunairudia kuiadhimisha sherehe hii? Ni kwa sababu ya umuhimu na ukuu wake. Ekaristi Takatifu ni kitovu, kilele, chemchemi, mwanzo na mwisho wa maisha yote ya kikristo na shughuli zote za Kanisa (Rej. Lumen Gentium 11, Presbyterorum Ordinis 5, 6). Hivyo, kwa kuwa tulipoiadhimsiha wakati wa Pasaka, siku ya Alhamisi Kuu jioni, hatukufanya kwa shangwe kubwa kwa kuwa msisitizo ulikuwa katika kukumbuka mateso ya Kristo, tunarudia kuiadhimisha kwa shangwe zaidi ili kumsifu na kumshangilia Kristo, hasa kwa njia ya maandamo, na kumshukuru kwa zawadi kubwa aliyotuachia ya kubaki na kukaa nasi nyakati zote katika Ekaristi Takatifu chakula chetu cha roho, Mwili na Damu yake, ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuka wake, nasi tumepata wokovu kwa ajili ya hayo. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umetuachia ukumbusho wa mateso yako katika sakramenti ya ajabu. Tunakuomba utujalie kuyaheshimu mafumbo matakatifu ya mwili na damu yako, tupate daima neema ya ukombozi wako ndani yetu.”
Somo la kwanza ni kutoka katika la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kum. 8:2-3; 14-16a). Linatueleza jinsi Waisraeli wakiwa jangwani, walivyojifunza kumtegemea Mungu kwa kila kitu ikiwemo chakula, manna aliyowapa Mungu kutoka mbinguni, ambayo ni mfano wa Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho. Ni katika tumaini hili wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Nimewalisha kwa unono wa ngano na kuwashibisha kwa asali itokayo mwambani” (Zab. 80:17). Na zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Msifu Bwana, Ee Yerusalemu; Msifu Mungu wako, Ee Sayuni. Maana ameyakaza mapingo ya malango yako, amewabariki wanao ndani yako. Ndiye afanyaye amani mipakani mwako, akushibishaye kwa unono wa ngano. Huipeleka amri yake juu ya nchi, Neno lake lapiga mbio sana. Humhubiri Yakobo neno lake, na Israeli amri zake na hukumu zake. Hakulitendea taifa lo lote mambo kama hayo, wala hukumu zake hawakuzijua. Aleluya” (Zab. 147:12-15, 19-20). Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 10:16-17). Nalo linatufundisha kuwa kupokea Ekaristi Takatifu ni kumpokea Yesu Kristo mzima na kuunganika naye, na muungano huu unatufanya sisi wenyewe tuwe wamoja na hivyo kwa kuwa tupo wamoja, tunapaswa kuishi kwa umoja na mapendo. Tunasoma hivi; “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, Je! Si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja”. Hii ina maana kwamba Ekaristi Takatifu ni ishara ya umoja na kifungo cha mapendo, na amana ya uzima wa milele (rej. KKK 1322 – 1323, 1409).
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 6:51-58). Nayo inatusihi na kutuasa tusadiki kuwa Yesu wa Ekaristi ni chakula kweli na cha uzima, sababu Yeye ametoa uhai wake ili kutupa sisi uzima wa Kimungu. Hivyo tukitaka kweli kupata uzima wa milele na kushiriki furaha za mbingu, inatupasa kuipokea Ekaristi Takatifu tukiwa katika moyo safi bila doa wala mawaa yoyote. Ni katika tumaini hili, mama Kanisa anatufundisha kuwa Ekaristi Takatifu ni Kristo mwenyewe aliyejitoa Sadaka ya upatanisho wetu na Mungu Baba. Sadaka hii huitwa Misa Takatifu, Ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana. Kwetu sisi ni sadaka ya shukrani kwa Mungu, aliyotuachia Yesu Kristo mwenyewe ili tumtolea Mungu Baba kwa nyakati zote katika karamu ya kuumega mkate, kusanyiko la Kiekaristi, Liturujia Takatifu, Sakramenti Takatifu sana ya Altare ambayo kwayo Yesu mwenyewe anamimina neema za wokovu kwa mwili wake ambao ni Kanisa (KKK 1407). Ni katika muktadha huu Papa Leo XIII anasema; “Ekaristi Takatifu ni roho ya Kanisa” (Denz.3364). Hivyo Kanisa haliwezi kitu pasipo yenyewe, na hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa na kusimama imara bila Ekaristi Takatifu. Ni katika Ekaristi tendo la Mungu kuutakatifuza ulimwengu na watu kumwabudu kama inavyopaswa hufanywa na hufanyika kwa njia ya Kristo mwenyewe, Pasaka wetu. Ndiyo maana ni katika adhimisho la Ekaristi, Kanisa hutolea maisha, masifu, mateso, sala na kazi za waamini na kuyaunganisha na sadaka ya Kristo kwa Mungu Baba. Kwa vile ni sadaka, Ekaristi hutolewa kwa waamini wote, wazima na wafu, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi ili kupata rehema ya Mungu, ambapo Kanisa la Mbinguni linaungana na matoleo ya Kristo (rej. KKK 1324 – 1327).
Ekaristi Takatifu kama Sakramenti, ni “Sakramenti ya Sakramenti”, ni Kristo mwenyewe (rej. KKK. 1211). Mtakatifu Tomaso wa Akwino anasema; Sakramenti zingine zinatuelekeza kwake. Hivyo hii ni Sakramenti ya utimilifu wa maisha ya kiroho na ndio mwisho ambao Sakramenti zingine zote hulenga, kwani ndani yake mno uwemo na uwepo wa kweli na halisi, ubinadamu na umungu wa Kristo mwenyewe (rej. KKK 1374). Mababa wa Mtaguso wa Trento walitoa tamko kuwa: “Kwa sababu Kristo mwenyewe alisema kwamba ulikuwa ni mwili wake kweli ambao alikuwa anautoa sadaka kwa namna ya mkate, na damu yake halisi kwa namna ya divai, imekuwa tayari imethibitishwa kwa Kanisa la Mungu, kwamba kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate na divai kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na ya kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake (KKK 1376). Uwepo huu huanza dakika ya mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwepo. Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai, na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao, kwa jinsi hii kwamba kuimega Ekaristi Takatifu, hakumgawanyi Kristo hata kidogo, uwepo wake unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika, na hata katika kila tone la damu yake uwepo wake umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima (KKK 1377). Huu ni ukweli wa kiimani aliotufunulia Kristo mwenyewe, nasi tunaamini na kusadiki hivyo.
Kristo anasema kuwa; “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu, hukaa ndani yangu nami ndani yake.” Maana yake ni kuwa tunapopokea Ekaristi Takatifu, tunakuwa na ukristo ndani mwetu tunakuwa kitu kimoja na Kristo, ndiyo maana tunaitwa wakristo. Hivyo mbele ya Ekaristi Takatifu, tofauti zetu za kisiasa, kivyama, kitaifa, kikabila, au kirangi, hazipaswi kuwa na nafasi kwa kuwa kila mmoja ana ukristo ndani yake. Ndiyo maana Didache, mafundisho ya mitume inafundisha kuwa, siku ya Bwana asiruhusiwe mtu yeyote aliye na ugomvi na jirani yake ajiunge na wengine katika kuumega mkate mpaka awe amefanya usuluhisho, la sivyo sadaka hiyo inakuwa ni batili (Didache 9,14,1-2). Hivyo, kwa mkristo kuinua upanga dhidi ya mwingine ni kwamba anajiinulia upanga mwenyewe na anamuinulia Kristo upanga. Ndiyo maana Saulo alipokuwa anawatesa Wakristo, Yesu alimuita na kumuuliza akisema; “Saulo, Saulo, kwanini wanitesa?” (rej. KKK 1391 – 1397). Ndugu wapendwa, ni hasara kubwa sana kutokupokea Ekaristi Takatifu kwa kujiwekea vikwazo na vizuizi. Nawasihi, fanyeni bidii kubomoa kuta za vizuizi na kutoa vikwazo, mpokee Ekaristi Takatifu, ili muungane na jamii ya waamini na kuwa kweli wakristo. Tukiwa na tofauti katika familia, katika nafasi za kazi, katika vyama vya siasa, tuiangalie Ekaristi Takatifu, ili iwe sababu yetu ya kusameheana, kuthaminiana, kuheshimiana na kupendana kwa kuwa ndiyo inayotuunganisha na kutufanya tuwe wamoja. Ni katika tumaini hili sala ya kuombea dhabihu inakazia kusema; “Ee Bwana, tunakuomba kwa wema wako ulijalie Kanisa lako neema ya umoja na amani; kwa maana umoja na amani huonyeshwa kwa fumbo katika dhabihu hizi tunazokutolea”. Kwa namna hii tunaanza kuonja furaha za mbinguni tungali bado tuko duniani kama sala baada ya komunyo inavyohitimisha maadhimishoya sherehe hii ikisema; “Ee Bwana, tunakuomba utujaze na furaha isiyo na mwisho ya kuutazama umungu wako. Tunaona ishara ya furaha hiyo hapa duniani katika kupokea Mwili na Damu yako takatifu.” Tumsifu Yesu Kristo!