Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Maandamano: Kuliishi, Kulitafakari, Kulitangaza na Kulishuhudia!
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi. Wapendwa Familia ya Mungu, Alhamisi baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo, sherehe ijulikanayo kama: “Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi.“ Sherehe hii huadhimishwa Alhamisi baada ya Sherehe ya utatu Mtakatifu, lakini kwa sababu za kichungaji, katika majimbo mbalimbali huadhimishwa Dominika baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu. Mama Kanisa ameamua hivyo ili kuwapa Watoto wake nafasi ya kufurahia, kumsifu, kumwabudu na kumpa Mungu heshima ya pekee katika fumbo la Ekaristi Takatifu, kwa maandamano yanayofanyika baada ya Misa Takatifu ili kuliishi, kulitafakari, kulishuhudia na kuonesha umuhimu na uhitaji wa Fumbo hili Takatifu katika Maisha yetu ya kiroho. Liturujia ya Neno la Mungu katika Sherehe hii inatutafakarisha kuwa, “Ekaristi Takatifu ni Chanzo na Kilele cha Maisha ya Mkristo.” Baba Mtakatifu Leo XIV kuanzia tarehe 6 hadi 12 Juni 2026 anafanya Hija ya 4 ya Kitume nchini Hispania kwa kunogeshwa na kauli mbiu: "Alzad la mirada" Yaani "Inua macho yako.” Yn 4:35.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi usiku tarehe 6 Juni 2026 anafanya mkesha na vijana wa kizazi kipya kutoka Hispania, kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo, yaani Ekaristi Takatifu: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini inayoadhimishwa Dominika tarehe 7 Juni 2026. Hii ni fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha imani yao katika Fumbo hili kuu la Ekaristi Takatifu, kwa kuunganisha sauti za nyimbo kama kielelezo cha moyo wa shukrani, kwa uwepo angavu wa Kristo Yesu katika Kanisa lake. Katika Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu ambaye kwa mapendo makubwa alimtoa kwetu mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, akatwaa mwili na kukaa kati yetu, akashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake, na bado amebaki nasi kwa daima katika maumbo ya mkate na divai. Tuombe neema ya kudumu katika ushirika na Kristo, kwa kumpokea daima kwa imani na katika hali ya neema katika Ekaristi Takatifu ili tuweze kunufaika na matunda yatokanayo na kule kupokea kwetu Fumbo hili Takatifu. Chimbuko la Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo: Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo ilianzishwa rasmi katika Kanisa kutokana na uwepo na kusambaa kwa ibada mbalimbali kwa heshima ya Ekaristi Takatifu, mapema katika karne ya 13AD. Kwa kusaidiwa na wanateolojia mbalimbali na viongozi wa Kanisa kwa wakati huo, Sherehe hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 1246 katika Jimbo la Liége huko Ubelgiji ikijulikana kama Corpus Christi, yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo.
Mwaka 1263, uliotokea muujiza wa Ekaristi Takatifu huko Bolsena, nchini Italia ambapo Hostia Takatifu ilivuja damu wakati wa Ibada ya Misa Takatifu wakati ambapo Padre aliyeadhimisha alikua na mashaka juu ya uwepo halisi wa Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Muujiza huu ulipelekea kukua na kusambaa kwa haraka kwa ibada kwa Ekaristi Takatifu, na kwa namna ya pekee Sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mwaka 1264 Baba Mtakatifu Urbano IV aliidhinisha Sherehe hii iadhimishwe katika Kanisa kote ulimwenguni. Alimwomba Mtakatifu Tomasi wa Aquino kuandika nyimbo na machapisho mbalimbali ya kiliturjia kwa ajili ya sherehe hii kama vile: “Pange Lingua, Tantum Ergo na Adore te.” Baadaye Mababa wa Mtaguso wa Trento (1545-1563) walifundisha kuwa, “Tunapaswa kumpa heshima Bwana wetu Yesu katika Ekaristi Takatifu hadharani ili wale wanaotazama Imani ya Wakristo Wakatoliki waweze kuvutwa na Yesu Ekaristi Takatifu, na kuweza kuamini katika Umungu wa Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai na mzima katika Fumbo Takatifu sana la Ekaristi Takatifu” Hii ilitokana na kuwepo kwa mafundisho mbalimbali ya uzushi juu ya Ekaristi Takatifu na juu ya uwepo halisi wa Kristo (Real Präsenz) katika maumbo ya Mkate na divai, kuabudu Ekaristi Takatifu nje ya Ibada ya Misa Takatifu na maandamano ya Ekaristi Takatifu.
Katika marekebisho ya Liturujia yaliyofanywa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican 1962-1965, Sherehe hii iliunganishwa na Sherehe ya Damu Takatifu ya Yesu ambayo huadhimishwa tarehe 1 Julai, ili kusisitiza taalimungu ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Na hivyo jina lilibadilika kutoka Corpus Christi yaani Sherehe ya Mwili wa Kristo na kuitwa Sollemnitas Sanctissimi Corporis et Sanguinis Christi, yaani Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo na ndivyo inavyojulikana hata sasa. Tunapoadhimisha Sherehe ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo, tukiongoza na Liturjia ya Neno la Mungu, tuna mafundisho matano yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Fundisho juu ya Uwepo halisi wa Kristo katika Ekaristi Takatifu (Real Presence of the Lord in the most holy Eucharist). Sherehe hii ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo inatukumbusha kuwa Ekaristi Takatifu sio tu alama, bali ni uwepo halisi, wa kudumu na wa kweli wa Yesu katika maumbo ya Mkate na divai. Uwepo huu halisi na kweli katika maumbo haya huanza katika mageuzo katika Adhimisho la Ekaristi Takatifu, kwa sala ya kuhani na kwa kunyoosha mikono yake juu ya mkate na divai. Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Mkate hugeuka kuwa mwili halisi wa Kristo na Divai kuwa Damu halisi ya Kristo, mabadiliko yajulikanayo kama “Transubstantiation.”
Ndugu mpendwa, kila mara tunapohudhuria Ibada ya Misa Takatifu tunaweza kujiuliza maswali kwamba, muujiza huu mkubwa namna hii katika Imani yetu hutokea vipi katika ibada ya Misa Takatifu? Ni mkate tu wa kawaida na divai, inawezekanaje kuwa mwili na Damu ya Kristo? Mababa wa Mtaguso wa Trento wanatufundisha hivi juu ya fundisho hili muhimu sana kuhusu Ekaristi Takatifu; wanatufundisha kwamba, “Kwa sababu ni Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba huu ndio mwili wangu (tukisoma katika Maandiko Matakatifu katika Adhimisho la Karamu ya mwisho, Mt 26:26-29; Mk 14:22-25; Lk 22:14-20; 1 Kor 11:23-26 na Injili ya Yohane sura ya 6), akautoa mwenyewe kwa namna ya mkate na damu kwa namna ya divai. Aliwaamuru Mitume na akawapa uwezo kufanya hivyo kwa ajili ya ukumbusho wake, akikamilisha sadaka hii pale msalabani siku ya Ijumaa kuu. Hivyo kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake.” Kristo anatualika tuwe na Imani thabiti kwake kwamba ni yeye, aliye hai, mzima na kweli katika maumbo haya ya mkate na divai. Tuombe neema ya kuimarika katika Imani. Tusiwe na shaka kwa kuwa tunampokea Kristo aliye hai na mzima katikati yetu. Kila mara tunapopokea Ekaristi Takatifu tumwombe Kristo atuongezee Imani. Uwepo huu halisi wa Kristo katika maumbo hayo hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwapo, yaani muda wote ambapo maumbo hayo hayajapoteza ile sifa yake ya asili kwa kuharibika.
Marekebisho ya Sheria ya Kanisa (Canon Law 939) yanasisitiza kuwa Hostia Takatifu katika tabernakulo zinapaswa kubadilishwa mara kwa mara ili kuzuia zisiharibike. Ndio maana tunaona mara kwa mara mapadre wakiwa wanabadilisha Hostia Takatifu iliyo katika tabernaklo. Kwa sababu za kimazingira, unyevu, joto au baridi, maumbo haya huweza kupoteza hali au sifa yake ya asili, yaani mkate ukapoteza ubora na sifa yake ya kuwa mkate, na divai kupoteza ubora au asili yake ya kuwa divai. Hivyo tunaalikwa kuhakikisha tunatunza vyema katika hali nzuri hostia ambazo hazijabarikiwa bado, lakini pia tusiziweke kwa muda mrefu sana, kwa kuwa mkate ukipoteza hadhi yake ya kuwa mkate, basi hakuna uwepo halisi wa Mungu katika hostia hizo, kwa kuwa utakua si mkate tena, wala divai itakuwa si divai tena halisi. Katika ibada ya Misa Takatifu katika matoleo, mkate na divai viletwe katika hali ya heshima, tusivichanganye na vitu vingine kama sabuni, vyakula, mapambo nk. viletwe kwa heshima kwa kuwa vinatumika kwa ajili ya Fumbo hili Takatifu sana la Ekaristi.
Pili: Ekaristi Takatifu ni chakula cha Kiroho kinachotupatia sisi uhai na uzima wa roho zetu. Tumshukuru Mungu daima kwa zawadi hii. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha kumbukumbu la Torati 8:2-13; 14-16a, ni hotuba ya Musa kwa wana wa Israeli wakiwa wamekaribia kabisa kuingia katika nchi ya Ahadi. Musa anawasihi kwamba kamwe wasisahau kwamba walifika hapo sio kwa mastahili yao bali ni kwa sababu Mungu alikuwa pamoja nao, na kwamba watakapofanikiwa kuingia katika nchi ya Ahadi, kamwe wasimsahau Mungu, wasisahau kushukuru, wasifikiri ni kwa nguvu na uwezo wao ndivyo vilivyowafikisha hapo. Wakiwa Jangwani ni Mungu aliwapa maji na chakula, aliwalinda na maadui, aliwaongoza mchana na usiku katika jangwa tupu litishalo, aliwasamehe walipomkosea na ni Mungu ambaye anakwenda sasa kuwapatia nchi ya Ahadi. Kumbe Chakula hicho alichowapa Bwana jangwani wana wa Israeli ndio mfano wa Ekaristi Takatifu katika Agano jipya. Ndugu mpendwa, Bwana wetu Yesu Kristo katika somo la Injili Takatifu kutoka Injili ya Yohane ile sura ya 6 anasema, “Mimi ndimi Chakula cha uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila Chakula hiki ataishi milele. Na Chakula nitakachowapa mimi ni mwili wangu wa ajili ya uzima wa ulimwengu. Kumbe tukitaka kuupata uzima wa Kimungu ndani mwetu hatuna budi kumpokea Yesu, Mkate wa uzima katika maisha yetu. Jangwa katika maandiko Matakatifu ni mfano wa maisha yetu ya sasa, kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli, maisha yaliyojaa majaribu na shida. Katika hayo yote tunapaswa kuona na kutambua uwepo wa Mungu aliye daima Katikati yetu. Ni wazi kwamba sisi wenyewe katika safari yetu ya maisha hatuwezi.
Kila mmoja wetu atafakari kwa kina katika Sherehe hii na kila mara tunapopokea Ekasti Tatakatifu, ni mambo mangapi Mungu amenitendea katika maisha yangu hata bila mastahili yangu? Katika hayo, ni mara ngapi nilirudi kumshukuru Mungu? Mungu anaponiinua, anaponibariki, anapoiinua familia yangu, anapobariki kazi zangu, anapobariki na kufanikisha utume wangu, amewabariki Watoto nk, je, bado natambua kuwa bila yeye siwezi lolote? Mara nyingi mafanikio yetu yanaweza kutufunga macho na kufikiri tunaweza kuishi kwa mkate pekee na kusahau Neno la uzima litokalo katika kinywa cha Bwana. Kila mara tunapopokea Ekaristi, tuombe neema ya kuwa watu wa Shukrani. Tuombe nguvu ya kusikia daima kutoka kwa Kristo na kutenda yale yampendezayo yeye. Neema ya Ekaristi Takatifu itupe nguvu ya kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu, na kumpa yeye nafasi ya kwanza. Kamwe usisahau kumshukuru Mungu, aliyekutoa katika dhiki, katika nyumba ya utumwa, aliyekupitisha katika jangwa tupu litishalo lenye nyoka na ng’e, nchi ya kiu isiyokuwa na maji, aliyekutolea maji katika mwamba mgumu, aliyekulisha jangwani kwa mana wasiyoijua Baba yako. Mwenyezi Mungu anasema na moyo wangu kama alivyokuwa ananena na wana wa Israel kwa kinywa cha Musa, kila mara, pale ninapofanikiwa na kumsahau yeye na kudhani kuwa peke yangu ninayaweza mambo yote. Nguvu hii tutaipata kama tunampokea na kukubali akae ndani mwetu. Hapo mioyo yetu haitainuka na kumsahau kwa kuwa anaishi daima ndani mwetu. Tunaalikwa kumtegemea Mungu kabisa. Kama vile Waisraeli walivyohitaji mana kila siku ili wasife jangwani, sisi tunahitaji Ekaristi ili roho zetu zisife katika jangwa la dhambi la dunia hii.
Tatu: Ekaristi Takatifu ni Ishara na kifungo cha Umoja na Upendo kati yetu na Mungu na kati sisi kwa sisi. (Koinonia/Communion). Kristo anatuambia katika somo la Injili Takatifu ya Yohane sura ya 6:51-18, “Aulaye mwili wangu na kuinywa Damu yangu hukaa ndani yangu nami hukaa ndani yake (Yn 6:56). Mtume Paulo hali kadhalika katika somo la pili, (1 Wakorintho 10:16-17) anasema: “Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Maana mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa kuwa sisi sote twashiriki mkate ule mmoja.“ Sherehe hii ya Mwili na Damu Takatifu sana ya Bwana wetu Yesu Kristo yatukumbusha kuwa tunapopokea Ekaristi Takatifu tunaingia katika ushirika na Kristo, anakaa ndani mwetu nasi tunakaa ndani mwake. Ndugu mpendwa, Ekaristi Takatifu yatupa nafasi ya kuingia katika ushirika na Mungu. Katika ibada ya misa Takatifu, Padre anapochanganya maji na divai wakati akiandaa vipaji, anasali na kusema, “Kwa fumbo la maji haya na divai hii tujaliwe kushiriki Umungu wa Kristo, yeye aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu” Kumbe Mungu aliye mtakatifu amekubali kuingia katika historia yetu ya dhambi ili aigeuze kuwa historia ya wokovu wa milele. Tunapoingia katika ushirika na Mungu tunaalikwa kuingia katika ushirika kati yetu sisi kwa sisi. Tunaalikwa kupokeana katika mazuri na madhaifu yetu, tunaalikwa kuchukuliana kwa upendo na upole, tunaalikwa kusameheana pale tunapokosana bila masharti. Kila mara tunapoharibu ushirika huu mtakatifu kwa sababu ya dhambi tunaalikwa kuendea sakaramenti ya Kitubio ili daima tuwe wamoja na Kristo na matunda ya uwepo wake ndani mwetu yaonekane wazi.
Nne: Ekaristi Takatifu ni ukumbusho wa Sadaka ya Kristo, ukumbusho Ukombozi wetu kutoka utumwa wa dhambi na mauti (Anamnesis). Mtume Paulo anapofundisha fundisho muhimu juu ya Karamu ya Bwana kwa jumuiya ya Wakristo wa Korintho aliwafundisha kwamba, Ekaristi sio tu chakula cha kawaida, sio tu karamu ya kawaida, bali ni sadaka ya ukumbusho wa mateso ya Bwana mpaka atakaporudi. Kama Wayahudi walivyosherehekea Pasaka yao ya kwanza, walipotoka utumwani misri na kila mara walipoadhimisha Pasaka, walikumbuka kila mara tendo hilo kubwa la ukarimu wa Mungu kwao, Mungu aliyewatoa utumwani misri na kuwaanzishia safari mpya ya ukombozi. Kumbe nasi taifa jipya la Mungu, kila mara tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu, tunakumbuka Fumbo kubwa la Ukombozi wetu, Fumbo la Pasaka. Tunasherehekea Zawadi kubwa ya ukarimu wa Mungu, aliyetutoa katika utumwa wa dhambi na mauti kwa sadaka ya mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo. Ndugu mpendwa, tunapoadhimisha Sherehe hii kubwa ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo tunapata nafasi kila mmoja wetu ya kutafakari juu ya Upendo na ukarimu huu mkubwa wa kimungu. Tunapata nafasi ya kutambua kwamba, Ekaristi ni zaidi ya kusanyiko, ni zaidi ya karamu ya kawaida. Ni sadaka, ni upendo, ni uzima, ni ukarimu wa kimungu. Ni Fumbo Takatifu sana ambalo kwalo tumepata uzima wa milele. Lakini pia sisi hatushiriki Ekaristi Takatifu tu kama watazamaji, bali tunashiriki katika tukio la kihistoria la ukombozi wetu, tunaloliadhimisha leo na sasa, tukikumbuka wakati uliopita katika wakati huu na sasa, na kwa matazamio ya wakati ujao. Je, mimi ninashiriki namna gani katika Ekaristi Takatifu? Ninajiandaa kikamilifu ili kweli niweze kushirikishwa neema zitokanazo na adhimisho hilo, neema inayoweza kubadili kabisa maisha yangu na kuanzisha kila kitu upya ndani mwangu? Tunapopokea Ekaristi tunakumbushwa kupenda, kwa kuwa ni sadaka ya upendo. Je, ninapenda namna gani katika maisha yangu ya kila siku? Ekaristi inatupa nguvu ya kuwa tayari kuwahudumia wengine kwa mapendo na sadaka kama Kristo alivyojitoa kwa ajili yetu. Tuombe neema ya kujitoa kikamilifu katika utumishi wetu, kila mmoja katika wito ambao Mungu amependa kumshirikisha, kama Padre, Baba na Mama wa Familia, wafanyakazi, watoto kwa wazazi, kila mmoja asiishi kwa ajili yake tu, bali daima tuwe tayari kuishi na kuyatoa maisha yetu kwa ajlli ya wengine.
Tano: Ekaristi Takatifu ni mwaliko kwetu sote kwenda kufanya Utume na kutoka ushuhuda kwa maisha yetu. (Eucharist and Mission). Zaburi ya 147 ambayo ni wimbo wa katikati katika Sherehe hii ya Mwili na Damu Takatifu ya Bwana wetu Yesu Kristo inasema, “Msifu Bwana Ee Yerusalemu.” Ni Zaburi ya shukrani. Zaburi hii inatualika sote kumsifu Mungu hadharani kwa baraka zake mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku, anayetulisha, anayetukinga, anayetuongoza, anayetuonea huruma, anayetufadhili na kutukirima kila neema na baraka za mbinguni. Zaburi hii katika sherehe hii inatufundisha kuwa imani yetu inapaswa kuonekana nje. Kila siku, baada ya kulishwa na Kristo katika Misa Takatifu, na kwa namna ya pekee katika sherehe hii, tunaitwa kwenda mitaani kushuhudia upendo wake kwa matendo, tukiwa na uhakika kuwa yeye anatupa ulinzi na amani. Ndugu mpendwa, Yerusalemu (ambalo ni mfano wa Kanisa au jumuiya ya waamini) inaitwa daima isikae kimya. Katika ulimwengu wa sasa, kuna mtazamo kwamba dini inapaswa kubaki moyoni au ndani ya nyumba ya ibada tu. Zaburi hii inavunja mtazamo huo kwa kutoka na kwenda kutoa ushuhuda mitaani. Tunapoandamana hadharani tukiwa tumemshika Kristo katika Ekaristi, tunawaonesha wale wasiomfahamu au waliokata tamaa kuwa Mungu yuko hai na anajishughulisha na maisha yetu. Ushuhuda wa hadhara haumaanishi tu kuimba, kupiga makofi na vigelegele mitaani katika maandamano, bali kwenda kuwasaidia kweli wenye shida. Kama vile Kristo alivyojitoa kuwa chakula, na sisi tunajifunza kujimega kwa ajili ya wengine kwa kuwasaidia maskini, wagonjwa, na wenye upweke. Huko ndiko kumpeleka Kristo mitaani.
Ekaristi Takatifu inatupa nguvu ya kushinda hofu na woga katika kumshuhudia Kristo. Kuishi kama Mkristo wa kweli katika ulimwengu wa sasa unaoenda kinyume na maadili ya Injili (kama vile rushwa, chuki, au mmomonyoko wa maadili) kunahitaji ujasiri mkubwa. Ujasiri huu tunaupata wapi? Tutaupata katika kuungana kabisa na Kristo katika Ekaristi takatifu. Tunaposherehekea sherehe hii tunaalikwa pia kutenga muda wetu kwa ajili ya kukaa na Kristo, kumwabudu yeye, Ekaristi Takatifu. Tuseme naye, tumtukuze, tumsifu, tumwombe na kumsikiliza anaposema nasi kila siku. Pia kutoa ushuhuda wa Ekaristi ni kuishi kweli ukisto wetu, kusimama imara katika imani yetu katika ulimwengu huu uliojaa kila aina ya mafundisho ya kupotosha. Tusitetereke imani yetu, tuyashike kiaminifu mafundisho msingi ya Imani yetu. Tunayo zawadi kubwa sana ambayo Kristo alipenda yeye mwenyewe kutupatia sisi, ndio Ekaristi Takatifu. Mwisho tunaalikwa pia kuwa na heshima ya pekee hasa katika kumpokea Yesu. Kanisa linatufundisha kuwa Yesu yupo mzima na hai katika kila kipande hata kidogo kabisa cha Hostia Takatifu. Tunakumbushwa kila tunapopokea Ekaristi takatifu kuhakikisha hakibaki hata kipande kidogo mkononi. Kwa kuwa tukiacha chembe hata hizo ndogo ndogo ziakaanguka ni sawa na kutupa Ekaristi nzima. Hivyo tuwe makini kila tupokeapo Ekaristi Takatifu. Hitimisho: Katika Sherehe hii ya Ekaristi Takatifu, tunamshukuru Mungu ambaye kwa mapendo makubwa alimtoa kwetu mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, akatwaa mwili na kukaa kati yetu, akashiriki ubinadamu wetu ili atushirikishe Umungu wake, na bado amebaki nasi kwa daima katika maumbo ya mkate na divai. Tuombe neema ya kudumu katika ushirika na Kristo, kwa kumpokea daima kwa imani na katika hali ya neema katika Ekaristi Takatifu ili tuweze kunufaika na matunda yatokanayo na kule kupokea kwetu Fumbo hili Takatifu.