Kambodia:watumwa wapya wa mji wa ulaghai&waliohamishwa ndio sura iliyofichwa ya mgogoro!
Na Paolo Affatato.
Kambodia inakabiliwa na dharura mbili za kibinadamu. Kwa upande mmoja, kuna watu waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo kwenye mpaka na Thailand; kwa upande mwingine, kuna mgogoro wa kimya kimya: ule wa waathiriwa wa 'miji ya ulaghai,' watu walionaswa katika biashara haramu ya binadamu, waliotekwa nyara na kutumiwa kama watumwa. Ndivyo anavyoandika Mwandishi wa habari na mwandishi wa insha, mhusika wa timu ya wahariri ya Asia katika shirika la Kipapa la habari za Kimisionari Fides. Akihojiana na Msimamizi wa Kitume huko Battambang, na ambaye ni Mjesuit wa Kihispania, Padre Enrique Figaredo Alvargonzález, alisimulia kwa kina jinsi Kanisa la Kambodia lilivyojitolea kwa sasa kushughulikia matatizo na vurugu zinazowaathiri hasa walio katika mazingira magumu zaidi. "Hali ya kijamii si bora zaidi," alisema Mwakilishi wa kitume. "Tatizo la kinachoitwa 'miji ya ulaghai' husababisha machafuko na umaskini. Tunahisi hivyo hasa katika jimbo la Battambang, karibu na mpaka, lakini kiukweli jambo hilo linaathiri nchi nzima," alibainisha.
Operesheni ya utekelezaji tangu 2025
Katika miaka ya hivi karibuni, Kambodia imekuwa mojawapo ya vituo vikuu vya Asia vya kile kinachoitwa “miji ya ulaghai," majengo yenye maboma yanayoendeshwa na mitandao ya uhalifu ya kimataifa, ambapo maelfu ya watu huajiriwa kwa ofa za kazi za uongo na kulazimishwa, chini ya tishio, kutekeleza ulaghai mtandaoni dhidi ya waathiriwa ulimwenguni kote. Tangu Julai 2025, serikali ya Kambodia imeanzisha operesheni kubwa ya utekelezaji, ikitangaza kufungwa kwa vituo karibu 200, kukamatwa kwa baadhi ya maafisa, na kurejeshwa kwa maelfu ya watu. Hata hivyo, mashirika ya kimataifa kama vile Amnesty International yanasisitiza kwamba vituo vingi vimehamishwa au kufunguliwa tena kwa njia nyingine, na kulaani ushirikiano unaoendelea kati ya makundi ya wahalifu na maafisa wa eneo hilo.
Zaidi ya hayo, kuna visa vilivyoandikwa vya kazi ya kulazimishwa, mateso, unyanyasaji wa kijinsia, kukamatwa kiholela, na mauaji. Ni katika suala hili hasa ambapo Caritas Cambodia, inayoongozwa na Padre Figaredo, kwa sasa inaelekeza nguvu zake nyingi: "Watu hawa wote ni waathiriwa wa biashara haramu ya binadamu," alielezea. "Wanaondoka katika nchi zao wakiwa na matumaini makubwa, wakidhani watapata kazi nzuri. Badala yake, wanaangukia mtegoni. Mara tu wanapofika, waandaaji wa mtandao wa uhalifu wanawanyang'anya pasipoti zao, wanawatishia, na kutumia vurugu kuwageuza kuwa watumwa."
Waathirika kutoka nchi za Asia na Afrika
Waathiriwa wanatoka katika nchi nyingi za Asia na Afrika. "Wanatoka Indonesia, Ufilipino, na China, lakini pia kutoka nchi kadhaa za Afrika," alielezea. "Baadhi yao wanafanikiwa kutoroka na kuja kwetu, wakiwa wamechoka na kukata tamaa, bila hati zozote za utambulisho kwa sababu pasipoti zao zimechukuliwa." Kwa mashirika ya kikanisa kama Caritas, hatua ya kwanza ni kuwakaribisha: "Jambo la kwanza ni kutambua ubinadamu wao unaoteseka na kuwakaribisha," alisema Msimamizi wa Kitume. "Tuna mahali ambapo wanaweza kukaa na kugundua upya kiwango cha ubinadamu, na watu wanaowajali bila kuwanyanyasa au kuwatelekeza. Kisha tunaanza mchakato mgumu sana, kufanya kazi na Wizara ya Mambo ya Ndani na balozi za nchi zao husika. Kwa kuwa hawana hati, tunahitaji kuzipata mpya ili kuwaruhusu kurudi katika nchi zao za asili," alibainisha.
Hata hivyo, mchakato huo mara nyingi ni mrefu na mgumu. "Wakati mwingine watu hutoka katika nchi ambazo hazina hata uwakilishi wa kidiplomasia nchini Kambodia," alisema. "Kisha tunapaswa kuwasiliana na Caritas wa nchi yao, hasa barani Afrika, ili iweze kusaidia mamlaka za mitaa kuwatambua." Kila kesi inahitaji utambuzi makini: "Si rahisi kila wakati kuelewa tunashughulika na nani," alibainisha Padre Figaredo. "Wakati mwingine hatujui kama tunazungumza na mwathiriwa au mtu anayetafuta tu njia ya kutoka katika hali ngumu. Baadhi wametekwa nyara. Wengine wanaweza kuwa sehemu ya shirika la wahalifu lakini sasa wanataka kutoka. Watu hawa pia wamenaswa kwa namna fulani: wakijaribu kuacha makundi ya wahalifu yaliyowaajiri, wana hatari ya kuuawa." Hii ndiyo sababu, aliongeza, "tunawakaribisha hata hivyo. Kwanza kabisa, wao ni wanadamu. Kila mtu anahitaji kupendwa, kutunzwa, na kusikilizwa. Wengi wameumia sana. Wanaishi bila usalama, wamepitia vurugu, wakati mwingine hata vurugu za kijinsia. Kila mtu hubeba majeraha yake mwenyewe, ana historia tofauti, na kila kesi inahitaji uangalifu maalum."
Tunapaswa kuwatunza
Katika miezi ya hivi karibuni, huduma hii imekuwa moja ya shughuli kuu za Caritas za hapa: "Tumezidiwa na kazi," anasema. "Kuna nyakati ambapo tunawakaribisha vikundi vya watu hamsini au sitini kwa wakati mmoja. Tunapaswa kuwalisha, kuwatunza, kuwasaidia kuungana tena na familia zao, kuwasiliana na mamlaka, na kuongozana nao hadi watakaporudishwa nyumbani." Sambamba na dharura hii ya kimya kimya, Kambodia inaendelea kushughulikia matokeo ya mvutano kando ya mpaka na Thailand. "Leo tuko katika hali ngumu," anasema Figaredo, anayeishi Battambang, moja ya majimbo ya mpakani. "Kuna usitishaji rasmi wa mapigano, na mawaziri wa mambo ya nje wanaendelea na mazungumzo yao. Lakini mpaka bado umefungwa, biashara imesimama, na wanajeshi wa Thailand na Kambodia bado wamepiga kambi wakikabiliana msituni. Mara kwa mara, bado kuna milio ya risasi." Kulingana na Misimamizi wa Kitume, hatari ni kwamba mantiki ya nguvu pekee ndiyo itakayotawala: "Tukitazama hali ya kimataifa kwa ujumla, tuna wasiwasi kuhusu matokeo ambayo hii inaweza kuwa nayo katika muktadha wetu: Ikiwa sheria ya kimataifa si kanuni inayoongoza tena na, katika mahusiano kati ya majimbo, kigezo pekee halali ni sheria ya wenye nguvu zaidi, basi kila mtu atahisi ana haki ya kutenda kwa njia ile ile na ni nguvu ya kijeshi pekee itakayohesabiwa, pamoja na mashindano ya silaha yanayotokana nayo.
Inasikitisha kuona mikataba ya kimataifa kupoteza thamani
Inasikitisha sana kuona kwamba mikataba ya kimataifa inaonekana kupoteza thamani." Padre Figaredo pia anaogopa kwamba mgogoro huo utaishia kufunika dharura zingine: "Vita hii inafunika visa vya biashara haramu ya binadamu, kashfa, na mateso ya walio hatarini zaidi. Na, kama kawaida, ni maskini hasa wanaolipa gharama hiyo." Matokeo ya kibinadamu ya mgogoro huo yanabaki kuwa makubwa nchini Kambodia. Kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa, katika miezi ya mwanzo ya 2026, bado kulikuwa na takriban watu 400,000 waliohamishwa ndani, huku kurejea kwa mamia ya maelfu ya wafanyakazi wahamiaji kutoka Thailand kumezidisha mgogoro wa kiuchumi katika majimbo ya mpakani, na kuacha familia nyingi bila kipato au matarajio.
Makundi mawili yaliyohamishwa
Msimamizi wa Kitume alielezea: "Kimsingi kuna makundi mawili ya watu waliohamishwa: la kwanza ni wale ambao hawawezi tena kurudi kwenye vijiji vyao kwa sababu sasa wako katika eneo linalodhibitiwa na Thailand." Kwao, serikali imejenga makazi mapya katika maeneo ya ndani, yenye maelfu ya nyumba. Bado si mali ya kudumu, lakini angalau wanaruhusu familia kuanza upya maisha ya kijamii. Kisha kuna waliohamishwa makazi ambao wamepata kimbilio katika mahekalu ya Wabuddha au na jamaa: "Nimetembelea jamii hizi," alisema. "Kuna watu wanaokaribishwa katika nyumba za watawa, wengine wanakaribishwa na wanafamilia, mara nyingi katika hali ngumu sana, na bado wengine wanaishi katika vijiji vipya. Katika baadhi ya makazi haya, pia kuna jamii za Wakatoliki, na tunatumaini siku moja kujenga kanisa."
Jibu la Kanisa
Jibu la Kanisa linategemea ushirikiano kati ya vyombo vyote vya kanisa: "Tumeunda kikundi cha pamoja cha kazi kinachoratibiwa na Caritas," alielezea Padre Figaredo. "Kila shirika au jamii hutoa mchango wake: Wajesuit hufanya kazi katika elimu, wengine hutunza watoto wenye ulemavu, bado wengine hutunza wazee na kusambaza chakula. Kila mtu ana jukumu lake dogo, lakini kila mtu hufanya kazi pamoja." Kwa Msimamizi wa Kitume, mtandao huu wa mshikamano, uliosukwa kwa uvumilivu na makundi mbalimbali ya Wakatoliki, leo hii unawakilisha mojawapo ya ishara halisi za matumaini kwa Kambodia ambayo inaendelea kukabiliana, mara nyingi mbali na uangalizi wa kimataifa, na majeraha ya vita, biashara haramu ya binadamu, na umaskini.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.