Msumbiji:Masista wamisionari wawapa faraja waathiriwa wa mafuriko huko Xai-Xai
Na Sr. Christine Masivo, CPS
Katika sehemu nyingi za dunia, maeneo ya pwani yanakabiliwa na mafuriko yasiyotabirika ambayo husababisha uharibifu, kuhamisha watu na kuvuruga maisha ya kila siku. Huko Maputo, mji mkuu wa Msumbiji, na katika eneo la Limpopo, ambapo Masista Wamisionari wa Damu Azizi wamekuwa wakihudumu kwa muongo mmoja, wakazi waliathiriwa na mafuriko, na masista walijitokeza mara kwa mara kutoa msaada halisi.
Huduma na programu
Kwa miaka mingi, utume wao umepanuka katika majimbo kadhaa ya nchi, ikiwa ni pamoja na Maputo, Gaza, Tete, na Nacala. Watawa hawa wanafanya kazi kupitia wizara za kilimo, elimu, afya, programu za kijamii na ya kichungaji, huku wakiendesha pia programu kwa ajili ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, wazee, watu wenye utapiamlo, na watu binafsi wanaoishi na ugonjwa wa virusi vya ukimwi. Masista wanafanya utume wao mara ili kukuza maendeleo shirikishi ya binadamu na kuleta matumaini kwa jamii zinazokabiliwa na matatizo.
Waathiriwa wa mafuriko huko Xai-Xai
Watawa hawa wamejitolea kuwahudumia watu walio katika mazingira magumu zaidi katika jamii, kuwafikia waliotengwa na kukuza utu wa kila mwanadamu. Sr. Lígia Alberto Muianga, mkuu wa Kanda ya Msumbiji, alisimulia jinsi "mafuriko makubwa yalivyokumba sehemu za Mkoa wa Gaza, na kuacha familia nyingi zikiwa zimekimbia makazi yao na kuhitaji msaada wa dharura katika wilaya ya Xai-Xai, hasa katika kitongoji chao." Jamii nyingi zililazimika kuondoka katika nyumba zao huku maji yakiyoongezeka na kuyafanya mazingira yao kuwa hatarini.
Watu waliohamishwa wasaidiwa
Katika kukabiliana na mgogoro huu, watawa hao walichukua hatua ya kuwasaidia wale wanaoishi katika hali hizi zisizo za kuvumilia. Baada ya waathiriwa kuhamishwa na mamlaka za mitaa hadi shuleni na vituo vikubwa kwa ajili ya usalama, masista hawa huenda kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa zaidi katika mtaa wao, wakiwasaidia takriban watu 1,600 waliohamishwa wakitafuta hifadhi, wakiwemo karibu watoto 600. Wengi hufika makazi haya wakiwa na nguo walizokuwa wamevaa, wakihisi wamevunjika moyo baada ya kupoteza nyumba, mali, na riziki zao.
Utume wa uokoaji wa huruma
Masista hawa hujihami mara moja wakati mafuriko yanapotokea kwa haraka na kuanza kuandaa chakula cha msaada kwa waathiriwa mara tatu kwa juma. Wao hupika chakula kwenye nyumba yao na kisha kusafirisha hadi mahali waathiriwa wa mafuriko wapo, na kuwagawia familia zilizohamishwa. Mwitikio wa kibinadamu haujawa wa watawa pekee. Kwa msukumo wa kujitolea na huruma yao, wanawake kadhaa wa eneo hilo hujiunga nao wakijitolea wakati wao kusaidia kuandaa na kusambaza chakula. Watawa hawa pia hutambua mahitaji mengine zaidi ya chakula na malazi, kama vile vitu vya usafi na mavazi, huku wakijitahidi kuhakikisha usalama wa waathiriwa.
Kuwasikiliza waathiriwa
Katika makazi ya waathiriwa, magodoro hupangwa ili familia waweze kupumzika huku wakisubiri maji ya mafuriko yapungue na maisha yaanze tena. Masista hao pia huhamasisha watu miongoni mwa jamii na washirika wa eneo hilo, wakiomba msaada zaidi ili kukidhi mahitaji ya dharura zaidi haswa wakati wa mafuriko. "Wakati wa ziara zao kwenye makazi, masista huchukua muda kusikiliza waathiriwa na familia zilizohamishwa na kutathmini mahitaji yao muhimu zaidi. Uwepo wa masista hawa huleta faraja na kurahisisha mapambano yao," alisema Sr. Ligia.
Tumaini katika mateso
Uwepo wa masista miongoni mwa waathiriwa huwa mwanga wa matumaini wakati huu wa mateso. Kujitolea kwao kunaonyesha moyo wa karama yao, kusimama na waliotengwa na wale wanaoteseka, kurejesha hadhi pale ambapo hakuna matumaini. Kupitia matendo yao rahisi lakini yenye nguvu ya huduma, kuandaa milo, kutembelea makazi ya walio athiriwa, na kuwapamoja na waliohamishwa, masista hawa wanaendelea kutekeleza utume ambao umewaongoza kwa zaidi ya karne moja nchini Msumbiji. Uwepo wao wa huruma na upendo miongoni mwa waliotengwa huleta uponyaji pale ambapo maisha ya wanadamu yamejeruhiwa.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.