Tarehe 7 Julai 2026 Ni Siku ya Kuombea Haki na Amani Tanzania!
Idara ya Mawasiliano Jimbo Katoliki la Mafinga, Mafinga, - Iringa
Wapendwa Mapadre, Watawa na Waamini wote wa Jimbo Katoliki la Mafinga, Neema na amani ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Tarehe 7 Julai tulitakiwa kufanya hija kwenye kituo chetu cha hija cha jimbo, Madibira. Hija hiyo imeahirishwa mpaka tarehe 26 Agosti. Katika roho ya imani, umoja na upendo kwa Taifa letu la Tanzania, na kwa kutambua kwamba Mungu ndiye Bwana wa historia na Mfalme wa amani ya kweli, ninawaelekeza na kuwaalika waamini wote wa Jimbo Katoliki la Mafinga kuifanya siku ya Jumanne, tarehe 7 Julai 2026, kuwa siku maalum ya sala kwa ajili ya Taifa letu. Kwa sababu hiyo, badala ya kushiriki hija ya Madibira siku hiyo, ninawaagiza na kuwaalika waamini wote pamoja na majirani zetu wenye mapenzi mema kubaki majumbani mwao kwa utulivu na amani. Wale watakaopata nafasi wahudhurie makanisani kwa ajili ya kumwabudu Yesu katika Sakramenti Kuu ya Ekaristi na kusali kwa bidii kwa ajili ya Tanzania yetu. Kwa namna ya pekee, sala zetu zielekezwe kwa nia zifuatazo: Kumwomba Mwenyezi Mungu aijalie Tanzania amani, umoja na mshikamano. Kuombea viongozi wa nchi katika ngazi zote wapate hekima, busara na moyo wa kuwatumikia wananchi kwa haki na uadilifu. Kuombea wananchi wote wa Tanzania waendelee kujenga utamaduni wa upendo, kuheshimiana na kutafuta mema ya wote.
Kuombea vijana, familia na makundi yote ya kijamii ili waishi katika ukweli, matumaini na mshikamano. Kumwomba Mama Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, mlinzi wa Taifa letu, ili tuishi kwa haki na amani. Ninawaomba Mapadre wote kuandaa vipindi vya Ibada ya Kumwabudu Yesu Ekaristi, Rozari Takatifu, Sala za Waamini na, inapowezekana, kuadhimisha Misa Takatifu kwa nia ya Taifa letu. Ninawaalika pia ndugu zetu wa madhehebu mengine na watu wote wenye mapenzi mema kuungana nasi katika kumwomba Mungu aliye chanzo cha amani na haki. Tukikumbuka maneno ya Mtume Paulo: "Na kwanza kabisa naagiza kufanyika dua, na sala, na maombezi, na shukrani kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tupate kuishi maisha ya utulivu na amani katika utauwa wote na ustahivu." (1 Timotheo 2:1-2). Bwana Yesu, Mfalme wa Amani, uibariki Tanzania. Bikira Maria, Mama wa Taifa letu, utuombee.
SALA YA KUIOMBEA TANZANIA: Ee Mungu Mwenyezi wa milele, Baba wa mataifa yote na wa watu wote, utuangalie kwa macho ya huruma sisi watu wako wa Tanzania, ambao nasi sasa twahesabika kati ya mataifa ya dunia. Kwa baraka yako uhuru wetu huu usipokonywe, na utuwezeshe kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo waana wa Mungu. Tunakuomba nchi yetu iwe ya amani, waliopotea wapatikane na waliotekwa wapate uhuru wao, walioumizwa wapone, na waliouawa wapate uzima wa milele na uovu ukome katika nchi yetu. Tunakuomba ubadilishe nyoyo za watenda maovu na washirika wao katika uovu ili zikuelekee wewe, kwani sisi tulio wanyonge hatuna uwezo wa kuzibadilisha nyoyo ovu. Uendelee kututawala na kutuongoza. Daima nchi hii iongozwe na viongozi ambao ni chaguo lako. Waangazie watawala hao, sheria wanazotunga kwa kutufaidia kwa mambo mema ya hapa duniani zipatane na Wewe uliyetuumba kwa ajili yako. Wajalie watu wetu wote paji lako la Imani.
Tukiwa Mahujaji wa Matumaini, tuthibitishe tusishindwe kupambana na maovu yawezayo kutufikia kutoka nje au ndani, tupe hekima ya kutafuta ukweli katika mambo yote, na kuishi kwa uaminifu katika amri zako. Ee Mwenyezi Mungu, uongozi wa kweli unatoka kwako, tunakuomba ujalie wale watakaosimamia na kuiishi Demokrasia ya kweli, Haki na Amani katika nchi yetu ili haki ituletee Amani ya kudumu. Washa nyoyo zetu na mapendo yako ya kimungu yatakayotuwezesha kushinda utengano, ushindani, na chuki ya ukabila au utaifa, na tuunganishe wote katika muungano wa kidugu utakaotuwezesha, kwa msaada wa neema yako, kutufanya tuwe umoja katika Wewe Baba wa wote. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina. Bikira Maria Mtakatifu Mkingiwa dhambi ya asili. Utuombee. Atukuzwe Baba.... Amina.