Papa Francisko Mifano ya Injili ya Huruma na Upendo wa Mungu Kwa Binadamu Mdhambi na Dhaifu

Papa Francisko, katika tafakari kuhusu Injili ya Dominika ya 24 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Lk 15:1-31: Yesu na wenye dhambi kuhusu: Kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea na mwana mpotevu, kielelezo cha Baba mwenye huruma na mapendo anasema, ni mifano ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu dhaifu na mdhambi, jibu kwa manung'uniko ya Mafarisayo na Waandishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo.

Sakramenti ya upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu.
Sakramenti ya upatanisho ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu.

Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja: msamaha wa dhambi, huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Mapadre waungamishaji kwamba, wao ni vyombo na mashuhuda wa upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini. Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake! Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu inapaswa kuendelea kumwilishwa katika maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia kama alama ya mwendelezo wa Mwaka wa Huruma ya Mungu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa tafakari yake kuhusu Injili ya Dominika ya 24 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa: Lk 15:1-31: Yesu na wenye dhambi kuhusu: Kondoo aliyepotea, shilingi iliyopotea na mwana mpotevu, kielelezo cha Baba mwenye huruma na mapendo anasema, ni mifano ya huruma ya Mungu kwa mwanadamu dhaifu na mdhambi.

Papa Francisko akishiriki chakula pamoja na maskini wa Jiji la Roma.
Papa Francisko akishiriki chakula pamoja na maskini wa Jiji la Roma.

Hili ni jibu makini dhidi ya manung’uniko yaliyokuwa yanayotolewa dhidi yake. “Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Mafarisayo na waandishi wakanung’unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.” Lk 15: 1-2. Wao waliona mtindo huu wa maisha kuwa ni kashfa ya mwaka, lakini kwa Kristo Yesu, kilikuwa ni kitendo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaoganga, kuponya na kuokoa na kwamba, Mungu anawapenda wote kama watoto wake bila ya ubaguzi. Sehemu hii ni kiini cha Injili ya Kristo; Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, unaowatafuta wale wote waliopotea. Mifano yote mitatu, inaonesha mapungufu katika maisha ya mwanadamu: Mchungaji amempoteza kondoo, mwanamke amepoteza shilingi na Baba mwenye huruma amempoteza Mwana, ingawa alikuwa na mwanae mkubwa, lakini akapiga moyo konde na kuendelea kumsubiri. Hiki ni kielelezo cha mtu anayependa kwa dhati, kwani hataki hata mara moja chochote kile kipotee. Baba Mtakatifu anasema huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Huruma hii inamsumbua na “kumnyima usingizi” kiasi cha kuacha yote na kuanza kumtafuta binadamu dhaifu na mdhambi, ili akimpata aweze kumbeba na kumweka mabegani mwake, kielelezo cha Baba mwenye huruma na mapendo thabiti, au Mama anayeteseka kwa kukosekana kwa mtoto wake mpendwa.

Huruma na upendo wa Baba wa Milele imwilishwe katika maisha ya watu.
Huruma na upendo wa Baba wa Milele imwilishwe katika maisha ya watu.

Mwenyezi Mungu anateseka pale mwanadamu anapokengeuka na kutopea katika dhambi na daima, anamsubiri ili aweze kutubu na kurejea tena, kama anavyosimulia Mzaburi akisema, “Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. BWANA ndiye mlinzi wako; BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume.” Zab 121: 4-5. Baba Mtakatifu katika hali na mazingira haya, anawatupia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, swali chokonozi, kwa kuwataka kutafakari maisha yao na kuangalia ikiwa kama kweli, Baba mwenye huruma na mapendo, amekuwa kwao ni mfano bora wa kuigwa? Mambo yepi yanayowakwamisha katika maisha yao? Je, wanajitaabisha kuwatafuta wale waliopotea na kutokomea kule kusiko julikana? Waamini wanapaswa kuwa wa kweli na watu wazi mbele ya jirani zao, mwaliko wa Kiinjili. Waamini wajitaabishe kuwatafuta jirani zao, kwa kuwaonesha huruma na mapendo; kwa kuguswa na mahangaiko ya wale wanaokosekana, ili wote watambue kwamba, wana thamani kubwa mbele na machoni pa mwenyezi Mungu. Waamini wakimbilie ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ambaye kamwe hachoki kuwatafuta na kuwapatia hifadhi watoto wake wapendwa!

Huruma ya Mungu
11 Septemba 2022, 15:28

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >