Katekesi ya Papa leo XIV:Matumaini huzaliwa katika ukimya na si katika kelele
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV akiongoza Katekesi yake Jumatano tarehe 17 Septemba 2025, siku ambayo Mama Kanisa katika Liturujia anamkumbuka Mtakatifu Robert Bellarmine, ambaye ni Somo wa Baba Mtakatifu kwa jina la Robert Francis, kwa hakika ilitoa chachu kweli ya siku ya ukaribisho kwa Papa kutoka kwa watu wapato 30,000, waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican kushuhudia katekesi hii ya kila Jumatano. Awali ya Yote kabla ya tafakari, Baba Mtakatifu aliwasalimia kila mtu kwa kuzunguka Uwanja mzima kupitia kigari cha kipapa, huku akibariki zaidi watoto wadogo wengi mno wa kike na kiume. Kwa njia hiyo katika Mwendelezo wa Mzunguko wa Katekesi ya Jubilei 2025, Yesu Kristo Tumaini letu, kifungu cha Pasaka ya Yesu, Papa amedadavua Kifo: Injili ya Yohane iliyosomwa: kaburi jipya ambalo lilikuwa alijawekwa mtu yeyote” (Yh 19:41).
Baba Mtakatifu Leo aliwagukia kaka na dada wapendwa kwamba: Katika safari yetu ya katekesi juu ya Yesu tumaini letu, leo tutatafakari fumbo la Jumamosi kuu. Mwana wa Mungu amelala kaburini. Lakini "kutokuwepo" kwake sio utupu: ni matarajio, utimilifu uliozuiliwa, ahadi iliyowekwa gizani. Ni siku ya ukimya mkuu, ambamo mbingu inaonekana kuwa bubu na dunia kutosonga, lakini ni hapo ndipo fumbo la ndani kabisa la imani ya Kikristo inatimizwa. Ni ukimya uliojaa maana, kama tumbo la uzazi la mama anayembeba mtoto wake ambaye hajazaliwa lakini tayari yuko hai. Mwili wa Yesu, ulioshushwa kutoka msalabani, umefungwa kwa uangalifu, kama mtu anavyofanya kwa kitu cha thamani. Mwinjili Yohane anatuambia kwamba alizikwa katika bustani, ndani ya “kaburi jipya ambalo lilikuwa alijawekwa mtu yeyote” (Yn 19:41). Hakuna kinachoachwa kwa bahati. Bustani hiyo inakumbusha Edeni iliyopotea, mahali ambapo Mungu na mwanadamu waliunganishwa.
Na kaburi hilo, ambalo lilikuwa halijawahi kutumika, linazungumza juu ya kitu ambacho bado kinapaswa kutokea: ni kizingiti, sio mwisho. Mwanzoni mwa uumbaji, Mungu alipanda bustani; sasa uumbaji mpya pia unaanza katika bustani: pamoja na kaburi lililofungwa ambalo litafunguliwa mapema. Jumamosi takatifu pia ni siku ya kupumzika. Kulingana na Sheria ya Kiyahudi, hakuna kazi itakayofanywa siku ya saba: hakika, baada ya siku sita za uumbaji, Mungu anapumzika (rej. Mwa 2:2). Sasa, Mwana pia, baada ya kumaliza kazi yake ya wokovu, anapumzika. Sio kwa sababu amechoka, lakini kwa sababu alipenda hadi mwisho. Hakuna cha kuongeza. Pumziko hili ni muhuri juu ya kazi iliyokamilishwa; ni uthibitisho kwamba kile ambacho kilipaswa kufanywa kimetimizwa kweli. Ni pumziko lililojaa uwepo uliofichwa wa Bwana. Papa alisisitiza kuwa tunajitahidi kusimama na kupumzika. Tunaishi kana kwamba maisha hayatoshi kamwe. Tunakimbilia kuzalisha, kujithibitisha wenyewe, na kuendelea. Lakini Injili inatufundisha kwamba kujua jinsi ya kuacha, ni tendo la uaminifu ambalo ni lazima tujifunze kulifanya. Jumamosi Takatifu inatualika kugundua kwamba maisha daima hayategemei kile tunachofanya, lakini pia jinsi tunavyojua jinsi ya kuacha kile ambacho tumeweza kufanya.
Kaburini, Yesu, ambaye ni Neno lililo hai la Baba, yuko kimya. Lakini ni katika ukimya huo ndipo maisha mapya yanaanza kuchanua. Kama mbegu katika ardhi, kama giza kabla ya mapambazuko. Mungu haogopi wakati unaopita, kwa sababu yeye pia ni Mungu wa kungoja. Kwa hivyo, hata wakati wetu "usio na maana", ule wa kutua, utupu, wakati wa tasa, unaweza kuwa tumbo la uzazi la ufufuo. Kila ukimya unaokaribishwa unaweza kuwa msingi wa Neno jipya. Kila wakati uliosimamishwa unaweza kuwa wakati wa neema, ikiwa tunaitoa kwa Mungu. Yesu, aliyezikwa ardhini, ni uso mpole wa Mungu ambaye hachukui nafasi yote. Yeye ndiye Mungu anayeruhusu mambo yafanyike, anayengoja, anayejiondoa ili kutuachia uhuru. Yeye ndiye Mungu anayemwamini, hata wakati kila kitu kinaonekana kumalizika. Na sisi, katika Sabato hiyo iliyoahirishwa, tunajifunza kwamba hatupaswi kuwa na haraka ya kufufuka tena; kwanza ni lazima tukae na kukaribisha ukimya, tukubali kukumbatiwa na mipaka.
Baba Mtakatifu aliendelea kusisisitiza kuwa “Wakati fulani tunatafuta majibu ya haraka, masuluhisho ya papo hapo. Lakini Mungu hufanya kazi kwa kina, katika wakati wa polepole wa uaminifu. Kwa hiyo Sabato ya maziko inakuwa tumbo la uzazi ambamo nguvu za nuru isiyoshindwa, ile ya Pasaka, inaweza kutokeza. Papa Leo XIV alieleza kwamba tumaini la Kikristo halizaliwi kwa kelele, bali katika ukimya wa matarajio yaliyojaa upendo. Sio uzao wa furaha, lakini wa kuachwa kwa uaminifu. Bikira Maria anatufundisha hivi: anajumuisha matarajio haya, uaminifu huu, tumaini hili. Inapoonekana kwetu kwamba kila kitu kimesimama, kwamba maisha ni barabara iliyofungwa, tukumbuke Jumamosi Kuu. Hata kaburini, Mungu alikuwa akitayarisha mshangao mkuu kuliko yote. Na ikiwa tunajua jinsi ya kukaribisha kwa shukrani kile ambacho kimekuwa, tutagundua kwamba, kwa usahihi katika udogo na ukimya, Mungu anapenda kubadilisha uhalisi, akifanya mambo yote kuwa mapya kwa uaminifu wa upendo wake. Furaha ya kweli huzaliwa na matarajio ya ndani, ya imani yenye subira, ya matumaini kwamba kile ambacho kimeishi katika upendo hakika kitafufuka kwenye uzima wa milele.
